RIWAYA
KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI
11
ILIPOISHIA
Wengine walikuwa wakisema.
“Nahodha utatuua wewe, kuna
watoto humu!”
“Alikuwa akivuta bangi, huyo
hana akili!” Mwanamke mmoja alisema kwa hasira.
Pamoja na kelele zote hizo
nahodha huyo hakumsikiliza mtu yeyote, aliendelea kukielekeza chombo hicho kwenye
mawimbi. Ile dharuba iliyokuwa ikitupiga haikumtia hofu hata chembe.
Pale ndipo nilipogundua
sababu ya baadhi ya manahodha kuvuta bangi, ni kutaka kupata uwezo wa kiakili
wa kukabiliana na ile hali endapo itatokea.
Yule mtu alionekana kama
mwehu. Wimbi linapokuja linatutosa. Na yeye alitota chapa chapa lakini
hakuonesha kupata hofu wala kujali. Siku ile niliapa kuwa sitasafiri tena na
jahazi na sikujua kama tungefika salama Pemba.
Yale mawazo ya kufa
yakanifanya nimkumbuke mke wangu. Nikakumbuka kwamba nilimuahidi kumtumia nauli
na nikahisi kwamba angenipigia simu kuniulizia tena.
Nikatoa simu yangu na kuizima
ili akipiga simu asinipate.
SASA ENDELEA
Upande mmoja wa akili yangu
ukaniambia kuwa hatua hiyo ingeweza kumzidishia wasiwasi mke wangu, jambo
ambalo linaweza kufanya aamue kukopa pesa ya nauli ili aje anifumanie.
Kama atafanya hivyo,
nilijiambia, akifika Korogwe hatanikuta na hivyo atawapa nafasi wale majini
wamtoe kafara.
Kile nilichokuwa sikitaki
ndicho kitakachotokea, nilijiambia.
Nikakumbuka pia nilikuwa
nimewaacha na njaa wale viumbe kule kwenye pango na nikapata hofu kuwa wanaweza
kufa.
Ilimradi nilijikuta
nimesongwa na mawazo mengi lakini niliomba Mungu tufike salama ili nijue
nitafanikiwaje kulitatua lile tatizo lililokuwa linanikabili.
Mungu si Athumani wala si
Huseni. Pamoja na dharuba zilizotupiga baharini tulifika salama Pemba. Tatizo
ni kuwa tulifika usiku.
Ikanibidi nitafute gesti. Mji
huo haukuwa na gesti nyingi kama ilivyo huku bara. Hata hivyo nilifanikiwa
kupata gesti moja katikati ya mji wa Chakechake Pemba. Nikalala hapo hadi
asubuhi.
Kulipokucha ndipo
nilipoulizia kwa wenyweji kilipo hicho Kisima cha Giningi.
“Kipo Kendwa” Kijana
aliyenipokea pale gesti ndiye aliyenijibu. Kabla sijamuuliza huko Kendwa ni
wapi akaendelea kuniuliza.
“Unataka kwenda Giningi?”
“Ndiyo nataka niende
nikapaone”
“Wewe unataka ufike katika
hicho kijiji au hapo kwenye kisima?”
“Nataka nifike hapo kwenye
kisima”
“Magari yapo yanayokwenda
huko”
“Nitayapata wapi?”
Kwa msaada wa yule kijana
aliyegundua kuwa nilikuwa mgeni ninayetoka bara nikafanikiwa kupata daladala
iliyonipeleka katika kijiji hicho kilichokuwa maeneo ya mashambani.
Nilipofika nilipata kijana
mwingine aliyenichukua kwa baskeli ya bodaboda hadi kilipokuwa kisima hicho cha
Giningi.
Kinapotajwa Kisima cha
Giningi mtu angeweza kudhani kuwa kilikuwa kisima cha kisasa na kilichokuwa
katika mazingira ya kupendeza. Lakini hakikuwa hivyo. Kisima chenyewe kilikuwa
ni cha kale sana na kilionekana kama hakikuwa kikitumika tena.
Kwa mujibu wa mzee mmoja
niliyemkuta hapo, kisima hicho ni cha kale sana na haikufahamika kilichimbwa
katika enzi ipi. Lakini kilipata umaarufu kutokana na baadhi ya wenyeweji
kuamini kuwa mahali hapo palikuwa na asili ya kimizimu na majini. Hivyo watu
mbalimbali walikuwa wakifika mahali hapo kufanya matambiko na mambo mengine ya
kiuganga.
Nilimsikiliza kwa makini yule
mzee kabla ya kujitambulisha kwake na kumueleza kuwa nimetoka bara na nilikuwa
na shida na mzee aliyekuwa anaitwa Habib Sultani.
“Ulikuwa unamtaka wa nini?”
Mzee huyo akaniuliza.
“Nina shida naye”
“Shida gani?”
“Nilisikia huyo mzee
anashughulika kuwapa watu majini ya kuwatajirisha”
“Ni kweli. Kwa hiyo wewe
ulikuwa unataka upate utajiri?”
“Hapana. Nina tatizo jingine”
“Nataka nikufahamishe kuwa
huyo mzee uliyemtaja ameshakufa”
Nikashituka na kumuuliza.
“Alikufa lini?”
“Ni muda sasa. Inafika miaka
mitatu”
Nikatikisa kichwa changu
kusikitika. Nikaona safari yangu ya kwenda Pemba ilikuwa ya bure.
“Ungenieleza mimi shida yako
labda ningekusaidia”
“Kwani wewe pia unahusika na
mahali hapa?”
“Mimi ndiye muangalizi wa
eneo hili. Mimi ndiye ninayefagia hapa kila siku na kusaidia watu shida
mbalimbali”
“Huyo Habib Sultani alikuwa
ni nani?”
“Yeye alikuwa mganga na ndiye
aliyeachiwa siri ya mahali hapa na babu yake”
“Sasa sijui utanisaidiaje
mzee wangu…”?
“Niambie tu shida yako wala
usihofu”
Nikamueleza yule mzee
matatizo yangu mwanzo hadi mwisho.
Yule mzee hakushituka hata
kidogo isipokuwa aliinama akafikiri kwa muda kidogo kabla ya kuniuliza.
“Una maana kuwa marehemu baba
yako kabla ya kufa kwake hakuwa amekuarifu kuwa alikuwa na jini kutoka hapa Giningi
linalompatia pesa?’
“Hakuniarifu. Nilizikuta zile
pesa baada ya yeye kufa na yule jini alinifuata usiku akanifahamisha kuwa
alinunuliwa na baba yangu kutoka hapa na akataka mimi nimrithi”
“Na wewe hukutaka?”
“ Sikutaka na sitaki!”
“Yule mke wake na yule mwanao
waliotolewa kafara bado wapo?”
“Wale bado wapo hai lakini
wakati wowote wanaweza kufa. Isitoshe nimeambiwa akifa mama, mke wangu naye
atachukuliwa. Ndiyo maana nimeharakisha kuja huku”
“Tangu nianze kuwa msimamizi
wa kisima hiki leo ndio mara ya kwanza kuona mtu anakataa pesa za majini ambazo
watu wengi wamekuwa wakizitafuta”
“Mimi ni mtu tofauti sana,
Najali utu wa watu, sijali pesa. Bora nife masikini kuliko kuwatoa muhanga
binaadamu wenzangu”
“Basi usiseme maneno mengi,
nataka nikuulize swali moja umeshatumia kiasi gani katika hizo pesa?”
“Sijatumia hata senti tano”
“Sasa mwanangu, mimi ni
muangalizi tu wa eneo hili. Mimi sina uwezo wa kumpa mtu jini wala kumtoa jini
na sijui kama jambo hilo unalolitaka linawezekana…”
“Mzee uliniahidi kuwa
utanisaidia” nikamkatiza yule mzee.
“Msaada wangu utaupata.
Nitakupeleka kwa mwana wa huyo Habib Sultani ambaye ameachiwa mikoba na huyo
baba yake. Sasa msaada zaidi utaupata kwa huyo”
“Sawa, basi nipeleke kwa huyo
aliyeachiwa hiyo mikoba”
“Lakini kuna mawili, anaweza
akusaidie au asikusaidie”
“Mimi ninachotaka wachukue
pesa zao pamoja na yule jini wao”
“Kwa sababu yeye siye
aliyemtoa huyo jini, sina uhakika kuwa ataweza kulifanya jambo hilo lakini
twende ukamsikilize mwenyewe’
Yule mzee akanipeleka katika
nyumba moja iliyokuwa katika kitongoji kile kile cha Kendwa.
Tulimkuta mtu mmoja aliyekuwa
amekaa kwenye kiti cha uvivu akivuta tasbihi. Alikuwa amevaa kanzu nyeupe na
kichwani alijifunga kilemba kikubwa.
“Maalim asalaam alaykum” Yule
mzee akamsalimia. Na mimi pia nikamsalimia.
“Waalaykum salaam” Mtu huyo
akatujibu.
“Tumepata mgeni kutoka bara.
Alikuwa na shida na marehemu Habib Sultani. Nimemwambia Sheikh Habib
allishafariki kitambo lakini yuko mwanawe”
Yule mtu akanitazama na
kuniambia.
“Karibu mgeni?”
“Huyo ndiye mwanawe marehemu Shikh Habib Sultani na yeye pia
anaitwa Sultani. Unaweza kumueleza shida yako” Yule mzee akaniambia.
Tangu nilipomuona mtu huyo
sikutarajia kuwa angekuwa ndiye huyo
mwana wa Habib Sultani. Kwa vile niliambiwa ni mwana, nilitarajia kumuona
kijana mdogo. lakini yeye hakuwa kijana mdogo. Alikuwa mtu mzima na kiumri
alikuwa amenizidi hata mimi.
“Mtolee kiti” Mtu huyo
akamwambia yule mzee niliyekwenda naye.
Yule mzee akaingia ndani ya
ile nyumba na kutoka na kiti akaniwekea
na kuniambia.
“Karibu ukae”
Nikakaa mbele ya yule maalim.
“Haya nieleze shida yako”
Nikaanza kumueleza mtu huyo
matatizo yangu mwanzo mpaka mwisho.
“Nadhani kulikuwa na makosa
yalifanyika kati ya marehemu Habib na baba yako” akaniambia.
“Makosa gani?”
“Huyo jini alimuhusu baba
yako tu na hizo pesa zilimuhusu baba yako tu. Lakini bila shaka baba yako
alikutaja wewe kama mrithi wake na ndio maana huyo jini alikufuata. Sasa kwa
bahati mbaya mzee Habib ameshakufa”
“Nimeambiwa kuwa wewe ndiye
mrithi wake. Nilitarajia kuwa ungeweza kunisaidia”
“Kwani usichotaka wewe ni
kitu gani, ni pesa au jini?” akaniuliza.
“Silitaki hilo jini?”
“Na pesa je?”