SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572
MWANAMKE 35
ILIPOISHIA
Kwa wakati ule Salama alikuwa
akifanya kazi Shirika la Posta. Nikapanga nimfuate nizungumze naye ili
nimueleze nia yangu ya kupeleka posa yangu kwa wazazi wake.
Siku iliyofuata nikaenda
kazini. Saa nne wakati wa kwenda kunywa chai nikaenda posta. Nikamkuta.
Nilisubiri watu wawili
aliokuwa akiwahudumia walipoondoka nikamsalimia.
“Hujambo mrembo?”
“Sijambo, sijui wewe”
“Mimi ni mzima tu kama unavyoniona, hivi kule Chumbageni unaishi mtaa
gani?” nikamuuliza.
Salama akanielekeza mtaa
anaoishi. Kwa vile na mimi nilikuwa mwenyeji wa mitaa ya Chumbageni niliifahamu
mpaka nyumba waliyokuwa wanaishi.
“Si ile inayotazamana na
Cumbageni Guest House?” nikamuuliza.
“Ndiyo hiyo hiyo”
“Natarajia kutuma mshenga
kwenu” nikamdokeza.
Salama hakunijibu kitu.
Nikaridhika. Kuwa kimya inachukuliwa na masheikh wa kiislamu kuwa ni ishara ya
kukubali, kwa vile suala hilo
tulishalizungumza.
Nilipotoka kazini jioni
nilikwenda kwa kaka nikamueleza kuhusu msichana huyo.
“Umeshazungumza naye”
akaniuliza.
“Niliwahi kuzungumza naye
siku nyingi lakini ilikuwa kama mzaha, leo ndio
nilimfuta kazini kwake nikamwambia kuwa nitatuma mshenga kwao akanyamaza.
Nimechukulia ishara kwamba amekubali”
“Sasa tujaribu kupeleka
ujumbe kwao?”
“Ndio hivyo”
SASA ENDELEA
“Kwa hiyo utaandika barua
utaniletea hapa, halafu mimi nitatafuta mzee mmoja niende naye. Unasema anaishi
wapi?’
“Anaishi chumbageni lakini
usiku tutakwenda kama tunapita njia ili nikuoneshe nyumba yao”
“Sawa, utanifuata saa ngapi?’
“Saa mbili usiku”
“Nitakusubiri”
Baada ya mazungumzo yetu na
kaka nikarudi nyumbani. Saa mbili usiku nikamfuata tena na pikipiki yangu.
Nilimpakia na kwenda kumuonesha ile nyumba aliyonielekeza Salama. Nilipata
uhakika kwamba sikuikosea kwani tulimkuta baba yake ambaye namfahamu, ameketi
barazani kwenye kiti cha uvivu akivuta mtemba wake.
Tukapita na pikipiki yetu.
Wakati tunarudi kaka
alinaimabia.
“Kama
nyumba ni ile nimeshaiona”
“Na yule mtu uliyemuona
ameketi barazani kwenye kiti cha uvivu ni baba yake”
“Kumbe baba yake ni yule
mzee?”
“Ndio yule”
“Basi tutamuona hapo kesho”
Nikamrudisha kaka nyumbani
kwake, akanisisitizia tu nisisahau kuandika barua ya posa.
Nilipofika nyumbani
niliiandika barua hiyo usiku ule ule nikaitia ndani ya bahasha. Kwa kawaida
barua za posa kama zile huwekwa kitu kidogo.
Nikatia shilingi elfu hamsini.
Asubuhi wakati naenda kazini
nikaipeleka ile barua kwa kaka. Kaka aliifungua kwa vile sikuwa nimeifunga
kabisa. Aliisoma kisha akaniambia.
“Umeiandika vizuri”
“Nimeweka na shilingi elfu
hamsini, sijui zinatosha”
“Zinatosha, hizi huwekwa kama ada tu”
“Sawa, sasa mimi naenda
kazini utatafuta mtu wa kwenda naye”
“Barua yako itafika leo leo”
Nikaenda zangu kazini.
Saa nne nikaenda posta kwa
Salama. Baada ya kusalimiana naye nilimwambia.
“Ujumbe wangu utaupata leo”
Salama akatabasamu.
“Naungojea” akaniambia.
Nilikuwa na hakika kwamba alijua ni mzaha wangu.
Jioni nilipotoka kazini
nilikwenda kwa kaka. Akaniambia.
“Barua yako imefika”
“Umeshaipeleka?” nikamuuliza
kwa tashiwishi.
“Tuliipeleka mchana. Mzee
ameniambia nifuatie majibu kesho”
“Hakukuwa na maswali yoyote
aliyokuuliza?”
“Kuuliza ni lazima.
Aliniuliza ile posa ilikuwa ni ya nani wangu. Nikamjibu ni ya mdogo wangu.
Akaniuliza anafanya kazi wapi nikamueleza. Akataka pia kujua unaishi wapi
nikamueleza”
“Yule mzee hatufahamiani
isipokuwa nafahamiana na binti yake”
“Aliuliza pia kama wewe ulishamueleza binti yake kuhusu nia yako”
“Ukamjibu nini?”
“Nilimwambia mlishazungumza
na mlikubaliana. Akaniambia kwamba atazungumza naye na kwamba nifuatie majibu
kesho”
“Kwa hiyo mtaenda tena hapo
kesho?”
“Tutakwenda”
“Sawa kaka”
Jioni yake niliporudi kazini
nikapitia kwa kaka kupata majibu.
Akaniambia. “Kazi
imekamilika”
“Kivipi?” nikamuuliza.
“Posa yetu imekubaliwa. Mzee
ameniambia wanataka mahari ya shilingi laki tano”
“Mahari yake ni shilingi laki
tano?” nikamuuliza kwa mkazo.
“Inaelekea yule mzee msomi.
Amesemi yeye hana mambo ya Kiswahili. Hakutaka kututajia gharama kubwa. Mimi
naona laki tano si nyingi”
“Sawa”
“Mimi mchango wangu
nitakusaidia shilingi laki moja”
“Mimi mwenyewe nitatoa laki
nne”
“Lini zitapatikana hizo laki
nne”
“Hata kesho zinaweza
kupatikana”
“Utaniletea asubuhi?”
“Nitakuletea jioni, wewe
utazipeleka kesho kutwa”
“Sasa tupange harusi, sipendi
uchumba wenu uchukue muda mrefu sana”
“Tukishalipa hizo pesa
tutakaa na mama tupange harusi itakavyokuwa”
“Sawa jitahidi upate jiko
lako”
“Nitajitahidi kaka”
Nikaagana na kaka na kwenda
nyumbani kwa mama. Nilimueleza ile habari. Akaniambia ameshaelezwa na mwanawe,
yaani kaka yangu.
“Ni jambo zuri” akasema.
“Kesho kutwa tutakuja kufanya
kikao cha harusi hapa kwako”
“Kwani mambo tayari?’
“kaka atapeleka mahari kesho
kutwa”
“Hizo shilingi laki tano?”
“Ndio”
“Umeshampa?”
“Nimemwambia nitampa kesho”
“Yeye atakusaidia shilingi
ngapi?’
“Ameniambia atanitolea
shilingi laki moja, mimi mwenyewe nitatoa laki nne”
“Kwa hiyo mnasubiri mmpeleke
mahari ndio tufanye kikao”
“Ndiyo”
“Mimi nawaunga mkono.
Nilitaka sana
wewe uwe na mke. Hilo
wazo nililitoa mimi”
“Lilikuwa wazo zuri na
natumaini nikiwa na mke matatizo yangu yatapungua’
“Utakuwa vizuri mwanangu”
“Sawa mama, basi mimi narudi
nyumbani”
Nikaagana na mama na
kuondoka.
JAMANI MNATAKA MSOME UPANDE
WA ZENA TU, LAKINI HUU UPANDE
WA AMOUR MNATAKA UPITE HARAKA
HARAKA. KWELI AU SI KWELI?
BASI KESHO MTAMUONA ZAINUSH
BINTI JABALKEYSS
No comments:
Post a Comment