Sunday, July 10, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 38

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI

MWANAMKE 38

ILIPOISHIA

Nikamkumbatia. Salma hakuchelewa kupata usingizi. Akalala fofo. Mawazo yakabaki kwangu.

Asubuhi tulipoamka nilimuuliza.

“Uliota tena”

“Hapana, sikuota” akaniambia.

Nikashukuru aliponiambia hivyo. Nikajitayarisha kwenda kazini. Muda wangu wa kutoka ulipowadia nikatoka.

Nilichapa kazi hadi saa kumi jioni nikarudi nyumbani. Nilikuta nyumba ilikuwa imefungwa. Funguo nilipewa na mpangaji mwenzangu wa upande wa pili.

“Mke wako aliondoka, akaniachia hizi funguo. Amesema ukija nikupe”

“Amekwambia amekwenda wapi?”

“Hakuniambia”

Nikazichukua zile funguo na kufungua mlango huku nikiwa na mawazo. Nilipoingia chumbani nilikuta karatasi ya barua iliyokuwa imeachwa kitandani. Nikaichukua na kuisoma.

Mwandiko ulikuwa wa mke wangu Salma. Iliandikwa.

“Nimelazimika kuondoka hapa nyumbani ili kuokoa maisha yangu. Ile ndoto ilinijia tena mchana. Nilimuota tena yule msichana. Aliniuliza kwanini sijaondoka. Akaanza kunitandika bakora. Ngozi yangu ya mgongo imeharibika kwa jinsi alivyonichapa. Hali yangu ni mbaya. Ninakwenda hospitali na nikitoka hospitali narudi kwetu. Naomba uniletee talaka yangu. Huyo msichana ninayemuota ameniambia kama nitaendelea kukaa ataniua”

Salama alimaliza barua yake kwa kuweka jina lake.

Kusema kweli maneno ya Salma aliyokuwa ameniandikia yalinishitua sana. Nilipomaliza kusoma barua ile niliona miguu ikininyong’onyea na kuishiwa na nguvu.

SASA ENDELEA

Nikakaa kitandani na kuanza kutafakari. Tayari nilihisi presha  yangu ikiwa juu na moyo ukienda mbio.

Nilirudia kuisoma tena ile barua. Nikaona kama uso wa Salma umetokeza katikati ya ile karatasi ukitamka yale maneno aliyoandika.

Nikaisikia waziwazi sauti yake ikimalizia kusoma barua hiyo kwa kuniambia.

“Naomba uniletee talaka yangu. Huyo msichana ninayemuota ameniambia kama nitaendelea kukaa ataniua…”

Nilihisi sasa mwili mzima ukipoteza nguvu. Tukio lile lilikuwa limenichoma mithili ya mkuki wa moto moyoni mwangu. Picha ya kuachana na Salama haikukubalika akilini mwangu. Si tu nilikuwa nampenda bali alikuwa ni kila kitu kwangu.

Tukio lile liliniashiria kwamba sitaweza tena kuishi na mke yeyote.

Zena amemtandika bakora Salma kama alivyowatandika wale vijana waliomuibia pochi.

Nilijua kuwa kama Salma asingeondoka na yeye angeuawa. Kuondoka kwake ulikuwa uamuzi wa maana ingawa sikuupenda.

Pia nilijua huo ulikuwa ndio mwisho wangu na Salma. Salama singeweza kurudi tena pale nyumbani na asingetaka tena kuishi na mimi.

Yale mawazo niliyokuwa nayo kwamba nikioa mke zena atakuwa mbali na mimi hayakuwa sahihi. Sikuweza kutambua huyu jini alikuwa na nia gani na mimi.

Kusema kweli nilisikia uchungu sana. Nikatikisa kichwa changu kusikitika. Nilishindwa kuvumilia machungu niliyokuwa nikiyasikia moyoni mwangu, nikaona machozi yakinitiririka.

Wakati nimeinamisha kichwa changu, nilihisi kama Zena amesimama mbele yangu akinicheka. Nikashituka na kudhani alikuwa Zena kweli. Kumbe yalikuwa ni mawazo yangu tu.

Nikajiuliza niende kwa kina salma nizungumze naye, lakini nikajiuliza tena ningekwenda kuzungumza naye nini wakati Salama ameshaamua kuondoka kusalimisha roho yake?

Nikajiambia kuwa si ajabu ameshagundua kuwa nina jini mwanamke ambaye hataki niwe na mke. Kama itakuwa hivyo nikifika kwao Salama anaweza kukataa nisizungumze naye zaidi ya kudai talaka yake kama alivyoniandikia kwenye barua.

Nilijihisi nilikuwa nimekabiliwa na uamuzi mgumu sana. Baada ya kuwaza kwa dakika kadhaa bila kupata ufumbuzi niliamua kutoka na kwenda kumueleza kaka kilichonitokea.

Kaka akapatwa na mshangao hasa nilipomueleza kuwa Salama ametandikwa bakora na Zena na ameshaondoka nyumbani.

“Sasa tufanye nini?” Kaka akaniuliza. Swali lake lilinikatisha tamaa. Nilichotarajia ni kupata ushauri kutoka kwake na sio mimi nimueleze yeye la kufanya.

Ilionesha mpaka kufikia kuniuliza tufanye nini ni kwamba alikuwa amekwama.

“Mimi sijui la kufanya. Nimekuja kwako ili nipate ushauri” nikamwambia.

“Mmh!” kaka aliguna kwanza kabla ya kuniambia.

“Sijui nikupe ushauri gani. Nikikwambia umbembeleze mke wako arudi ni kwamba atatandikwa tena na nikikwambia muache huko huko kwao, unyumba wenu utakuwa haupo tena!”

“Yaani tangu sasa unyumba wetu hauko tena, anadai nimpe talaka yake!”

“Ndio hapo sasa!”

“Mimi siwezi kumpa talaka. Nataka nipambane na hili tatizo kwa nguvu zote”

“Utapambana nalo kivipi?”

Swali hilo likanifanya nihamaki. Niliona kama vile kaka hakuwa pamoja na mimi.

“Kaka kwa mara ya kwanza naona una maswali ya kunikatisha tamaa” nikamwambia huku nikitikisa kichwa kusikitika.

“Hapana Amour, usinifikirie hivyo. Mimi niko pamoja na wewe. Nimekuuliza ili unieleze jinsi tutakavyopambana na hilo tatizo”

Nilikuwa nimeshahamaki. Nikaondoka kwenye kiti.

“Sasa unakwenda wapi?” Kaka akaniuliza.

“Niache kwanza” nilimwambia na kufungua mlango ili nitoke.

Kaka akanyanyuka.

“Hebu subiri Amour…!”

Nikatoka haraka. Nilipanda pikipiki yangu nikaiwasha na kwenda kwa mama.

Mama alivyouona uso wangu alijua kulikuwa na jambo lisilo la kawaida. Akaniuliza.

“Kulikoni?”

“Kuna matatizo yametokea” nikamwambia na kumueleza tatizo la kutandikwa bakora kwa mke wangu na kuondoka nyumbani.

“Nimekwenda kwa kaka, kaka ameshindwa kunisaidia kimawazo. Sasa mimi naondoka nyumbani nitakwenda kokote ambako naona nitapata msaada. Kama itashindikana, basi bora nife huko huko!”

Nilipomwambia hivyo mama nilitoka na kupanda pikipiki yangu. Mama alikuwa ametoka nje akinisemesha lakini sikujua alikuwa akiniambia nini na sikutaka kumsikiliza. Nikaondoka.

Nilirudi nyumbani, nikapanga baadhi ya nguo zangu kwenye begi. Nilikuwa na akiba ya pesa nilizokuwa nimeziweka kwenye kabati. Nikazichukua.

Kwa vile kichwa kilikuwa kimenichafuka, nilimuachia funguo mwenzangu wa upande wa pili nikaenda kulala gesti.

Kitu ambacho kilinikera sana, niliota Zena amesimama kwenye jangwa akinicheka. Alikuwa akinicheka hadi anayumba kama mlevi.

Asubuhi kulipokucha nilitoka nikaenda kituo cha mabasi. Nilipanda basi la kuelekea Dar. Nilifika Dar saa sita mchana nikaenda kutafuta gesti. Nilipopata gesti niliacha begi langu na kwenda kwenye mkahawa uliokuwa karibu kupata chakula kwani sikuwa nimekula chochote tangu subuhi.

Baada ya kula chakula nilirudi pale gesti. Kulikuwa na mgeni mmoja wa kipemba aliyekuwa amepangisha chumba. Tulikutana ukumbini. Nikamsalimia na kumuuliza kama alikuwa anatoka Zanzibar.

“Natoka Mwanza, ndio niko safarini kuelekea Zanzibar” akaniambia.

“Unakwenda Unguja au Pemba?”

“Mimi naenda Pemba”

“Unatarajia kwenda lini?”

“Kesho asubuhi Mungu akipenda”

“Basi tutaondoka sote, nilikuwa na tatizo linalohusu huko Pemba na nitakueleza”

“Ni tatizo gani?”

“Hebu njoo huku chumbani kwangu nikueleze”

Yule mtu alikubali kuingia chumbani kwangu. Nikamueleza yale matatizo yangu.
ITAENDELEA KESHO hapahapa kwenye uhondo wa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment