Wednesday, April 13, 2016

OMBAOMBA DAR NGANGARI


OMBAOMBA katika jiji la Dar es Salaam wamemjibu Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda wakisema hawawezi kuondoka kwa vile ‘mjini kila mtu ana kazi yake’.

Wamesisitiza kuwa hawawezi kuondoka Dar es Salaam kwa sababu wamekuja kutafuta kipato.

Baadhi ya ombaomba walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana, baada ya Gazeti hili kutaka maoni yao kuhusu tamko la Makonda kwamba atafanya operesheni ya kuwakamata Aprili 18 mwaka huu.


“Mimi siwezi kurudi Dodoma kwa sababu nauli ni kubwa. Nilikuja jana kwa kulipa Sh 20,000 sasa mimi nitapata wapi fedha nyingine? Kama anataka tuondoke atupatie nauli.

“Kama hawezi kutupatia nauli atupeleke popote sisi tutaendelea kuomba tuweze kujipatia kipato kwa ajili ya kujikimu maisha.

“Kama unavyoniona mimi na familia yangu nimekimbia Dodoma kutokana na mafuriko… sasa wakiniambia nirudi nitaenda wap?.
Pamoja na kunipatia nauli wanifanyie mpango wa nyumba ya kuishi,” alisema mmoja wa ombaomba hao, Amina Ramadhani aliyekuwa eneo la Mnazi Mmoja.

Mwingine aliyekuwa amekaa na watoto wake wanne na ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema: “Kila mmoja na kazi yake hapa mjini.


“Sisi tutaendelea kuomba kwa sababu ndiyo kazi yetu inayotupatia kipato cha kuendeshea familia zetu”.
Ombaomba mwingine ambaye naye alikuwa eneo la Mnazi Mmoja na pia hakutaka kutaja jina lake alisema viongozi wa Serikali nao ni wazazi kwa hiyo wanapaswa kuangalia namna ya kuwasaidia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makonda alisema muda wa ombaomba katika jiji umekwisha hivyo amewataka kufungasha virago vyao na kurudi makwao.

Alisema amefanya utafiti na kugundua kuwa asilimia 80 ya ombaomba wanatoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam na asilimia 20 ni wakazi wa jiji.

Makonda alieleza masikitiko yake kuwa ombaomba hao wamekuwa wakiwatumia watoto wao kuomba ili kujipatia kipato.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment