Tangakumekuchablog
Korogwe, KIKOSI
Maalumu cha Kupambana na Mihadarati Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, imewakamata
watu wanne kwa tuhuma za kusafirisha mirungi kilo 121 wakati wa ukaguzi wa
magari zoezi linalofanywa masaa 24 kila siku.
Zoezi hilo linalosimamiwa na Kamanda
wa Operesheni Wilaya ya Korogwe, Jeremiea Ouko, linadaiwa kufanikiwa baada ya
kuziba njia na mbinu zitumiwazo na wasafirishaji wa njia ya barabara na njia za
panya.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, Mihayo Msikhella, aliwataja watu hao
kuwa ni, Said Seif (29), Mbwana Kassim (37), Athumani Abdalla (19) na Salim Hussein (19) wote wakiwa ni wakazi wa Korogwe.
Alisema watu hao walikuwa
wakisafirisha kwa kutumia gari aina ya Noah na kufunga kwenye magunia ya mkaa
kuficha ushahidi jambo ambalo polisi waligundua baada ya kusikia harufu kali ya
mirungi.
“Ile gari ilipofika katika kizuizi
cha Kwasunga dereva alikataa kusimama baada ya polisi kulisimamisha, iliwapa
wasiwasi na kuifukuzia na ndipo iliposimama na wakati wakijaribu kukimbia
wakadakwa” alisema Msikhella na kuongeza
“Waligoma kufungua magunia na kudai
kuwa ni mkaa na wakiushusha utatoa vumbi, polisi ilishusha kumbe magunia
waliyapaka mkaa ili kuficha ushahidi na kukutaka mirungi kibao” alisema
Alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa
kituo kikuu cha polisi cha Chumbageni kwa mahojiano na upelelezi
utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kwa upande wake Kamanda wa
Operesheni Korogwe, Jeremia Ouko , aliwataka wamiliki wa magari na madereva
kuacha kutumiliwa na wasafirishaji mihadarati na kusema kuwa ukaguzi wa magari
na wasafirishaji wa njia za panya wakiwemo wa pikipiki polisi watakuwa wako
kazini.
Alisema mbinu zote za kusafirisha
mirungi na madawa mengine polisi inazitambua hivyo kuwataka watu kuacha
kutumiliwa na kwa tama ya pesa ambazo wakigundulika wateja wao huwaruka.
“Kuna baadhi ya madereva huingiwa na
tama ya pesa na hubadilikwa na roho bila
kujali mzigo ambao wanabebea, tama yao mwisho huwa majuto kwani polisi sasa
hivi wako makini na madawaya kulevya” alisema Ouko
Aliwataka wamiliki wa magari ya
abiria na mizigo kuwapa tahadhari madereva wao kuacha kubeba mihadarati na
mizigo ya magendo kwani polisi inafanya upekuzi yakinifu .
Mwisho
Kamanda wa Polisi Tanga, Mihayo Msikhella, akiwaonyesha mirungi iliyokamatwa kizuizi cha Kwasunga Korogwe katika Operesheni tokomeza mihadarati juzi.
Kamanda wa Operesheni Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, Jeremia Ouko, akitoa viroba vya mirungi vilivyokamatwa wakati wa Operesheni tokomeza madawa ya kulevya katika kizuizi cha polisi Kwasunga juzi.
No comments:
Post a Comment