ZULIA LA FAKI
NILIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 18
ILIPOISHIA
“Maana yake mtu amekufa
halafu anakuja kuonekana tena”
“Sasa yule si mtu yule yule”
“Ni nani sasa?”
“Kwanza mtu akifa hawezi
kuonekana tena”
“Mbona mimi nimemuona Ummy?”
“Uliyemuona si Ummy”
“Ni yeye. Licha ya kunielekeza kwao alinipa namba ya simu yake na nilimuonesha ndugu yake
pale nyumbani kwao akasema ni namba ya
Ummy kweli”
“Kwani ulifika kwao kumuulizia?’
“Ndiyo, nilifika jana”
“Wakakuambia nini?”
“Wakaniambia hivyo hivyo
kwamba Ummy alikufa”
“Si ndiyo nilivyokueleza
mimi?”
SASA ENDELEA
Nilihisi kwamba maelezo ya
Mzaramu badala ya kunisaidia yalizidi kunichanganya.
Mzaramu hakutaka kukubaliana na miimi
kwamba niliyemuona alikuwa ni Ummy wakati nilikuwa na imani kuwa niliyekutana
naye alikuwa ni Ummy Nasri.
Kitu muhimu kilichonifanya
niamini kuwa niliyemuona ni Ummy
Nasri aliyedaiwa kufa ni ile picha ya Ummy
niliyooneshwa na baba yake huku mdogo wake akikiri kwamba namba ya simu
niliyopigiwa na Ummy ilikuwa namba ya
Ummy kweli. Mdogo wake huyo alikuwa
ameikariri.
Sasa kulikuwa na vitu viwili
vilivyonitia mawazo. Kwanza ni yale maelezo ya Mzaramu kwamba Ummy kabla ya
kufa alikuwa na uhusiano na mzee mmoja
ambaye Mzaramu alinithibitishia kuwa ndiye yule niliyemuonesha katika picha iliyokuwa kwenye simu yangu.
Picha hiyo
ilikuwa ni ya babu yangu marehemu mzee Limbunga. Hivyo maelezo ya
Mzaramu yalionesha kwamba babu yangu alikuwa na uhusiano na Ummy.
Kitu cha pili
kilichoniitia mawazo ni maelezo ya Ummy
kwamba anazijua siri za malli ya babu
yangu. Inawezekana kweli anaijua siri ya
mali ya babu yangu kwa vile alikuwa na uhusiano naye. Ila kinachotatanisha hapo
ni kuwa Ummy mwenyewe anadaiwa kuwa alishakufa.
Yakanijia mawazo yale yale
kwamba niliouona ulikuwa mzuka wa Ummy, yaani iliwezekana kuwa Ummy alishakufa
kweli lakini nilichokutana nacho kilikuwa kivuli chake. Nilishasikia hadithi
nyingi za watu waliokufa kuonekana tena ikidaiwa kuwa ni mizuka ya watu hao.
Lakini mara nyingi mizuka
hiyo inapotokea inakuwa na sababu.
Sasa nikajiambia labda
nijaribu kutafuuta sababu ya kutokea kwa mzuka wa Ummy ambaye aliwaua watu wote
waliokuwa wakidaiwa na babu yangu na
kusababisha nisilipwe pesa ambazo ningelipwa na watu hao.
Nikajiuliza kama Ummy alikuwa
mzuka ni kwanini aliwaua watu hao halafu aniambie kuwa anaijua siri ya mali ya
babu yangu na kutaka nikutane naye?
Kwa kweli kila nilivyowaza
niliona sivyo na kila nilivyojiuliza sikupata jibu. Hapo ndipo
nilipozidi kuchanganyikiwa.
“Mbona umeduwaa rafiki
yangu?” Mzaramu akaniuliza akiwa hajui
yaliyokuwa yanapita akilini mwangu.
Nikazinduka kutoka katika
mawazo yangu na kumwambia.
“Nilikuwa nafikiria hadithi uliyonieleza”
“Kahawa imekutosha?”
akaniuliza.
“Imetosha. Ni kiasi gani?”
“Sijakuuzia, nimekupa
kiurafiki kwa vile siku nyingi
hatujaonana”
“Asante, nakushukuru sana.
Naona nikuage, tutaonana siku nyingine”
Nilipoondoka kwa Mzaramu
nilikusudia nipite pale nyumbani kwa kina Ummy na kama nitakutana na yule mzee
nisalimiane naye.
Wakati nipo barabarani nikitembea
kwa miguu kuelekea upande ule ilikokuwa nyumba ya mzee Nasri, nikakutana na
mdogo wake Ummy akitokea dukani.
Msichana huyo aliponiona
akasimama.
“Kaka wewe ndiye uliyekuja
nyumbani jana ukatuambia kuwa ulimuona dada?”
akaniuliza.
“Ndiye mimi”
“Jana ulitutia wasiwasi sana.
Ilibidi mama aende kwa mganga kumueleza kuhusu kuonekana kwa Ummy ambaye
alishakufa. Mganga akamwambia kwamba huyo aliyeonekana alikuwa Ummy kweli,
amechukuliwa msukule”
“Amechukuliwa msukule na
nani?” nikamuuliza.
“Huyo mganga alimwambia
amechukuliwa msukule na mwanamke mmoja
ambaye aliwahi kugombana naye”
“Waligombania nini?”
“Huyo mwanamke alikuwa akidai
kuwa marehemu alikuwa anatembea na mume wake”
Nikayakumbuka yale maelezo ya
Mzaramu. Nikafikiri kidogo kisha nikamuuliza.
“Kama alichukuliwa msukule
mbona yuko vizuri tu, anaongea kwenye simu na nilikutana naye Botswana,
Zimbabwe na Afrika Kusini. Mtu aliyechukuliwa msukule anapanda ndege?”
“Hayo ni maelezo ya huyo
mganga lakini baba alipoelezwa amesema hataki mambo ya kishirikina, anachojua
yeye ni kuwa mwanawe amekufa, huyo aliyeonekana siye mwanawe”
“Mimi pia hayo madai ya
kuchukuliwa msukule sikubaliani nayo. Waganga wengine wanakisia tu”
“lakini wewe una hakika kuwa
ulimuona dada?”
“Nilimuona na ni yeye aliyenielekeza nije kwenu. Mimi
nilikuwa sijui kwamba amekufa”
“Na tangu jana hajakupigia
simu?”
“Hajanipigia bado”
“Na wewe hujampigia?”
“Sijampigia”
“Ungempigia umuulize vizuri”
“Kusema kweli
nimetishika baada ya kusikia kuwa
alishakufa”
“Hebu jaribu kumpigia sasa
hivi?”
Nikatoa simu na kuitafuta
namba ya Ummy, nilipoipata nikampigia.
Simu ikaita. Nikajua
itapokelewa ili nimpe mdogo wake azungumze naye lakini simu haikupokelewa.
Ilipokata nikapiga tena.
“Hapokei simu?” nikamwambia
yule msichana.
“Labda alikudanganya tu?”
ITAENDELEA kesho hapahapa Usikose Uhondo huu nini kitatokea, je simu itapokelewa na mdogo wake atazungumza nini na dada yake ambaye anauhakika ameshafariki?