Salim Mohammed, Mwananchi
Tanga,JESHI la Polisi kituo kikuu cha
Chumbageni Tanga kinamshikilia dereva wa bodaboda, Moris Daffa (49) mkazi wa
Pongwe kwa tuhuma kuendesha pikipiki mwendo kasi na kumgonga mtembea kwa miguu,
Florida Msanga(70) na kufa papo hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, kaimu kamanda wa polisi
Mkoani Tanga, Juma Ndaki, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 11 jioni baada
ya ajuza huyo kuvuka barabara na kukumbana na dereva wa bodaboda na kumgonga na kufa papo hapo.
Alisema bibi huyo alikuwa anavuka barabara kukimbilia mifugo
yake mbuzi na kondoo na kutokea na dereva wa bodaboda akiwa mwendo kasi na
hivyo kumsababishia kifo.
“Kwa sasa tunasema kuwa tunamshikilia dereva na pikipiki yake
wakati uchunguzi unaendelea----tutaoa taarifa hapo baadae na kuwaiteni na
kuwapa taarifa kamili” alisema Ndaki na kuongeza
“Yule bibi alikuwa anakatisha barabara kuifukuzia mifugo yake
na mara akatokea dereva wa bodaboda na kumsomba mzimamzima na kufariki papo
hapo” alisema Ndaki
Alisema wakati wa kutokea ajali hiyo dereva wa pikipiki
alijaribu kukimbia lakini wapita njia wakiwemo abiria wa mabasi ya Wilayani
waliweza kumfukuza na kumkamata na ndipo polisi ilipotaarifiwa na kufika muda
huo huo.
Akizungumzia suala zima la usalama wa barabani, kaimu kamanda
amewataka watumiaji wa vyombo vya moto kufuata sheria pamoja na kuacha kutembea
mwendo kasi jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wao na watembea kwa
miguu.
Alisema polisi itafanya msako wa kuwabaini madereva feki
wakiwemo wasio na leseni za udereva pamoja na kuvamia maegesho ya bodaboda na
hivyo kuwataka wanaoendesha vyombo hivyo wasio na leseni kuacha kufanya hivyo.
Alisema msako huo utakuwa endelevu ikiwa ni kuwabaini watu
wasio na sifa za udereva kuwafikisha mahakamani baada ya matukio mengi ya ajali
kuongezeka na chanzo kikiwa ni uzembe wa madereva.
No comments:
Post a Comment