SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 15
ILIPOISHIA
Zena akacheka. Alipofanya
hivyo haiba ya uso wake ilibadilika na kuwa ya kupendeza zaidi.
“Uliniona katika umbo gani?”
akaniuliza.
“Mwili wako ulikuwa na
manyoya marefu na miguu yako ilikuwa na kwato kama
ya punda. Kwa kweli nilipatwa na uoga mkubwa”
“Ndiyo maana siku ile
uliponiona kule Mabanda ya Papa ukaongeza
mwendo mpaka ikatokea ile ajali?”
“Kumbe unajua. Ni kweli
niliongeza mwendo baada ya kukuona wewe”
Msichana akacheka tena.
“Hukupaswa kunikimbia. Iile
umbo uliloniona nalo nyumbani siku ile ndilo umbo langu kwa maana mimi si
binaadamu bali ni jini”
“Nilishafahamu kuwa wewe si
binaadamu. Binaadamu hawezi kuwa na umbo kama
lile”
“Nimefurahi kama umenielewa,
kwa hiyo usiniogope tena”
“Kukuogopa ni lazima kwa
sababu sijakuzoea”
“Taratibu
tu utanizoea. Mimi nimekuwa na wewe kwa miaka mingi bila wewe mwenyewe kujua”
“Umekuwa
na mimi kwa miaka mingi?”
“Ndiyo. Naweza kusema tangu ukiwa kijana
mdogo”
“Ulikuwa uko wapi?”
“Nilikuwa na wewe”
“Sijawahi kukuona”
SASA ENDELEA
“Ni kweli. Sikutaka unione
wala kujitambullisha kwako kwa sababu muda wa wewe kunitambua mimi ulikuwa
haujafika”
Nikaguna. Lakini niliguna
moyoni mwangu.
“Siku ile niliyokuazima
kitabu ndio siku ambayo nilipanga kujitokeza rasmi kwako”
Nikabaki kimya nikimsikiliza.
Maneno yake yalikuwa yameshitua akili yangu.
“Samahani kwa matatizo yote
yaliyokutokea ambayo kwa namna moja au nyingine niliyasababisha mimi. Haikuwa
kusudio langu kukusumbua bali nililazimika kufanya vile ili uweze kunitambua”
Zena aliendelea kuniambia.
“Umeniambia
kwamba wewe ni jini, ni jini wa aina gani na unaishi wapi?” nikamuuliza ili
niweze kumuelewa vizuri.
“Mimi ni jini wa ukoo wa Ummi
Subian, yaani nimechanganya kabila mbili, upande mmoja ni ruhani na upande
mwingine ni subian. Yaani ninatumia bara na pwani lakini zaidi mila zangu ni za
kipwani”
Nilidhani alikuwa amemaliza.
Akaendelea.
“Umeniuliza
ninaishi wapi. Kwetu ni Sham na kwa hapa Afrika Mashariki maskani zangu zipo
katika eneo lote hili la pwani ya Afrika Mashariki kuanzia Somalia, Kenya
na Tanzania.
“Niliwahi kukwambia jina
langu ninaitwa Zena. Baba yangu anaitwa Jabalkeys na mama yangu ni Ummi Mariam.
Huko ujinini mimi natambulika kama Zainush
binti Jabalkeys”
Alipofika hapo Zena
alinitazama akaniuliza.
“Umenielewa
vizuri?”
“Nimekuelewa” nikamjibu.
“Kuna kitu kimoja nataka
nikwambie” akaniambia.
“Niambie”
“Nimekuchunuka na ninataka
uwe mume wangu. Ninakuahidi kuwa nitakupa utajiri”
Nikashituka.
“Kama
wewe ni jini, nitawezaje kuwa mume wako?” nikamuuliza.
“Majini huoana na binaadamu. Kama huamini nenda kwa bibi yako aliyemzaa baba yako,
muulize baada ya kuachika yeye mume wake alioa mke gani?”
“Una maana gani, una maana
kwamba babu yangu alioa jini?” nikamuuliza kwa mshangao.
“Nataka uende ukamuulize
yeye, akueleze”
“Sawa. Nitakwenda kumuuliza”
“Tutakutana lini tena?”
“Niambie wewe”
“Unadhani ni lini utakuwa na
jibu?”
“Labda keshokutwa”
“Basi nitakutafuta”:
“Sawa”
Zena akafungua mkoba wake.
Nilikuwa namtazama pembeni mwa macho yangu.
Nikaona akitoa kitita cha
noti nyekundu. Nilizikisia zilikuwa zaidi
shilingi milioni moja. Akanipa bila kuzihesabu.
“Chukua
hizo zitakusaidia” akaniambia.
“Asante
sana”
nikamwambia.
Zena akafunga mkoba wake na
kunitazama huku akitabasamu.
“Una kitu chochote unataka
kuniambia?” akaniuliza.
“Hapana, sina kitu cha
kukwambia”
“Basi tuagane uende zako na
mimi niende zangu”
“Mimi nashukuru tu kukutana
na wewe”
Huku tabasamu likiendelea
kutawala usoni kwake akaniambia.
“Asante”
Akanyanyuka.
“Kwaheri” akaniaga na
kuondoka.
Nikiwa bado nimekaa
nilimtazama wakati akienda zake. Alivuka viti kadhaa kabla ya kutokea kwenye
njia iliyokuwa ndani ya bustani. Kulikuwa na vijana wawili waliokuwa wamekaa
katika kiti kimoja nyuma yetu. Walikuwa na baskeli waliyokuwa wameiegesha mbele
ya kiti walichokuwa wamekaa.
Walipomuona yule msichana
Zena anaondoka waliinuka wakapakiana kwenye baskeli na kumfuata.
Wakati wanampita, yule kijana
aliyekuwa amepakiwa nyuma aliuvuta mkoba wa Zena akauchomoa na kuuchukua. Zena
alipogutuka vijana hao walimpita na baskeli na kukimbia.
Zena akabaki amesimama akiwatazama vijana hao kwa hasira. Mkoba wake
ulikuwa umekwenda!
Nikanyanyuka kwenye kiti na
kumfuata haraka. Wale vijana walikuwa wameshafika barabarani wakaelekea upande
wa Chumbageni kwa mwendo wa kasi.
“Wamepora mkoba wako?”
nikamuuliza.
“Basi waache tu, huwezi
kuwafanya kitu” Zena alisema. Sauti yake ilikuwa tulivu lakini ilionesha
ghadhabu.
“Wale vijana walikuwa wamekaa
muda mrefu nyuma yetu, kumbe walikuwa na lao wanalongojea”
“Hakuna tatizo”
Nilikuwa nafuatana naye
kuelekea kwenye lango la kutokea kwenye bustani hiyo.
“Dah!....”
“Usijali, waache tu. Mimi
nakwenda zangu”
Ile teksi iliyomleta Zena
ikatokea tena na kusimama mahali pale pale pa mwanzo.
Zena akaifuata na kujipakia.
Teksi ikaondoka. Niliisindikiza kwa macho hadi ilipokata kona.
“Majini pia wanapanda teksi!”
nikajisemea moyoni mwangu kisha
nikaanza kutembea kwa miguu kurudi nyumbani.
MAMBO HAYO!!!! HEBU TUFANYE
SUBIRA HADI HAPO KESHO. TUOMBE UHAI TU, TUAMKE SALAMA
No comments:
Post a Comment