SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572, 0655 340572
MWANAMKE 10
ILIPOISHIA
Hakimu aliandika kisha akaamuru aitwe
shahidi mwingine.
Shahidi aliyeitwa baada ya
hapo alikuwa afisa wa shirika la umeme.
Ushahidi alioutoa ulihusu
uharibifu uliosababishwa na ajali hiyo. Alitoa takwimu za gharama kama alizozitoa shahidi aliyemaliza kutoa ushahidi wake.
Alipomaliza kutoa ushahidi huo nilimuuliza.
“Ulimuona mtu aliyesababisha
ajali hiyo?’
“Sikumuona” akajibu. Ndilo
jibu nililokuwa nalitaka.
“Kwa hiyo hujui ni nani
aliyesababisha ajali hiyo?”
“Nimeambiwa kuwa ni wewe”
“Nimeshasema kuwa sikuwa mimi”
“Kama
si wewe kwanini walikukamata?”
“Walinikamata kwa makosa. Wao
ni binaadamu wanaweza kukosea”
Jibu hilo
liliwafanya baadhi ya watu waliokuwa wakisikiliza shauri hilo kucheka kimya kimya.
“Mahakama ndio itajua kama ulikamatwa kwa makosa”
“Lakini kwa maoni yako kama mimi sikuhusika bado nitalazimika kulipia gharama
uliyoitaja?”
“Suala hilo tunaliachia mahakama”
“Sawa”
SASA ENDELEA
Baada ya shahidi huyo
kumaliza kutoa ushahidi wake hakimu aliahirisha kesi kwa wiki moja.
Nilikuwa nikienda kazini kama kawaida ila pikipiki yangu ndiyo ilikuwa imezuiwa na
polisi. Wakati mwingine nilikuwa nikijipa moyo kuwa nitashinda kesi na wakati
mwingine nilikata tamaa. Niliona jela ilikuwa inaningoja kwa vile sikuwa na
pesa za kulipa faini wala kulipia gharama za shirika la umeme.
Siku ya kesi ikawadia. Upande
wa mashitaka ukaeleza
kuwa ulikuwa umemaliza mashahidi wake. Na mimi nikatakiwa nipeleke mashahidi kama nilikuwa nao.
Nikasema kwamba sikuwa na
shahidi. Kesi ikaahirishwa tena ili kuupa nafasi upande wa mashitaka kuandaa
maelezo ya mwisho ya kuishawishi mahakama inione kuwa nina hatia. Na pia kunipa
nafasi mimi ya kuandaa utetezi wangu baada ya kusema kuwa sikuwa na shaahidi.
Kuahirishwa kwa kesi hiyo
kulifanywa kwa wiki mbili. Wiki mbili zikapita kwa haraka, tukakutana tena
mahakamani.
Upande wa mashitaka ukatoa maelezo
yake ya mwisho ya kuionesha mahakama kuwa nilikuwa na hatia.
Mwendesha Mashitaka alisema “
Ushahidi uliotolewa hapa umethibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa kosa
aliloshitakiwa mshitakiwa limetendeka na aliyehusika ni mshitakiwa aliyeko
kizimbani”
Akaendelea.
“Ushahidi wa raia mwema muuza
machungwa katika eneo la Mabanda ya Papa umethibitisha wazi kuwa mshitakiwa
hakusimama mahali ambapo alitakiwa asimame ili kupisha magari na pikipiki
zinazotoka upande wake wa kulia na hivyo kusababisha gari lililokuwa linapita,
kufunga breki ghafla na kusababisha ajali”
“Ushahidi wa polisi wa usalama wa barabarani umethibitisha kuwa baada
ya ajali kutokea mshitakiwa alikimbia na alikuja kukamatwa baada ya wiki mbili”
Mwendesha Mashitaka
akaendelea kueleza.
“Kukamatwa kwake kuliwezeshwa
na msamaria mwema aliyekuwa akiuza machungwa katika eneo hilo ambaye aliwatajia polisi namba ya
pikipiki hiyo pamoja na muhusika mwenyewe”
Baada ya hapo Mwendesha
Mashitaka alitaja vifungu vya sheria za usalama barabarani ambavyo alidai
nilivikiuka na kuieleza mahakama kuwa nilistahili kupewa adhabu kali ikiwemo
kulipia gharama za za shirika la umeme.
Mwendesha Mashitaka huyo
alikwenda mbali zaidi akataja adhabu ya kifungo nilichostahili kwa kosa langu
ni kwenda jela miaka mitano au kulipa faini siyopungua shilingi milioni kumi
pamoja na kulipa ghrama za uharibu niliousababisha.
Hakujua ni jinsi gani alikuwa
amenishitua na hakujua ni jinsi gani nilikuwa nikimlaani kwa kutaka kuniharibia
maisha yangu. Hapo hapo niliona uso
wangu ukifadhaika kama vile tayari nilikuwa nimeshahukumiwa.
Baada ya maelezo marefu ya
Mwendesha Mashitaka, hakimu alinitaka nijitetee. Nikaanza kujitetea.
“Mheshimiwa hakimu licha ya
maelezo marefu ya Mwendesha Mashitaka ya kutaka nifungwe na kulipa faini, bado
ninaisisitizia mahkama yako kuwa si mimi niliyetenda kosa. Mimi nimefananishwa
tu kwa bahati mbaya. Mimi sijavunja sheria yoyote ya barabarani”
Nikaendelea kueleza.
“Nilishangaa sana nilipoona nakamatwa
na kuambiwa nimesababisha ajali. Jambo hilo si kweli. Mashahidi
wote waliokuja kutoa ushahidi dhidi yangu ni waongo wakubwa, wamerubiniwa na
polisi ili nipatikane na hatia. Kwa hiyo naiomba mahakama yako inione sina
hatia na iniachie huru”
Hakimu aliandika maelezo
yangu kisha
akapanga tarehe ya kutoa hukumu.
Wakati niko uraiani nikisubiri hukumu yangu, nilikonda
kwa mawazo. Ningekuwa ni mtu mwenye uwezo wa kulipa faini na kulipia gharama
zilizotakiwa, nisingejali.
Lakini nillikuwa masikini niliyekuwa nikitegemea mshahara wa kila mwezi ambao
mimi mwenyewe pia haukunitosha.
Nilijiambia kama
nitafungwa miaka mitano maisha yangu yatakuwa yameharibika. Nitakapotoka hapo
nitakuwa sina kazi, sina bazi. Nitakuwa ninaanza maisha upya nikiwa sina
uhakika wa kupata kazi mahali pengine.
Pia sikuwa na uhakika kuwa
nitaweza kukaa gerezani kwa miaka mitano. Itakuwa ni kifo. Si ajabu
nikarudishwa nikiwa maiti.
Katika kipindi hicho nikuwa
naswali na kuomba Mungu. Nilimkumbuka Mungu sana.
Lakini sikuacha kumfikiria
yule msichana wa kijini aliyenisababishia lile balaa. Nilikuwa nikijiambia kama si yeye balaa lile lisingenitokea.
Niliwahi kueleza kwamba nilikwenda kwa mganga kuroga ile kesi. Katika
kipindi hicho cha kusubiri hukumu nilikwenda tena kwa waganga wasiopungua
watatu.
Niliambiwa kulikuwa na mganga
mmoja wa kimakonde aliyekuwa akiishi Kijiji cha Kigombe wilaya ya Muheza ambaye
alikuwa hodari wa kuzima kesi, nikaenda na kaka yangu.
Baadaye tena nilikwenda kwa
mganga mwingine aliyekuwa wilaya ya Mkinga. Alikuwa sharifu aliyekuwa akitumia
uganga wa vitabu. Akanifanyia visomo vya kuzima kesi.
Mganga wa tatu alikuwa
Pangani. Yeye alikwenda kunifanyia kafara baharini akanitabiria kwamba nitapata
misukosuko mingi lakini nitakuja kuwa tajiri.
Siku moja kabla ya hukumu
niliota ndoto ya kutisha. Ndoto ile ilikuwa kama
inanitabiria kifungo. Niliota mzee mmoja aliyevaa nguo nyeupe akiniambia kuwa
uganga niliofanya ulikuwa wa bure.
Kwa pembeni yangu nilimuona
yule msichana wa kijini amesimama akinicheka. Alikuwa amebeba mkoba uliokuwa
umeja kinyesi ambacho alikuwa akikichota na kunirushia, mpaka mwili wangu wote ukatapakaa
kinyesi.
Hapo hapo nikaona nimesimamishwa kwenye
kizimba. Hakimu akaniambia amenitia hatiani na kunihukumu kifungo cha miaka saba
jela bila faini na kunitaka nililipe shirika la umeme shilingi milioni kumi na
tano.
Nikamuona mama yangu ambaye
alikuwa hapo mahakamani akiangua kilio.
BADO SAFARI NI NDEFU.
WASOMAJI WETU MUWE NA SUBIRA KIDOGO. HADITHI BADO NI NDEFU. Je nini kitatokea?
Jibu utalipata katika blog yako ile ile ya TANGA KUMEKUCHA.
No comments:
Post a Comment