Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Euducation Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma na kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Wabunge wawili waliohama CCM hivi karibuni, James Lembeli na Ester
Bulaya wamepitishwa katika kura za maoni kuwania ubunge kupitia chama
chao kipya.
Wakati Lembeli akipitishwa kwa kura za kishindo kuwania ubunge katika
Jimbo la Kahama Mjini, Bulaya alishinda katika nafasi ya viti maalumu
baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha Jimbo la Bunda Mjini.
Wanasiasa hao sasa wanasubiri uteuzi wa Kamati Kuu ya Chadema utakaofanyika Agosti 5 na 6.
Katika uchaguzi huo wa juzi, mbunge huyo wa zamani wa Kahama
aliwabwaga wenzake 13 aliogombea nao akipata kura 168 kati ya 262
zilizopigwa, akifuatiwa na John Katibu aliyepata kura 45, Peter Shita
(17) na Emmanuel Madoshi aliyepata kura 10.
Wengine ni Muta Nyerere (4), Felician Maige (4), Zacharia Obadia (3),
Tadeo Mwati (2), Arnold Mtajwaka (2), Prosper Denga (2), Deusdedit
Madinda (1), Reuben Macheyeki (1). Victor Mbwana na Richard Makingi
waliambulia patupu. Katika uchaguzi wa viti maalumu, Winfrida Mwinula
alishinda kwa kura 34 akifuatiwa na Salome Makamba aliyepata kura 30.
Kama isingekuwa ni kura za maoni za viti maalumu zilizomfuta machozi,
Bulaya alikuwa tayari ametupwa nje baada ya kuanguka katika Jimbo la
Bunda Mjini.
Bulaya aliyekuwa miongoni mwa makada saba wa chama hicho waliokuwa
wanawania kuliwakilisha jimbo hilo, alipata kura 37 kati ya 182
zilizopigwa akiwa nyuma ya Pius Masururi aliyeibuka mshindi kwa kura 65
na Magembe Makoye aliyepata kura 40.
Baadaye katika mkutano wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha),
uliofanyika baadaye usiku, Bulaya alipata kura 71 kati ya 110
zilizopigwa na kuwabwaga Godliver Masamaki aliyepata kura 31, Joyce
Sokombi (4), Minza Shani (3), Dk Jane Nyamsenda (1) na Alice Wandya
aliyeambulia patupu.
Awali, Bulaya alikwaa kisiki baada ya jina lake kuwa miongoni mwa
waliokatwa na kamati ya utendaji inayosimamia majimbo hayo wakidaiwa ni
wageni katika chama; wapenda fujo na matabaka, akiwa pamoja na Chacha
Nyamhanga, Sulemani Daudi lakini walirudishwa kundini baada ya kikao cha
viongozi na watiania.
Katika Jimbo la Bunda Vijijini, Sulemani Daudi aliibuka mshindi kwa
kura 84 kati ya 127 zilizopigwana kuwashinda John Masenza aliyepata kura
14, Dk Lucas Webiro (11), Frank Mongateko (8), Edgar Chibura (5) na
Mathias Bandio aliyepata kura mo
MWANANCHI
Tume ya Uchaguzi (NEC) leo imetangaza kuongeza siku nne zaidi za
uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia teknolojia ya BVR baada ya idadi
kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam kuitikia wito wa zoezi hilo.
Awali zoezi hilo lilikuwa likamilike kesho, Julai 31, lakini sasa
litaendelea hadi Agosti 4, mwaka huu ili kukabiliana na idadi kubwa ya
watu waliojitokeza kujiandikisha.
Kwa mujibu wa chombo hicho chenye mamlaka ya kusimamia shughuli zote
za uchaguzi nchini, hadi jana, zaidi ya wakazi 1,000,000 walikuwa
wamekwishaandikishwa jijini Dar es Salaam.
Ikizingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Nec
inatarajia kuandikisha jumla ya wakazi zaidi ya 2.8 milioni wa jiji hilo
lenye idadi kubwa ya watu nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, hadi sasa jumla
ya zaidi ya watu 18 milioni wamekwishajiandikisha wakati tume ilitarajia
kuandikisha watu kati ya 22 milioni na 23 milioni.
NIPASHE
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inatarajia
kuanza kuwasaka viongozi wa umma waliotumia nafasi zao vibaya ikiwamo
kuiba na kujilimbikizia mali ndani na nje ya nchi.
Viongozi hao watasakwa na Takukuru kupitia kitengo maalum
kilichoanzishwa mwaka jana ambacho kimeanza kupewa mafunzo nchini
Uingereza.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah (pichani), aliyasema
hayo jijini Dar es Salaam juzi alipokuwa akijibu baadhi ya maswali ya
waandishi wa habari.
Dk. Hoseah aliyasema hayo muda mfupi baada ya kufungua mafunzo ya
watumishi wa Takukuru ambao wapo katika kitengo hicho ili kuwajengea
mbinu na uwezo wa kufanya uchunguzi dhidi ya viongozi walioiba na
kujilimbikizia mali.
Alisema kitengo hicho cha Takukuru pia kitakuwa na kazi ya kupambana
na masuala ya utakatishaji wa fedha haramu kwa kuwa tatizo hilo linazidi
kukua hapa nchini.
Aliongeza kuwa kitengo hicho kilianzishwa rasmi mwaka jana, lakini
hakikuanza kazi yake kutokana na kuchelewa kupatikana mtalaam wa kutoa
mafunzo kwa watumishi hao.
”Tumejizatiti kukabiliana na viongozi wa umma waliojilimbikizia mali
kwa kutumia watalaam wetu ambao wanapatiwa mafunzo,” alisema.
Dk. Hoseah alisema huu ni mwanzo na kwamba watahakikisha wanafanya
kazi vizuri ili kuwabaini watu walioiba na kujilimbilikizia mali huku
akisema kwamba sheria ni msemeno
Kuhusu wanasiasa wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa hususan
katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, Dk. Hoseah alisema mtu
yeyote asithubutu kufanya hivyo kwa kuwa Takukuru imesambaa kila wilaya
na kwamba watakamatwa.
”Hawa wagombea wasifanye mchezo mchafu, ninawaonya kwa kuwa tutawakamata popote walipo,” alisisitiza.
Aliwaonya wanasiasa wanapita maeneo mbalimbali na kuanza kuchonga
barabara na kutoa zawadi nyingine kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa na
Takukuru itawashughulikia.
Aliongeza kuwa mtu yeyote atakayepindisha sheria kwamba Takukuru ipo
macho muda wote na itawamulika wanasiasa ama wapambe wao ambao watataka
kuwahonga wananchi kuwashawishi wawapigie kura.
Hata hivyo, kauli ya Dk. Hoseah imekuwa ya kawaida kutolewa kwa kuwa
aliwahi kutangaza vita na wala rushwa wakubwa hapa nchini huku akiahidi
kuwaburuza mahakamani, lakini mpaka leo hakufanya hivyo.
NIPASHE
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amekanusha kumshushia
kipigo Dk. Joseph Chilongani, ambaye ni mgombea mwenzake katika mchakato
wa Chama Cha mapinduzi (CCM), kupata mgombea ubunge Jimbo la Kongwa.
Awali ilidaiwa kuwa Jumatatu jioni Ndugai, alitumia fimbo kumpiga Dk.
Chilongani, ambaye alipoteza fahamu kabla ya kupelekwa hospitali ya
wilaya hiyo, ambako aliendelea na matibabu mpaka jana aliporuhusiwa.
Mganga Mkuu wa Wilaya, Festo Mapunda, alilieleza NIPASHE jana kuwa walimruhusu kutokana na hali yake kiafya kuwa nzuri.
Naye Naibu Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, hakuwa tayari kueleza ikiwa
mpaka jana alikuwa amepokea taarifa rasmi ya tukio hilo kutoka kwa
walalamikaji badala yake alisema Dk. Chilongani, jana aliendelea na
kufanya kampeni kama kawaida.
Madai dhidi ya Ndugai yalielezwa na Dk. Chilongani, kuwa sababu ya
mtafaruku huo ilikuwa mzozo uliyoibuka kati ya Ndugai na mgombea
mwingine, Simon Ngatunga, na baadaye Ndugai kumtuhumu Dk.
Chilongani kuwa alikuwa akitumia simu yake ya kiganjani, kumrekodi
video ili kusambaza mitandaoni. Hata hivyo Ndugai alisema jana kuwa
miongoni mwa wagombea tisa wanaowania nafasi hiyo, baadhi wamepandikizwa
kwa lengo la kufanyia fujo.
“Tangu tuanze kampeni, wagombea mapandikizi wanafanya kazi ya
kunitukana na kunidhalilisha kila tunakokwenda, mmoja ananiporomoshea
matuzi ikitokea nikajibu, wanakuwa wameshapanga mmoja wao wa kunirekodi
ili wazidi kunidhalilisha mitandaoni,” alieleza Ndugai
Alisema tukio la Jumatatu, wakiwa kwenye mkutano wa hadhara Ngatunga,
alimtukana matusi ya nguoni na kusababisha mzozo kati yao, wakati watu
wakiendelea kumsihi ampuuze yule kijana huyo akagundua Dk. Chilongani
akitumia simu yake kumrekodi.
“Nilishamuonya mara kadhaa aache kujifanya mwandishi wa habari, kwa
kuachukua video tena akinilenga mimi tu, lakini hakusikia nilichofanya
niliigonga ile simu aliyokuwa akiitumia kuchukua video,” Ndugai alisema.
“Nikaigonga nikimwambia hebu usiendelee kunichukua video na kikamera
chako hicho simu ikaanguka chini, nikashangaa kuona na yeye akijiangusha
chini kama wachezaji wa mpira wa miguu, ambao hujiangusha kwa lengo la
kusingizia wamefanyiwa fujo ili wenzao wapewe kadi nyekundu.”
Kwa mujibu wa Ndugai, hakumpiga Dk. Chilongani wala hakujaribu kumpiga Ngatunga.
NIPASHE
Hofu imetanda ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na
wananchi kwa ujumla kutokana na kutoonekana kwa Katibu Mkuu wa chama
hicho, Dk. Willibrod Slaa, katika matukio mawili makubwa ya kisiasa
yanayohusu mustakabali wa chama hicho.
Dk. Slaa hakuonekana siku ya kihistoria Jumanne wiki hii, iliyokuwa
maalum kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kutangaza kujivua
uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga Chadema.
Kadhalika, Dk. Slaa hakuonekana jana makao makuu ya chama wakati
Lowassa alipofika kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia chama hicho
akitarajiwa kuwakilisha Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa),
katika hafla iliyotikisa jiji la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na
viongozi wa juu wa Chadema.
Hata hivyo, Dk. Slaa alihudhuria kikao cha dharura cha kamati kuu ya
Chadema Jumapili iliyopita ambacho kiliendelea hadi usiku wa manene na
hoja kuu ikiwa ni kujadiliana na Lowassa na kumpokea katika chama hicho.
Dk. Slaa alionekana katika baadhi ya picha zilizovuja kutoka katika
kikao hicho akiwa na viongozi waandamizi wa Chadema huku akijadili jambo
na Lowassa, ambaye katika siku za hivi karibuni ambekuwa gumzo kubwa
baada ya kubadili upepo wa siasa za Tanzania.
Tangu juzi kumekuwa na mijadala mirefu ndani ya mitandao ya kijamii,
juu ya aliko Dk. Slaa, wengine wakibashiri kuwa ameamua kuacha siasa.
Hata hivyo, Dk. Slaa mwenyewe hajawa radhi ama kupokea simu yake au
kujitokeza hadharani kujibu maswali ya umma juu ya kinachomsibu.
Mbali na kutokuonekana Chadema, Dk. Slaa pia hakuonekana kwenye
mkutano wa Ukawa, uliofanyika Jumatatu wiki hii makao makuu ya Chama cha
Wananchi (CUF), ambao wenyeviti wenza wa umoja huo walimkaribisha
Lowassa kujiunga nao.
Wakati wa Dk. Slaa akiadimika kwenye hadhara, viongozi waandamizi wa
Chadema kwa nyakati tofauti wameithibitishia NIPASHE kuwa kila kitu
“kimedhibitiwa” kuhusu tetesi kwamba kiongozi huyo amesusa.
“Sikiliza brother Dokta yuko freshi. Kila kitu kinakwenda kama
tulivyopanga. Hakuna ukweli wa lolote juu ya madai eti Dokta anakwenda
CCM,” kilisema chanzo chetu kilichoomba kutotajwa kwa sasa.
Wakati hali ikiwa hivyo, kuna taarifa kwamba Dk. Slaa anashinikizwa
sana na watu wa ndani ya familia yake ambao wanadaiwa kusumbuliwa zaidi
na ubinafsi, hasa baada ya mabadiliko ya kisiasa ambayo yamekikumba
chama hicho kufuatia kujiunga kwa Lowassa.
Watu hao wa ndani wa familia ya Dk. Slaa wanadaiwa kuwa walikuwa
wamejiandaa kuwa sehemu ya harakati za katibu mkuu huyo kuwania tena
urais mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2010.
“Sisi tunawaza jinsi ya kuivunjavunja CCM, lakini wapo watu wanawaza jinsi ya kuwa sijui nini sijui nani?
Hapa tunatafuta njia ya kuing’oa CCM hata kama ni kwa kutumia nguvu ya shetani,” alisema kiongozi mmoja wa Chadema.
Lowassa aliamua kujiunga Chadema baada ya kuchoshwa na siasa
zilizojaa chuki za kumzuia kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kusaka
tiketi ya kuwania urais kupitia CCM.
Katika hatua nyingine, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu,
aliliambia NIPASHE kwamba, Dk. Slaa alishiriki vikao vyote muhimu
vilivyoafiki, Lowassa kujiunga na chama hicho.
“Jana (juzi) usiku nilikuwa naye na wiki hii alishirika kikao cha kamati kuu ambacho mliona picha kwenye mitandao,” alisema.
Alipoulizwa alipo, Dk. Slaa, Lissu hakutoa majibu ya moja kwa moja
zaidi ya kusema kwamba akiwapo mwenyekiti kwenye kikao chochote inatosha
na siyo lazima, viongozi wote wa kitaifa wawepo.
Kuhusu Naibu Katibu wa Chadema, Tanzania Bara, John Mnyika na yeye
kutoonekana katika mikutano hiyo, alijibu kwa kifupi kwamba anaumwa.
Licha ya kutafutwa mara kadhaa kupitia simu yake ya mkononi juzi na
jana, Dk. Slaa hakupatikana badala yake mtu mmoja mwanamke alipokea na
kusema mpigaji amekosea namba.
Alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno ili aeleze kilichomsibu kushindwa
kuhudhuria matukio muhimu ya kumkaribisha Lowassa pia hakujibu.
NIPASHE
Mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa
Ujenzi, Dk. John Magufuli (pichani), ameiomba serikali kuendelea
kujenga barabara ya lami awamu ya pili hadi makao makuu ya Wilaya ya
Simanjiro toka KIA, huku akiwataka Watanzania kukataa watu
wanaowatenganisha kwa misingi ya ukabili, dini na vyama vya siasa.
Alitoa wito huo jana wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi kwa
ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ya kilomita 26 toka KIA hadi
Mererani, Manyara iliyohudhuriwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Bilal.
Alisema ni vizuri Watanzania wakaendeleza na kuwaogopa baadhi ya watu
wanaotaka kuwatenganisha kwa misingi ya vyama, ukabila na udini, kwani
hakuna tija kwa Taifa.
“Haya maendeleo hayachagui ukabila, dini wala vyama vya siasa, ndio
sababu serikali inajenga barabara kila mahali bila kujali chama gani
kipo mahali hapo, hiyo ndiyo misingi tulionayo,” alisema.
Alimuomba Makamu wa Rais kuendeleza barabara hiyo hadi makao makuu ya
Simanjiro, katika awamu ya pili baada ya kumalizika awamu ya kwanza.
Dk. Magufuli alisema ujenzi wa barabara ya KIA hadi Mererani
amekabidhiwa mkandarasi China Hennan International Cooperation Group Co.
Ltd , ambaye alimtaka kuikamilisha kwa wakati.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo utagharimu Sh. bilioni 32.2 na
kumtaka mkandarasi huyo kuajiri vijana wa eneo hilo ili nao wanufaike na
matunda ya miradi ya eneo lao.
Alisema hadi sasa serikali inaendelea na ujenzi wa barabara za lami
kilomita. zaidi ya 17,000 kati ya hizo 5,500 zimekamilika kwa kiwango
cha lami, jambo ambalo ni la kupongezwa na kila mpenda maendeleo.
Alisema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kutokana na kuwapo kwa
machimbo ya madini ya Tanzanite ambayo yanaingizia mapato makubwa
serikalini.
Dk. Bilal alimsifia Dk. Magufuli kuwa ni jembe na anastahili
kupeperusha bendera ya urais ya CCM, kutokana na kazi alizofanya bila
kutetereka.
Aliwaomba wananchi kuacha kuhujumu mradi huo kwa kuiba vifaa, badala yake wavilinde ili kumpa moyo mkandarasi.
“Lakini nimepokea ombi la Dk. Magufuli la kutaka barabara iendelee
awamu ya pili hadi makao makuu ya wilaya na itakuwa hivyo, pia
tutafikiria kuyaleta maji eneo hili haraka iwezekanavyo,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick
Mfugale, alisema barabara hiyo itakuwa na vituo vya mabasi vitano na
madaraja matano na inakadiriwa kudumu kwa miaka 20.’
MTANZANIA
Idara ya uhamiaji nchini imesema inawashikilia wahamiaji haramu 2,048
kutoka nchi mbalimbali kwa tuhuma za kujiandikisha kwenye Daftari la
Kudumu la Wapigakura.
Naibu kamishna wa uhamiaji na msemaji mkuu wa idara hiyo, Abbas Mussa
alisema jana kuwa wahamiaji hao wanatoka nchi za Kenya, Burundi na
Uganda.
Alisema walikamatwa katika mikoa 14 wakijifanya ni Watanzania, lakini
ilibainika kuwa siyo raia baada ya idara hiyo kufanya uchunguzi kwenye
vituo vya uandikishaji.
“Baadhi yao tumewafikisha mahakamani, lakini wengine bado uchunguzi
unaendelea na wakibainika nao watachukuliwa hatua,” alisema Mussa.
Aliongeza kuwa wengi ya wahamiaji hao walifika mikoa ya Kagera, Mara,
Tanga, Kigoma, Rukwa, Kilimanjaro, Ruvuma, Geita, Shinyanga, Mtwara,
Pwani, Mbeya, Morogoro na Dar es Salaam.
“Inasikitisha sana, kwani baadhi ya waliokamatwa walishajiandikisha na kupewa vitambulisho kama raia wa Tanzania,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, Idara imeamua kuongeza maofisa katika vituo ili kuendelea kuwabaini wahamiaji hao.
Mussa aliwataka wananchi kutoa taarifa mara wanapobaini watu ambao siyo raia wanajiandikisha.
Aliongeza kuwa maombi ya hati za kusafiria yameongezeka maradufu
kutoka hati 4,938 Julai 2014 hadi 8,703 Julai 2015 kwa upande wa Bara na
kutoka hati 588 Julai 2014 hadi hati 1,028 Juni 2015 kwa upande wa
Zanzibar.
Alisema idara inawataarifu wananchi kuwa siyo lazima kubadilisha hati
inapokwisha muda wake, badala yake mmiliki anaweza kubadili na kupatiwa
nyingine wakati wowote atakapokuwa akisafiri.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog