SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572
MWANAMKE 33
ILIPOISHIA
Kwa mara ya kwanza niligundua
hata mlevi anaweza kuwa na manufaa yake. Sikutarajia kuwa Mgosingwa mlevu wa
gongo na pombe ya mnazi angeweza kunisaidia. Licha ya msaada wa kucha za maiti
alioniahidi, kile kitendo chake cha kuiokota leseni yangu na kuja kunipa
mwenyewe bila kuipeleka polisi ulikuwa msaada mkubwa kwangu.
Nilimshukuru sana
nikijua kama si yeye ningeumbuka. Pengine muda
ule ningekuwa niko mahabusi.
Ilipofika saa nne usiku
nililifunga lile shepe sehemu ya nyuma ya siti ya pikipiki yangu nikatoka.
Nilikwenda katika lile eneo
la makaburi analolinda Mgosingwa. Niliposimamisha tu pikipiki, Mgosingwa
akajitokeza. Alitazama kila upande, alipoona kuko kimya akasogea kwenye
pikipiki yangu na kunisaidia kulifungua lile shepe.
Ile hewa yake ya mwilini tu
ingetosha kumlewesha mtu. Alikuwa akinuka pombe aina ya gongo kama
vile alikuwa mtambo wa kuitengenezea. Muda ule tayari alikuwa ameshalewa.
Sikumlaumu. Kulinda makaburi
wakati wa usiku ilikuwa kazi ya kutisha. Alihitaji kupata kitu cha kutuliza
akili yake, vinginevyo anaweza kuota ndoto za maiti waliozikwa usiku kucha.
Hatukuungumza chochote.
Alipochukua lile shepe, alinionesha ishara kuwa tukutane asubuhi akatokomea
makaburini.
Nikapanda pikipiki yangu na
kuondoka. Nilipofika nyumbani nilifikia kuoga na kulala.
Kulikuwa kunaanza kupambazuka
nilipoamshwa usingizini kwa kishindo cha mlango wa mbele uliokuwa unabishwa.
Nikatazama saa yangu na kuona ilikuwa saa kumi na mbili kasorobo. Nikajiuliza
ni nani abishae mlango? Sikupata jibu.
Nikashuka kitandani na kuvaa
suruali yangu kisha nikafungua mlango wa chumbani mwangu na kutoka ukumbini.
Nilikwenda kwenye mlango wa mbele na kuuliza.
“Nani abishaye?”
“Ni mimi Mgosingwa!”
nikaisikia sauti ya Mgosingwa ikisikika kwa nje.
“Ahaa ni wewe!” nikasema huku
nikifungua mlango.
SASA ENDELEA
Nikamuona mgosingwa amesimama
mbele ya mlango. Kando ya baraza ya nyumba niliyokuwa naishi kulikuwa na
baskeli iliyoegeshwa. Katika kiti chake cha nyuma ilikuwa imefungwa shepe.
“Kumekucha mgosingwa. Habari
ya leo?” Mgosingwa akaniambia kwa uchangamfu.
“Nzuri Mgosingwa, je
umefanikiwa?”
“Nisifanikiwe kwanini?”
akaniuliza huku akitia mkono kwenye mfuko wa shati lake na
kutoa kibiriti.
Nilidhani alikuwa anataka
kuwasha sigara lakini alipokifungua alikielekeza mbele ya macho yangu. Nikaona
alikuwa ameweka kucha nyeupe.
“Ndio hizo Mgosingwa?”
nikamuuliza.
“Si ulitaka kucha za maiti?”
“Ndiyo”
“Ndio hizo nimekuletea”
“Ulifukua kaburi?”
“Kulikuwa na kaburi moja la
maiti iliyozikwa jana, nililifukua usiku nikaikata kucha ile maiti kisha
nikalifukia kama nilivyolikuta. Kucha zenyewe
ndio hizo”
Nilizitazama vizuri zile
kucha alizoziweka ndani ya kibiriti kisha nikakifunga.
“Asante
sana Mgosingwa”
nikamwambia Mgosingwa kisha nikamtazama.
“Mgosingwa fanya basi hayo
makwarukwaru” Mgosingwa akaniambia huku akinitazama kwa jicho la tamaa.
Makwarukwaru ni lugha ya
mitaani. Mgosingwa alikuwa akimaanisha nimpe pesa.
“Makwarukwaru yapi
Mgosingwa?”
“Si tuliongea jana,
nikikuletea hizo kucha utanipa shilingi elfu ishirini”
“Mgosingwa si nilikupa kumi?’
“Ndio, ikabaki kumi”
Nikatia mkono kwenye mfuko wa
suruali yangu na kutoa noti za shilingi elfu kumi nikampa.
“Asante Mgosingwa, wewe hata kama utataka mguu wa maiti niambie nitakupatia”
“Sawa bwana”
Mgosingwa akachukua baskeli
yake na kuniaga. Na mimi nikarudi ndani.
Nilipoingia ndani nilikwenda
kuoga nikavaa na kutoka na pikipiki yangu. Nikaenda kwa yule mganga wa kipemba.
Kwa vile ilikuwa bado mapema nilisubiri nje ya gesti hadi mlango wa gesti
ulipofunguliwa, nikaingia.
Nilibisha mlango wa chumba
cha mganga. Baada ya muda kidogo mlango ulifunguliwa. Mganga aliponiona tu
akanikumbuka.
“Oh karibu, wewe si ndiye
yule jamaa uliyekuja juzi?” akaniuliza.
“Ndiye mimi”
“Karibu ndani”
Alinipisha kwenye mlango
nikaingia mle chumbani.
“Kaa kwenye kiti” akaniambia
na kuongeza.
“Bahati yako umenikuta, leo
ndio siku yangu ya kuondoka. Naenda Arusha. Nilikutazamia jana sikukuona”
“Jana sikufanikia kupata zile
kucha”
“Sasa leo umezipata?”
“Nimezipata”
“Ni kucha za maiti khaswa?”
“Ni kucha za maiti. Kuna mtu
alifukua kaburi jana usiku akamkata kucha maiti”
Nilitia mkono kwenye mfuko
wangu wa shati nilikoweka kile kibiriti alichonipa mgosingwa.
“Kama
umezipata hizo kucha nitaahirisha safari yangu ili nikufanyie kazi yako” Mganga
alinaimbia.
Nilikitoa kile kibiriti.
“Ni hizi hapa” nikamwambia na
kukifungua kile kibiriti na kumuonesha.
“Ziko wapi. Mbona sioni kitu”
Mganga akaniuliza.
Nikashituka na kuangalia
ndani ya kile kibiriti.
Hamkuwa na kitu. Kibiriti
kilikuwa kitupu kama mkono uliorambwa!
Mbali ya kukichomoa kabisa
kwenye ganda lake
sikuona chochote.
“Jamani zile kucha zimekwenda
wapi?” nikajiuliza kwa mshangao.
“Ulikuwa umezitia humu?”
Mganga akaniuliza.
“Ndio, nilizitia humu. Wakati
naondoka nyumbani zilikuwamo!”
“Sasa zimekwenda wapi?”
“Sijui”
“Au umezimwaga bila kujua?’
“Sijazimwaga. Nilipoondoka
nyumbani kucha zilikuwemo. Nikakitia hiki kibiriti mfukoni na sijakitoa mpaka
muda huu”
“Basi itakuwa ni miujiza”
“Sasa miujiza hii inatokea
wapi?”
Mganga akawa anafungasha vitu
vyake kwenye begi lake
alilokuwa ameliweka
kitandani. Niliona kama amenipuuza.
“Sasa miujiza hii imetokea
wapi?’ nikamuuliza tena.
“Hilo
jini limekutawala sana,
itakuwa vigumu kuliepuka” Mganga akaniambia huku akiendelea kupanga nguo zake.
“Limenitawala kivipi?’
“Wauliza jibu, wewe huoni
mambo yako yanakwenda ovyo unadhani ni kwa sababu ya nini?’
Sikumpinga, mambo yangu
yanaenda ovyo kweli.
“Ndio sababu hizi kucha
zimepotea?” nikamuuliza.
Mganga hakunijibu. Badala
yake aliniambia.
“Kazi kama hizo sizitaki
kabisa, zitaniletea nuksi bure”
“Wewe ndiye mtaalamu
nilitegemea kuwa utanisaidia”
“Sitaweza kukusaidia, naomba
uende zako. Nina safari ya arusha nisije nikachelewa gari” Mganga aliniambia
akionesha wazi kukasirika.
Sikuwa na jingine isipokuwa
kuinuka kwenye kiti. Nikamuga na kuondoka zangu. Nilivyomuaga hata hakunijibu
kitu. Sijui nilimkosea nini. Alikuwa amehamaki mara moja.
Wakati natoka mle chumbani
yale maneno yake kwamba hilo jini limenitawala sana na kwamba itakuwa
vigumu kuliepuka, yalikuwa yakinirudia akilini mwangu.
Kusema kweli niliondoka pale
gesti nikiwa na fadhaa sana.
Nilipanda pikipiki yangu. Sikutaka kwenda kwa kaka ingawa hapakuwa mbali na
pale gesti, nikaenda kazini kwangu.
Nilifanya kazi huku nikiwaza
jinsi zile kucha zilivyopotea kwenye kibiriti. Kwa kuzingatia maneno ya yule
mganga iliwezekana kwamba zile kucha zilipotezwa na Zainush.
Lakini kubwa ambalo lilinitia
fadhaa ni yale maneno ya yule mganga kwamba hilo
jini limenitawala sana
na itakuwa vigumu kuliepuka.
Kama mganga wa majini amesema hivyo, je juhudi zangu za
kumuondoa zainush zitafanikiwa kweli, nikajiuliza kwa fadhaa.
Mganga mwenyewe amenifukuza,
nikaendelea kuwaza, bila shaka na yeye alikuwa amepata hofu baada ya kuona
jinsi zile kucha zilivyotoweka kwenye kibiriti.
“Una nini leo Amour?” Wafanya
kai wenzangu walikuwa wakiniuliza.
“Nikoje?’
NGOMA ITAENDELEA KESHO.
No comments:
Post a Comment