HADITHI na FAKI A FAKI 0715 340572
MWANAMKE 8
ILIPOISHIA
Polisi huyo alinionesha
kikaratasi kilichokuwa kimeandikwa namba za usajili za pikipiki yangu.
“Ndiyo” nikamkubalia polisi
huyo baada ya kukiangalia kile kikaratasi.
“Tunakuhitaji wewe na hiyo
pikipiki yako”
“Mimi nina nini na pikipiki
yangu ina nini?” nikawauliza.
“Uliwahi kufanya makosa ya
barabarani wiki mbili zilizopita”
“Sijawahi kufanya kosa lolote
labda mmeifananisha pikipiki yangu”
“Tutajua huko kituo cha
polisi. Kwa sasa tutaondoka na wewe twende nyumbani kwako tuichukue hiyo
pikipiki, twende nayo kituo cha polisi”
Sikuwa na la kupinga.
Nikakakamatwa. Polisi hao ambao walikuja na gari lao walinipakia kwenye gari hilo, nikaenda nao
nyumbani kwangu.
Niliwatolea pikipiki yangu,
walipoiona tu wakasema ndiyo waliyokuwa wanaitafuta kwa karibi wiki mbili.
Nikafikishwa kituo cha
polisi. Huko ndiko nilikoelezwa kuwa tarehe fulani siku fulani nilisababisha
ajali eneo la Mabanda ya Papa baada ya kuendesha pikipiki kwa uzembe na kuvunja
sheria za barabarani.
Nikaelezwa kuwa kutokana na
uzembe wangu wa kutosimama mahali ambapo nilipaswa kusimama ili nipishe gari
lililokuwa linatoka kuliani kwangu, nilisababisha gari hilo aina ya Toyota Landa
Cruiser linikwepe na kugonga nguzo ya umeme na kutumbukia kwenye mfereji.
Ingawa nilijitahidi kukana
kosa hilo
nilifikishwa mahakamani baada ya kulala ndani kwa siku moja. Katika mahakama ya
Chumbageni nikashitakiwa kwa makosa matatu.
Kosa la kwanza lilikuwa
kuendesha kwa uzembe, kosa la pili kusababisha ajali na kosa la tatu kuharibu mali
na kulitia hasara shirika la Umeme iliyokadiriwa kufikia shilingi milioni kumi
na mbili.
Niliyakana mashitaka yote na
kumuomba hakimu anipe dhamana. Ndugu zangu walikuwa wamejitokeza kutaka
kuniwekea dhamana.
SASA ENDELEA
Hakimu aliruhusu dhamana
iliyokuwa na masharti magumu. Hata hivyo ndugu zangu walimudu masharti yote
waliyopewa wakanitoa.
Shauri hilo lilikuwa limeahirishwa kwa wiki moja.
Nilipoachiwa kwa dhamana ndugu zangu walinipeleka nyumbani kwa mama yetu ambaye
wakati huo alikuwa yuko hai. Nikawaeleza mkasa uliokuwa umenitokea kuanzia kisa
kile cha Zena aliponipeleka nyumbani kwake hadi siku ile nilipomuona tena na
kusababisha ile ajali.
Mama yangu na ndugu zangu
walishangaa waliposikia kisa hicho.
“Inabidi uende kwa mganga,
huyo jini atakuletea matatizo” Mama akaniambia.
“Tatizo la Amour nikuwa ana
usiri sana,
kwanini hakutueleza tangu mapema?” kaka yangu akanilaumu.
“Sikujua kama
yangekuwa makubwa kiasi hiki?’ nikajitetea.
Jioni ya siku ile nikapelekwa
kwa mganga mmoja aliyekuwa akiishi Mnyanjani. Nilikuwa mimi, mama yangu na kaka
Abdul.
Tukamueleza mganga tatizo
langu. Mganga akatazama ramli kisha
akatuambia.
“Amour amekumbwa na jini
anaitwa Ummi Subian, ni jini wa kike ambaye amemfanyia vitisho na kumsababishia
kukabiliwa na kesi”
“Huyo jini ataendelea
kumfuata tena?’ Mama yangu akamuuliza mgamga.
“Alilolitaka huyo jini ameshalipata, hatamfuata
tena kwa sababu anajua atafungwa. Hii kesi imemkalia vibaya” Mganga akasema.
“Sasa tunataka kuizima hii
kesi, itawezekana?’ Abdul akamuuliza mganga.
“Itawezekana. Hakuna
kisichowezekana”
“Tunataka utufanyie hiyo
kazi, itagharimu shilingi ngapi?”
“Itgharimu shilingi laki moja
na mbuzi mweusi”
“Punguza kidogo. Shilingi
laki moja hatuna”
“Sipunguzi. Kama
nilivyowambia hii kesi imekaa vibaya. Kazi inayotakiwa ni kubwa”
“Haya, tutatoa hiyo shilingi
laki moja”
“Ninataka na mbuzi mweusi na
kipande cha kaniki.
Siku muafaka wa kazi yenu ni jumamosi”
“Kwa hiyo tuje jumamosi”
Abdul akamuuliza.
“Mje siku ya jumamosi saa
mbili asubuhi pamoja na hivyo vitu”
“Sawa. Tumekuelewa.
Tukaondoka.
Siku ya jumamosi tukaenda
tena kwa mganga huyo. Tulienda na gari aina ya Toyota ya wazi. Tulikuwa tumepakia mbuzi
tuliyekuwa tumeagizwa.
Tulipofika, wasaidizi wa
mganga huyo walitupokea tukakaribishwa ndani. Baada ya muda kidogo mganga
akaanza kazi. Kazi ilianzia pale nyumbani kisha
ikahamia makaburini.
Yule mbuzi alichinjwa
akavalishwa ile kaniki
na kuzikwa kwenye kaburi.
Mganga akatuambia.
“Kesi nimeshaizika”
“Sasa nitaachiwa au..”
nikamuuliza.
“Utakwenda kusikia huko huko
lakini kwa upande wangu hakuna kesi tena”
“Tunashkuru kama
itakuwa hivyo” Mama akamwambia mganga.
Tuliporudi nyumbani kwa
mganga tulimpa ile shilingi laki moja aliyotaka tukaondoka.
Nilipata matumaini sana, ingawa sikuwa na
uzoevu na mambo ya kwenda kwa waganga. Tarehe ya kesi ilipowadia nilifika
mahakamani nikasomewa tena mashitaka yangu, nikayakana.
Hakimu akasema alikuwa tayari
kuanza kusikiliza shauri hilo.
Upande wa mashitaka ukaeleza
kwamba ulikuwa na mashahidi ambao walikuwa tayari kutoa ushahidi wao.
Hakimu akataka mashahidi hao
waanze kuitwa ili watoe ushidi wao.
Akaitwa shahidi wa kwanza
ambaye ni dereva wa Toyota
iliyogonga nguzo ya umeme.
Akaeleza jinsi tukio zima
lilivyotokea.
Baada ya kumaliza kutoa ushidi
wake ikafika zamu yangu ya kumuuliza maswali.
“Unamjua huyo mtu aliyekuwa
akiendesha hiyo pikipiki?” nikamuuliza.
“Ninamjua” akajibu.
“Ni nani?”
“Ni wewe”
“Nani
alikwambia kwamba ni mimi?”
“Nilikuona mwenyewe”
“Ulipata muda gani wa kuniona
na kunikariri wakati umesema gari lako liliingia kwenye mfereji na mimi
nilikimbia?”
“Nilikuona kabla”
“Sasa mimi nakwambia siye
huyo mtu, mmenifananisha tu”
“Ni wewe”
Baada ya mtu huyo kutoa
ushahidi wake aliitwa shahidi mwingine, muuza machungwa katika eneo la Mabanda
ya Papa.
Kumbe yeye ndiye aliyekuwa
amewatajia polisi namba za pikipiki yangu. Siku ile ya ajali aliniona na
aliiona pikipiki yangu. Akaieleza mahakama kuwa amekuwa akiniona mara kwa mara
nikipita na pikipiki katika eneo lile.
Huku akiongozwa na Mwendesha
Mashitaka wa serikali shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa siku na tarehe hiyo
alikuwa akiuza machungwa yake jirani na Barabara ya Pangani katika eneo hilo la Mabanda ya Papa.
“Nini kilitokea?” Mwendesha
Mashitaka akamuuliza.
“Ilitokea
ajali”
“Ilitokea
ajali gani? Hebu tueleze”
“Kulikuwa na pikipiki moja
inakuja kutoka barabara ya Taifa. Ile pikipiki ilitakiwa isimame kwenye
mzunguko wa barabara nne uliopo pale lakini haikusimama”
“Baada ya hapo nini
kilitokea?’
“Kulikuwa na gari aina ya Toyota
Land Cruicer likitokea
Gofu, lilikuwa linapita kwenye ule mzunguko likalazimika kuikwepa ile pikipiki.
Katika kuikwepa pikipiki, gari hilo
lilikwenda kugonga nguzo ya umeme”
“Baada ya kugonga nguzo ya
umeme lilikwenda wapi?”
“Liliingia kwenye mfereji”
“Ni athari gani ilitokea
baada ya nguzo ya umeme kugongwa?”
“Kwanza
nguzo yenyewe ilivunjika halafu baadhi ya nyaya zilikatika na nyingine zilitoa
cheche za moto hali iliyosababisha mfadhaiko mkubwa”
“Wakati tukio hilo linatokea, mwenye
pikipiki alisimama”
“Hapana, hakusimama. Alipita
moja kwa moja na kuendelea na safari yake”
“Wewe uliiona hiyo pikipiki?’
“Ndiyo niliiona”
“Ilikuwa
ni aina gani”
“Kama
sikosei ilikuwa aina ya Honda ya rangi nyeusi”
“Namba
yake ya usajili
uliiona”
“Niliiona”
Akaitaja. Ilikuwa
ndio namba ya pikipiki yangu.
DUH! JAMAA NDIO AMEKWISHA! HEBU FUATILIA HAPO KESHO UJUE NINI KITATOKEA?
HAYA YOTE UNAYAPATA KATIKA
BLOG YAKO HII YA TANGA KUMEKUCHA
No comments:
Post a Comment