Wednesday, May 3, 2017

TANGA PRESS CLUB YAADHIMISHA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI KWA KUOA DAMU




Daktari wa hospitali ya Rufaa ya Bombo Tanga  kitengo cha maabara, Stivin Mnyawoga, akimtoa damu Kamanda wa Polisi Tanga, Benedickti Wakulyamba wakati wa uchangia damu salama kwa hiari zoezi lililoratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Tanga (Tanga Press Club TPC) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari na kufanyika katika viwanja vya klabu hiy leo..



Daktari kitengo cha maabara  hospitali ya Bombo Tanga, Hamis Juma Kayoga, akimtoa mdamu Sadik Shembilu wakati wa zoezi la uchangiaji damu salama liliratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Tanga (TPC) ikiwa ni maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani leo.



Daktari wa hospitali ya Bombo Tanga, Fransisi Julias  kitengo cha maabara, akimtoa damu, Abdalla Yussuf mkazi wa Mikanjuni wakati wa zoezi la uchangiaji wa damu salama liliratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari wa Tanga (TPC) ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani leo.



Daktari wa hospitali ya Bombo Tanga kitengo cha maabara, Stivin Mnyawoga, akimtoa damu mwandioshi wa Radio Nnuor ya Tanga wakati wa uchangia damu kwa hiari zoezi lililoratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari wa Tanga (TPC) na kufanyika katika viwanja vya klabu hiyo leo.



 Mwandishi Pamela akitoa damu wakati wakati wa maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari inayoadhimishwa leo Duniani kote. Mwandishi huyo mbali ya kutoa chupa moja aliomba kutoa nyengine kutokana na kuwa na damu nyingi lakini alikataliwa na madaktari baada ya kupewa elimu ya utoaji damu kwa hiari.


Tuesday, May 2, 2017

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI , NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 20

ZULIA LA FAKI 0655 340572
 
NILIKIONA CHA MTO URITHI WA BABU 20
 
ILIPOISHIA
 
Niliendelea kujiambia kama msichana huyo amekiri kuwa ni mzuka, atakuwa ni muuaji tu. Pengine alikuwa na kisasi na  babu yangu ambaye niliambiwa alikuwa mwanamke wake.
 
Nitakutanaje na kuzungumza na mzuka? Nilijiuliza huku nikifikiria niende Mwananyamala nikamjulishe mzee Nasri kuhusu yale maelezo ya Ummy.
 
Hata hivyo upande mmoja wa akili yangu ulinikataza kwenda Mwananyamala kwa vile nilijua yule mzee atapuuza maelezo yangu kwa ile imani yake kuwa Ummy alishakufa na aliyekufa hawezi kurudi tena duniani.
 
Sasa nifanye nini, huyu msichana ataendelea kuniandama?”  nikajiuliza
 
Sikuweza kupata jibu la haraka kwa vile akili yangu ilikuwa imetaharuki. Nilijiambia nitakapotulia na kurudi katika hali ya kawaida, huenda nitajua nitafanya nini.
 
Wakati nazungumza na Ummy nilikuwa nimesimama kwa kutaharuki, nikakaa kwenye kochi na kuendelea kuwaza.
 
SASA ENDELEA
 
Hisia zangu tangu nianze kumfahamu Ummy sasa zilikuwa zimebadilika. Mwanzo nilikuwa nikihisi kuwa Ummy alikuwa binaadamu anayetumia miujiza kuua watu. Nilijua hivyo tangu nilipoanza kumuona kule Botswana.
 
Na hata pale nilipomkimbia katika chumba cha hoteli aliponiita, nilimkimbia kwa hofu  kuwa alitaka kuniua kama alivyowaua wale wadeni wa marehemu babu.
 
Lakini sasa mtazamo haukuwa huo. Hisia zangu zilikuwa upande mwingine kwamba Ummy hakuwa muuaji mwenye miujiza kama nilivyokuwa nikidhani bali alikuwa mzuka wa mtu aliyekwisha kufa  miaka mitano iliyopita.
 
Kama Ummy aliyekufa alikuwa binadamu, huyu Ummy wa sasa si binaadamu tena. Huu ni mzuka kama alivyoniambia wenyewe. Hauna akili ya kibinaadamu. Mara nyingi mzuka  unapotokea unakuja kuua watu halafu unapotea.
 
Niliwaza kwamba mimi pia  nilikuwa katika orodha ya kuuawa na mzuka huo kwani wale waliouawa kwanza walikuwa wako pamoja na mzuka huo kiurafiki wakidhani alikuwa binaadamu mwenzao. Na wote waliuawa katika mazingira ya kimapenzi.
 
Sasa kama mzuka huo wa Ummy umeanza kuniambia kuwa umenipenda, ndio unataka kunitia kamba ili uniue kirahisi.
 
Lakini wakati nawaza hivyo suala la mali za babu lilikuwa likitikisa kichwa changu. Kwanini mzuka huo aliniambia unazijua siri za mali ya babu yangu?.
 
Ilikuwa ni muhimu nikutane naye lakini niliogopa. Huenda hapo tutakapokutana ndio nikauawa hapo hapo.
 
Nikajiuliza niende nikaripoti polisi ili Ummy akamatwe na kuhojiwa? Au, niliendelea kujiuliza, niende kwa mganga ili anieleze ukweli kuhusu kiumbe huyu na nia yake kwangu?
 
Wazo la kwenda polisi sikuafikiana nalo. Nilijiambia polisi hawashughulikii masuala ya mizuka. Ningeweza kudai kuwa huyu msichana anadaiwa kuwa alikufa miaka mitano iliyopita lakini ninamuona na ananipigia simu kutaka nikutane naye.
 
Madai hayo yanaweza kuwavutia polisi wamuandalie mtego  na kumkamata. Lakini nikajiuliza kama Ummy ni mzuka kweli, anaweza kukamatika au ninajidanganya?
 
Wazo zuri, niliendelea kujiambia, ni la kwenda kwa  mganga.  Mganga anaweza  kunitegulia kitendawili hiki.
 
Baadaya kuwaza hivyo nikaamua niende kwa mganga mmoja wakati ule alikuwa akikaa Chanika. Alikuwa mzigua wa Handeni. Alikuwa akifahamiana  na babu na kuna siku niliwahi kwenda kwake nikiwa na babu.  Babu yangu licha ya utajiri aliokuwa  nae alikuwa mshirikina sana.
 
Siku ambayo nilikwenda naye kwa mganga huyo alikwenda kumroga mfanyabiashara mwenzake ambaye naye alikuwa na vituo vya mafuta. Walikuwa wakishindana kibiashara na babu akaamua kuingiza na uchawi.
 
Siku hiyo nakumbuka, mganga alizika mbuzi watatu wakiwa hai kwenye kaburi la mwanamke aliyekufa zamani. Juu ya kaburi pakamwagwa mchanga wa alama za viatu za mfanyabiashara aliyekuwa akishindana na babu yangu.
 
Babu alikuwa ametuma watu kuzitafuta alama za viatu  za mfanyabiashara huyo kwa dau la  shilingi milioni tatu kwa mtu atakayefanikisha kuzipata. Watu hao wakawa wanamuandama mfanyabiashara huyo usiku na mchana mpaka wakafanikiwa kupata alama zake.
 
Alama hizo walizipata aliposhuka kwenye gari na kukanyaga mchanga kabla ya kwenda kulikagua eneo ambalo alitaka kulinunua pale Ubungo.
 
Baada ya mchanga huo kumwagwa juu ya kaburi hilo palikutwa kibao kilichokuwa na jina lake. Baada ya siku saba mfanyabiashara huyo aliaga dunia baada ya gari lake kugongwa na lori la mafuta! Babu akafurahi.
 
Mganga huyo alikuwa mzigua aliyetoka Handeni. Wenyeji wa Chanika walimpa jina la “mashine ya kuua”
 
Tangu kipindi hicho miaka mingi ilikuwa imepita na sikuwahi kwenda kwake tena kwa vile sikuwa na tabia za kwenda kwa waganga wa kienyeji. Hiyo tabia alikuwa nayo  babu yangu.
 
Nikaona niende nikamueleze matatizo yangu nikiamiini kuwa anaweza kunipatia ufumbuzi.
 
Nikaenda  kwa gari langu
  
Nilipofika niliikuta ile nyumba yake ambayo wakati ule ilikuwa ikiendelea kujengwa, ilikuwa imeshakamilika. Lakini nilikuta msururu wa watu.
 
Ikabidi  na mimi nipange msitari. Hadi nafanikiwa kuingia katika chumba chake cha uganga ilikuwa karibu saa kumi na moja jioni. Nilikuwa na matumaini madogo sana kama angelishughulikia suala langu kwa vile  muda ulikuwa umekwenda sana.
 
Mganga mwenyewe alikuwa amenisahau, nikamkumbusha. Mara moja akamkumbuka babu yangu lakini mimi hakunikumbuka.
 
“Wewe ni mjukuu wa yule mzee?” akaniuliza.
 
“Ni mimi lakini babu mwenyewe alishakufa”
 
Mganga akashituka.
 
“Kumbe mzee Limbunga alikufa?”
 
“Alikufa”
 
“Alikufa mwaka gani?”
 
“Alikufa mwaka huu”
 
“Kwa hiyo wewe ndiye umesimamia shughuli zake?”
 
“Ni mimi lakini kuna matatizo yamejitokeza”
 
“Matatizo gani?”
 
“Wewe unajua kuwa mzee Limbunga alikuwa tajiri lakini alipokufa mali zake hazikuonekana”
 
“Kwanini?”
 
“Sijui”
 
ITAENDELEA kesho usikose uhundo huu

SOKONI DEEP SEA TANGA



 Mchuuzi wa samaki soko la Deep Sea Tanga, Hassan Shamba akipanga mafungu samaki wake kusubiri wateja, fungu moja na samaki aina ya change alikuwa akiuza 10,000 hadi 15,000 na samaki aina a kolekole lilikuwa likiuzwa 20,000.
Wachuuzi wengi Tanga wamedai kuksoa soko la uhakika la kuuzia samaki kama ilivyo Dar es Salaam badala huuza kwa wateja mmoja mmoja jambo ambalo wamedai kuwa uchuuzi wao hauna tija bali ni kujikimu na maisha ya kutwa.






MAREKANI YADONDOSHA MABOMU KOREA KASKAZINI

Ndege za kuangusha mabomu aina ya B-1B Lancer zikipaa juu ya Korea Kusini awaliMeli kubwa ya kubeba ndege ya Marekani ya Carl Vinson ikiwa kusini mwa Japan JumamosiMaafisa wa Korea Kusini wamesema ndege mbili za Marekani zimeangusha mabomu zimepaa juu ya anga la rasi ya Korea.
Ndege hizo za kivita zilipaa angani kama sehemu ya juhudi za kuzuia vitisho na uchokozi kutoka kwa Korea Kaskazini.
Ndege hizo aina ya B1-B zilishiriki operesheni ya pamoja na ndege za kivita za Korea Kusini.
Kupaa kwa ndege hizo kumetokea wakati ambapo Rais Trump ametoa taarifa za kukanganya kuhusu msimamo na sera ya Marekani dhidi ya Pyongyang.
Bw Trump aliambia Fox News kwamba msimamo wa Korea Kaskazini kuhusu mpango waker wa kufanyia majaribio makombora ya nyuklia ni wa kukera.
Alikuwa awali amesema kwamba yuko tayari kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un, iwapo kutakuwepo na mazingira mahsusi.

Monday, May 1, 2017

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI, NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 17

ZULIA LA FAKI 0655 340572
 
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 19
 
ILIPOISHIA
 
“Hakunidanganya. Baba yako alinionesha picha  yake, ndiye yeye  niliyemuona na hata namba ya simu anayotumia ulisema ni yake”
 
“Namba ya simu ni yake kweli, niliikariri  kichwani mwangu”
 
“Basi ndiyo ujue niliyemuona alikuwa ni Ummy kweli”
 
“Sasa mbona hapokei simu?”
 
“Tena mwanzo alikuwa akinipigia yeye, ndiyo nikaipata hii  namba yake”
 
“Basi atakapokupigia tena utakuja kutuambia”
 
Nikaagana na yule msichana. Sikwenda kwao tena. Nikaenda kupanda daladala na kurudi nyumbani.
 
Vile nafika nyumbani tu, simu yangu ikapigwa. Nilipoangalia namba inayonipigia, nikaona  namba  ya Ummy.
 
Nilishituka halafu mwili ulinisisimka.
 
SASA ENDELEA
 
Nikajiuliza niipokee au nisiipokee? Kama nitaipokea msichana huyo atanieleza nini? Nikajiambia chochote ambacho ataniambia kitazidi kuniweka njia panda kwa vile nimeshathibitisha kuwa msichana huyo alikuwa ameshakufa.
 
Vile vile tayari nilikuwa na hofu ya kuzungumza na mtu ambaye kuna ushahidi kuwa alikuwa amekufa.
 
Lakini kwa upande mwingine nilikuwa na shauku ya kumsikia yeye mwenyewe atakachojibu kuhusu madai kuwa alikuwa ameshakufa miaka  mitano iliyopita.
 
Nikajiambia nisipopokea simu yake, bado nitabaki kuwa njia panda kwani sitapata mtu mwingine wa kunipa ufafanuzi kuhusu madai ya kufa kwake.
 
Mbali na hayo, bado nilitaka kujua ni siri gani ambayo alitaka  kunieleza kuhusu mali za babu yangu. Nikaamua kupokea ile simu.
 
“Hello!” Nikasema kwa sauti ya kujikaza ili nisioneshe hofu niliyokuwa nayo.
 
“Hello! Kassim unajua nimekupenda sana, ninataka uwe mume wangu!”
 
Maneno hayo yalinishitua. Niwe mume wa mtu aliyekwisha kufa!
 
“Natumaini kuwa naongea na Ummy?” nikamuuliza.
 
“Mimi ni Ummy Nasri”
 
“Uliniambia nifike nyumbani  kwenu Mwananyamala, nimefika jana na leo lakini sikukuona”
 
“Ulimkuta nani?”
 
“Nilimkuta baba yako mzee Nasri”
 
“Vizuri sana. Alikuambia nini?”
 
“Aliniambia maneno ya kunishitusha sana”
 
“Kama yapi”
 
“Aliniambia kwamba mwanawe anayeitwa Ummy alikwishakufa miaka mitano iliyopita”
 
“Na mimi ni nani?”
 
“Umeniambia kuwa wewe ni Ummy Nasri”
 
“Na uliyembiwa amekufa ni nani?”
 
“Ni Ummy Nasri”
 
“Sasa una shaka gani?”
 
“Kwanza nataka unieleze ni kwanini nimeambiwa kuwa umekufa?”
 
“Kuna umuhimu wa mimi na wewe kukutana”
 
“Kwanza nataka ujibu, kwanini nimeambiwa kuwa umekufa?”
 
“Ndiyo maana nikakwambia kuna umhimu tukutane ili tuzugumzie hilo pamoja na kukueleza kuhusu mali za babu yako”
 
Nikanyamaza kwa sekunde kadhaa nikifukiria la kumjibu.
 
“Lakini ni kweli kuwa ulikufa?” nikamuuliza baada ya kimya kifupi.
 
“Ni kweli?”
 
“Sasa wewe ni nani?”
 
“Ni Ummy”
 
“Umekubali kuwa ulishakufa, sasa mbona uko hai?”
 
“Mimi ni kivuli cha Ummy”
 
“Sijakuelewa. Kivuli maana yake nini?”
 
“Maana yake ni mzuka wa Ummy!”
 
Moyo wangu ulipiga kwa nguvu kisha ukaanza kunienda mbio. Nikahisi mkono ulioshika simu ulikuwa ukitetemeka.
 
“Kassim tutakapokutana kila kitu utakielewa vizuri”
 
“Unadhani nitakutanaje na mzuka?”
 
“Tutakutana tu  na tutazungumza, usijali”
 
“Mmmh…!”
 
Pakapita kimya kingine.
 
“Niambie nikiuone wapi na muda gani?” Sauti ya Ummy ikautanzua ukimya uliokuwepo.
 
“Acha nifikirie kwanza”
 
“Ufikirie nini Kassim?”
 
“Umenitisha. Umeniambia kwamba wewe ni mzuka”
 
“Sasa unataka ufikirie nini?”
 
Sikujibu.
 
“Kassim!” Sauti ya Ummy ikaita kwenye simu.
 
Sikujibu. Nilibaki nimeduwaa kama gogo.
 
“Nitakupa muda wa kufikiria lakini usizidi saa arobaini na nane”
 
“Sawa” nikamuitikia.
 
Ummy akakata simu.
 
Yale maneno ya kwanza ya Ummy kuwa ananipenda na anataka niwe mume wake, yalipita katika akili yangu.
 
Nikajiambia hata wale watu aliowaua kule Buswana. Zimbabwe , Afrika Kusini na hapa Dar, inaelekea walianzana kwenye mapenzi,
 
Kitendo cha kuniambia anataka niwe mume wake si tu kimebadili mada yake ya kwanza ya kutaka tukutane ili anieleze ziliko mali za babu yangu bali pia nilifikiri kwamba ilikuwa ni hatua  ya kutaka kuniua.
 
 
ITAENDELEA kesho hapa hapa usikose ni kitaendelea wa Kassim akiwa katika mtihani mzito wa kusuka au kunyoa