SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 14
ILIPOISHIA
“Ameniambia hakutokea kwa
sababu nilikwenda pale nikiwa na wewe”
“Yaani alitaka uwe peke
yako?”
“Ndiyo hivyo”
“Kumbe alituona tuko wawili!”
“Bila shaka”
“Sasa amekwambiaje?”
“Ameniambia tukutane tena
kesho saa nne”
“Kwani anataka nini?”
“Sijajua”
“Sasa wewe umeamuaje?”
“Nataka ushauru wako”
“Mimi nakushauri nenda”
“Basi nitakwenda”
“Kwa sababu hujui anataka
kukwambia nini. Pengine anataka kukwambia kitu cha maana kwako”
“Ni kweli”
“Huwezi jua, anaweza kukupa
utajiri”
“Unasema kweli kaka?”
“Wewe nenda kamsikilize,
usiogope”
“Sawa. Nitakwenda”
Baada ya kuzungumza na kaka
kwa dakika kadhaa nikamuaga.
“Basi kaka mimi narudi
nyumbani”
SASA ENDELEA
“Acha nikusindikize”
Kaka akanisikindikiza hadi
eneo la stendi ya mabasi, tukaachana.
Siku iliyofuata nikajiandaa
kwenda kukutana na yule msichana. Nilipotoka nyumbani nilikwenda nyumbani kwa
mama. Nikamjulisha kwamba ndio ninakwenda kukutana na yule msichana wa kijini.
“Jana nilipokwambia uende ukakutane na
kaka yako ulikwenda?” Mama akaniuliza.
“Nilikwenda nikamjulisha
akaniambia niende nikakutane naye”
“Na wewe mwenyewe
umeridhika?”
“Sina la kufanya mama,
inabidi niende nikamsikilize”
“Basi omba Mungu. Mungu
atakusaidia”
“Sawa mama”
Saa tatu na nusu nikaondoka
nyumbani kwa mama. Kwa sababu ya kihoro nilichokuwa nacho hata chai sikuwahi
kunywa. Kusema kweli sikujisikia kunywa chai.
Nilipofika katika bustani ya
Uhuru ilikuwa saa nne kasoro dakika tano. Nikakaa mahali pale pale nilipokaa na
kaka jana yake.
SASA ENDELEA
Nikaanza kutupia macho watu
waliokuwa wakipita barabarani hasa wasichana nikitazamia ningemuona Zena akiwa
mmojawao.
Dakika zikandelea kupita.
Zena sikumuona. Mara kwa mara nilikuwa nikitazama saa yangu. Hakukuwa na siku
ambayo saa ilinishughulisha kama siku ile.
Kila baada ya muda mfupi nilikuwa
nilitazama saa.
Mpaka inafika saa nne kasoro
dakika moja niliinua uso wangu nikawa ninaangalia barabarani upande ambao nilitarajia
kuwa Zena angetokea. Niliangalia kwa shauku yenye hofu kwa kujua kuwa muda wowote ningemuona
Zena.
Kutoka saa nne kasoro dakika
moja nilianza kuhesabu sekunde kwani dakika hazikuwepo tena.
Nilianza kuhisi baridi ya hofu
ikininyemelea mwilini. Sikujua yule msichana atakapotokea atanieleza nini. Ile
picha ya kumuona siku ile akiwa na miguu ya kwato na mwili wenye manyoya kama wa shetani ilianza kunijia akilini mwangu. Picha
hiyo ndiyo iliyonitisha na kunikumbusha mkasa mzima ulionitokea siku ile.
Ghafla niliona teksi
ikisimama kando
ya barabara jirani na bustani ya uhuru. Ilikuwa
teksi ya rangi nyeupe na sikujua ni kwanini niliikodolea macho.
Mara nikamuona msichana
mrembo akishuka. Alikuwa amevaa dera la mikono mirefu lenye ushungi uliofinika
kichwa chake na kuteremka hadi usawa
wa kiuno chake.
Alikuwa amevaa miwani ya jua
iliyoficha uso wake lakini midomo yake iliyokolezwa rangi ya waridi ilitokeza
na kuonekana waziwazi.
Mara tu aliposhuka kwenye
teksi alianza kutembea kuelekea katika lango la bustani ya uhuru kwa hatua za taratibu.
Zilinichukua sekunde kama tano hivi kumtambua. Alikuwa ni Zena!
Ile akili yangu iliponiambia
kuwa ni Zena, moyo wangu ulipiga kwa nguvu mara moja kisha
ukatulia.
Nikaona waziwazi pumzi zangu zimebadilika. Nilikuwa ninahema kwa nguvu. Nikawa
nashindana na mapafu yangu kuyazuia ili nisionekane
kuwa ninapumua hivyo.
Zena alishaingia
kwenye eneo
la bustani, akawa anatembea kuelekea mahali nilipokuwa kwa mwendo ule
ule wa taratibu. Alionekana wazi kuwa mtu mwenye ahadi adhimu.
Wakati anazidi kunikaribia,
upande mmoja wa akili yangu ulishindwa kuamini kuwa yule msichana alikuwa ni
jini. Alikuwa mzuri sana.
“Asalaam alay kum”
akanisalimia aliponikaribia kabla ya kuketi kando yangu.
Hapo hapo niliskia harufu ya
manukato aliyokuwa amejitia na hewa ya mahali hapo ikawa ni ya mawaridi.
“Wa alayka salaam”
nikamuitikia huku nikijaribu kutabasamu ili kuficha fadhaa niliyokuwa nayo
usoni.
Alipoona ninatabasamu na yeye
akatabasamu.
“Ninaitwa Zena” akaniambia
ingawa sikuwa nimemuuliza jina.
Akaongeza. “Habari ya tangu
jana?”
“Nzuri. Sijui yako wewe”
“Mimi mzima. Tukikutana kama hivi hatuna budi kumshukuru Mungu”
“Ni kweli”
Msichana akajiweka sawa na
kuutoa mkoba wake uliokuwa umezibwa na ushungi wake aliokuwa amejitanda. Akaufungua
na kukitoa kile kitabu changu nilichomuazima siku ile.
“Nimekurudishia kitabu chako
ulichokuwa umeniazima” akaniambia huku akinipa kitabu hicho.
Wakati nakipokea akaniambia.
“Samahani kwa kukucheleweshea
kitabu chako”
“Bila samahani. Nilikuwa nimeshakisahau kutokana
na misuko suko”
“Pole”
“Asante”
Msichana akageukia upande
wangu. Ilikuwa vyema kuwa alivaa miwani,
vinginevyo angenipa wakati mgumu kutazamana naye.
“Ni kwaninini siku ile
uliondoka nyumbani bila kuniambia, ukaacha pikipiki yako na viatu
vyako?” akaniuliza.
“Siku ile nilitishika sana. Nilikuona katika
umbo tofauti kabisa!” nikamwambia.
Zena akacheka. Alipofanya
hivyo haiba ya uso wake ilibadilika na kuwa ya kupendeza zaidi.
“Uliniona katika umbo gani?”
akaniuliza.
“Mwili wako ulikuwa na
manyoya marefu na miguu yako ilikuwa na kwato kama
ya punda. Kwa kweli nilipatwa na uoga mkubwa”
“Ndiyo maana siku ile
uliponiona kule Mabanda ya Papa ukaongeza
mwendo mpaka ikatokea ile ajali?”
“Kumbe unajua. Ni kweli
niliongeza mwendo baada ya kukuona wewe”
Msichana akacheka tena.
“Hukupaswa kunikimbia. Iile
umbo uliloniona nalo nyumbani siku ile ndilo umbo langu kwa maana mimi si
binaadamu bali ni jini”
“Nilishafahamu kuwa wewe si
binaadamu. Binaadamu hawezi kuwa na umbo kama
lile”
“Nimefurahi kama umenielewa,
kwa hiyo usiniogope tena”
“Kukuogopa ni lazima kwa
sababu sijakuzoea”
“Taratibu
tu utanizoea. Mimi nimekuwa na wewe kwa miaka mingi bila wewe mwenyewe kujua”
“Umekuwa
na mimi kwa miaka mingi?”
“Ndiyo. Naweza kusema tangu ukiwa kijana
mdogo”
“Ulikuwa uko wapi?”
“Nilikuwa na wewe”
“Sijawahi kukuona”
JAMANI MMEYASIKIA MANENO
HAYO?! MWANAMKE WA KIJINI KAMHUSUDU BINAADAMU! MAKUBWA!!!! KWELI DUNIANI KUNA
MAMBO! SIJUI MAZUNGUMZO YAO
YATAENDELEAJE? HEBU TUKUTANE TENA HAPO KESHO. RAMADHANI KARIIM.
No comments:
Post a Comment