MTANZANIA
UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamemuonya Rais Jakaya Kikwete, wakisema ndiye mwenye dhamana ya kulinda usalama wa wananchi na akiendelea kutumia vibaya vyombo vya dola, Novemba mwaka huu watamburuza Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Zanzibar na viongozi wa Ukawa, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Kibanda Maiti wenye lengo la kutafuta wadhamini kwa mgombea urais wa umoja huo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa.
Akizungumza katika mkutano huo jana mjini hapa Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalimu Seif Sharif Hamad, alisema CCM wanahubiri amani wakiwa majukwaani lakini wakishuka wao ndio wa kwanza kuivunja.
“Kama kuna watu wana nidhamu ni watu wa Ukawa, Mbeya, Arusha, watu wawalikuwa wanasubiri kwa amani, polisi wanapiga mabomu, wao ndiyo wanaleta tensheni katika nchi, siyo wafuasi wa Ukawa.
“Namwambia Kikwete (Rais), atimize wajibu wake, akifanya vinginevyo watakwenda ICC, Kikwete ondoka kwenye nchi ikiwa salama kama ulivyokabidhiwa ikiwa salama, wananchi wakukumbuke kuwa umeiacha salama,” alisema Maalim Seif ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar kupitia umoja huo.
Mbatia
Akihutubia katika mkutano huo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amewataka wanasheria wa Ukawa, kuanza kuandika matukio yote yanayotokea nchini kwa sasa ili wayawasilishe katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu (ICC).
“Tumeshawaagiza mawakili wetu waandike matendo yote maovu yanayofanywa, waandikie ICC, wapeleke nakala kwa mabalozi wote ili Fatou Bensouda (Mwendesha mashitaka Mkuu wa ICC) aje aanze kuangalia yanayofanyika hapa.
“Tumechoka kudanganywa, tumechoka kuibiwa ushindi wetu, mwaka huu tunasema, hapana, hapana. Walikuja kuandikisha watu wao hapa na baada ya Ukawa kutangaza mgombea watu wao wote sasa wamehamia Ukawa,” alisema Mbatia.
Alisema Watanzania kwa sasa wanataka mabadiliko kwa asilimia 99, na jeshi la polisi likiendelea kuvunja amani, Novemba mwaka huu watakwenda ICC.
Juma Duni
Naye Mgombea Mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji, alisema ni bahati mbaya sana watawala wanadhani kutumia mabavu kutawasaidia kubaki madarakani jambo ambalo kwa sasa haliwezi kutokea.
Lowassa na Kingunge
Kwa upande wake Lowassa alisema kitendo cha CCM kumvua wadhifa wake Kamanda wa UVCCM, Kingunge Ngombale Mwiru kwa sababu tu mwanasiasa huyo mkongwe alitumia demokrasia kueleza hisia zake ni kuchuma laana.
Alisema Kingunge ambaye ni mmoja wa waasisi wa TANU na CCM, alikuwa amebaki kama mfano ndani ya chama hicho kutokana na historia yake.
“Nianze kwa kueleza masikitiko yangu kwa hatua aliyochukuliwa mzee Kingune jana (juzi), mzee huyu alibaki kama kielelezo cha TANU, yote yaliyomfika ni kutokana na kutoa maoni yake, hatua waliyochukua ni laana… laana ya Kingunge itawapata,” alisema Lowassa.
Lowassa alisema amefika Zanzibar kuomba wadhamini kwa sababu anataka kupambana na umaskini na anauchukia.
“Nilivyoona sipewi nafasi ya kupambana nao huko CCM nikaondoka, niliondoka kwa maneno ya Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa) kwamba Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyatapa ndani ya CCM watayapata nje ya CCM, naifahamu Tanzania,” alisema Lowassa.
Akizungumzia kuhusu Katiba mpya, alisema tangu wakati wa G55 alikuwa ni muumini wa Serikali tatu na kwamba hata kwenye Tume ya Jaji Wairioba alisema hilo.
“Nilisema nataka Serikali tatu lakini Muungano ubaki, muungano huu siyo wa uongozi ni wa watu. Nataka Muungano imara ndani ya watu imara, Serikali tatu inayozingatia mahitaji ya watu sawa ya watu wa Zanzibar na wale wa Bara,” alisema.
MTANZANIA
WANANCHI na wagombea udiwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Kata nane za Manispaa ya Morogoro wamevamia ofisi za chama hicho wakitaka ufafanuzi wa majina ya wagombea wa udiwani waliokatwa wakiwa wameshinda katika kura za maoni.
Ghasia hizo zilizuka saa 9.00 mchana baada ya makundi ya wagombea kutoka katika Kata za Kionda, Kichangani, Kilakala, Lukobe, Mlimani, Boma, Mjimpya na Kiwanja cha Ndege kuvamia ofisi hiyo kupata ufafanuzi wa sababu za majina yao kukatwa wakati wakiwa wameshinda katika kura za maoni.
Wanachama walivamia gari la mwenyekiti wa Chadema wa wilaya na kumzuia asiondoke hadi atakapotoa ufafanuzi wa madai hayo.
Mmoja wa wagombea aliyekatwa jina lake huku akiwa ameongoza katika mchakato wa kura za maoni, Mwanahenzi Shaha alisema ameshangazwa na hatua hiyo.
“Mimi katika Kata ya Mlimani nimeshinda kura za maoni lakini nashangaa leo naambiwa jina langu hakuna na tayari ameteuliwa mtu mwingine hii ni rushwa,” alisema huyo kwa hasira.
Mmmoja wa wanachama aliyekuwapo katika msafara huo aliyejitambulisha kwa jina la Fiderik Boniface, alidai kitendo cha viongozi wa wilaya na mkoa kukata baadhi ya wagombea kitaleta madhara makubwa katika chama.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Chadema ngazi ya wilaya na mkoa hazikuzaa matunda baada ya simu zao kutokuwa hewani jana.
MTANZANIA
LICHA ya Chama Cha Mpinduzi (CCM) kuamuru kurudiwa uchaguzi katika baadhi ya majimbo yakiwamo yaliyokuwa yanaongozwa na mawaziri wa Rais Jakaya Kikwete, hatimaye chama hicho kimewatosa rasmi.
Kutoswa kwa mawaziri hao kunatokana na kushindwa kwao kwenye kura za maoni za marudio ambako pia wana CCM wamebwaga katika mchakato huo na kusubiri hatima ya Kamati Kuu ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema baada ya kurudiwa uchaguzi katika majimbo kadhaa hatimaye Kamati Kuu imefanya uteuzi wa mwisho huku ikiwaweka kando mawaziri hao.
Alisema kikao kilichofanyika jana chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kimefanya uteuzi huo kutokana na matokeo ya kura za maoni.
Katika matokeo hayo ya kura za maoni, mawaziri waliojikuta wakiangukia pua ni pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titus Kamani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge.
Nape alisema katika kikao hicho cha CC pamoja na mambo mengine, kilikuwa na ajenda ya kupitisha majina ya wagombea katika majimbo yaliyorudia uchaguzi pamoja na Uchaguzi Mkuu
“Tumepitisha majina ya wagombea katika majimbo tisa tuweze kusimamisha wagombea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu,” alisema Nape.
Aliwataja wagombea waliopitishwa katika majimbo hayo kuwa ni aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry (Ukonga), Edward Mwalongo (Njombe Kusini) na Venance Mwamoto (Kilolo).
Wengine ni Profesa Norman Sigala (Makete), Dk. Raphael Chegeni (Busega), Edwin Ngonyani (Namtumbo), Martin Msuha (Chilonwa), Joel Makanyanga (Mbinga Vijijini) na Mohamed Mchengerwa (Rufiji).
Akizungumzia wanachama wa chama hicho wanaoendelea kulalamikia matokeo ya kura za maoni, Nape alisema wagombea hao walipaswa kuandika barua ya malalamiko yao kwa kamati kuu iweze kupitiwa na kutolewa uamuzi.
“Hakuna malalamiko yaliyowasilishwa kwenye kamati hii ambayo hayajafanyiwa kazi jambo ambalo lilisaidia baadhi ya majimbo kurudiwa uchaguzi, hivyo basi wanachama wao wanapaswa kuacha malalamiko nje ya vikao.
“Kama wanaona chama hakijawatendea haki na kwamba CCM haiwezi kuwaletea maendeleo wanaweza kufanya uamuzi mgumu wa kujiunga na vyama vya upinzani ambako wanaamini wanaweza kutendewa haki.
“Ikiwa kuna mwanachama ambaye anaona haki anaweza kuipata akiwa upinzani na siyo CCM basi anaweza kwenda kutafuta hiyo haki, lakini kama CCM hatushughuliki na malalamiko ya nje bali tunashughulika na matatizo ya wananchi na malalamiko ya ndani ya vikao,” alisema.
NIPASHE
Aliyewahi Mbunge wa Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo (pichani), ambaye aligombea Jimbo la Mbinga Vijijini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kura za maoni, anadaiwa kudai arudishiwe vifa vyake alivyokipatia Chama kwa ajili ya kampeni.
Kayombo alikwenda ofisi za CCM wilayani humo Agosti 14 na kutaka arudishiwe vifaa vya matangazo, baada ya kushindwa kwenye kura za maoni Agosti Mosi 2, mwaka huu.
Mmoja wa makada alisema Kayombo alichukua hatua hiyo akisema viongozi wa Chama wilaya hawamtaki.
Katibu wa CCM wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wamesikitishwa na kitendo hicho.
“Tunajua kitendo cha kutunyang’anya vipaza sauti ni hasira baada ya kushindwa, kwenye uchaguzi wa kura za maoni,” alisema Chinowa.
Alipotafutwa Kayombo, alisema kuwa madai hayo siyo ya kweli na kueleza kuwa Chama kimekuwa kikiviazima vifaa vyake mara kwa mara kwa kuwa yeye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec).
“Siku za kwanza za kampeni hawakuvitumia vipaza sauti vyangu, walisema vimeharibika. Baadaye walinunua vipya na wakavipeleka majimbo ya Mbinga Mjini na Vijijini,” alisema Kayombo na kuongeza:
“Majuzi nilikwenda nikakuta havijatunzwa vizuri , nikawaambia wanirudishie vifaa vyangu.”
Kadhalika, Kayombo alisema hakushindwa kura za maoni kwa kuwa matokeo ya kata mbili hayajajumuishwa.
Katibu wa CCM wa mkoa wa Ruvuma, Vellena Shumbusho, alisema amelazimika Chinowa kumkabidhi haraka Kayombo vifaa vyake anavyodai.
Alisema Kayombo alikuwa amevinunua na kuvikabidhi kwenye Chama kwa ajili ya kusaidia matangazo wakati wa kampeni za kura za maoni Jimbo la Mbinga Vijijini lilikuwa na wagombea ubunge nane waliochuana katika kura za maoni.
Martin Msuha aliyeongoza kwa kura 13,354, Kayombo (12,068), Deodatus Ndunguru (7,060), Humprey Kisika (545) na Dk. Silverius Komba (3,941).
NIPASHE
Hali ya hewa ndani ya Chama cha ACT- Wazalendo ambacho kinaongozwa na Zitto Kabwe, imechafuka, baada ya Kamati Kuu kumpitisha na kumchukulia fomu ya urais, Prof. Kitila Mkumbo, huku mwenyewe akisita kulipokea jukumu hilo.
Kufuatia hatua hiyo, Prof. Kitila ameandika katika mtandao wa kijamii kuwa hajaandaliwa kisaikolojia kupeperusha bendera ya chama hicho katika nafasi ya urais na jukumu hilo wapewe viongozi wengine waandamizi.
Tofauti na ilivyozoeleka kwa wagombea kwenda na wafuasi wao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuchukua fomu za kugombea urais, kwa upande wa ACT – Wazalendo, Katibu Mkuu, Samson Mwigamba, jana alikwenda Nec kumchukulia fomu Prof. Kitila ambaye inadaiwa viongozi wakuu wa chama hicho wamekutana naye kwa mazungumzo ya kumshawishi akubali kupeperusha bendera ya chama hicho kuelekea Ikulu.
Mapema asubuhi jana Prof. Kitila alifika ofisi za chama hicho Kijitonyama na kuondoka na majira ya saa 5:00 asubuhi wafuasi zaidi ya 100 wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali walivamia ofisi hiyo na kumbana Mwigamba kuwaeleza kwanini chama hicho kinachelewa kuweka wazi mchakato wa mgombea wake wa urais.
Habari zinasema kuwa licha ya Prof. Kitila kutokuwapo kwenye kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichopitisha uamuzi wa kumtaka apeperushe bendera ya chama hicho katika nafasi ya urais, lakini ulipitishwa uamuzi wa kwamba abebe jukumu hilo zito.
Wakati Kamati Kuu kiamua hivyo, hadi jana alasiri hapakuwapo na makubaliano na Prof. Kitila, lakini viongozi wakuu wa chama walikuwa kwenye mazungumzo naye.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwigamba alisema alichukua fomu hiyo saa 4:00 asubuhi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Kamati Kuu iliyokutana Agosti 15, mwaka huu.
Alisema pamoja na azimio hilo, Kamati Kuu ilipitisha majina ya wagombea ubunge nchi nzima, wagombea udiwani na kupokea ripoti ya wataalamu washauri juu ya ushiriki katika harakati za uchaguzi wa rais.
“Baada ya kupokea taarifa na mapendekezo yao tukajiridhisha kwa mustakabali wa taifa, chama kinahitaji kusimamisha mgombea urais, ndipo nilipoagizwa kwenda kuchukua kwa sababu muda unaenda zianze kujazwa ili Ijumaa ambayo ndiyo siku ya mwisho zirudishwe,” alisema Mwigamba.
Alisema Kamati Kuu imeamua hivyo kwa kuwa Prof. Kitila ni mwadilifu, mzalendo wa kweli, anaweka mbele maslahi ya Taifa na kwamba ana sifa zote za kuliongoza taifa na mgombea mwenza atakuwa ni Mwandishi wa habari mkongwe, Hawra Shamte.
Hata hivyo, Hawra, alipoulizwa kuhusu maamuzi hayo ya Kamati Kuu, alisema hana taarifa zozote na kwamba hadi jana jioni hakuarifiwa chochote.
Alisema wakati mgombea huyo anakutana na viongozi wakuu wa chama hicho, fomu hiyo itaendelea kusambazwa mikoani ili kusaka wadhamini na kwamba walianza kufanya hivyo jana.
“Tofauti yetu na wengine hatutakuwa na ziara kwenye kusaka wadhamini, nimeenda na wanachama wengine watatu kuchukua fomu na sikuwa na msururu wa watu na hivyo hivyo kwenye kusaka wadhamini itakuwa kimya kimya,” alisema Mwigamba.
Alipoulizwa juu ya utayari wa Prof. Kitila kupeperusha bendera hiyo, alisema: “Hatuna wasiwasi, tunaamini atakubali uamuzi wa Kamati Kuu, anajua ni wajibu kubeba jukumu chama kinapomuhitaji.”
Aidha, Mwigamba alisema kama itashindikana kwa Prof. Kitila, ni lazima chama hicho kisimamishe mgombea mwingine katika nafasi hiyo.
KITILA: SINA MAANDALIZI
Katika kundi la mtandao wa kijamii la chama hicho la Whatsaap, lijulikanalo kama ACT Taasisi Imara, Prof. Kitila aliandika taarifa ya kuwashukuru wanachama na viongozi kwa imani yao kwake, lakini alisema hawezi kubeba jukumu hilo.
“Naomba niwashukuru nyote kwa imani kubwa mliyonayo juu yangu katika kukiwakilisha chama katika nafasi ya urais, naishukuru Kamati Kuu kwa imani yake kwangu hata kufikia hatua ya kupitisha azimio la kuniomba kugombea urais kwa chama chetu. Jana CC (Kamati Kuu) ilituma ujumbe maalum nyumbani kwangu kwa ajili ya kuzungumza na familia na jamaa zangu juu ya ombi hilo,” alisema katika andiko hilo na kuongeza:
“Nimekuwa nikitafakari tangu Alhamisi nilipoombwa rasmi kutafakari uwezekano wa mimi kugombea baada ya juhudi zetu za kutafuta mgombea kushindikana. Nimefanya mawasiliano mapana ndani ya familia, chama, chuoni ninapofanyia kazi, kanisani kwangu na kwa watu na taasisi mbalimbali ninazohusiana nazo.”
Alisema baada ya tafakari na mawasiliano mapana (consultations), ameona hana utayari na maandalizi ya maana ya kisaikolojia, kifamilia na kisiasa kumuwezesha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
“Najua nimewaangusha sana katika uamuzi wangu huu, lakini naamini kwamba mtaheshimu uamuzi wangu na kwamba hamtaacha kuthamini mchango wangu katika chama kwa sababu ya kukataa kugombea urais,” alisema na kuongeza:
“Nasikitika kwa tuhuma ambazo baadhi ya wanachama wetu wanarusha katika mitandao ya kijamii na sehemu nyingine. Nathamini na kuheshimu haki ya wanachama kuonyesha hasira kwa jambo wasilolipenda…nawasihi wanachama wajizuie kuzusha mambo yatakayochochea chuki ndani ya chama na kukatishana tamaa.”
Aidha, alishauri wanachama wengine waandamizi waombwe wachukue jukumu hilo na kuwataja kuwa ni Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo na Katibu Mkuu, Mwigamba na kwamba wakati hayo yakitafakariwa wasisahau malengo mapana ya chama waliyojiwekea katika uchaguzi huo.
Alisema mafanikio waliyofikia ni kuweka wagombea ubunge na udiwani kata na majimbo mengi nchini.
Mwigamba alipoulizwa juu ya taarifa hiyo, alijibu: “Sina simu ya whatsaap ila naenda kwenye kikao hadi leo (kesho) nitawapa taarifa.”
WAFUASI WAKUSANYIKA
Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo yalikuwa na ujumbe wa ‘wamenunuliwa’ na mgombea wa Chadema, Edward Lowassa ili wasisimamishe mgombea urais.
Wafuasi hao walikaa kwa saa nne nje ya ofisi hizo wakiimba nyimbo mbalimbali.
HABARILEO
MKAZI wa Chuo, tarafa ya Shimbi Kwandele wilayani Rombo, Kilimanjaro, Fidensia Salvatory (27) anashikiliwa na Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumuua kwa kumnywesha sumu mwanawe wa miezi sita kwa madai ya kukerwa na wakwe zake.
Mwanamke huyo anadaiwa kumnywesha sumu ya panya mwanawe huyo kama sehemu ya kupunguza hasira zake baada ya kukerwa na manyanyaso kutoka ukweni anakoishi na mumewe.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema tukio hilo limetokea Agosti 15 mwaka huu majira ya saa 8.30 mchana nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo.
Akielezea tukio hilo Kamanda Ngonyani alisema siku ya tukio baba mzazi wa mtoto huyo, Salvatory Baltazary alifika nyumbani kwake majira ya mchana na kukuta mwanawe akiwa amelala kitandani akiwa anatokwa na povu mdomoni na puani hali iliyoashiria kupata madhara.
Alisema baada ya kuona hali hiyo alitoa taarifa Polisi ambao walifika nyumbani hapo na kumpeleka mtoto hospitali huku wakiokota baadhi ya vitu vilivyokuwa vimehifadhi sumu hiyo.
Kamanda Ngonyani alisema askari hao walikuta pakiti iliyokuwa na unga unaodhaniwa sumu ya panya iliyotumika kumuua mtoto huyo.
Alisema Polisi ilimkamata mtuhumiwa na baada ya mahojiano alikiri kumpa sumu mtoto wake kwa madai ya kuchoshwa na manyanyaso kutoka kwa wakwe zake.
HABARILEO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa kitashinda Uchaguzi Mkuu mwaka huu kwa sababu kina mtandao mkubwa wa wanachama kuanzia ngazi ya chini na kwamba kufurika kwa wananchi katika mikutano ya Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa sio ushindi, kikisema kura ni mahesabu.
Aidha, kimesema kuwa mgombea huyo wa Chadema na umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa), amedanganywa na wapambe wake kuihama CCM na kumkejeli ikisema gari la wagonjwa linapaswa kuwekwa nyumbani kwake siku ya uchaguzi kwani CCM itapata ushindi wa uhakika asubuhi.
Akitoa taarifa kuhusu kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisisitiza kuwa ushindi wa chama hicho tawala na kikongwe hauna shaka kutokana na mtandao wake kuanzia ngazi ya chini.
Akijibu swali kuhusu kufurika kwa wananchi katika mikutano ya mgombea huyo wa Chadema, Nape alisema: “Kwa walioanza siasa jana ndio watashituka. Mwaka 2010 Slaa (Dk Willibrod) katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni Mbeya alipata watu wengi kuliko wale aliopata Edward. Lakini kura alizopata Mbeya utashangaa. “Kupata watu wengi mkutanoni hakutushangazi kwani kura ni mahesabu, hawa (Chadema na mgombea wao) wanatoka pointi moja kwenda nyingine. CCM ina mtandao, ukiondoka mjumbe wa nyumba kumi anapitia watu wake anasafisha nyayo zenu,” alisema kiongozi huyo.
Nape aliongeza kuwa wapinzani wote wametoka ndani ya CCM kuanzia kwa Augustino Mrema mwaka 1995 na hadi katika chaguzi nyingine zilizofuta na zote wapinzani walishindwa, na hata safari hii CCM itashinda.
Akimgeukia Lowassa, Nape alisema Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu kwa kashfa ya zabuni ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, amedanganywa na wapambe wake na kuondoka chama tawala, na kwamba licha ya kuhamia huko, CCM itamshinda asubuhi na kuwataka wanaotishia kukihama kufanya hivyo na si kuleta shinikizo.
“Katika mchakato wa uchaguzi si wote watakaoridhika na matokeo kwa sababu kuna wengi wanajiandaa kushinda na sio kushindwa, na matokeo yanapokuwa hivyo, wanakuwa hawaridhiki na hapo ndipo wanazungumzia kwenda upande wa pili, na hasa kwa shinikizo la wapambe.
“Hili limetokea kwa Edward, amekwenda upande wa pili, amedanganywa na watu, tutampiga. Ushindi wa CCM ni wa uhakika, sio wa matumaini. Matumaini yapo Angaza, CCM ni ya uhakika. Tutashinda asubuhi. Tumesema ni mpambano kati ya wagombea na makapi,” alisema Nape na kuongeza: “Zipo mechi ambazo unajua hii utashinda. Yanga na Lipuli ya Iringa unajua matokeo yake.
Tunataka mgombea mwenzetu apelekewe ambulance (gari la wagonjwa) nyumbani kwake, kwani ushindi kwetu ni uhakika.” Kuhusu wanaolalamika na kutishia kuhama, alisema malalamiko hayawezi kutolewa barabarani kwani chama hicho kina utaratibu wake na yale yote yaliyolalamikiwa yakiwamo ya udiwani, yamefanyiwa kazi. “Tulisema wakati ule wa mchakato wa kutafuta mgombea wa urais kuwa hatutafanya kazi kwa shinikizo.
Tunajua uimara wa chama chetu, kama kuna watu wanataka kwenda upande wa pili waende. Lakini CCM haiwezi kufanya kazi kwa vitisho na shinikizo. Tatizo ni kwamba kunatokea wagombea 12, halafu unasema lazima uwe wewe. Kuna watu (wanaotaka kuhama) wanafanya hivyo kwa shinikizo la viroba na hela,” alisema Nape.
HABARILEO
MUIMBAJI maarufu hapa nchini wa nyimbo za Injili, Rose Muhando anatafutwa na waandaaji wa tamasha la Injili wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa madai ya kutoonekana kutumbuiza kama jinsi walivyokubaliana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Zephania Simoni ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Uratibu alisema wameingia hasara ya Sh milioni 4.3 kutokana na tamasha hilo kuvurugika baada ya kutapeliwa na Muhando.
Alifafanua kuwa tayari walikuwa wameishamkabidhi kiasi cha Sh 1,700,000 muimbaji huyo na ameshindwa kufika na hivyo kuonesha wazi kuwa amewatapeli.
Alisema wameamua kuripoti tukio hilo kituo cha Polisi cha wilayani humo na kupewa RB namba ORK/RB 395/2015 kwa Rose na kuanza kumsaka popote alipo ili kukabiliana na kesi hiyo wilayani Simanjiro.
Wameshangazwa kwa mtumishi huyo wa Mungu kujiingiza katika masuala ya kutapeli na ndio maana wameamua kuchukua hatua za kisheria.
Awali, alisema siku ya tamasha wakati wakiwa wanamsubiri siku moja kabla ya tamasha alisema yupo njiani anakuja majira ya mchana mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Lucas alitupigia simu na kutuambia Rose hatakuja yupo kwa mgombea Urais anasaini mikataba ya kumnusuru katika kusaidia kampeni, “ alisema Simon.
Akafafanua kuwa baada ya kupata taarifa hiyo na kuingia shaka walianza kumtafuta Muhando bila mafanikio kupitia simu yake ya kiganjani siku nzima hadi anatoa taarifa hii hawajawahi kuwasiliana naye.
Akionesha vielelezo vya makubaliano na jinsi fedha zilivyotumwa kwa Rose, inaonesha kwa nyakati tofauti kuanzia Aprili 4 amekuwa akitumiwa fedha hizo kwa ajili ya tamasha na hatimaye mkataba aliosaini Rose Muhando Julai 7 mkoani Dodoma kuthibitisha kuchukua Sh milioni 1.5 kwa ajili ya tamasha hilo na baadaye kutumiwa Sh 200, 000 kwa ajili ya kwenda Simanjiro.
Hata hivyo, Muhando alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi ili kuthibitisha madai hayo simu yake iliita na wakati mwingine ilikuwa ‘busy’ na baadaye kwa mara ya nne ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mdogo wake, lakini hakutaka kujitambulisha na alipoulizwa juu ya madai haya alisema Rose ni dada yake hivyo akija atamwambia apige simu.
“Rose ni dada yangu na haya madai ndio tunayasikia na siwezi kuzungumzia suala hili kwa sasa kwani mimi ni mdogo wake, lakini nimesikia ila akija ntamwambia akupigie kisha akakata simu lakini sauti ilisikika kama ya Rose mwenyewe”.
Hivi karibuni mwanamuziki huyo alikuwa akidaiwa Sh 6,000,000 na alilipiwa na promota mashuhuri wa nyimbo za Injili Alex Msama ambaye mara nyingi wamekuwa wakifanyakazi pamoja.
MAJIRA
UGONJWA wa kipindupindu umeripotiwa katika Jiji la Dar es Salaam na watu wawili wamethibitika kufa. Wengine zaidi ya 30 wamelazwa katika hospitali za Mwananyamala na Sinza zilizopo Manispaa ya Kinondoni.
Kutokana na tishio la ugonjwa huo, shughuli za kampeni za kisiasa za uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu wa Rais, wabunge na madiwani, zilizo kuwa zianze mwishoni mwa wiki hii, zimesogezwa mbele. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alithibitisha hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya ugonjwa huo kupitia Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC 1).
Alisema watu hao wawili waliofariki, mmoja ni mwanamume na mwingine ni mwanamke na wanatoka Manispaa ya Kinondoni. Mkuu huyo wa Mkoa alisema ugonjwa huo umethibitika baada ya vipimo vya maabara vya watu hao, kuthibitisha.
“Watu wawili akiwemo mwanamume na mwanamke wamefariki dunia baada ya vipimo vya maabara kuthibitisha ugonjwa huo. Hata hivyo, hakuna taarifa zozote za ugonjwa huo katika manispaa za Temeke na Ilala,” alisema Sadiki.
Alisema endapo hali hiyo itaendelea kuwa mbaya, itabidi mamlaka za Dar es Salaam kusogeza mbele kampeni za kisiasa, zinazotarajiwa kuanza mwisho mwa wiki hii ili kuepusha mikusanyiko ya watu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty, alisema wagonjwa wengine 30 wapo chini ya uangalizi maalumu katika hospitali za Mwanayamala na Sinza, ambapo 19 wapo Sinza na 11 Hospitali ya Mwananyamala. Wengine wanne wameruhusiwa na kurudi nyumbani.
“Sampuli za wagonjwa sita zilizochukuliwa, wanne kati yao wamethibitika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo,” alisema Natty.
Alisema wamepata dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo. Jitihada mbalimbali zinaendea kuchukuliwa ikiwemo kupulizia dawa kwenye madimbwi ya maji.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Dk Jackson Makanjo, aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kuchukua tahadhari, ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kula, na unapotoka chooni. Alitoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam, kuhakikisha wanachemsha maji ya kunywa na kuepuka kula ovyo vyakula vya mitaani.
Alisema ugonjwa huo ulianzia eneo la Kwa Ali Maua huko Kijitonyama na kisha kuenea maeneo ya jirani ya Tandale, Manzese na Mwananyamala.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment