Ndege mmoja ambaye inaaminika alitoka nchini Finland amepatikana katika uwanja wa ndege wa Entebbe nchini Uganda.
Ndege
huyo aina ya Osprey kwa sasa anatunzwa na maafisa wa kituo cha
kuwahudumia wanyama cha Uganda Wildlife Education Centre (UWEC). Ndege huyo mkubwa, aina ya mwewe, aligunduliwa na
maafisa wa uwanja wa ndege katika njia inayotumiwa na ndege kupaa na
kutua katika uwanja wa huo wa Entebbe.
Isaac Mujaasi, afisa wa
mauzo na mawasiliano katika UWEC, ameambia BBC kwamba ndege huyo alikuwa
ameumia katika mabawa yake baada ya kugongwa na ndege iliyokuwa inapaa. Alikuwa na pete yenye maelezo kumhusu mguuni ambayo
inaashiria kwamba alimilikiwa na makumbusho ya historia asilia nchini
Finland.
Bw Mujaasi anasema waliwasiliana na maafisa wa makumbusho hao ambao wamethibitisha kwamba ndege huyo ni wao. “Hili lilituthibitishia kwamba ndege huyu alisafiri
kutoka Helsinki, Finland,” Bw Mujaasi amesema. “Tutamtibu ndege huyo na
akipona tutamwachilia na huenda akarejea kwao.”
Afisa huyo hata
hivyo amesema ni kawaida kwa ndege kuhama kutoka Ulaya, hasa wakati wa
majira ya baridi na kukimbilia maeneo yenye joto.
No comments:
Post a Comment