Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma zikiwemo za umeme, komputer pamoja na kozi ya Kiingereza. Kituo pia kiko na Hostel.Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
Katibu Mkuu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,
alisema Magufuli hawezi kushindana na Ukawa, kwani kwenye jimbo lake la
Chato chama hicho kimechukua sehemu kubwa ya uongozi kuanzia ngazi ya
mitaa na kata.
Dk. Slaa alisema ikiwa kwenye jimbo lake
mwenyewe Ukawa wamempita kwa nafasi hizo, hatakuwa na uwezo wa
kushindana nao katika nafasi hiyo ya juu kabisa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alipongeza mchakato wa mchujo uliofanywa na CCM katika kumpata mgombea.
Hata hivyo alisema Magufuli anahitaji msaada wa kidiplomasia kwani utendaji wa mtu akiwa Waziri ni tofauti na wakati akiwa Rais.
“Walikuwa
na mchakato mgumu kidogo hasa walipofikia kundi la watano, napongeza
walipofikia. Huyo mgombea waliyempata, Watanzania wanamfahamu, ni
mchapakazi…lakini utendaji wa mtu akiwa Waziri ni tofauti na akiwa
Rais…anahitaji msaada wa kidiplomasia,” Dk. Bisimba.
Mhadhiri mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana,
alisema CCM hawajafanya makosa kumteua Magufuli kuwapeperushia bendera
kwani ni mtu ambaye hajitambulishi kimakundi huku akijipatia umaarufu
katika utendaji na uchapaji wake wa kazi katika wizara ikiwamo ya
Ujenzi.
Alisema, Magufuli ni mtu ambaye anafaa
kukiwakilisha CCM kupambana na vyama vya upinzani kwani akiwa Waziri,
wizara yake haina historia yoyote ya kashfa katika taarifa za Ofisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi
Mussa Salim, aliipongeza CCM kwa kufanikiwa kuvunja makundi yaliyokuwa
yametawala kabla ya kupatikana kwa mgombea huyo.
Alisema CCM kumpitisha Dk. Magufuli kumevunja makundi yote yaliyokuwamo, jambo ambalo halikutarajiwa.
NIPASHE
Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), Amina Salum Ali na Waziri wa Katiba na sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, wameahidi kumuunga mkono Dk. John Magufuli katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Balozi Amina ameandika historia mpya
kisiasa, baada ya kumtangulia kwa kura, Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa
Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Asha Rose Migiro.
Mwanadiplomasia huyo kutoka Zanzibar
ambaye alipata kura 253 (asilimia 10.5) ya kura zote 2,422 zilizopigwa
na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
amekishukuru chama chake, kwa kumuamini na kumpigia kura zilizompaisha
kisiasa na kuangukia nafasi ya pili.
“Niko
tayari kumuunga mkono mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli ambaye wajumbe
wa Mkutano Mkuu wamemwamini na kumpigia kura za kishindo. Makundi
yamekwisha na mie yangu nimeyapeleka kwake ili kukisaidia chama changu
kushinda kwa kishindo,” Balozi Amina.
Naye Dk. Migiro ambaye alifanikiwa
kupenya kuwamo katika kundi la tatu bora alisema: “Nilipopata taarifa za
awali za matokeo, nilimpigia simu Dk. Magufuli. Kwa niaba ya familia
yangu kwa sababu unajua mume wangu ni mwalimu wa Magufuli.”
“Niwaombe
wagombea wenzangu 42, tuliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania kiti
hiki, tuvunje makundi na kumsaidia mwenzetu aliyeshinda katika mchakato
ndani ya CCM akibebe chama chetu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu,
dhidi ya vyama vya upinzania.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais,
(Muungano), Samia Hassan Suluhu, ambaye ndiye mgombea Mwenza wa Dk.
Magufuli, amekishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwapa fursa
wanawake.
“Wanawake, tumepewa heshima kubwa,
hatuna sababu ya kukaa nyuma, naombeni mnifuate kwa sababu
nimewafungulia njia nafasi za juu za madaraka.”
NIPASHE
Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani
Mara, imeombwa kupeleka walimu katika Shule ya Msingi Nambaza baada ya
baadhi ya walimu kudai kufanyiwa vitendo vya kishirikina kwa kuingiliwa
kimwili nyakati za usiku na hivyo kusababisha kuikimbia shule hiyo.
Wakifunga kikao cha mwisho cha madiwani wa halmashauri hiyo mjini Bunda, baadhi ya madiwani akiwamo wa kata ya Nansimo, Sabatho Mafwimbo,
alisema kutokana na walimu wawili wa Shule ya Msingi Nambaza kufanyiwa
vitendo hivyo vya ushirikina, hivi sasa shule hiyo imepwaya walimu baada
ya baadhi yao kukimbia.
“Mkurugenzi,
tunaomba halmashauri yako ituletee walimu katika shule hiyo ili
zitakapofunguliwa wanafunzi wafundishwe kuziba pengo la wale walioamua
kukimbia,” Mafwimbo.
Alisema hivi karibuni walimu wawili wa
kike wa shule hiyo, waliingiliwa ndani ya nyumba zao kwa njia
zinazoadaiwa za kishirikina na kuwaingilia kimwili bila wenyewe
kujitambua hali iliyowafedhehesha walimu hao.
Kufuatia tukio hilo, mwananchi mmoja
aliuawa na wananchi wenye hasira kijijini hapo baada ya kutuhumiwa kuwa
miongoni mwa ‘wachawi’ waliotenda ushirikina huo huku wengine saba
wakazi wa kijiji hicho wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa
mawili ya kupanga, kutenda kosa la ushirikina na kuwaingilia kimwili
walimu hao.
Mwenyekiti wa Halmashauri, Joseph Marimbe,
aliwataka wananchi wa kijiji hicho kuachana na vitendo vya ushirikina
kwa sababu hali hiyo inasababisha walimu kuogopa kufundisha shule hiyo.
MWANANCHI
Saa chache baada ya Dk John Magufuli kutangazwa kuwa mteule wa CCM kuwania urais, ulinzi umeimarishwa kwa mgombea mwenyewe, nyumbani kwake eneo la Ada Estate, Dar es Salaam na jimboni Chato mkoani Geita.
Muda mfupi baada ya kuwapo taarifa kuwa Magufuli anaongoza kura za
wajumbe wa Mkutano Mkuu, aliongezewa ulinzi usiku huo na hadi jana muda
wote, alionekana akiwa na walinzi watano.
Jimboni Chato, nyumbani kwake eneo la Rubambambangwe, polisi walionekana wakitanda tangu jana asubuhi tofauti na siku nyingine.
Askari hao wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chato, Alex Mkama walionekana nyumbani hapo tangu asubuhi hata kabla matokeo yaliyompa ushindi Dk Magufuli hayajatangazwa.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alikwenda nyumbani kwa Dk Magufuli
kuzungumza familia yake, hakuruhusiwa na polisi waliokuwa kwenye lango
kuu la kuingilia, walidai wamepewa maelekezo ya kutoruhusu watu kuingia.
“Naomba usiingie ndani wala
kupiga picha eneo hili, hayo ndiyo maelekezo ninayokupa na niliyopewa,
vinginevyo mtafute RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) akupe ruhusa,” alisema mmoja wa askari hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema polisi walikuwa wanatekeleza jukumu lao kwa umma la kulinda raia na mali zao kutokana na wananchi kwa makundi kusherehekea ushindi wa mteule huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema polisi walikuwa wanatekeleza jukumu lao kwa umma la kulinda raia na mali zao kutokana na wananchi kwa makundi kusherehekea ushindi wa mteule huyo.
Konyo alisema ulinzi huo ulilenga kuweka na kuimarisha usalama kwenye makazi ya familia hiyo.
Hata hivyo, Konyo alipotakiwa kuzungumzia kuzuia watu kupiga picha
kwenye makazi hayo alikata simu na hata alipopigiwa tena hakupokea.
Nyumbani kwake, Ada Estate, ulinzi ulianza kuimarishwa mara tu baada
ya kiongozi huyo kutangazwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM.
Mmoja wa walinzi hao ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema
wameongezwa walinzi wengine wanne mara baada ya matokeo ya mjini Dodoma
kutangazwa.
Magari kadhaa yenye namba za serikali na magari ya polisi yalionekana yakiingia na kutoka nyumbani kwa Magufuli.
MWANANCHI
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli ameelezewa na
watu mbalimbali kuwa ni mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, lakini
Rais Jakaya Kikwete amehitimisha yote kwa kumpachika jina la
“tingatinga”.
Rais Kikwete alisema hayo baada ya Magufuli kutangazwa kuwashinda
makada wengine wawili waliopigiwa kura na Mkutano Mkuu wa CCM baada ya
kuzoa kura 2,104, sawa na asilimia 87.08, ushindi ambao alisema unaakisi
kumalizika kwa makundi yaliyoibuka kwenye mbio za kuwania kuteuliwa na
CCM kugombea urais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Balozi Amina Salum Ali alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 253
(sawa na asilimia 10.4), wakati Dk Asha Rose Migiro alikuwa wa mwisho
kwa kupata kura 59 (asilimia 2.4). Jumla ya kura zilizopigwa kwenye
mkutano huo mkuu zilikuwa 2,422 na kura sita tu ndio ziliharibika.
“Kila mtu anaitwa jembe,”
alisema Rais Kikwete alipokuwa akianza kutaja sifa za Magufuli ambaye
amewahi kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na pia Waziri wa Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi.
“Lakini huyu ni zaidi ya jembe.
Ni tingatinga… Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumili ujinga, ni mtu
ambaye anataka kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza.”
Kikwete aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli kuhusu utendaji wake
akisema kuwa alipokuwa akifuatilia wakandarasi kwenye miradi ya ujenzi,
alidiriki kuwatimua pale alipobaini walikuwa wakifanya kazi kinyume na
makubaliano.
“Tunaamini kuwa utawaongoza Watanzania vizuri,” alisema Kikwete akimgeukia mbunge huyo wa Chato.
“Tulikuwa na wagombea 338
lakini sasa tunaye mmoja na tuna kundi moja tu la CCM. Timu Magufuli
imeshaondoka. Wengi walidhani CCM itafia hapa, lakini ushindi huu ni
ishara kuwa CCM ni moja.
“Tunatakiwa kuacha kuteuwa watu
kwa urafiki na kujuana ili tushinde kwa sababu imani huzaa imani. Sina
shaka kuwa tutashinda lakini ushindi hauji hivi hivi lazima tuwe na
mikakati mizuri, mipango thabiti na utekelezaji makini,” alisema.
Rais Kikwete ni mmoja kati ya watu wengi waliohojiwa na Mwananchi
kuhusu mteule huyo wa CCM, ambaye hakuwa akitajwa kama kinara kwenye
mbio za urais kabla ya kufikia hatua hiyo ya kujadiliwa na vikao vya
juu.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Mussa Iyombe, aliyefanya kazi
na Dk Magufuli kwa zaidi ya miaka 10, alisema iwapo atachaguliwa kuwa
rais basi wavivu wajitayarishe kukimbia kwani Waziri huyo ni mchapa kazi
wa hali ya juu.
MWANANCHI
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi
ambaye pia alikuwa mwanamkakati katika kambi ya Edward Lowassa katika
mbio za urais, amesema kambi yake inamuunga mkono mgombea urais
aliyeteuliwa na chama kwa sababu anauzika.
Dk Nchimbi akizungumza na gazeti hili
jana alisema Dk John Magufuli ni mgombea anayeuzika tofauti na wengine
na kwamba kambi yao inamuunga mkono katika kukiwezesha chama kuendelea
kushika dola.
Alisema linapofika suala la maslahi ya
chama wote wanakuwa kitu kimoja na kwamba uwezo na utendaji wa Dk
Magufuli ni wa hali ya juu, kiasi kwamba ni rahisi kumnadi kwa wananchi.
Dk Nchimbi ambaye baada ya Kamati Kuu
kutangaza majina matano ya wanaowania kuteuliwa, yeye na wajumbe wenzake
wawili wa Kamati Kuu, Sophia Simba na Adam Kimbisa walitoka hadharani wakisema wanajitenga na maamuzi ya kamati hiyo kwa kuwa imekiuka katiba ya CCM.
Alisema baada ya vikao vya CCM
kumpitisha Dk Magufuli, kambi yao imeamua kumuunga mkono kwakuwa ni
mtendaji mzuri wa kazi anazopewa na mifano ipo mingi katika wizara
alizoziongoza.
Dk Nchimbi alitoa mifano ya utendaji wa
Dk Magufuli kwa kuwa ameweza kujenga barabara, kukamata meli za kigeni
zinazovua kwa njia haramu katika bahari ya Tanzania na kupambana na
ujenzi usiofuata sheria hasa kwenye maeneo ya barabara.
MWANANCHI
Wananchi wa kitongoji cha Bomani wamemkamata kijana mwenye miaka 28 anayedaiwa kukutwa akimnajisi bata.
Shuhuda wa tukio hilo Sacina Nangere
alisema akiwa na wenzake walisikia kelele za bata nyuma ya nyumba kwa
muda mrefu na kuamua kukimbia kuangalia kuna nini, na alipofika alimkuta
mtuhumiwa huyo akifanya kitendo hicho.
“Nilirudi kukimbia kumwita mama akaone na alipofika huyo jamaa alimtupa bata na kukimbilia kwa jirani alikokua amefikia”.
Mmiliki wa bata huyo Susana alisema
akiwa jikoni akiandaa chakula mtoto wake alimwita na kumwambia akaone
mgeni wa jirani yake anachomfanyia bata wao.
“Sikuamini
macho yangu hadi anamtupa bata na kuondoka, tulipiga yowe na wananchi
wakanisaidia kumkamata wakati akijaribu kutoroka”.
Balozi wa nyumba 1o alisema mama huyo
alifika nyumbani kwake akiwa na bata aliyenajisiwa huku akiomba msaada
na alipoangaliwa alikutwa kweli ameharibiwa na kijana huyo.
Kamanda wa Polisi Bukombe George Kyando
alithibitisha kukamatwa kwa kijana huyo na kwamba baada ya uchunguzi wa
vipimo vya akili vimeonyesha ana akili timamu na taratibu zinafanyika
kumfikisha mahakamani.
JAMBOLEO
Akihutubia mamia ya wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma
jana baada ya kupitishwa na CCM kuwania urais, Dk. Magufuli alitangaza
vita ya kupambana na wazembe, mafisadi, wala rushwa na wabadhirifu kuwa
atapambana nao kwa nguvu zake zote.
Dk. Magufuli alisema: “Wazembe
na wabadhirifu watakaokuwa pamoja na wezi na wala rushwa
nitawashughulikia kwa upole sana. Nitalinda uhuru wa mipaka yetu kwa
kuwa ni ya watu wote ingawa nita-deal na mtu atakayehatarisha uhuru
wetu…Watanzania najua wana matumaini makubwa na mimi.”
Aidha, mgombea huyo aliwaeleza wakazi
wa Dodoma kuwa iwapo atapewa ridhaa na Watanzania kuwa Rais wa Tanzania
atahahikisha vijana wanatatuliwa changamoto za ajira kwa haraka na kwa
kasi zaidi.
“Nataka
niwahakikishie Watanzania na wana -CCM kwa ujumla kwamba CCM ipo tayari
kwa mageuzi ya uhakika na ya haraka kwa watu wote. Sitawaangusha
Watanzania na vyama vingine vyenye itikadi tofauti na Chama cha
Mapinduzi,” alisema na kushangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Aliwapa matumaini wanachama waa chama
hicho kwamba hatawaangusha kwani dhamana aliyopewa ni kubwa hivyo
atahakikisha CCM inapata ushindi mkubwa wakati wa uchaguzi mkuu.
“Leo
ni siku muhimu katika chama chetu, hata kwangu mimi mwenyewe… naona ni
siku muhimu. Sitawaangusha Oktoba..narudia tena sitawaangusha…hata wale
wa vyama vingine sitawaangusha, ” alisema na kuongeza.”
“Nitatekeleza
mambo yote yaliyomo ndani ya ilani ya uchaguzi kuhusu masuala ya
barabara, viwanja vya ndege, maji, umeme na mengine nitahitaji sana
msaada kutoka kwenu.”
Dk. Magufuli katika mkutano huo
alitambulishwa na Rais Jakaya Kikwete, muda mfupi baada ya kutangazwa
matokeo yaliyompa ushindi wa kupeperusha benderea ya CCM wakati wa
uchaguzi mkuu dhidi ya vyama vya upinzani.
Baada ya kuchaguliwa na Mkutano Mkuu
wa CCM kuwa mgombea urais wa chama hicho, Dk. Magufuli alimteua Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia mambo ya Muungano,
Samia Hassan Suluhu kuwa mgombea wake mwenza.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment