Tuesday, June 7, 2016

WAFANYABIASHARA WENYE VIWANDA TANGA WAPEWA SOMO



Tangakumekuchablog
Tanga, MKUUwa Wilaya ya Tanga, Abdallah Lutavi, amewataka wafanyabiashara wenye viwanda Tanga kutangaza biashara zao ndani na nje ya nchi na kutobweteka na soko la ndani.
Pia amewataka wajasiriamali wadogo wadogo kulitumia soko la  pamoja la Afrika Mashariki (EAC) kwa kutangaza biashara zao na kupata uzoefu kutoka kwa wenzao ndani ya soko hilo la pamoja.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa maonyesho ya nne ya Kimataifa (Tantred), Lutavi amewataka wafanyabiashara hao kuyafuata masoko na kuacha kusubiri wateja kuwafuata viwandani kwao.
Alisema siri ya kukua kwa masoko ya bidhaa ni kuwa tayari kuyafuata  popote yalipo  kwa njia ya maonyesho na kujitangaza jambo ambalo linaweza kuongeza kasi ya ukuaji wa soko  na uzalishaji.
“Kuna ushindani mkubwa wa bidhaa za viwandani na zile za wajasiriamali wadogo wadogo katika masoko ya ndani na nje ya nchi, ila tukumbuke kuwa siri ya mafanikio ni kujitangaza” alisema Lutavi na kuongeza
“Tusiogope kuingia katika masoko ya ushindani na tujitambue kuwa bidhaa zetu ziko na ubora zaidi ya wao ila kwa woga ndio sababu ya wenzetu kupiga hatua na kuonekana za kwao ni bora zaidi yetu” alisema
Alisema Serikali iko na mpango wa kuvifufua viwanda vilivyokufa Tanga hivyo kuwataka wenyeji kujifunga vibwebwe hasa baada ya ujio wa mradi wa bomba la mafuta na kuwaachia mwanya wageni kutoka nje.
Kwa upande wake , Mwenyekiti wa TCCIA, Deogratius Mhumba, aliwataka wajasiriamali wadogowadogo Tanga kuwa wabunifu wa kazi zao na kuingia katika masoko ya ushindani.
Alisema wajasiriamali wengi wa kazi za mikono  hawatambuliki baada ya kazi zao kuzikalia majumbani hivyo kushindwa kutambulika na kuwataka kuwaiga wenzao ndani ya Jumiya ya Afrika Mashariki.
“Tuko na wajasiriamali wazuri wa kazi za mikono lakini hawatambuliki si ndani wala nje ya nchi , wamekuwa wakizikalia kazi zetu  majumbani badala ya kuzitangaza hata katika mitandao “ alisema Mhumba
Aliwataka wajasiriamali hao kuwa na ujasiri wa kuthubutu kwa kuyafuata masoko na kutangaza kazi zao nje ya nchi na kuwa tayari kupoteza gharama ambazo baadae faida yake inaonekana.
                                           Mwisho

No comments:

Post a Comment