Tangakumekuchablog
Mlalo, MBUNGE
wa jimbo la Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, amewataka wakulima wa matunda na
mbogamboga jimboni humo kuongeza nguvu ya kilimo kwa madai kuwa pembejeo za kilimo
na masoko ya uhakika yanapatikana.
Akizungumza katika hafla fupi ya
kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua kuwa Mbunge wao jana na
kuwashirikisha Madiwani, Wenyeviti wa vijijini na wa Chama pamoja na maofisa
kilimo na biashara, Shangazi alisema anataka kulirejesha jimbo hilo katika
hadhi yake ya kuzalisha matunda na mbogamboga.
Alisema wakulima wengi wa matunda na
mbogamboga wamepunguza kasi ya kulima kutokana na kukata tamaa ya upatikanaji
wa soko la uhakika na pembejeo za kilimo
hivyo kulima kilimo cha mazoea.
“Kwa heshima na taadhima ndugu zangu
wazee wangu mashangazi na wajomba nawashukuru kwa kuniunga mkono kwenu na leo
hii kusimama hapa kama mbunge---nawaahidi sitakuwa mbunge wa kutafutwa kwa
tochi” alisema Shangazi na kuongeza
“Mimi ni mbunge wenu na niko tayari
kushirikiana na kila mmoja ili kulienua jimbo letu kiuchumi hasa kukiendeleza
kilimo chetu cha mbogamboga na matunda na masoko niwambie kuwa yapo” alisema
Akizungumzia fursa za mikopo kwa
vijana na vikundi vya ushirika, Shangazi alisema pesa hizo zipo ila hitolewa
kwa utaratibu na hivyo kuwataka wananchi kuchangamkia ili kujikomboa na
umasikini.
Aliwataka wananchi wanawake na
wanaume na vijana kuunda vikundi vya ujasiriamali ili kuweza kupata vursa za
mikopo katika taasisi za fedha pamoja na asilimia kumi na asilimia 5 za
halmashauri zilizotengwa kwa wanawake na vijana.
“Ndugu zangu ziko njia nyingi za
kupata pesa na kujikwamua na umasikini----undeni vikundi vitakavyotuwezesha kupata mikopo
katika taasisi za fedha na ziko tuchangamke” alisema Mbunge huyo
Alisema ili kulifanikisha hilo
amedai kuleta wataalamu ambao watatoa elimu kwa vikundi vya ujasiriamali ikiwa
lengo ni kuhakikisha maisha ya watu yanabadilika na kufanya kazi kwa
ustadi na yenye tija.
Mwisho
Mbunge wa jimbo la Mlalo, Rashid Shangazi akiwaonyesha Cheti cha pongezi kilichotolewa na Umoja wa Watu wa Mlalo wanaoishi Dar es Salaam umati wa watu waliofurika kumsikiliza ikiwa ni kikao chake cha kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo.
Mbunmge wa jimbo la Mlalo , Rashid Shangazi akizungumza wakati wa kikao cha shukrani kwa wananchi wake baada ya kumchagua kuwa Mbunge wao, watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza
No comments:
Post a Comment