Saturday, April 2, 2016

HUKUMU YA WACHINA WALIOTOROSHA NOTI ZA 500

Hii ndio Hukumu ya wachina waliotorosha noti za 500

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu raia wawili wa China kulipa faini ya Sh. milioni 50 au jela miaka 11 baada ya kukiri kusafirisha Sh. milioni 20 za Tanzania kwenda nchini kwao bila kibali kutoka kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Washtakiwa hao ni mfanyabiashara Sun Ning (39) na Fen Quan (51).

Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Cyprian Mkeha.

Mbali na adhabu hiyo, mahakama imeamuru fedha walizokutwa nazo washtakiwa kurejeshwa kwa mshtakiwa wa kwanza.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu alisema kwa kuwa washtakiwa wamekiri kufanya makosa hayo, mahakama inawatia hatiani.

Akifafanua adhabu kwa washtakiwa, alisema kosa la kwanza washtakiwa watalipa faini ya Sh. milioni 10 ama kwenda jela miaka mitano.

Kosa la pili, washtakiwa watalipa faini ya Sh. milioni 20 ama kwenda jela miaka mitano.

“Mahakama hii inawahukumu kulipa faini ya Sh. milioni 20 ama kwenda jela mwaka mmoja na adhabu ya kifungo itakwenda sambamba,” alisema Hakimu Mkeha.

 Juzi, washtakiwa hao walipandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kusafirisha fedha noti za Sh. 500 zenye thamani ya Sh. milioni 20 bila kibali cha Gavana wa BoT.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, akisaidiana na  Wakili wa Serikali Estazia.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya  2015 na 2016 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, washtakiwa walikutwa na fedha hizo mali ya Tanzania.

Ilidaiwa kwamba katika shitaka la kwanza kati ya Agosti 15 na 31, mwaka jana ,washitakiwa hao walisafirisha noti 10,000  za  Sh. 500 zenye thamani ya Sh. milioni tano kwenda China bila kibali kutoka kwa Gavana wa BoT.

Katika shitaka la pili kati ya Desemba 22 na 31, 2015 washtakiwa  katika viunga vya uwanja huo, walisafirisha noti  10,000 za  Sh. 500  zenye thamani ya  Sh. milioni tano bila kibali kutoka kwa Gavana wa BoT.

Shtaka la tatu, washtakiwa hao wanadaiwa kwamba Machi 15, 2016 walikutwa wakisafirisha noti 40,000 za Sh. 500 zenye thamani ya Sh.milioni 20 kwenda China kibali.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa hao walikiri kutenda kosa hilo na kusomewa maelezo ya kesi ambapo ilidaiwa kwamba Sun ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Feng Shi Trading, aliingia nchini Machi 13, mwaka huu.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment