MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 3, inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Tiba Asilia cha Mkombozi Sanitarium Clinic Tanga, Mkombozi wako Tanga mkabala na ofisi za Freys na wako na mashine za kisasa za kupimia mwili mzima na kutoa ushauri wa kitaalamu, simu 0654 361333
ILIPOISHIA
Uwazi uliokuwa mbele yangu ulikuwa
ni wa chumba kipana kilichokuwa kinatoka moshi kama
vile kulikuwa kumewashwa moto ingawa moto huo sikuuona. Nikabaki nimesimama
nikiangalia huku na huku.
Ghafla nikasikia sauti kutoka
chumba kingine. Zilikuwa sauti za wanawake waliokuwa wakisemeshana kwa lugha
ambayo sikuielewa. Nilipata uhakika wa kutosha kuwa sauti mojawapo ni ya yule
msichana niliyemfuata.
Nikaenda upande ule
nilikosikia sauti hizo. Palikuwa na uwazi uliotokana na kung’olewa kwa mlango.
Nikasimama pembeni mwa ukuta na kuchungulia ndani ya uwazi huo. Nikawaona
wanawake wawili waliokuwa warefu kama mnazi.
Mmoja alikuwa amechutama akipulizia moto na mwenzake alikuwa amesimama.
Aliyesimama nilimtambua,
alikuwa ni yule msichana niliyemfuata pale..
Hata hivyo hawakuwa na maumbo
ya kibinaadamu. Licha ya kuwa warefu, walikuwa na nywele ndefu nyeupe. Pia
waliota manyoya marefu mwilini. La kutisha zaidi walikuwa na miguu yenye kwato kama za punda!.
Moyo wangu ulishituka sana. Hapohapo yule
msichana ninayemfahamu aligeuza uso na kuniona. Macho yake yalikuwa
yamebadilika na kuwa na mboni zilizosimama kama
za paka na zilikuwa za rangi ya kibluu.
“Wewe umefuata nini huku?”
akaniuliza kwa fadhaa.
Hapo hapo nilianguka na kupoteza fahamu.
Sikujielewa tena.
Nikiwa katika usingizi mzito
nilisikia sauti ya yule msichana wa pili ikiuliza.
“Ni nani?”
“Si yule kijana
niliyekwambia” Sauti ya yule msichana ninayemfahamu ikajibu.
“Ulimuonesha hili geto letu?”
“Sikumuonesha labda alinifuata”
“Amefuata koti lake”
“Atakoma! Si nilimwambia
nitampelekea kesho”
Hapo hapo nikajiona nazinduka.
lakini badala ya kujikuta niko kwenye lile gofu, nilijiona ninazindukia kwenye
lindo langu, bunduki yangu nikiwa nimeishika mkononi. La kushangaza zaidi ni
kuwa lile koti langu nililomuazima yule msichana nilikuwa nimelivaa!.
Nikashituka na kujiuliza
nimefikaje hapa, wakati nilianguka na kupoteza fahamu nikiwa ndani ya lile
gofu.
Nani aliyenileta hapa?
Nilijiuliza.
Kumbu kumbu zangu za mwisho
zilikuwa ni za mazungumzo kati ya wale wasichana wawili. Baada ya hapo
sikukumbuka kitu kingine.
Nilijikuta nimelala mbele ya
lindo langu, nikainua uso wangu na kuangalia huku na huku, sikuona mtu yeyote.
Nilikuwa peke yangu. Nikainuka na kuketi. Niliikagua ile bunduki na kugundua
ilikwa na risasi zake sawasawa. Shaka yangu kuhusu bunduki ikaisha.
Sasa nikawa najiuliza yule
msichana na yule mwenzake niliyemkuta naye, walikuwa viumbe wa aina gani?
Sikupata jibu.
Ile hofu iliyonipata ndani ya
lile gofu nilikuwa bado ninayo. Nilijuta kumfuatilia yule msichana lakini
nilishukuru kujikuta nipo salama.
Hata hivyo nilijiambia kama
yule msichana atatokea tena mahali hapo muda ule, ningeliacha lindo na
kumkimbia. Sikutaka kukutana naye tena katika maisha yangu..
Sikujua ni kitu gani
kilichonifanya nitupe macho kwenye lango la lile ghala. Nikashituka nilipoona lango hilo lilikuwa wazi.
Nikanyanyuka haraka na kwenda kuliangalia. Nilikuta makufuli yalikuwa
yamevunjwa. Nilitoa tochi yangu ndogo na kumulika mle ndani. Ghala hilo lilikuwa karibu tupu
kwani vitu vyote viilivyokuwamo vilikuwa vimesafishwa.
Huo ulikwa ni mshituko
mwingine nilioupata. Ghala limeibiwa! Huenda majambazi hao walikuja wakati
nimemfuatilia yule msichana. Wakakuta hakuna mlinzi, wakavunja na kuiba kila
kitu
Kwa kweli nilichanganyikiwa.
Nilipiga mluzi na kutikisa kichwa changu kwa fadhaa.
Sasa nimekwisha!,
nikajiambia.
Kama ghala limevunjwa nani atakuwa mtuhumiwa namba moja?.
Jibu lilikuwa rahisi. Mtuhumiwa namba moja nitakuwa mimi.
Nitamueleza nini mwenye mali
au nitawaeleza nini polisi?. Kwa vyovyote vile itaonekana nimekula njama na
majambazi waje wavunje na kuiba.
Jela nilikuwa ninaiona kwenye
macho yangu. Hakukuwa na chochote cha kuninusurisha na kifungo.
Nikatoa simu yangu.
Sikukumbuka kupiga mahali popote zaidi ya polisi.
Iliwachukua nusu saa tu
polisi kufika katika eneo hilo.
Nilijua kuwa walifika kwa haraka si kwa sababu niliwapa taarifa za kushitusha
za kuvunjwa kwa ghala bali kituo kikuu
cha polisi hakikuwa mbali sana na eneo hilo.
Walifika polisi sita wakiwa
ndani ya Land Rover 110, kila mmoja akiwa na bunduki yake begani.
Niliwaeleza juu ya tukio la
kuvunjwa kwa ghala hilo na kuibiwa kwa mali
zilizokuwamo.
Swali la kwanza ambalo mmoja
wa polisi hao aliniuliza lilikuwa.
“Wewe ulikuwa wapi wakati
majambazi hao wanavunja ghala?”
Ilibidi niseme uongo wa
kipumbavu kuwa nilikuwa nimepitiwa na usingizi. Na nilipozinduka nikakuta ghala
limeshavunjwa.
“Haiwezekani. Wewe na hao
majambazi mmekula njama moja!” Polisi hao wakaniambia.
Walilikagua lile ghala
lililovunjwa kisha wakaniuliza kama nimeshamuarifu mkuu wangu wa kazi na mwenye
mali
Nikajibu “Bado sijawaarifu”
“Tupe namba ya simu ya mkuu
wako wa kazi”
Nikawapa namba ya mkuu wangu
wa kazi. Nilikuwa nikiifahamu kwa kichwa.
Polisi hao wakampigia simu na
kumuarifu juu ya kuvunjwa kwa ghala hilo
pamoja na wizi uliotokea.
“Tunakuomba ufike hapa haraka
sana ukiwa na
askari mwingine kwa sababu huyu tutaondoka naye”
Polisi huyo akakata simu na
kuniambia
“Maelezo yako hayaridhishi. Utakuwa
mtuhumiwa wetu namba moja”
Sikuwa na la kumjibu kwani
mazingira ya tukio zima yanaonesha na mimi ninahusika.
Mkuu wangu wa kazi James
Makete alifika dakika chache baadaye
akiwa na askari mwingine.
ITAENDELEA KESHO
Kwa habari,hadithi, matukio, elimu na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog
|
Friday, April 1, 2016
MWANAMKE ALIENICHUNUKI SEHEMU YA ( 3 )
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment