MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 4
Akajitanbulisha na kuelezwa
na polisi hao kilichotokea. Makete hakuamini. Alikwenda kulikagua ghala hilo na kupigwa na bumbuazi.
“Imekuwaje Alfred?”
akaniuliza.
Nilimueleza kama nilivyowaeleza
polisi.
“Lakini Alfred hukuja hapa
kulala, ulikuja kulinda hili ghala”
‘Nilipitiwa mzee”
“Sasa sisi tunakwenda naye
kwa hatua zaidi. Askari wako mwingine ataendelea kulinda hili ghala. Asubuhi
uje kituo cha polisi cha Chumbageni pamoja na mwenye ghala hili” Polisi mmoja akamwambia mkuu
wangu.
Nilikabidhi bunduki kwa
askari mwenzangu kisha nikapakiwa kwenye gari la polisi.
Karibu njia nzima polisi hao
walikuwa wakinisema mimi. Walinituhumu kwamba nimekula njama na hao majambazi
waliovunja lile ghala na kwamba endapo hawatapatikana nitashitakiwa peke yangu.
Tulipofika kituo cha polisi
nilihojiwa na maelezo yangu yaliwekwa katika jalada kisha nikatupwa mahabusi.
Humo mahabusi nilikuta watu
kadhaa, wengine wakiwa wamelala kwa mtindo wa kukaa huku wengine wakiwa macho.
Nilitafuta kipembe nikaketi kwa kujiegemeza kwenye ukuta.
Ilikuwa ni mara yangu ya
kwanza katika maisha yangu sio tu kukamatwa na polisi, bali kutiwa mahabusi.
Usiku ule ndio niliiona na kuijua mahabusi ilivyo. Chumba kidogo lakini kilijaa
watu wengi. Kilikuwa na joto na hakikuwa na harufu ya kupendeza kwani choo hakikuwa
mbali.
Hata hivyo adha iliyokuwemo
humo ndani haikunizuia kujiambia kuwa hukumu ya kosa langu ni kifungo
kisichopungua miaka 30 jela. Ukilinganisha miaka hiyo na umri wangu, ilikuwa
wazi kuwa ningefia jela au nitatoka jela nikiwa nimeshazeeka.
Nililia bila kujali kuwa
mahabusi wenzangu walikuwa wakiniangalia. Kwa upande mwingine nilikuwa
nikimfikiria yule msichana aliyenisababishia nipate balaa hili.
Sikujua alikuwa kiumbe wa
aina gani. Alipokuja katika lindo langu na kuzungumza naye alikuwa binaadamu wa
kawaida lakini nilipomuona tena akiwa ndani ya lile gofu hakuwa mwanaadamu.
Alikuwa amebadilika. Alikuwa mrefu kupita kiasi, mwili wake ulikuwa umeota
manyoya marefu na alikuwa na miguu yenye kwato kama
ya punda
Kila nilivyojaribu kuliwaza
umbo lake, mwili wangu ulikuwa ukisisimka.
Sikuweza kujua alikuwa kiumbe wa aina gani.
Wakati ninalia, usingizi
ulikuja kunichukua ghafla. Nikaota eti yule msichana amekuja kule mahabusi
kuniangalia. Akaniambia.
“Mimi sikukuambia unifuate,
ulinifuata mwenyewe. Unaona sasa!”
“Lakini wewe ndiye
uliyesababisha. Kama ungeniletea koti langu,
haya yasingetokea” na mimi nikamjibu.
“Sasa sikiliza nikwambie,
najua una uchungu na unanilaumu mimi. Nitakuonesha mali zilizoibiwa zilikopelekwa.
Twende”
Nikaona nimetoka mahabusi na
yule msichana. Tukaenda katika eneo moja linaloitwa Kisosora katika barabara inayoelekea Mombasa. Akanionesha
nyumba moja na kuniambia.
“Vitu vilivyoibiwa vimewekwa
ndani ya nyumba hii. Na mwenye nyumba hii anawajua wote waliohusika kuvunja
ghala na kuiba”
“Sasa nikiulizwa nimejuaje
kuwa vitu vilivyoibiwa vimeletwa humu, nitajibu nini? Si nitaonekana
ninahusika?” nikamuuliza msichana huyo.
“Basi nitakuja mwenyewe kituo
cha polisi asubuhi niwambie polisi nimeona vitu vikiingizwa usiku ndai ya
nyumba hii”
Aliponiambia hivyo
nikazinduka. Nikaona kulikuwa kumeshakucha.. Waliingia polisi wawili
wakatuhisabu kwa kutuita majina. Walipomaliza kutuhisabu waliondoka. Kila
mahabusu akaenda kunawa uso na kurudi. Baada ya muda kidogo tuliletewa uji.
Ulikuwa uji wa sembe uliotiwa chumvi. Baadhi ya mahabusu waliletewa chai kutoka
majumbani kwao.
Ilipofika saa mbili asubuhi
alikuja polisi kuniita. Nikaenda naye katika ofisi ya afisa upelelezi wa
wilaya. Afisa upelelezi mwenyewe alikuwa ameketi kwenye kiti. Pia kulikuwa na
polisi wawili miongoni mwa wale polisi walionikamata usiku wakiwa wesimama huku wakiwa na bunduki walizokuwa wamezibeba tumboni.
Mbali ya polisi hao kulikuwa
na raia sita waliokuwa wamewekwa chini. Nilishuku kuwa walikuwa ni wahalifu.
Mara tu nilipoingizwa katika
ofisi hiyo afisa upelelezi aliwauliza wale watu kama
walikuwa wananifahamu. Wote wakajibu kuwa hawakuwa wakinifahamu. Na mimi
nikaulizwa kama nilikuwa nawafahamu watu hao.
Baada ya kuwaangalia sikuona yeyote niliyekuwa namfahamu. Nikatikisa kichwa na
kujibu kuwa siwafahamu.
“Una hakika kuwa hakuna yeyote unayemfahamu miongoni mwa watu
hawa?”Afisa upelelezi akaniuliza kwa mkazo.
“Nina hakika, hakuna
ninayemfahamu” nikamjibu.
“Basi mrudishe” afisa
upelelezi akamwambia yule polisi aliyenileta huku akiwa ameshikilia bunduki yake huku nikiwa na hofu kweli kweli.
Nikarudishwa mhabusi. Sikujua
watu wale walikuwa kina nani na kwanini nilipelekwa kuulizwa kama
ninawafahamu ilhali siwafahamu.
Baadaye tena kama saa nne hivi nilitolewa nikapelekwa tena katika
ofisi ya afisa upelelezi wa wilaya. Nilimkuta afisa upelelezi, mkuu wangu wa
kazi na mtu mmoja mwenye asili ya kiasia ambaye nilihisi alikuwa ndiye mmiliki
wa ghala lililovunjwa.
Afisa upelelezi akaniambia
kwamba mnamo saa moja asubuhi alifika msichana mmoja pale kituoni ambaye alidai
alikuwa mkazi wa eneo la Kisosora. Akawaeleza
kuwa aliona gari likishusha vitu usiku katika nyumba moja.
“Akaendelea kutueleza kwamba
alishuku kuwa vitu vile vilivyokuwa vinashushwa vilikuwa vya wizi hivyo
akatuomba twende katika nyumba hiyo kuchunguza” Afisa upelelezi huyo akaniambia
na kuendelea.
“Tukaenda katika nyumba hiyo
ambayo yule msichana alituelekeza. Tulifanya upekuzi na tuligundua kuwa vyumba
viwili vya ndani na vyumba vitatu vya uani vilikuwa vimejaa mali ambayo tuliikamata.
“Vilevile tulikamata watu
wawili tuliowakuta wamelala katika chumba kimoja. Baada ya kuwahoji tuligundua
kuwa walikuwa majambazi kwani mmoja wao tulikuwa tunamtafuta. Wakatueleza
kwamba walikwenda kuvunja ghala moja usiku huko Gofu na waliwataja wenzao wanne
ambao pia tulikwenda kuwakamata” Afisa
upelelezi aliendelea kuniambia.
Akaniambia mwenye ghala
lililovunjwa alipooneshwa ile mali iliyoletwa pale kituo cha polisi
alithibitisha kuwa ni mali
yake iliyoibiwa na kuonesha hati zote za umiliki.
“Tulipokuita mara ya kwanza,
wale uliowakuta walikuwa ndio majambazi wenyewe tuliowakamata. Tulipowahoji
wote walisema hawakujui na wewe tulipokuuliza ulisema huwajui. Sisi tulikuwa
tunadhani mlishirikiana, kumbe haikuwa hivyo. Kwa hiyo kwa vile mali
iliyoibiwa imepatikana na majambazi waliohusika wamekamatwa, tumeamua
kukuachia. Mshukuru sana yule dada aliyewezesha
kupatikana kwa ile mali
na wale majambazi kukamatwa”
Nikashusha pumzi ndefu za
faraja. Hapohapo niliikumbuka ile ndoto niliyoota nikiwa mahabusi. Yule
msichana aliniambia atakuja yeye pale kituoni kutoa taarifa kuhusu majambazi hao,
na ndivyo ilivyokuwa.
Ingawa niliachiwa na kutakiwa
kufika tena hapo kituoni kesho yake asubuhi, nilikutana na zahama jingine.
Nilipofika ofisini kwetu nilipewa barua ya kufukuzwa kazi kwa kosa la kufanya
uzembe na kulala nikiwa katika lindo na kusababisha lindo kuvunjwa na mali
kuibiwa.
Baada ya kupewa barua hiyo
nilishukuru na kurudi nyumbani. Niliketi kitandani na kujiambia, balaa hilo la kukamatwa na hatimaye kufukuzwa kazi,
ulikuwa mkosi uliotokana na yule msichana ambaye mpaka muda ule sikuweza kutambua
alikuwa kiumbe wa aina gani.
ITAENDELEA KESHO
Kwa habari, matukio, michezo na hadithi ni hapahapa Tangakumekuchablog
|
Sunday, April 3, 2016
MWANAMKE ALIENICHUNUKU SEHEMU YA ( 4 )
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment