SIMULIZA ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 44
ILIPOISHIA
Kwa sababu ya njaa niliyokuwa
nayo nilikula sana
mpaka nikahisi kwammba ningevimbiwa. Pilau ilikuwa nyingi hatukuimaliza.
Nilimuacha Mapama akiendelea
kula.
“Ukiwa katika hali ya baridi
unatakiwa ule sana”
Mapama aliniambia.
Tonge zake zilikuwa kubwa na
nilihisi alikuwa akimeza bila kutafuna.
Alipotosheka na yeye
aliiacha. Akairudisha sinia kwenye kabati.
Baada ya kuosha mikono Mapama
alinipa maji ya kunywa nikayanywa. Na yeye akanywa.
“Sasa baridi hatutaisikia.
Tunaweza kuendelea na safari” Mapama akaniambia.
Tukakaa na kuendelea
kuzungumza. Mara moja moja alikuwa akitazama mitambo. Nilikuwa nimejifunza
kwamba boti haikuwa ikiendeshwa kama gari.
Haihitaji kushikiliwa sukani
wakati wa kuendesha. Unaweza kuweka muelekeo wako na ukaiacha iende yenyewe.
Ndivyo Mapama alivyokuwa
akifanya. Hatimaye Mapama alianza kusinzia. Alikuwa akisinzia huku akishituka.
“Nikuache uangalie, mimi
najinyoosha kidogo” akaniambia.
Nikajua kuwa pilau aliyokuwa
ameila kwa wingi ilikuwa imemlewesha.
“Wewe lala, baadaye
nitakuamsha” nikamwambia.
Mapama akajitupa chini. Baada
ya muda kidogo nilimsikia akikoroma.
Huku boti ilikuwa ikiendelea
na safari. Masaa yalipita. Saa yangu ilikuwa imesimama kutokana na kuingia maji
ya chumvi, sikuweza kujua ilikuwa saa ngapi.
SASA ENDELEA
Mawazo yangu yalikuwa ni
kurudi kwetu salama. Nilijiambia Zena alikuwa amenifikishia mkasa wa kutatanisha
sana ambao sikutegemea kama
ungenitokea.
Niliamini kuwa siku zangu za
kufa bado zilikuwa mbali, vinginevyo ningelikwishakufa.
Kama nisingekufa kwenye ile ajali ya meli, ningekufa
wakati Zena ananikokota baharini. Na kama
nisingekufa baharini, ningekufa kwenye kile kisiwa chenye majoka na baridi.
Lakini bado, japo
nilinusurika kote, wale washenzi wenye ile boti wangeniua kama
walivyowaua wale polisi waliowatosa. Na kama
hawakuniua ningeuliwa na lile joka lililowaua watu wote na kumbakisha Mapama na
mimi. Mpaka muda ule nilishindwa kujua joka lile lilitoka wapi na pia
nilishindwa kujua jinsi nilivyonusurika.
Kusema kweli niliona
kunusurika kwangu kulikuwa kwa ajabu sana.
Wakati nikiwa kwenye
mchanganyiko huo wa mawazo huku macho yangu yakitazama mbele tunakoelekea,
niliona kitu kama kimulimuli kikielekea upande
wetu. Nikashituka na kuangaza macho vizuri.
“Nini kile?” nikawa najiuliza
kimoyo moyo.
Baadaye kidogo niligundua
kuwa ilikuwa boti iliyokuwa na kimuli muli na ilikuwa na maandishi yaliyosomeka
POLISI KENYA.
“Mama yangu we!”
Kwa haraka nikamuamsha
Mapama.
“Hebu amka uone!”
“Nini?” Mapama aliniuliza
akiwa bado amefumba macho.
“Polisi. Kuna boti ya polisi
inatuufuata. Amka!” nikamwambia.
“Polisi?”
“Tunafuatwa na boti ya
polisi!”
Mapama akainuka.
“Iko wapi?” akaniuliza.
“Inakuja, imewasha
kimulimuli. Simama uione”
Mapama akainuka na kuitazama
ile boti kwenye kioo. Nilidhani angeanza kubabaika kama
nilivyokuwa nikibabaika mimi. Badala yake nilimuona akiizima boti na kujipekua
mifukoni. Alitoa burungutu la pesa za Kenya akalishika mkononi.
“Usiogope” akaniambia na
kuongeza.
“Watakwenda zao sasa hivi”
Ile boti ya polisi
ikatufikia. Ikawa ubavu kwa ubavu na boti yetu. Mapama akalirusha lile
burungutu la noti kwenye ile noti. Polisi mmoja akalidaka. Hapo hapo nilimsikia
akisema.
“Safari njema”
Mapama akaiwasha boti.
Tukaendelea na safari. Ile boti nayo ikaelekea upande mwingine.
“Wale wanataka pesa tu”
Mapama akaniambia na kuongeza.
“Kila tunapokuja huku tajiri
wetu anatupa pesa maalum kwa ajili ya kuwapa polisi wa Kenya wanaofanya doria baharini.
Wao wenyewe wanajua, wakiiona hii boti wanafuata pesa tu. Hawakagui kitu”
“Mimi nilikuwa na wasiwasi sana. Nilijua tutaishia
polisi”
“Hapana. Hizi ni kazi zetu za
kila siku, lazima tujuane na polisi. Huwezi kuvuka kwenda Somalia bila kukupamba nao”
“Kile kimulimuli kilinitisha
kweli”
“Ile ni mikwara tu ya kutaka
pesa. Hebu iangalie kama utakiona tena
kimulimuli”
Nikatazama upande ule
ilikoelekea ile boti. Sikuona kimulimuli wala sikuiona boti yenyewe.
“Boti yenyewe haionekani
tena”
“Ni kwa sababu wamekizima
kimulimuli”
“Huko Somali itakuwaje
sijui?”
“Hakuna tatizo. Huyo
tunaempelekea huu mzigo ni mtu mzito sana.
Serikali pia inamjua”
Baada ya hapo tukabaki kimya.
Hatimaye aflfajiri ilianza
kuchomoza. Sikuona dalili yoyote ya kufika Somalia. Usingizi ukaanza kuniuma.
“Uliniambia tutaingia Somalia
wakati wa alfajiri” nikamwambia Mapama.
“Bado kidogo, usiwe na
wasiwasi”
“Nasikia usingizi”
nikamwambia.
“Lala kidogo”
Nikajilaza pale chini.
Usingizi ukanichukua hapo hapo.
Mpaka nakuja kuzinduka
lilikuwa jua la utosi. Mapama ndiye aliyeniamsha. Boti ilikuwa imesimama na
kulikuwa na boti nyingine kubwa iliyokuwa imesimama kando ya ile boti
tuliyokuwamo. Ilikuwa boti kubwa na nzuri.
“Tumeshafika?” nikamuuliza
Mapama.
Sikujua kabisa kuwa Mapama
angenigeuka na kunisaliti kwa magaidi..
Bila shaka, zile boti ndio
zilikuwa zimekutana. Ile boti ya pili ilikuwa ndiyo ile ambayo Mapama
aliniambia tutakutana nayo tutakapoingia Somallia ili ifaulishe ule mzigo wa
pembe za ndovu.
Wakati ule namuuliza Mapama kama tumeshafika, niliona mtu mmoja akitoka katika boti
ile ya pili na kuingia katika boti ya Mapama. Alikuwa kijana. Ingawa alikuwa
mwembamba alionekana kunawiri na alivaa mavazi yalliyompendeza japo shati
alilovaa lilionekana kubwa kutokana na wembamba wake.
Alikuwa Msomali mweusi mwenye
nywele za singa. Mkono mmoja alikuwa ameshika kichanga cha mirungi aliyokuwa
akitafuna na mkono mwingine alishika sigara iliyokuwa ikifuka moshi.
Katika kiganja cha mkono wake
wa kushoto alivaa pete kubwa iliyokuwa inang’ara.
Niliukadiria umri wake
kutozidi miaka thelathini na mitano. Alikuwa amenizidi kiumri kidogo.
Kijana huyo alisalimiana na
Mapama aliyekutana naye nje ya kile kijichumba nilichokuwemo. Nilimshangaa
Mapama kwa jinsi alivyokuwa ametaharuki kiasi kwamba alipuuza hata kunijibu
nilipomuuliza kama tumeshafika. Alikuwa
amebadilika kabisa. Niliona kama hakuwa mwenzangu tena.
Aliposalimiana na yule
msomali alimuonesha ule mzigo wa Pembe. Msomali huyo aliutazama kisha
akamuuliza.
“Wenzako wako wapi?”
“Nilikuja nao lakini tulipata
matatizo makubwa”
“Matatizo gain?”
“Nitakueleza. Wambie jamaa
wafaulishe huu mzigo”
Msomali huyo alitumia lugha
ya kisomali kuwambia wasomali wenzake waliokuwa katika ile boti ya pili waingie
katika boti ya Mapama na kufaulisha ule mzigo. Wasomali hao walioonekana kama wapagazi wakaingia na kuanza kazi.
Mapama na yule msomali
niliyemdhania kuwa ndiye tajiri wa ule mzigo wakaingia katika ile boti
nyingine. Sikujua walikwenda kuzungumza nini. Baada ya muda Mapama alirudi peke
yake na kuniambia.
“Yule jamaa anataka kukuona?”
“Jamaa gani?” nikamuuliza.
“Yule msomali niliyekuwa
nazungumza naye”
“Kwani mimi nahusikaje?”
“Sasa utakwenda au utaleta
ubishi?” Mapama akaniuliza kwa ukali.
Kabla sijamjibu, Msomali
mwenyewe akatokeza kwenye ile boti na kuninyooshea mkono kama
ishara ya kuniita, nikaenda. Niliingia katika ile boti akanishika mkono na
kuniingiza katika chumba kilichokuwa katika boti yake.
Chumba hicho kilikuwa kikubwa
kuliko cha boti ya Mapama na kilikuwa kizuri kilichozungukwa na kuta za vioo.
Ndani kilikuwa na sehemu ya kulala na makochi ya kukalia.
“Karibu, kaa hapo” Msomali
akaniambia akinionesha moja ya makochi yaliyokuwa katika kile chumba.
Nikakaa.
“Asalaam alaykum” Msomali
akaniambia huku akiketi upande wa pili wa chumba hicho.
“Waalaika Salaam” nikamjibu
kwa sauti iliyonywea huku nikimtazama usoni kwake.
“Nimeelezwa na Nahodha kuhusu
wewe na mkasa uliowatokea mlipokuwa mnakuja. Ameniambia kulitokea joka kama nondo na kuwaangamiza wenzake, ni kweli?”
“Ni kweli”
“Kwani walitaka kukufanya nini?”
“Walitaka kuniua”
“Wapumbavu wale, mtu unaomba
msaada wanataka kukuua. Sasa hilo
joka lilitoka wapi?”
Nikabetua mabega yangu.
“Sijui”
“Bila shaka hilo ndilo lililokuokoa usiuawe, ungekuwa
umeshatoswa na kuliwa na papa”
Hapo sikumjibu kitu.
“Wewe unaitwa Umar?” Msomali
akaniuliza.
“Hapana”
“Unaitwa Amiri?”
“Hapana”
“Basi utakuwa unaitwa Amour”
Nikamkubalia.
“Ndio naitwa Amour,
umejuaje?”
Msomali huyo akacheka. Badala
ya kunijibu akaniambia.
“Nataka twende Somali mara
moja”
Nikashituka na kumuuliza.
“Kwani hapa tuko wapi?’
MAMBO HAYO! PANA FUMBO GANI
HAPA?
LEO NIMEWAPA NDEFU KWELI ILI KUTULIZA KIU YENU LAKINI ITABIDI TUKUTANE TENA KWSHO
No comments:
Post a Comment