SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 9
ILIPOISHIA
“Kulikuwa na pikipiki moja
inakuja kutoka barabara ya Taifa. Ile pikipiki ilitakiwa isimame kwenye
mzunguko wa barabara nne uliopo pale lakini haikusimama”
“Baada ya hapo nini
kilitokea?’
“Kulikuwa na gari aina ya Toyota
Land Cruicer likitokea
Gofu, lilikuwa linapita kwenye ule mzunguko likalazimika kuikwepa ile pikipiki.
Katika kuikwepa pikipiki, gari hilo
lilikwenda kugonga nguzo ya umeme”
“Baada ya kugonga nguzo ya
umeme lilikwenda wapi?”
“Liliingia kwenye mfereji”
“Ni athari gani ilitokea
baada ya nguzo ya umeme kugongwa?”
“Kwanza
nguzo yenyewe ilivunjika halafu baadhi ya nyaya zilikatika na nyingine zilitoa
cheche za moto hali iliyosababisha mfadhaiko mkubwa”
“Wakati tukio hilo linatokea, mwenye
pikipiki alisimama”
“Hapana, hakusimama. Alipita
moja kwa moja na kuendelea na safari yake”
“Wewe uliiona hiyo pikipiki?’
“Ndiyo niliiona”
“Ilikuwa
ni aina gani”
“Kama
sikosei ilikuwa aina ya Honda ya rangi nyeusi”
“Namba
yake ya usajili
uliiona”
“Niliiona”
Akaitaja. Ilikuwa
ndio namba ya pikipiki yangu.
SASA ENDELEA
“Je aliyekuwa akindesha
pikipiki hiyo ukimuona unaweza kumtambua?”
“Naweza kumtambua”
“Yuko hapa mahakamani?”
“Ndiyo yupo. Ni yule pale”
Akaninyooshea kidole mimi.
“Asante
sana”
Baada ya mtu huyo kumaliza
kutoa ushahidi wake, niliambiwa kama nina
maswali nimuulize.
“Unajua hapa Tanga kuna
pikipiki ngapi za aina ya Honda?” nikamuuliza.
“Ziko nyingi”
“Ambazo ni rangi nyeusi kama pikipiki yangu?’
“Ziko nyingi”
“Unawezaje kuzitofautisha?”
“Kivipi?”
“Nina maana una uhakika gani kama pikipiki ulioiona ni yangu na si ya mtu mwingine?’
“Wewe unapita pale kila siku
na pikipiki yako. Pikipiki yako ninaijua na wewe mwenyewe ninakujua”
“Je nikikwambia kwamba sikuwa
mimi bali alikuwa mtu mwingine utakataa?’
“Ndiyo nitakataa”
“Sasa mimi nakwambia sikuwa
mimi?”
“Alikuwa nani?”
“Sijui”
Yule mtu akanyamaza.
Mwendesha Mashitaka akasimama
na kumuuliza yule mtu.
“Mtu uliyemuona siku hiyo
ndiye huyo hapo au siye?”
“Ndiye yeye” shahidi akajibu.
Mwendesha Mashitaka kakaa.
Kesi ikaahirishwa kwa juma
moja.
Kipindi kile cha kesi ile
kilinifanya niwe mnyonge sana.
Nilijiuliza kama nitatakiwa nilipe faini au
fidia ya uharibifu uliotokea, nitalipa nini? Kwa vile uharibifu ulikuwa mkubwa
niliamni fidia yake pia itakuwa kubwa. Nilijiuliza nitapata wapi pesa za kulipa
fidia hiyo ambayo kwa vyovyote vile ingekuwa ni mamilioni ya pesa.
Kila wakati nilikuwa
nikimlaani yule msichana wa kijini aliyenisababishia matatizo yale. Niliomba nisikutane naye tena
milele na milele.
Siku ya kesi ilipowadia
nillifika mahakamani. Upande wa Mashitaka uliendelea kupeleka mashahidi. Safari
hii aliyesimamishwa kizimbani kutoa ushahidi alikuwa polisi wa usalama
barabarani aliyepima ile ajali iliyotokea.
Alitoa vielelezo yake ikiwa
ni pamoja na ramani ya ajali aliyokuwa ameichora.
Ramani hiyo ilionesha kuwa
nilifanya kosa la kutosimama katika alama ya
L iliyokuwa kwenye mzunguko wa barabara nne uliopo eneo la Mabanda ya
Papa.
Ramani hiyo iliendelea
kuonesha kwamba wakati nafanya kosa hilo
kulikuwa na gari aina ya Toyota
Land Cruiser likitokea upande wangu wa
kulia ambalo nilipaswa kulipisha lipite lakini sikufanya hivyo.
Hivyo gari hilo lililazimika kunikwepa na kwenda kugonga
nguzo ya umeme inayomilikiwa na shirika la umeme na kuivunja.
Katika ushidi wake polisi
huyo alieleza kwamba nguzo ya umeme niliyoivunja pamoja na nyaya zilizokatika
zina thamani ya shilingi milioni kumi.
Akaeleza kwamba ili kurudisha
mfumo wa upatikanaji umeme katika eneo hilo
shirika la umeme litalazimika kutoa shilingi milioni kumi na tatu ikiwa ni
pamoja na gharama ya ufundi.
“Pesa hizo zitapaswa zilipwe
na mshitakiwa kwa sababu alifanya kosa hilo
kwa uzembe na kutozingatia sheria za barabarani” akasema.
Hapo ndipo moyo wangu
ulipotaharuki. Nitazitoa wapi shilingi milioni kumi na tatu za kuwalipa shirika
la umeme? Nikajiuliza.
Polisi huyo alipomaliza kutoa
ushahidi wake, hakimu aliniambia kama nina
swali nimuulize.
Nilikuwa nimefadhaika sana kiasi kwamba sikuweza
kuuliza swali lolote lakini niliona kukaa kimya kutaionesha mahakama kuwa kweli
nilitenda kosa, nikamuuliza polisi huyo.
“Hiyo ramani uliyoitoa
aliichora nani?”
“Niliichora mimi”
“Unapochora ramani ya ajali kama ile unapata maelezo kutoka kwa nani?”
“Kutoka kwa wale wahusika wa
ajali na mashahidi”
“Kwa maoni yako mimi ni
muhusika wa ajali?’
“Ndiyo”
“Nilikuwepo wakati unachora
ramani hiyo?”
“Hukuwepo”
“Je niliweka saini yangu kuonesha
kuwa nimekubaliana na ulichokichora?”
“Saini yako haipo”
“Kwa maana hiyo ni kwamba ramani uliyochora sikubaliani nayo”
“Kwanini saini yake haipo?”
hakimu akamuuliza polisi huyo.
“Ni kwa sababu wakati
tunachora ramani, yeye mwenyewe hakuwepo” Polisi
huyo akajibu.
“Alikuwa wapi?”
“Alikuwa mafichoni, yaani
baada ya kusababisha ile ajali alikimbia. Tulimpata wakati tukiwa tumeshachora
ramani”
“Jibu umelisikia?” hakimu
akaniuliza.
“Nimelisikia lakini
halinihusu mheshimiwa, wananihusisha tu na hiyo ajali lakini sikuhusika mimi”
“Ushahidi umetolewa hapa kuwa
ni wewe” Polisi huyo aliyekuwa akitoa ushahidi
aliniambia.
“Sikubaliani na ushahidi huo”
nikamjibu.
“Wewe mwenyewe umeonekana na
kutambuliwa, pikipiki yako imeonekana na kutambuliwa na namba ya usajili ya
pikipiki yako pia imeonekana na kutambuliwa, sasa unakataa nini?”
“Kwa vile sikuhusika lazima
nikatae”
“Una swali jingine” hakimu
akanuiliza.
“Sina swali jingine”
nikamjibu.
Hakimu aliandika kisha akaamuru aitwe
shahidi mwingine.
Shahidi aliyeitwa baada ya
hapo alikuwa afisa wa shirika la umeume.
Ushahidi alioutoa ulihusu
uharibifu uliosababishwa na ajali hiyo. Alitoa takwimu za gharama kama alizozitoa shahidi aliyemaliza kutoa ushahidi wake.
Alipomaliza kutoa ushahidi huo nilimuuliza.
“Ulimuona mtu aliyesababisha
ajali hiyo?’
“Sikumuona” akajibu. Ndilo
jibu nililokuwa nalitaka.
“Kwa hiyo hujui ni nani
aliyesababisha ajali hiyo?”
“Nimeambiwa kuwa ni wewe”
“Nimeshasema kuwa sikuwa
mimi”
“Kama
si wewe kwanini walikukamata?”
“Walinikamata kwa makosa. Wao
ni binaadamu wanaweza kukosea”
Jibu hilo
liliwafanya baadhi ya watu waliokuwa wakisikiliza shauri hilo kucheka kimya kimya.
“Mahakama ndio itajua kama ulikamatwa kwa makosa”
“Lakini kwa maoni yako kama mimi sikuhusika bado nitalazimika kulipia gharama
uliyoitaja?”
“Suala hilo tunaliachia mahakama”
“Sawa”
ITAENDELEA KESHO
No comments:
Post a Comment