NILIJUA NIMEUA 5
ILIPOISHIA JANA
“Ni elfu sita”
“Punguza, fanya tano. Mimi ni
mteja wako wa kila siku”
“Haya nipe”
Mariam akafungua pochi na
kutoa noti ya shilingi elfu tano akanipa. Akafungua mlango wa teksi na kushuka.
Aliagana na mwenzake na
kwenda kubisha mlango wa nyumbani kwao. Nami nikaanza safari ya kuelekea Kange.
Nilipofika Kange Nilimuuliza
msichana anakwenda mtaa gani, akaniambia nikate kushoto. Nilipokata kushoto
akanielekeza mtaa ambao anaoishi.
Nilipofika katika mtaa huo
alinionyesha nyumba aliyotaka nimpeleke. Ilikuwa nyumba nzuri kuliko aliyokuwa
anaishi Mariam.
“Unanidai kiasi gani?”
Msichana akaniuliza niliposimamisha teksi.
“Nipe elfu kumi”
SASA ENDELEA
Msichana hakubishana.
Alifungua pochi yake akatoa noti ya shilingi elfu kumi na kunipa. Akafungua
mlango na kushuka.
Alikwenda kwenye baraza ya
ile nyumba na kupiga simu.
Nilimsikia akisema.
“Asiya nifungulie mlango”
Nikaiondoa teksi na kumuacha
hapo hapo.
Wakati narudi jijini nilikuta
gari limeegeshwa kando ya barabara. Taa zake za nyuma zilikuwa zinawaka. Wakati
nalikaribia gari hilo
niliona mtu aliyekuwa kando yake akinipungia mkono kunisimamisha.
Wazo nililolipata kwanza ni
kuwa gari hilo
lilikuwa limeharibika na kwamba mtu aliyekuwa akinipungia mkono ama alikuwa
anataka msaada au alikuwa anahitaji huduma ya teksi yangu.
Kwa vile nilikuwa kwenye
mwendo wa kasi nililipita gari hilo
na kwenda kusimama mbele. Hapo hapo mawazo yangu yakabadilika. Niliwaza kwamba
huenda gari hilo
liliegeshwa kwa hila lionekane limeharibika kumbe ni majambazi wanaosubiri
magari yasimame waanze kupora watu.
Nilikuwa nimechelewa
kufikiria hilo.
Nilikuwa nimeshasimamisha teksi na jamaa aliyenisimamisha alikuwa ameshafika
kwenye dirisha la teksi yangu!
Chini ya siti yangu ya
dereva, siku zote huweka parange (sime ya kimasai) kwa ajili ya kujihami endapo
kutatokea tatizo la kuvamiwa na mtu au watu wenye nia mbaya.
Kwa vile sikuwa na uhakika
kuwa mtu huyo aliyenisimamisha alikuwa na nia mbaya au nzuri, tayari
nilishapeleke mkono wangu wa kulia kuushika mpini wa parange iliyokuawa chini
ya siti niliyokalia.
Nilikuwa nimejiweka tayari, kama atakuwa na nia mbaya niweze kukabiliana naye.
“Samahani bwana” Mtu huyo
akaniambia. Ingawa sauti yake ilikuwa tulivu nay a kibinaadamu, ilikuwa
imeficha taharuki.
“Unasemaje?” nikamuuliza
nikiwa nimemkazia macho kusoma mawazo yake.
“Mimi ni daktari wa hospitali
ya Bombo. Nimepigiwa simu kuitwa hospitali, kuna mama mjamzito anahitaji
kufanyiwa operesheni ya dharura sasa hivi. Kwa bahati mbaya gari langu
limeharibika njiani. Naomba unipeke Bombo haraka” akaniambia.
“Kusema kweli nilimuelewa.
Nikamuuliza.
“Na hilo gari lako je?”
“Ningeomba kama itawezekana
unisaidie kulivuta niliondoe mahali hapa”
“Hiyo itakuwa ni kazi
nyingine” nikamwambia.
“Naomba msaad wako kaka, sina
jinsi na siwezi kuliacha hapa”
“Unataka nilivute hadi wapi?”
“Hadi Bombo. Nitaliegesha
sehemu. Kutakapokucha nitajua la kufanya”
“Utanilipa kiasi gain?”
“Sema wewe”
“Kulivuta hilo gari lako pamoja na kukufikisha wewe
Bombo utanilipa elfu ishirini”
“Sawa. Nitakulipa”
Alipokubali kima changu
nilifungua mwa gari nikashuka.
“Una kamba?” nikamuuliza.
“Kamba sina’
Nilikuwa na kamba ya akiba
kwenye boneti la teksi yangu. Nilikwenda nyuma ya gari, nikafungua boneti na
kutoa kamba. Nikaiweka chini.
Kisha niliisogeza teksi mbele
ya gari la mtu huyo lililokuwa pembeni. Nikashuka tena na kufunga ncha moja ya
kamba nyuma ya gari langu na ncha nyingine nikaifunga mbele ya lile gari.
Nilipomaliza nilimwambia mtu huyo ajipakie kwenye gari lake.
Wakati anajipakia na mimi
nilikwenda kwenye mlango wa teksi nikaufungua na kujipakia. Nilitia gea na
kuiondo teksi taratibu. Kamba ilinyooka na kukaza kabla ya kuanza kulivuta gari
la nyuma.
Niliingia barabarani nikawa
naendesha taratibu. Kwa vile niliendesha kwa mwendo mdogo tulifika Bombo saa
kumi na mbili asubuhi.
Nilishuka kwenye teksi
nikaifungua ile kamba na kuiweka kwenye boneti.
ITAENDELEA KESHO , usikode uhondo huu hapo kesho
No comments:
Post a Comment