Uchambuzi huu unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Nchi imesimama. Hii ndiyo sentensi
inayofaa kuelezea tukio la jana la mgomo wa madereva nchini kote ambao
kwa mara ya kwanza ulisababisha mabasi yote kutoka Dar es Salaam kwenda
mikoani na nchi jirani kushindwa kuondoka.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT), kushindwa kutoa huduma kwa sababu yoyote ile.
Tangu asubuhi hadi jioni, hakuna basi
hata moja lililotoka wala kuingia katika kituo hicho hadi abiria
walipoanza kukata tamaa na baadhi yao kuondoka na wengine kuanza
kushinikiza kurejeshewa nauli.
Mgomo huo ambao ni mwendelezo wa ule
uliofanyika Aprili 9, mwaka huu ulipewa uzito na madereva hao baada ya
ahadi walizopewa na Serikali kutofanyiwa kazi kama ilivyoahidiwa na
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.
Tofauti na wa awali, safari hii mpaka
inatimu saa 11.00 jioni hakuna kiongozi yeyote aliyejitokeza katika
kituo hicho kusikiliza kilio cha madereva hao.
Hata hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameunda kamati ya iliyotangazwa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta ya kusimamia usafiri barabarani itakayowakutanisha wadau wote ili kutatua matatizo katika sekta hiyo kila yanapotokea.
Tangu saa 2.30 asubuhi, polisi
walijaribu kuyasindikiza mabasi waliyodhani madereva wake wako tayari
kuondoka Ubungo lakini walishindwa baada ya kutoungwa mkono.
Mkuu wa Trafiki Ubungo, Inspekta Yussuf Kamotta akiwa na Inspekta Solomon Nkindwa
ambaye pia ni mkaguzi wa magari, waliingia katika basi la Kampuni ya
Master City na kuliondoa kituoni hapo wakiwa na mmiliki wa kampuni hiyo,
Abdallah Mohammed huku wakimtafuta dereva bila mafanikio na kulazimika kulitafutia sehemu salama ya kuliegesha baada ya madereva kulizingira.
Kutokana na vurugu zilizotokea nje ya
kituo hicho, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya
watu waliokuwa katika makundi.
Nje ya UBT, magari sita ya polisi
yaliegeshwa katika makutano ya barabara za Sam Nujoma, Nelson Mandela na
Morogoro wakati mengine yakielekea Mwenge na Buguruni kwenda
kukabiliana na tishio lolote ambalo lingeweza kutokea.
MWANANCHI
Raia watatu wa Ugiriki na Mtanzania mmoja wamepandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la
kughushi muhuri wa Mkuu wa Jeshi Polisi Nchini (IGP).
Akisoma hati ya mashtaka jana, Wakili wa Serikali, Mununila Munisi
alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchaulu kuwa washtakiwa
walitenda kosa hilo katika tarehe na muda usiofahamika wilayani Ilala.
Alidai kwamba katika shtaka la kwanza washtakiwa hao kwa pamoja kwa
nia ovu, walighushi muhuri huo wa IGP wakionyesha ni halali na umetolewa
na Jeshi la Polisi la Tanzania wakati wakijua si kweli.
Shtaka la pili wanadaiwa kuwa katika tarehe zisizofahamika jijini Dar
es Salaam, walighushi taarifa ya upotevu wa mali inayotolewa na jeshi
hilo la polisi wakionyesha ni halali na imetolewa na polisi wakati
wakijua siyo kweli.
Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai
upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba ipangwe tarehe nyingine.
Hakimu aliwataka washtakiwa hao wawe na wadhamini wawili wa kuaminika na kila mmoja atasaini bondi ya Sh5 milioni .
Pia, washtakiwa hao hawaruhusiwi kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam
bila kibali cha mahakama na wametakiwa kuwasilisha hati zao za
kusafiria.
Washtakiwa wote walishindwa kutimiza masharti hayo na hivyo wamerudishwa rumande.
NIPASHE
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge,
amefungua kesi ya kikatiba dhidi ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa
Umma na maazimio ya Bunge kuhusiana na malalamiko ya ukiukaji wa maadili
ya uongozi.
Chenge, anatuhumiwa kupokea fedha kutoka kwa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd Sh. bilioni 1.6.
Chenge aliitwa katika Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo ambazo ni kinyume cha maadili.
Hata hivyo, alipinga akisema kuwa baraza
hilo halina mamlaka ya kumhoji kwa kuwa liko katika Mahakama ambayo ina
mamlaka kuliko baraza, na kueleza kuwa atafungua kesi ya kupinga
mahakamani.
Katika maombi yake, lililowasilishwa
masjala kuu ya Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Chenge
ameorodhesha sababu 13 za kupinga mwenendo wa baraza na mapendekezo
yaliyowasilishwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati ya Bunge na Hesabu za Serikali (PAC) kuhusiana na shauri hilo.
NIPASHE
Wakati kukiwa kumebaki miezi mitano kufanyika uchaguzi mkuu, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ametamka kuwa safari hii hatakubali kunyang’anywa urais wa Zanzibar kama ilivyozoeleka katika chaguzi zilizopita.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo juzi jioni
baada ya wafuasi wa CUF kufika nyumbani kwake Mbweni, Zanzibar kwa
ajili ya kumkabidhi Sh. 1, 500,000 za kuchukulia fomu ya kugombea urais.
“Safari hii, wakitaka wasitake, nakuwa Rais wa Zanzibar kwa ridhaa ya wananchi,” Maalim Seif.
Alidai kuwa CUF kimekuwa kikishiriki
uchaguzi mkuu tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa na kushinda chaguzi
hizo zilizopita, lakini hakipewi ushindi.
CUF kilimsimamisha Maalim Seif kugombea urais mwaka 1995, 2005 na 2010 .
Maalim Seif alisema uchaguzi wa mwaka
huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, hakuna atakayemzuia kuchukua dola
kwani CUF kina kila sababu ya kushinda.
NIPASHE
Idadi ya watu wanaoingia nchini kutoka
Burundi kukimbia machafuko ya kisiasa kupitia mkoani Kigoma, imezidi
kuongezeka kutoka 1,645 hadi kufikia 1,852.
Kati ya hao, 1,252 tayari wameshasajiliwa kama wakimbizi rasmi na kupelekwa katika kambi ya Nyarugusu, wilayani Kasulu.
Hayo yalibainishwa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, wakati wa mahojiano na
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
wizara ya mambo ya ndani juzi, hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu, mkoa
huo ulikuwa umeshapokea idadi ya watu 500 walioingia kupitia vijiji
sita vya Kibuye, Kagunga, Kosovo, Kakonko, Sekeeye na Kigaye.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, hali ya
usalama katika maeneo ya mipakani, imeimarishwa na kutoa wito kwa wakazi
wa maeneo hayo kutoa taarifa kwa uongozi wa vijiji iwapo kuna mgeni
asiyefahamika kufika maeneo hayo.
Kwa upande wake, Afisa wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Maurice David, alisema hadi juzi jioni idadi ya wakimbizi walioingia mkoani humo ilifikia 1,645.
Hata hivyo, aliongeza kuwa idadi ya
wakimbizi waliofika kabla ya kuzuka upya kwa vurugu hizo nchini humo
ilikuwa 46, lakini hadi jana mkoa mzima ulikuwa umepokea jumla ya
wakimbizi takribani I, 852.
Burundi imekumbwa na vurugu kutokana na
maandamano yanayofanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Bujumbura, kwa
wananchi kupinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kutaka kugombea tena urais kwa muhula wa tatu kinyume cha katiba ya nchi hiyo.
MTANZANIA
Mkazi wa kijiji cha Ndelete, Kiteto Saria Kidali amefariki dunia baada ya kunyongwa na shuka alilokua amejifunika wakati anaendesha pikipiki.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana
asubuhi wakati Kidali alipokuwa akitok,ea shambani kwake ambapo shuka ya
mwendesha pikipiki huyo ilinasa kwenye tairi ya nyuma na kisha kumbana
shingo hadi alipopoteza maisha na kudondoka chini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Christopher Fuime alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.
Mashuhuda walisema walipata taarifa
kutoka kwa abiria mmoja wa basi aliyekuwa akitokea Kiteto kwenda Arusha
ambaye aliuona mwili wa mtu huyo ukiwa chini.
HABARILEO
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili
na Utalii jana ilikataa kujadili bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii
huku ikiwataka Waziri na watendaji wake kuondoka ukumbi wa mikutano wa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dar es Salaam ambako walikuwa wakutane kwa majadiliano.
Sababu kubwa imetajwa ni wizara hiyo
kushindwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na kamati hiyo, ikiwemo
kukaidi amri ya Mahakama Kuu ya kutaka kuanza mara moja utekelezaji wa
tozo mpya kwenye Hifadhi za Taifa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu, ya Maliasili na Utalii, James Lembeli alitoa uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam wakati kamati hiyo ilipokutana na wizara hiyo chini ya Waziri wake Lazaro Nyalandu ambaye alikiri kuwapo kwa tatizo katika ripoti huku akiahidi kufanyia kazi.
“Hatuwezi
kupitia bajeti hii, kwa sababu maagizo tuliyotoa awali hayajatekelezwa,
sasa tuna uhakika gani kama tukipitia hii bajeti yao ya mwaka 2015/16,
watakwenda kutekeleza tutakachoagiza?” Lembeli.
Alisema kimsingi, wizara hiyo imekwenda
kinyume na makubaliano yao na kwamba ni vyema wizara hiyo ikaenda
kujipanga na kufanya marekebisho ya maagizo yaliyotolewa kisha kurejea
kujadili bajeti hiyo.
Lembeli aliyataja maagizo yaliyotolewa
na kamati hiyo kuwa ni pamoja na utaratibu wa kiingilio kwenye hifadhi,
ambapo tozo iliyotakiwa ni kila mtalii anapoingia anachajiwa kiingilio
na akitoka na kutaka kuingia tena ni lazima alipe.
Waziri Nyalandu alikiri kuwepo na
matatizo kwenye maagizo ya ripoti hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi hiyo
jana na wataalamu wa wizara hiyo ili wahakikishe wanatatua changamoto
hizo, na leo wanaweza kutoa ripoti hiyo ili kamati ijadili bajeti yao.
HABARILEO
Mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Annuary Ally, raia wa nchi jirani ya Kenya ametiwa mbaroni na polisi baada ya kukutwa akivunja mashine ya kutolea fedha (ATM) ya Benki ya Barclays, Tawi la Stendi Kuu ya mabasi jijini hapa.
Kwa mujibu wa Ofisa Mikopo wa benki hiyo, Regina Kitali mtuhumiwa huyo alifika katika benki hiyo saa 5:15 asubuhi jana na kuingia katika mashine ya ATM kwa lengo la kutoa fedha.
Lakini baada ya dakika chache walisikia
mtikisiko usiokuwa wa kawaida katika mashine hiyo na kumlazimu mmoja wa
wafanyakazi wenzake kutoka nje kwenda kuangilia ni kitu gani.
Alisema baada ya mfanyakazi huyo kuingia
ndani ya chumba hicho alimkuta Ally akiwa anajaribu kung’oa mashine
hiyo ili apachike mashine maalumu aliyokuwa nayo kwa lengo la kuchukua
fedha zilizokuwa ndani ya ATM hiyo.
Alisema baada ya kuona hali hiyo
alimuuliza Ally kuna tatizo gani na kutaka kujua kama anahitaji msaada,
lakini mtuhumiwa huyo alimjibu kuwa anataka kutoa fedha na alipotakiwa
kupewa msaada alijifanya mbabe kwa kutaka kumtoa nje mfanyakazi huyo wa
benki.
“Kufuatia
hali hiyo mwenzetu alitoka nje mara moja na kubonyeza kengele ya
tahadhari kuomba msaada kutoka kampuni ya ulinzi inayolinda katika tawi
hili huku wengine tukipiga simu kuomba msaada wa polisi,” .
Kwa mujibu wa Regina wakati mtuhumiwa
akiendelea kung’oa mashine hiyo polisi wa kikosi cha FFU walifika eneo
hilo na ndipo mtuhumiwa alipotoka nje na kuwaponyoka polisi na kuanza
kukimbia kwa lengo la kutoroka.
Alisema walianza kupiga kelele za kuomba
msaada ambapo raia wema walijitokeza na kuanza kumkimbiza mtuhumiwa
huyo kwa kushirikana na polisi na kufanikiwa kumkamata katika eneo la
benki ya NBC tawi la Meru huku akiwa na vitambulisho vingi vya aina
mbalimbali pamoja na mashine hiyo maalumu.
Baada ya mtuhumiwa huyo kutiwa mbaroni
alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano zaidi ili sheria iweze
kuchukua mkondo wake.
Yote haya unayapata kupitia hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment