SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572
MWANAMKE 12
ILIPOISHIA
Msichana huyo aliyekuwa
ameweka begani mkoba wa rangi ya samli, alitoka kwenye mabenchi ya kukalia
mahakamani akaongozwa na polisi kulekea sehemu ya kulipia pesa.
Wakati akitembea watu wote
walikuwa wamegeuza uso wakimtazama. Pengine ni mimi peke yangu niliyejua kuwa
hakuwa binaadamu, bali alikuwa jini aliyekuwa akijigeuza binaadamu.
Mama yangu na kaka yangu
ambao walikuwepo hapo mahakamani wakiwa wameketi katika safu za mbele pia
walikuwa wamepigwa na butwaa wakimtazama yule msichaana bila kumuelewa.
Polisi mwingine alinishusha
mimi kizimbani na kunipeleka pale mahali ambapo Zena alitakiwa kunilipia faini
na gharama za shirika la umeme.
Kitendo kile cha Zena
kilikuwa kimenishitua na kunishangaza sana.
Kwanza sikuwa nikijua kwamba alikuwepo pale mahakamani na kama
alikuwepo sikujua alijuaje kuwa nilikuwa na kesi na kwamba siku ile ningetakiwa
kulipa pesa hizo.
Nikasimamishwa karibu naye.
Alikuwa amevaa baibui la kiiran lililonakishiwa mistari ya rangi ya samli.
Alikuwa amejitia manukato yaliyokuwa yakisikika. Wakati ameuweka mkoba wake juu
ya meza na kufungua zipu nilimuona kama adui
ambaye ghafla amegeuka na kuwa mkombozi wangu.
Siku za nyuma nilikuwa
nikijiambia nitakapomuona popote nitamkimbia. Lakini siku ile sikuweza
kumkimbia kwani yeye sasa alikuwa kama
kimbilio langu.
Baada ya kufungua mkoba wake
alitia mkono ndani ya mkoba huo na kutoa mabunda ya noti nyekundu na kuyaweka
juu ya meza. Nilihesabu jumla ya mabunda ishirini na moja ambayo aliyatoa.
“Hizo hapo shilingi milioni
ishirini na moja. Milioni sita za faini na shilingi milioni kumi na tano za
shirika la umeme” akasema.
Pesa hizo zilihesabiwa na
kuthibitishwa kuwa zilikuwa ni kiasi kilichotakiwa.
SASA ENDELEA
Pamoja na pesa hizo kulipwa,
utaratibu wa kuachiwa kwangu ulichukua karibu saa nzima. Wakati natoka katika
jengo la mahakama sasa nikiwa huru nilikuwa nimefuatana na Zena. Mama yangu na
kaka yangu walikuwa nyuma. Bado walikuwa hawajui yule msichana alikuwa nani.
Tulipotoka nje ya mahakama
Zena akaniambia.
“Ningependa nikutane na wewe
leo saa kumi na moja jioni katika bustani ya Uhuru Park”
Wakati ule nilijihisi kuwa
mdogo kama piritoni, nikamwambia.
“Sawa”
“Timiza ahadi”
“Nitatimiza’
“Sawa. Mimi nakwenda zangu”
Zena akaondoka na kuniacha.
Mama na kaka yangu wakafika nilipokuwa nimesimama.
“Yule msichana ni nani?” kaka
akaniuliza.
Zena alikuwa ameshakata kona na kutupotea.
“Yule si ndiye msichana
aniliyewambia”
“Yupi?”
“Si ndiye yule jini mwenyewe
aliyenipeleka kule Mikanjuni siku ile”
Mama na kaka walishituka.
“Kumbe ndiye yule!” Kaka
akasema kwa mshangao.
“Sasa mbona amekulipia pesa?’
Mama akaniuliza.
“Sijui mwenyewe”
“Alikuwa anakueleza nini?”
aliuliza kaka.
“Ameniambia nikutane naye
Bustani ya Uhuru Park leo saa kumi na moja jioni”
Nilipowambia hivyo mama yangu
aliguna.
“Mkutane kwa ajili gani?”
akaniuliza.
Nikabetua mabega yangu.
“Sijui. Ameniambia hivyo tu”
“Na wewe umemjibu nini?” Kaka
akaniuliza.
“Nimemwambia nitakwenda
kukutana naye”
“Usiende peke yako,
tutakwenda sote. Mimi pia nataka kumuona” Kaka akasema.
“Ni vizuri mwende nyote,
asiende peke yake” Mama alisisitiza.
“Sawa. Tutakwenda pamoja”
nikawambia.
Baada ya hapo tukaondoka.
Tulikwenda kupanda teksi tukarudi nyumbani kwa mama.
Hatua ile ya kuachiwa huru na
mahakama ilinifariji sana
kwani tayari nilikuwa ninakwenda kufungwa. Yule mwanamke wa kijini ambaye ndiye
aliyenitia katika tatizo lililonikabili aliibuka kama
mkombozi wangu bila mimi kutarajia.
Nilipata wasiwasi
aliponiambia nikutane naye katika bustani ya uhuru. Nikawa najiuliza alikuwa
anataka nini tena wakati ile kesi ilikuwa imeshakwisha. Na kama
ni uhusiano wetu ulikuwa haupo tena.
Kusema kweli sikupenda tena
kuwa karibu na yule msichana. Kitendo cha kumkubalia kukutana naye kilitokana
na hofu tu.
Nilishindwa kumkatalia. Angeweza kunizushia tatizo jingine.
Nilikaa kwa mama hadi saa
kumi na moja jioni. Kaka aliondoka tangu saa tisa akarudi dakika chache kabla
ya saa kumi na moja.
“Naona muda umewadia”
akaniambia nakuongeza.
“Twenzetu”
“Sawa. Twende”
Tukamuaga mama na kuondoka.
Tulipanda tena teksi ikatupeleka Bustani ya Uhuru ambayo ilikuwa karibu na
baharini. Kutoka barabara ya tisa hadi mahali hapo ulikuwa mwendo wa karibu
kilometa mbili.
Bustani ya Uhuru ilikuwa
katika eneo la mijini kabisa. Enzi hizo tulizoea kukuita uzunguni.
Ilikuwa bustani nzuri ya kupendeza yenye eneo la mita
kumi hivi za mraba. Mbali ya kuzungushiwa ukuta mfupi ilikuwa na mti ya
vivuli na viti vilivyotengezwa kwa saruji.
Mida kama
ile ya jioni watu mbalimbali hupenda kufika katika bustani hiyo kupunga upepo
au kupumzika.
Tulipofika, tayari watu
walikuwa wakionekana wamejilisi katika kila kona. Tulipata kiti kilichokuwa
kitupu chini ya mti mmoja tukakaa.
Niliangaza macho yangu kila
upande kuona kama yule mwanamke ameshafika lakini sikumuona. Walikuwepo watu wengine tu.
“Naona bado hajafika”
Nikamwambia kaka ambaye alitazama saa yake.
“Saa kumi na moja bado”
akaniambia.
“Bado dakika ngapi?’
“Bado dakika mbili”
“Basi atafika sasa hivi”
Tukasubiri.
Saa kumi na moja ikafika.
Hatukuona mtu. Dakika zikaendelea kwenda. Kila wakati kaka yangu alikuwa akitazama saa yake.
Haukupita muda mrefu akaniambia.
“Sasa ni saa kumi na moja na
nusu”
Na mimi nikatazama saa yangu.
Ni kweli ilikuwa saa kumi na moja na nusu.
Nikaangaza macho yangu kila
upande.
“Mbona hatokei?” nikajiuliza
lakini kwa sauti iliyosikika.
“Labda ameghairi”
“Yeye alinisisitiza kwamba nisivunje ahadi”
“Basi tuendelee kusubiri,
anaweza kutokea”
Tukaendelea kusubiri hadi saa
kumi na mbili jioni.
“Sidhani kama atakuja tena”
Kaka akaniambia.
“Basi twenzetu”
“Twenzetu”
Tukanyanyuka.
“Ametupotezea muda wetu bure”
Kaka akasema.
“Nashukuru pia hivyo ambavyo
hakutokea’
Kaka akacheka.
“Kwanini useme hivyo?’
“Yule mwanamke mimi
nilishapanga nisikutane
naye tena!”
“Lakini ndiye aliyekuokoa”
“Kwani yale matatizo si
ameniletea yeye!”
Tulikuwa tumeshatokea
barabarani.
“Naona turudi kwa miguu tu”
nikamwambia kaka.
Tukarudi kwa miguu.
Tulipofika nyumbani kwa mama,
mama akatuuliza.
“Mlikutana naye?”
“Hakuja” nikamjibu.
“Tumekaa mpaka tumechoka”
Kaka akaongeza.
“Kwanini asije na alikwambia
mkutane hapo saa kumi na moja”
“Labda amebadili mawazo”
nikamwambia.
“Ndiyo vizuri”
TUNAPIGA STOP KWA LEO. Si
unajua huwezi kuupata utamu wote kwa siku moja! Hadithi ni ndefu halafu
inasisimua ile mbaya! Lakini yote haya ni kwa ajili ya kuwaburudisha wasomaji
wa blog yetu hii ya TANGA KUMEKUCHA! Kila unapokaa kumbuka. TANGA KUMEKUCHA! Si Tukutane tena kesho.
No comments:
Post a Comment