MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KUFANYIKA MACHI 8, 2016
Wizara ya Maendeleo ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto inawataarifu wananchi wote
kuwa tarehe 8 Machi ya kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine
wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake,
hutoa fursa kwa Serikali, wananchi, wadau, na wanawake wenyewe kupima
utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba ya Kimataifa, Kikanda na
Kitaifa inayohusu masuala ya maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia.
Siku ya wanawake Duniani
husisitiza kujenga mshikamano wa wanawake wote duniani, kuhamasisha
jamii kutafakari kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake ya kila
mwaka; kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na
Serikali na asasi mbalimbali yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
katika kuwaendeleza wanawake; na kuhamasisha jamii kuhusu utekelezaji wa
sera na mipango mbalimbali ya Serikali yenye lengo la kudumisha Amani,
Usawa na Maendeleo.
Kaulimbiu ya kitaifa ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2016 inasema “50 – 50 Ifikapo 2030; Tuongeze Jitihada”. Kaulimbiu
hii inasisitiza kuwa na mikakati thabiti yenye mwelekeo wa kufikia
Agenda 2030 ya malengo inayohimiza kufikia asilimia 50 kwa 50 ya
ushiriki wa wanawake na wasichana katika nyanja zote za maendeleo.
Kuanzia mwaka 2005 Serikali
ilipitisha uamuzi kuwa, maadhimisho haya yafanyike Kitaifa kila baada ya
miaka mitano kutoa muda wa utekelezaji wa maazimio na kupima mafanikio
yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano. Mwaka 2015 Maadhimisho
yalifanyika Kitaifa mkoani wa Morogoro. Kwa mwaka 2106, mikoa yote
itaadhimisha siku hii katika maeneo yao kwa kuzingatia hali na mazingira
ya mikoa husika. Kwa mfano mkoa wa Dar es salaam, utaadhimisha siku hii
katika Manispaa ya Kinondoni. Wizara inatoa wito kwa mikoa yote
kuhamasisha wananchi na wadau wote kushiriki maadhimisho ya siku hii
adhimu na kuzingatia ujumbe wa kauli mbiu ya mwaka 2016.
Rai yangu kwa wadau wote ni kuwa,
tuunge mkono jitihada za Serikali katika kutoa haki na ushiriki sawa
katika fursa za uongozi wa kisiasa na kiuchumi; na kupima mafanikio
yaliyofikiwa na kuweka mipango yenye matokeo makubwa, na kubainisha
shuhuda za wanawake waliotoa mchango uliotukuka katika kuwezesha
maendeleo ya wanawake wenywe na taifa kwa ujumla.
Nashauri wanahabari wote
kuelimisha jamii kuhusu kaulimbiu ya Siku ya Wanawake kwa mwaka 2016 ili
kila mwananchi aweze kutambua jukumu alionalo katika kufikia lengo la
ushiriki sawa wa wanawake na wasichana katika uchumi; afya, elimu,
ajira, sheria na siasa ifikapo mwaka 2030.
Nawatakia mafanikio mema katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu.
Sihaba Nkinga
KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment