Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma ikiwemo umeme wa majumbani, Computer na Kiingereza. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete
amesema idadi ya wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania urais ni kubwa,
hivyo ni lazima wawape viongozi muda wa kuwachuja lakini akawataka
wasiwanunie baada ya kufanya uamuzi.
Rais Kikwete alisema hayo jana katika
hotuba yake ya kuvunja Bunge ambayo iliibua waziwazi ushabiki kwa
wagombea, hasa baada ya kumtaja aliyekuwa waziri mkuu wake wa kwanza,
Edward Lowassa kwa ajili ya kumshukuru.
Akitoa salamu zake kwa wagombea hao, Rais Kikwete aliwapongeza na kuwatakia mafanikio mema katika safari yao.
“Wale
wanaogombea urais waliomo humu (bungeni) nawatakia kila la kheri na
nawashukuru kwa kuonyesha nia ya kunipokea mzigo huu mzito. Nawatakiwa
heri katika matamanio yenu,” alisema Rais Kikwete ambaye aliingia Ikulu mwaka 2005.
“Mko wengi, wote ni vigogo na mmetupa kazi kama kamati kuwachuja kwa hiyo msitununie tukifanya maamuzi.”
Wakati akihitimisha hotuba hiyo, Rais
aliwashukuru watu mbalimbali waliofanya kazi kwenye Serikali yake,
lakini hali ilikuwa tofauti alipomtaja Lowassa ambaye alifanya naye kazi
kwa miaka miwili.
Alimshukuru pia, Makamu wake, Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na baadaye wabunge na viongozi wengine.
Alianza kwa kuwashukuru huku akiwataja
majina. Kila alipotaja majina ya viongozi hao, wabunge walipiga makofi
kwa kugonga meza zao. Hata alipomtaja Dk Bilal na Pinda, wabunge hao
walishangilia kwa kawaida.
Hata hivyo, alipofikia kutaja jina la
Lowassa, kelele za wabunge zilikuwa maradufu, wengi wao wakipiga meza
kushangilia, hali iliyomfanya Rais Kikwete anyamaze kwa sekunde kama 50
na ndipo Lowassa aliposimama na kuinamisha kichwa kuonyesha kukubali
shukrani hizo.
Wabunge waliendelea kumshangilia hadi
alipoketi na ndipo Rais Kikwete akaendelea kutoa shukrani kabla ya
kuhitimisha hotuba yake ya saa mbili na dakika 20.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amelihutubia Bunge
la 10 kwa mara ya mwisho, akijikita katika takwimu zinazoonyesha
mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya Nne imeyapata tangu alipoingia
Ikulu mwaka 2005, lakini akakiri kutofanikiwa kulifufua Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL).
Hali iliyokuwa mwaka 2010 wakati
alipohutubia Bunge hilo kwa mara ya kwanza, ndiyo iliyojirudia jana
baada ya wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kususia vikao na kuwaacha wapinzani wachache.
Rais Kikwete, ambaye alihutubia kwa saa
2.20 alitangaza kulivunja Bunge la 10 lakini akasema litavunjwa rasmi
Agosti 20, akieleza kuwa shughuli ya jana ilikuwa kama “kitchen party au send off”.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete
alimmwagia sifa Spika Anne Makinda, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na viongozi mbalimbali wa Serikali, wananchi na
chama chake kwa kumuamini, huku akisisitiza kuwa anaondoka madarakani na
kuiacha nchi ikiwa salama.
Huku akishangiliwa na wabunge, Rais
Kikwete alieleza kuwa Serikali yake ilipata mafanikio katika utawala
bora, uhuru wa habari, vita dhidi ya rushwa, kukua kwa mapato ya
Serikali, maadili ya viongozi, mihimili ya Serikali, uanzishwaji wa
wilaya mpya, nyongeza ya mishahara, mifugo na uvuvi.
Ushiriki wa wanawake katika uongozi,
kukuza uchumi, utalii, viwanda, madini, umeme, uchukuzi, huduma za
kibenki, michezo, masilahi ya wafanyakazi, burudani, ajira, utamaduni,
Muungano, amani na umoja ni masuala mengine ambayo mkuu huyo wa nchi
ameeleza yalikuwa na mafanikio.
“Desemba
30, 2005 nilipozindua Bunge la Tisa nilielezea mtazamo wangu kuhusu
nchi yetu na kutaja majukumu ya msingi na vipaumbele vya Serikali ya
Awamu ya Nne. Nilisema tutatekeleza wajibu wetu na vipaumbele hivyo kwa
ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya,” alisema.
Alifafanua kuwa Julai 16, 2010 wakati wa
kuvunja Bunge la Tisa alieleza mafanikio yaliyopatikana na changamoto
zake na Novemba mwaka huohuo wakati akilizindua Bunge la 10, aliahidi
kutekeleza vipaumbele vya Serikali kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi
zaidi, jambo ambalo alisema amelifanya kwa kiwango kikubwa.
Alisema marais waliopita, Benjamin Mkapa
na Ali Hassan Mwinyi walifanya mambo mengi mazuri lakini hawakumaliza
yote na kusisitiza kuwa kila jambo lina changamoto zake.
“Hata Baba wa Taifa hakumaliza yote na mimi ninamuachia Rais ajaye ayamalize yale ambayo mimi sikuyamaliza,” Rais Kikwete.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Rais
alisema licha ya juhudi kubwa iliyofanywa na Serikali, bado kuna
changamoto katika upatikanaji wa masoko ya uhakika na bei nzuri kwa
mazao ya wakulima.
MWANANCHI
Baada ya vikao mfululizo wiki hii, hatimaye Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unatarajia kumtangaza mgombea urais wake kesho.
Taarifa zilizopatikana jana zimeeleza kuwa baada ya kikao cha
viongozi wa ngazi za juu wa Ukawa, umoja unaoundwa na NLD, Chadema, CUF
na NCCR – Mageuzi kilichofanyika juzi, mambo kadhaa yameafikiwa na kama
hakutokuwa na mabadiliko yoyote, mteule wa urais kupitia umoja huo
atabainishwa.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi
alithibitisha kuwa tayari makubaliano ya kugawana kata na majimbo kwa
nafasi za udiwani na ubunge yamekamilika na kilichobaki ni utekelezaji.
“Tumeshakubaliana namna ya
kugawana kata na majimbo 13 yaliyobaki na Jumamosi tutaweka wazi kwa
wananchi. Pamoja na hilo pia tutamtangaza mgombea urais na chama
anachotoka,” Dk Makaidi.
Siku chache baada ya baadhi ya wabunge kupewa adhabu ya kutohudhuria
vikao vya Bunge na Spika Anne Makinda, Jumanne ya wiki hii Chadema
ilifanya mkutano wa dharura kujadili mambo kadhaa ya kitaifa.
Siku moja baada ya kikao hicho, viongozi wa waandamizi wa Ukawa
walikutana na kujadili mambo yanayohusu umoja huo kuelekea Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba.
Hata baada ya vikao hivyo, mpaka jana Chadema iliendelea na vikao
vyake vya ndani kujadili mambo kadhaa kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya
Ukawa kinachotarajiwa kufanyika leo kupitisha jina la mgombea urais.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika
alithibitisha kuendelea kwa vikao vya ndani vya chama hicho na kueleza
kuwa hawezi kusema chochote kwa sababu ajenda bado zinajadiliwa na
kwamba kesho taarifa za uhakika zitatolewa kwa vyombo vya habari.
MTANZANIA
Mbinu chafu zilizosukwa ndani ya CCM za kumuengua aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa zimevuja.
Chanzo cha kuaminika kilisema uongozi wa juu wa Chama hicho ulimwagiza jaji mmoja kuandika waraka mzito kumhusu Lowassa.
Jaji huyo alipewa maelekezo katika waraka huo kuhakikisha anaweka maelezo kuwa Lowassa amevunha sheria za uchaguzi.
“Huwezi
kuamini kuna jaji mmoja amepewa kazi ya kuandika waraka mzito wa
kuupeleka kwa kamati ya maadili na baadaye kamati kuu, eti Lowassa
amekiuka sheria za Uchaguzi…tumeshangazwa mno na hatua hii, ndio maana
kwa siku mbili mfululizo kamati ya amaadili zimeshindwa kukaa kwa sababu
zinasubiri waraka huo”.
“Hatuelewi
kinachoendelea baada ya Rais kulivunja Bunge, tuliambiwa kamati
inakutana lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea,kuna siri gani ambayo
imejificha kwenye kamati hizi?? walihoji.
Chanzo hicho kilisema huo ni mkakati mpya kw akina na watu kadhaa kumuengua Lowassa.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete,
amesema baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho siyo waaminifu na
wamejinufaisha na mali za chama hicho hali ambayo imekigeuza kuwa
ombamba kwa wafanyabiashara.
Akifungua jengo jipya la mikutano la
kimataifa la chama hicho, Dodoma Convention Centre, Rais Kikwete
alieleza kusikitishwa kwake na ubadhirifu unaofanywa na viongozi hao,
ambao wameanza kugawana viwanja, kujenga majumba, wengine kujimilikisha
rasilimali za chama hicho na wengine kuweka mapato ya rasilimali zake
mfukoni.
“Msitembee
tu kwa matajiri kwenda kuombaomba, wanawadhalilisha bure. Inashangaza
kuona chama hiki biashara yake kubwa ni kulaza magari ya watu na sijui
mapato yake yanakwenda wapi…Tunazo rasilimali, tunayo mitaji, lakini
hatuzitumii rasilimali hizo kupata mapato,”Rais Kikwete.
Kufuatia hali hiyo, Rais Kikwete
amemwagiza Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana, kuunda kitengo maalum
cha ukaguzi wa mali za chama hicho, ikiwa ni pamoja na kumteua Mkaguzi
Mkuu atakayezunguka nchi nzima kufanya uhakiki wa mali zake na kutoa
taarifa kwa uongozi wa juu.
Alisema CCM imekuwa ikitumia sera ya
ujamaa na kujitegemea, lakini hivi sasa wameipotezea kwa kutegemea
wafadhili na wakati mwingine chama hicho kimejikuta kikienda kuchukua
fedha za moto (rushwa), ambazo zinakilazimisha kutumia muda mwingi
kujisafisha.
“Kama ni mtaji ni mtaji mfu, lazima
tuitoe ile ‘dead capital’ iwe hai; sijui tumekutwa na nini au viongozi
wetu wana maarifa mafupi. Kazi ya kujipanga foleni, kila siku ya
kukimbilia kwa matajiri itaisha lini, wanawadhalilisha tu, mnapata aibu,
sijui mtaondokana nao lini?” alihoji.
Alidai kwamba Jiji la Dar es Salaam peke
yake, CCM ina viwanja zaidi ya 420, lakini haviendelezwi na matokeo
yake vimegeuka karakana ya biashara ya kulaza magari.
“Watu wote pale wanaangusha magorofa na
wanapata mapato. Viwanja vile biashara kubwa ni ya kulaza magari, mapato
yenyewe ya kulaza magari sijui hata anachukua nani, lini tutazinduka
kwenye usingizi huu…Tambueni kwamba ardhi ile ni mtaji,”alisisitiza Rais
Kikwete.
NIPASHE
Tanzania ni kati ya nchi tatu barani Afrika zenye watoto wengi wenye utapiamlo.
Takwimu hizo zilitolewa jana bungeni na
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Rukia Kassim Ahmed.
Mbunge huyo, alitaka kujua serikali
inachukua hatua gani mahususi za kuhakikisha inapambana na tatizo hilo
la watoto kudumaa kiakili.
Akijibu swali hilo, Dk. Kebwe alisema
tatizo la watoto kudumaa kiakili lipo katika nchi nyingi duniani na
linatokana na ulaji duni wa vyakula vyenye virutubisho vya kutosha.
Alisema watoto milioni 199 sawa na
asilimia 33 duniani wa chini ya miaka mitano walikuwa wamedumaa hadi
kufikia mwaka 2000. Alisema juhudi zinafanyika kupunguza tatizo hilo
hadi kufikia watoto milioni 161 sawa na asilimia 25 kwa mwaka 2013.
Dk. Kebwe alisema kutokana na utafiti wa
Kidemografia wa Afya wa mwaka 2010, asilimia 42 ya watoto chini ya
miaka mitano walionekana kuwa na udumavu kutokana naa urefu wa kimo
kutolingana umri wao.
Mbali na Tanzania, alitaja nchi nyingine zenye tatizo hilo kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Ethiopia.
Dk. Kebwe alitaja njia pekee ya kuondokana na utapiamlo kuwa ni wazazi kupata elimu ya kuwapatia lishe watoto wao.
Alisema ni muhimu mama kumnyonyesha mtoto wake kwa muda wa miezi sita bila kumpatia chakula kingine.
Alisema kwa sasa serikali inaendelea na
utoaji wa elimu kwa jamii ili kuhakikisha watoto wanapatiwa lishe bora
katika makuzi yao yote.
“Iwapo jamii itapata elimu inayotolewa
na serikali kwa ajili ya kuwapatia lishe bora watoto waliopo chini ya
miaka mitano ni wazi tatizo hilo linaweza kupungua kwa kiasi kikubwa”
alisema.
HABARILEO
Serikali imetangaza kuanzishwa kwa mkoa
mpya wa Songwe na wilaya mpya sita zikiwemo Ubungo, Kigamboni na
Tanganyika. Mkoa wa Songwe ulikuwa sehemu ya Mkoa wa Mbeya.
Licha ya Ubungo na Kigamboni za Dar es
Salaam, Tanganyika ya Kigoma, wilaya nyingine zilizoanzishwa ni Kibiti
mkoani Pwani, Songwe mkoani Songwe na Malinyi mkoani Morogoro .
Akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa
20 wa Bunge jana mjini hapa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema ugawaji
wa maeneo hayo unafanyika kila baada ya muda kwa kuzingatia mambo
mbalimbali ikiwemo ongezeko la idadi ya watu na pia kuharahisisha
utendaji wa serikali.
Kuongezwa kwa Mkoa wa Songwe kunafanya
idadi ya mikoa ya Tanzania Bara kufikia 26.Mikoa mingine iliyoongezwa
katika Serikali ya Awamu ya Nne ni Geita, Katavi, Njombe na Simiyu.
Awali, mikoa ya Tanzania Bara ilikuwa 21, ambayo ni Arusha,
Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi,
Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Rukwa, Ruvuma,
Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.
Zanzibar ipo mikoa mitano, ambayo ni Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Mkoa wa Mjini, Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Waziri Mkuu alisema pia Serikali imepandisha hadhi Halmashauri za Wilaya
Malinyi, Buchosa, Madaba, Manyoni, Mpimbwe, Nsimbo, Mlale, Itilima,
Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kyerwa, Chemba, Mbogwe, Nyang’wale, Butiama,
Mkarama, Kaliua, Bumbuli na Msalala.
Alizitaja halmashauri za miji na Manispaa zilizoanzishwa ni Chalinze,
Ifakara, Newala, Kondoa Mafinga, Nanyumbu, Mbulu, Mbinga, Bunda,
Tunduma, Nzega, Handeni, Kasulu, Geita, Masasi, Ilemela, Kahama na Nzega.
Pia alisema kuna tarafa mpya tano ambazo
ni Mchemwa iliyopo Newala, Mchichila, Mangombwa, Mambamba na Mangombya,
zote zipo Tandahimba. Pia kuna kata mpya 586 zimeanzishwa sehemu
mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, yapo maeneo
ambayo ni chini ya utawala wa Rais moja kwa moja na yapo ambayo yapo
chini ya mamlaka ya Waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa.
Pia alizungumzia uboreshaji wa Daftari
la Wapiga Kura na kusema kuwa unaendelea vizuri na uchaguzi utafanyika
Oktoba 25 kama ilivyopangwa.
Alisema uandikishaji unaenda vizuri na
kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeshaandikisha watu milioni
11.2, kati ya watu milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa. Mikoa ya Dar
es Salaam na Zanzibar uandikishaji haujaanza.
Alisema uchaguzi utakuwa huru na wa haki, amani na utulivu, hivyo wananchi wajiandae kuchagua viongozi watakaoona wanafaa.
HABARILEO
Misemo na mifano aliyotoa Rais Jakaya Kikwete wakati anahutubia Bunge jana ilikuwa kivutio kikubwa kwa wabunge hao.
Katika kila mfano aliokuwa anatoa katika
hotuba hiyo ulionekana kuwagusa wabunge na kupiga meza kwa nguvu
kumshangilia na hivyo kusababisha mara kwa mara hotuba hiyo iliyochukua
karibu saa mbili na nusu kusimama mara kwa mara.
“Wewe
ndiwe mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu wa juu kabisa katika
mhimili huu wa kutunga sheria na umeidhihirishia dunia kuwa wanawake
wakipewa nafasi wanawezaaaa,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa na wabunge hao alipokuwa akimuelezea Spika wa Bunge, Anne Makinda.
“Hata
hivyo, tahadhari kubwa lazima iendelee kuchukuliwa kwani watu wenye nia
mbaya kwa nchi yetu au na umoja wetu hawajaisha na hawajafurahi kwamba
hawajafaulu. “Huenda wakajaribu tena. Tunachotakiwa kufanya ni kuendelea
kushikamana ili hata wakijaribu tena washindwe na walegee,” alisema Rais Kikwete.
Pia Rais aliwafurahisha wabunge
aliposema idadi ya wanawake imeongezeka kwa kiasi kikubwa na kutania
kuwa ndiyo maana wengine wanaoa wawili wawili.
“Mtakubaliana
nami kuwa katika kipindi hiki uhuru wa habari na uhuru wa watu kutoa
maoni yao umepanuka sana. Tanzania kuna magazeti ya kila siku 16 na kati
ya hayo ya Serikali ni mawili tu, Daily News na HabariLeo. Je, hakuna
uhuru hapo?“ Rais Kikwete.
“Mwisho
lakini sio mwisho wa umuhimu, naishukuru sana familia yangu. Namshukuru
mke wangu Bi Salma Kikwete kwa mchango wake mkubwa ulionipa utulivu wa
kutekeleza majukumu yangu. “Upo msemo kwamba, “kwa kila mwanamume mwenye
mafanikio, yuko mwanamke”, nawaambia ni kweli.
Shukrani zangu, pia, kwa wanangu na
wajukuu zangu kwa kunivumilia pale walipomkosa baba yao na babu yao.
Karibuni mambo yatakuwa tofauti mtaniona mara kwa mara kiasi kuwa huenda
mkanichoka,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa na wabunge.
“Ninapoagana
na Bunge letu natambua kuwa baadhi ya Wabunge mnarudi kutetea viti
vyenu nawatakia kila la heri. Wale wanaogombea Urais waliomo humu
nawatakia kila la heri, na nawashukuru kwa kuonesha nia ya kunipokea
mzigo huu mzito. Nawatakia heri katika matamanio yenu,” alisema.
Kwa habari ,matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment