HADITHI
UNA SIKU CHACHE ZA KUISHI 44
ILIPOISHIA
Zainush alikuwa akitabasamu.
“Usimpe kero mama” Omar
akamwambia Zainush.
“Namkera kwa ajili yako.
Hutaki kunisikiliza mimi. Unamsikiliza mchumba wako aliyeko Ujerumani” Zainush
akamwambia.
“Umar una mchumba Ujerumani?”
Sauti ya Ummi Mariam ikasikika kutoka upande wa pili wa pazia.
“Nilikuwa naye lakini
nimeamua kuachana naye”
“Afadhali uachane naye.
Zainush atakusumbua na anaweza kumdhuru”
“Sitamuoa tena. Kwanza baba
yake ndiye huyo rais wetu anayetaka kuniua”
“Mwache kabisa. Wewe kuwa na
Zainush. Utakubali kumuoa Zainush?”
Omar hakujibu.
“Jibu sasa. Utakubali
kunioa?” Zainush akamuuliza.
SASA ENDELEA
“Nitakubali” Omar akajibu.
“Mwache aseme kwa hiyari
yake, usimlazimishe” Ummi Mariam akasema.
“Amesema amekubali”
“Eti Omar unakubali kwa
hiyari yako?”
“Nimekubali” Omar akasema.
“Sawa. Sasa mtapanga wenyewe
siku ya kuoana”
“Kwani ni lazima tuoane huku
huku?” Omar akauliza.
“Ni hiyari yenu. Mtakavyoamua
wenyewe”
“Basi tutapanga na Zainush”
“Sawa”
“Lakini unavyoona, ninaweza
kuja kuwa rais?”
“Utakuwa lakini kwa sharti
moja”
“Sharti gani?”
“Sharti
hilo ni kwamba wakati wote ukuwa kwenye harakati zako uwe sambamba na Zainush”
Ummi Mariam alimwambia Omar.
“Nakubaliana
na hilo” Omar alimwambia huku akimkubalia kwa kichwa.
“Zainush
ni mjanja na anaweza kujigeuza sura za watu mbalimbali. Naamini kwamba
atakusaidia sana”
“Mara
nyingi anapenda kujigeuza kama mimi na kwa kweli amenisaidia sana”
“Na
ataendelea kukusaidia. Yeye anapenda sana uwe rais na yeye awe mke wako”
“Ameshaniambia
hivyo”
“Halafu
waangalie sana watu walio karibu yako. Baadhi yao ni watu waliopachikwa
kukuhujumu wewe na kuhujumu chama chako”
“Mimi
sitaweza kuwajua wote lakini nikiwa na Zainush nitaweza kuwajua”
“Usimtegemee
Zainush kwa kila kitu. Zainush ni kiumbe kama wewe. Kuna mambo mengine uwe
makini nayo wewe mwenyewe. Umenielewa?”
“Nimekuelewa.
Umesema sawa”
“Vile
vile mtegemee Mungu”
“Ni
kweli”
Pakapita
kimya cha sekunde kadhaa kabla ya sauti ya Ummy Mariam kusikika tena.
“Sasa
utarudi lini nyumbani kwako?”
Omar
akamtazama Zainush.
“Eti
Zainush utanirudisha lini?”
“Tutakwenda
kupanga sasa hivi, inawezekana ikawa kesho au keshokutwa” Zainush akasema.
“Kwanini
unamchelewesha?” Ummi Mariam akamuuliza.
“Ni
kwa sababu ya usalama wake. Omar bado anatafutwa”
“Sawa
lakini usimuweke sana huku, ukiona hali imekuwa shwari mrudishe haraka”
“Sawa
maa”
“Umar
urudi salama kwenu” Ummy Mariam alimuaga.
“Asante
mama na wewe ukae salama”
“Mimi
naitwa Ummy Mariam, mama yake Zainush”
“Nimefurahi
kukufahamu”
“Na
mimi pia nimefurahi kukufahamu. Ishaallah tutaonana tena”
“Panapo
majaliwa”
“Haya
Zainush, nendeni. Usiku mwingi, mwenzako anataka kulala” Ummy Mariam alimwambia
Zainush.
“Mama
naye! Kwani amekwambia ana usingizi?”
“Kwani
mpaka aniambie, yeye ni binaadamu usiku analala, si jini kama wewe”
“Omar
nyanyuka twende zetu” Zainush akamwambia Omar.
Omar
akanyanyuka.
Wakatoka.
Wakati wanarudi Zainush akamwambia Omar.
“Vipi
unajisikia njaa?’
“Hapana,
sihitaji kula saa hizi”
“Au
unataka ugali uliouzoea kwenu?”
“Hapana,
lile bokoboko nililokula bado nalisikia tumboni”
“Sasa
unaonaje tukatembee kidogo?”
“Tukatembee
usiku huu?’
“Huku
kwetu harakati zinaendelea usiku na mchana”
“Tutakwenda
kutembea wapi?”
“Twende
gulioni. Nataka nikanunue asali”
“Ni
mbali sana”
“Si
mbali sana”
“Twende”
Wakaenda.
Kwa vile walikuwa wakitembea huku wakizungumza walikwenda mwendo mrefu bila
Omar kujua. Omar aliona barabara za ujinini. Walipishana na punda waliobebeshwa
mizigo. Zainush alimwambia Omar punda hao walikuwa wakitoka kwenye gulio.
Pia
walipishana na watu mbalimbali weusi na weupe waliokuwa wamevaa mashuka kama
waarabu na wengine wako na madevu hadi chini.
Kitu
ambacho kilimshangaza Omar ni kuwa kila waliyepishana naye alikuwa na ndevu
ndefu zilizokaribia kufika chini.
Zainusha
alimtambulisha Omar kuwa hao walikuwa majini wakiwa kwenye harakati zao. Lakini
majini hao hawakuwa wakizungumza. Kila mmoja alikuwa akiendelea na hamsini zake
kimya kimya.
Hatimaye
walifika hapo kwenye gulio. Ulikuwa uwanja ulioonekana kama jangwa. Kulikuwa na
mkusanyiko mkubwa wa majini uliokuwa umeshamiri kelele.
Majini
walikuwa wakinadi bidhaa zao na wengine wakiuza na kununua. Palikuwa na mitindo
tofauti ya biashara, kuanzia ule wa kuuza kwa mnada, kuuza kwa kupatana bei na
kuuza kwa kubadilishana vitu, toa mali upewe mali.
Zainush
alimwambia Omar pesa zilizokuwa zinatumika ni za falme za kiarabu, pesa
ya India, Ujerumani na China.
“Kwanini
zinatumika pesa hizo tu?” Omar akamuuliza.
“Kwa
sababu majini hupenda kutembelea katika nchi hizo kununua vitu”
“Una
maana bidhaa na vitu ninavyoviona hapa vimetoka katika nchi ulizotaja?”
“Baadhi
yake si vyote, vingine vimetoka hapa hapa”
Kulikuwa
na vyombo vya kaure na vilivyofinyangwa kwa udongo kama vile sahani, mabakuli,
vyungu na mitungi.
Pia
kulikuwa na ngozi za wanyama zilizokaushwa, mabusati, miswala, mazulia na vitu
vingine ambavyo Omar hakufahamu matumizi yake.
Baada
ya kuzunguka pande zote wakiwa wamefuatana pamoja, walitokea kwenye mnada wa
asali na uyoga. Zainush akanunua kibuyu cha asali kwa real ya Oman yenye
thamani ya shilingi elfu moja.
Wakati
wanaondoka Omar alimuona mnunuzi akinunua ndama wa mbuzi kwa kutoa kuku wanne.
Kitu
ambacho kilimchusha Omar ni harufu za majini hao ambazo Omar hakuwa amezizoea.
Kama vile Zainush aliyaelewa mawazo ya Omar akamuuliza.
“Unasikia
harufu tofauti?”
Omar
akacheka kidogo.
“Kwanini
umeniuliza hivyo?”
“Nimejua
kuwa ni lazima utakuwa unasikia harufu ambayo hukuizoea”
“Ni
kweli”
“Na
wenzako pia wanakusikia wewe una harufu tofauti na wao. Wanakugundua wewe ni
binaadamu kwa harufu yako ingawa wewe mwenyewe hujisikii”
“Una
maana wameshanigundua kuwa si mwenzao?”
“Wameshakugundua
lakini wanakuona uko na mwenyeji wako”
“Unilinde
wasije wakanidhuru”
“Hakuna
kitu kama hicho”
“Naona
umetoa real, umeipata wapi?” Omar akayabadili yale mazungumzo.
“Umeishangaa
ile? Mbona nina pesa nyingi za nchi za kiarabu”
“Unazipata
wapi?”
“Kote
huko ninafika. Wakati mwingine nikiishiwa ninaiba”
“Unaiba?
Unaibaje?”
“Ninaiba
benki usiku. Ninaingia bila kuonekana na kutoka na pesa”
“Kumbe
unafanya hivyo?”
“Lakini
mama yangu hajui na sipendi ajue. Unataka kuonja kidogo?”
Zainush
alikuwa akiramba ile asali.
“Hebu
nipe”
Zainush
akampa Omar kile kibuyu cha asali. Omar naye akaionja.
“Tamu
kweli”
Hapo
hapo kibuyu kikaporwa juu kwa juu. Aliyekipora alikimbia nacho.
Je ni
nani aliyekipora kibuyu hicho na nini kitatokea? Usikose toleo lijalo