SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 11
ILIPOISHIA
Katika kipindi hicho nikuwa
naswali na kuomba Mungu. Nilimkumbuka Mungu sana.
Lakini sikuacha kumfikiria
yule msichana wa kijini aliyenisababishia lile balaa. Nilikuwa nikijiambia kama si yeye balaa lile lisingenitokea.
Niliwahi kueleza kwamba nilikwenda kwa mganga kuroga ile kesi. Katika
kipindi hicho cha kusubiri hukumu nilikwenda tena kwa waganga wasiopungua
watatu.
Niliambiwa kulikuwa na mganga
mmoja wa kimakonde aliyekuwa akiishi Kijiji cha Kigombe wilaya ya Muheza ambaye
alikuwa hodari wa kuzima kesi, nikaenda na kaka yangu.
Baadaye tena nilikwenda kwa
mganga mwingine aliyekuwa wilaya ya Mkinga. Alikuwa sharifu aliyekuwa akitumia
uganga wa vitabu. Akanifanyia visomo vya kuzima kesi.
Mganga wa tatu alikuwa
Pangani. Yeye alikwenda kunifanyia kafara baharini akanitabiria kwamba nitapata
misukosuko mingi lakini nitakuja kuwa tajiri.
Siku moja kabla ya hukumu
niliota ndoto ya kutisha. Ndoto ile ilikuwa kama
inanitabiria kifungo. Niliota mzee mmoja aliyevaa nguo nyeupe akiniambia kuwa
uganga niliofanya ulikuwa wa bure.
Kwa pembeni yangu nilimuona
yule msichana wa kijini amesimama akinicheka. Alikuwa amebeba mkoba uliokuwa umejaa
kinyesi ambacho alikuwa akikichota na kunirushia, mpaka mwili wangu wote ukatapakaa
kinyesi.
Hapo hapo nikaona nimesimamishwa kwenye
kizimba. Hakimu akaniambia amenitia hatiani na kunihukumu kifungo cha miaka
saba jela bila faini na kunitaka nililipe shirika la umeme shilingi milioni
kumi na tano.
Nikamuona mama yangu ambaye
alikuwa hapo mahakamani akiangua kilio.
SASA ENDELEA
Nilipozinduka usingizini
niliona jasho limenitoka mwili mzima na moyo ulikuwa ukinienda mbio.
Niliwasha taa kisha nikalaani. Saa
yangu ilionesha ilkuwa saa kumi alfajiri. Sikulala tena. Mawazo yangu yote
yalikuwa kwenye kufungwa. Nilijua kuwa ile ndoto ilkuwa imenibashiria kifungo
ambacho ningepambana nacho siku ile.
Asubuhi kulipokucha nilipanga
vitu vyangu vizuri kwa kujua kuwa ninakwenda kufungwa. Nilipomaliza nilikwenda
kuoga, nikarudi kuvaa.
Nilihakikisha kila kitu
nimekiweka sawa ndipo nilipotoka. Nilikwenda nyumbani kwa mama yangu barabara
ya tisa ambako nilimkuta kaka yangu akinisubiri.
Baada ya kusalimiana nao,
nililetewa chai nikanywa. Kwa sababu ya fadhaa niliyokuwa nayo nilikunywa
kikombe kimoja tu na silesi tatu za mkate.
Kaka yangu akaitazama saa
yake.
“Inakaribia kuwa saa mbili
sasa” akasema.
Na mimi nikatazama saa yangu.
“Twendeni. Muda umekaribia sana” nikawambia.
“Ngoja nikuombee Mungu” Mama
akaniambia.
Nilitaka kuwaeleza kuhusu ile
ndoto niliyoota lakini nikoana hakukuwa na haja. Kaka yangu angeona
niliota kwa sababu ya uoga wa kufungwa,
wakati yeye siku zote alikuwa akiniambia niache uoga kwa vile alikuwa akiamini
kuwa ningeshinda ile kesi.
Mama yangu akaniombea dua
iliyonipa faraja sana.
Baada ya dua yake ndefu akatuambia.
“Sasa twendeni”
Tukatoka. Tulipanda teksi
iliyotupeleka mahakamani. Tuliingia ndani ya mahakama tukakaa kusubiri hakimu
aingie.
Muda ulipowadia hakimu
aliingia. Sauti ya koooort ikasikika. Watu wote tukasimama kutoa heshima ya
mahakama kisha
tukaketi pamoja na hakimu.
Jalada la kesi yangu ndilo
lililoitishwa kwanza. Lilipotajwa jina langu nikasimama na kupanda kizimbani.
Hakimu akaniambia kwamba siku
ile ndio angesoma hukumu ya kesi yangu. Nikamwambia “Sawa”
Nilikuwa nimeshajitolea kwa lolote litakalotokea,
kufungwa au kuachiwa huru.
Hakimu alianza kutaja kesi
iliyokuwa inanikabili. Akaeleza kwamba nilikana mashitaka niliyoshitakiwa na
hivyo hukumu yake ilitegemea sana
ushahidi uliotolewa mahakamani.
Hakimu aliendelea kuuchambua
ushidi huo uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashitaka kuanzia shahidi wa
kwanza hadi wa mwisho.
Mwisho wa maelezo yake hakimu
alisema, ameridhika kwamba ushahidi huo ulikuwa wa kweli na haukuwa na shaka
yotote licha ya mimi mshitakiwa kuupinga.
Hakimu alipofika hapo
nilishituka nikajiambia ubashiri wa ndoto niliyoota sasa ulikuwa unatimia.
Miguu ilianza kunitetemeka
lakini nilijikaza kiume. Nikajiambia wanaofungwa pia ni binaadamu kama mimi.
“Kwa sababu hiyo nimekutia
hatiani mshitakiwa katika makosa yote uliyoshitakiwa” hakimu akasema kisha akanitazama.
“Mshitakiwa uliopo mbele
yangu ninakuhukumu kifungo cha miaka mitatu au ulipe faini ya shilingi milioni
sita. Na pia ninakuamuru ulilipe shirika la umeme shilingi milioni kumi na tano
kutokana na hasara uliyolisababishia shirika hilo”
Moyo wangu ulishituka na
miguu yangu ikazidi kutetemeka.
“Utatumikia kifungo au
utalipa faini pamoja na kulifidia shirika la umeme?’ Hakimu akaniuliza.
Sikuwa hata na la kujibu,
ndipo nilipomuona msichana mmoja miongoni mwa watu waliokuwa wakisikiliza
hukumu yangu akinyanyuka.
“Mheshimiwa nitamlipia faini
mshitakiwa pamoja na gharama aliyotakiwa kulipa” akasema.
Nikamtazama vizuri msichana
huyo.
Unadhani alikuwa nani?
Alikuwa Zena. Yule msichana
ambaye nilimgundua kuwa ni jini!
“Utamlipia wewe faini ya
shilingi milioni sita na shilingi milioni kumi na tano za kulilipa shirika la
umeme?’ Hakimu akamuuliza.
“Ndiyo mheshimiwa”
“Unazo hapo?”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Haya nenda kalipe”
Msichana huyo aliyekuwa
ameweka begani mkoba wa rangi ya samli, alitoka kwenye mabenchi ya kukalia
mahakamani akaongozwa na polisi kulekea sehemu ya kulipia pesa.
Wakati akitembea watu wote
walikuwa wamegeuza uso wakimtazama. Pengine ni mimi peke yangu niliyejua kuwa
hakuwa binaadamu, bali alikuwa jini aliyekuwa akijigeuza binaadamu.
Mama yangu na kaka yangu
ambao walikuwepo hapo mahakamani wakiwa wameketi katika safu za mbele pia
walikuwa wamepigwa na butwaa wakimtazama yule msichaana bila kumuelewa.
Polisi mwingine alinishusha
mimi kizimbani na kunipeleka pale mahali ambapo Zena alitakiwa kunilipia faini na
gharama za shirika la umeme.
Kitendo kile cha Zena
kilikuwa kimenishitua na kunishangaza sana.
Kwanza sikuwa nikijua kwamba alikuwepo pale mahakamani na kama
alikuwepo sikujua alijuaje kuwa nilikuwa na kesi na kwamba siku ile ningetakiwa
kulipa pesa hizo.
Nikasimamishwa karibu naye.
Alikuwa amevaa baibui la kiiran lililonakishiwa mistari ya rangi ya samli.
Alikuwa amejitia manukato yaliyokuwa yakisikika. Wakati ameuweka moba wake juu
ya meza na kufungua zipu nilimuona kama adui
ambaye ghafla amegeuka na kuwa mkombozi wangu.
Siku za nyuma nilikuwa
nikijiambia nitakapomuona popote nitamkimbia. Lakini siku ile sikuweza
kumkimbia kwani yeye sasa alikuwa kama
kimbilio langu.
Baada ya kufungua mkoba wake
alitia mkono ndani ya mkoba huo na kutoa mabunda ya noti nyekundu na kuyaweka
juu ya meza. Nilihesabu jumla ya mabunda ishirini na moja ambayo aliyatoa.
“Hizo hapo shilingi milioni
ishirini na moja. Milioni sita za faini na shilingi milioni kumi na tano za
shirika la umeme” akasema.
Pesa hizo zilihesabiwa na
kuthibitishwa kuwa zilikuwa ni kiasi kilichotakiwa.
SHABASH!!! HUYO KWELI NI
MWANAMKE WA SHOKA! Je nini kitatokea? Sidhani kama kuna blog nyingine hapa
nchini yenye utamu kama hii!
TUONANE HAPO KESHO.
No comments:
Post a Comment