Misri:aliyekuwa rais Morsi kunyongwa
Mahakama moja nchini Misri imetoa amri ya kunyongwa kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Mohammed Morsi.
Mahakama hiyo ilimpata na hatia aliyekuwa rais wa Misri Mohammed Morsi kufuatia kuvunjwa kwa magereza mwaka wa 2011.Kauli hii ni msumari katika kidonda cha Morsi ambaye alikuwa tayari anatumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa kuamrisha kukamatwa kwa waandamanaji waliopinga utawala wake.
Morsi aling'olewa mamlakani na jeshi mwezi Julai mwaka wa 2013 kufuatia kipindi kirefu cha maandamano dhidi ya utawala wake.
Kuanzia hapo chama chake cha the Muslim Brotherhood kimepigwa marufuku huku mamia ya maelfu ya wafuasi wake kukamatwa na vyombo vya dola.
Kufuatia uamuzi huo wa kifo , sasa kauli nzima na ruhusa itapatikana tu baada ya uamuzi kutumwa kwa kadhi mkuu nchini humo ambaye sasa ndiye atakayetoa uamuzi wa mwisho iwapo Morsi ataonja mauti au la .
Sheria za nchi hiyo hata hivyo zinamruhusu Morsi kukata rufaa licha ya uamuzi wa kadhi mkuu.
Morsi na wafuasi wake wamekuwa wakishikilia kuwa mashtaka dhidi yake yamechochewa na uhasAma wa kisiasa baina yake na uongozi ulioko sasa.
Morsi amekataa katakata uhalali wa mahakama iliopo sasa.
Morsi aliweka rekodi ya kuwa kiongozi wa kwanza kuchaguliwa katika uchaguzi wa haki na huru.
Hata hivyo utawala wake ulikumbwa na wimbi la maandamano baada ya kujilimbikizia madaraka akiwa amehudumu kwa mwaka mmoja tu ya kuwa Ofisini.
No comments:
Post a Comment