MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 5
Imetungwa na FAKI A FAKI
0655340572
Baada ya kutafakari kwa kina,
nilijiambia yaliyopita yameshapita, sasa ni kuganga yaliyopo na yajayo. Kama ni
yule msichana sitaweza kumjua. Na kama ni kazi
nimeshafukuzwa. Sasa liliopo ni kujaribu kuandika barua kuomba sehemu nyingine.
Kulikuwa na makampuni mengi ya ulinzi yaliyokuwa yanahitaji walinzi hasa vijana
kama mimi.
Siku ileile niliandika barua
kadhaa na kuzipeleka katika ofisi za makampuni mbalimbali ya ulinzi.
Nilitegemea katika makampuni hayo sitakosa kampuni mojawapo itakayonipatia
kazi.
Usiku wa siku ile kabla
sijalala, nilisoma biblia yangu, nikasali na kuomba. Nilitegemea kwa uwezo wa
Mwenyezi Mungu sitakaa muda mrefu kabla ya kupata kazi.
Ingawa nilikuwa nimesongwa na
mawazo mengi kwa kuachishwa kazi ghafla, sikuchelewa kupata usingizi nikalala.
Nikazinduka usiku mwingi. Nikahisi kama kulikuwa na mtu ananiita. Nikatega
masikio yangu kusikiliza.
Kwanza palipita ukimya wa kama dakika moja hivi kisha nikasikia tena sauti ikiita jina langu.
Ilikuwa sauti ya mwanamke niliyoitambua. Lakini sikuweza kukumbuka mara moja
ilikuwa sauti ya nani na alikuwa wapi.
“Alfred! Alfred!” Sauti hiyo
iliendelea kuita. Moyo wangu ulishituka. Nikaendelea kutega masikio.
Niligundua kuwa ile sauti
ilikuwa ikitokea mlango wa nje.
Ni nani anayeniita usiku huu?
Nilijiuliza bila kupata jibu. Sauti iliyokuwa ikiniita iliacha kwa muda kisha
ilianza kusikika tena. Na sasa aliyekuwa akiita alianza kubisha mlango.
Hapo hapo akili yangu
ikazinduka. Nilitambua kuwa ile sauti ilikuwa ya yule msichana niliyemuazima
koti langu.
Ameijuaje nyumba ninayoishi
na kwa nini amenifuata nyumbani? Anataka nini? Nilijiuliza kwa mshituko.
Ataita na kubisha mpaka watu
wa nyumba nzima wataamka, mimi sitatoka, nikajiambia.
Na kweli, aliita na kubisha
mpaka ile sauti ikapotea, kukawa kimya. Hata hivyo mimi sikulala tena mpaka
asubuhi.
Ile ilikuwa ni mara ya
kwanza. Usiku wa siku ya pili yake nilishituka tena usingizini nikaisikia ile
sauti ikiniita. “Alfred! Alfred!”
Safari hii aliita na kubisha
mara chache tu kisha nikasikia mlango wa nje unafunguliwa. Moyo wangu
ulishituka. Hakukuwa na mtu yeyote mle ndani aliyeuliza “wewe nani?” Nikahisi
pengine sauti ya msichana huyo na sauti ya kufunguliwa kwa ule mlango
nilizisikia peke yangu.
Baada ya mlango huo
kufunguliwa nilisikia mlio wa ko! ko! ko! hapo ukumbini. Nikahisi ulikuwa mlio
wa viatu ama wa kwato za yule msichana. Punde tu nilisikia mlango wa chumba
changu unabishwa huku ile sauti ya msichana ikiita jina langu. “Alfred!
Alfred!”
Moyo ulikuwa ukinienda mbio kama uliotaka kutoka. Nilinyamaza kimya. Nilikuwa
nimejifinika shuka gubigubi. Msichana aliendelea kubisha na kuniita kwa karibu
dakika mbili. Alipoona siitikii wala sifungui mlango, nilisia anaondoka. Alirudi
mlango wa nje akatoka kisha akafunga mlango. Baada ya hapo sikusikia kitu tena.
Kwa kweli sikulala tena.
Niliendelea kukaa macho hadi saa 12 asubuhi. Nikawa mtu wa kwanza kutoka
chumbani. Nilikwenda mlango wa mbele nikitegemea ningeukuta mlango huo ukiwa
umefunguliwa lakini nilikuta umefungwa kwa ndani vile vile.
Nikajiuliza yule msichana
aliufunguaje na kuweza kuingia wakati mlango huo ulifungwa kwa ndani? Kwa kweli
sikuweza kupata jibu.
Nilirudi chumbani nikakaa kitandani
na kufikiria kwamba msichana huyo anaweza kuharibu maisha yangu kama ambavyo alishaanza kuyaharibu. Sikuweza kujua ni
kitu gani kilichomfanya anifuatefuate.
Hofu yangu ilikuwa kwamba
usiku wa juzi alibisha mlango wa mbele, usiku uliofuata akaingia ndani na
kubisha mlango wa chumba changu. Usiku wa leo anaweza kuja kuingia chumbani
mwangu!
Baada ya kutafakari vizuri
nilitoka nikaenda kupiga mswaki na kuoga. Niliporudi nilivaa kisha nikatoka.
Nilikwenda katika kibanda cha mama lishe ambako hunywa chai kila asubuhi.
Nikanywa chai kisha nikatoka.
Nilikuwa nimeamua kwenda kwa
Mchungaji wa kanisa letu ili nimueleze matatizo yangu nione jinsi ambavyo
atanisaidia.
Nilikuwa nimepata hofu kuwa
endapo sitamueleza Mchungaji, yule msichana wa ajabu anaweza kuendelea
kunifuatafuata wakati sikujua lengo lake
lilikuwa nini. Na baya
zaidi nilishuku kuwa usiku ule angeweza
kuniingilia chumbani mwangu.
Wakati nataka kuingia katika
wigo wa kanisa niliona msichana amesimama pembeni mwa lango la kanisa
akiniangalia kwa macho makali huku amekunja uso. Nilipomuangalia vizuri niliona
alikuwa ni yule msichana wa ajabu.
Nikashituka na kugeuza uso
wangu haraka nikijifanya sikumuona. Nikaingia ndani ya ua wa kanisa. Baada ya
kupiga hatua tatu dukuduku lilinishika, nikageuza uso nyuma kumuangalia.
Akanionesha ishara ya kuniita.
“Njoo “ akaniambia bila kutoa
sauti. Aliniambia kwa midomo tu kama
anayezungumza na mtu asiyesikia.
Nilipoona ananiita niligeuza
tena uso wangu na kuendelea kwenda. Lakini sikufika mbali niligeuka tena
nyuma kumuangalia
Sasa nilimuona amesimama
katikati ya lango akiniita kwa kunipungia mkono.
“Nimekwambia njoo!”
akaniambia bila kutoa sauti yake.
Nikawa ninaenda huku
namuangalia yeye. Alipoona nazidi kwenda aliacha kuniita. Akawa ananitazama kwa
uso wa huruma kama kiumbe kisicho na hatia.
Alikuwa na uso wenye sura ya mvuto. Macho yake makubwa yalilegea na kutoa nuru
ya kunilaani kwa kutomjali.
Wakati ninakwenda huku
naangalia nyuma, nilimkumba mtu aliyekuwa anatoka. Nikageuka haraka na kumuomba msamaha. Kumbe alikuwa Mchungaji.
“Bahati mbaya, endelea tu”
akaniambia alipoona nimegwaya.
“Nilikuwa nakuja kwako”
“Na mimi nilikuwa natoka
lakini naweza kurudi kwa ajili yako”
“Nitakushukuru baba, nina
matatizo makubwa”
Mchungaji huyo alinipeleka
katika ofisi yake akanikaribisha kwenye kiti kisha na yeye akaketi.
“Sasa unaweza kuzungumza
shida yako” akaniambia.
Nikamueleza matatizo yangu
tangu mwanzo hadi yalipofikia.
Mchungaji akashangaa.
“Sijawahi kusikia kisa kama hicho
ulichonieleza!”
“Na huyo msichana nimekutana
naye kwenye lango sasa hivi, alikuwa ananiita. Pale nilipokukumba nilikuwa
namtazama yeye!” nikamwambia.
“Kwanini usinioneshe pale pale?.
Hebu twende”
Mchungaji aliinuka na mimi
nikanyanyuka. Tukatoka kwenda kwenye lango. Tulipofika hatukumkuta yule
msichana.
“Naona ameshaondoka alikuwa
amesimama hapa”
Nilimuonesha Mchungaji mahali
alipokuwa amesimama yule msichana.
“Pia nataka twende
ukanioneshe hilo
gofu ambamo uliwakuta” Mchungaji akaniambia na kuongeza “Tutakwenda kwa gari
langu”
“Sawa, twende nikakuoneshe”
ITAENDELEA KESHO
|
Monday, April 4, 2016
HADITHI SEHEMU YA ( 5 ) MWANAMKE ALIENICHUNUKU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment