Thursday, July 7, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 37

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572

MWANAMKE 37

ILIPOISHIA

Nakumbuka hadi leo jinsi sheikh mmoja alivyonifungisha ile ndoa.

Aliniita jina langu kisha akaniambia nimuitikie “Labaika”

“Labaika” nikamuitikia.

Akaniita tena.

“Amour Amrani”

“Labaika” nikamuitikia.

“Ninakuozesha Salama binti Riyami kwa mahari mliyokubaliana, umekubali?”

“Ndiyo” nikamuitikia huku midomo yangu ikitetemeka. Sikujua ilitetemeka kwa sababu gani.

“Hapana. Hilo silo jibu linalotakiwa ujibu. Unatakiwa useme nimekubali kumuoa Salama binti Riyami kwa mahari tuliyokubaliana”

“Sawa”

“Amour binti Amraani” Sheikh akaniita tena.

“Labaika”

“Ninakuozesha Salama binti Riyami kwa mahari mliyokubaliana, umekubali?”

Nikayakumbuka yale maneno aliyonifundisha.

“Nimekubali kumuoa Salama binti Riyami kwa mahari tuliyokubaliana” nikajibu.

Sheikh alirudia tena kuniambia hivyo mara  tatu na mimi nilijibu mara tatu. Baada ya hapo ikasomwa hutuba ya ndoa iliyochukua karibu nusu saa.

SASA ENDELEA

Baada ya ndoa kufungwa nilipewa mawaidha. Niliambiwa siku ile nimeoana na Salama kwa wema, kwa hiyo niishi naye kwa wema na kumpa huduma zote zinazopaswa kutolewa kwa mke.

Sheikh aliendelea kuniambia kuwa kama itabidi kuachana, pia tuachane kwa wema kwani hivyo ndivyo ambavyo tumeusiwa na mtume wetu.

Baada ya hapo halua na tende pamoja na visheti ziikagaiwa. Watu wakala na kufurahi.

Baada ya shughuli kumalizika tukaenda nyumbani kwa mke. Nilikuwa nimekodi magari matano. Tulipofika tulikuta shamra shamra zikiendelea. Tuliingia chumbani kwa mke wangu aliyekuwa amepambwa vilivyo.

Nikampa mkono. Hapo hapo sheikh akatuombea dua na kututakia afya njema na maisha mema ya ndoa. Tulipiga picha za kumbukumbu zikiwemo za mnato na za video.

Ikafuatia pilau. Mimi na mke wangu tuliletewa sahani ya pamoja na jagi la juisi.

Tulishindwa kula sana kwa sababu ya zile hekaheka. Si unajua siku ya ndoa mtu unapata fadhaa kidogo.

Baada ya shughuli zote kumalizika, mtu aliyekuwa amesimamia ndoa upande wangu alitaka tuondoke. Wenyeji wetu wakapinga na kutaka tuendelee kuwepo kwa vile sherehe ilikuwa ikiendelea.

“Hapana, sisi hatukufuata sherehe hapa. Tumekuja kuoa” Msimamizi wangu alisema.

“Na ndoa ni sherehe, kama mtaondoka mapema hakutakuwa na sherehe tena” alijibiwa na msemaji wa upande wa mke wangu.

“Tatizo ni nini? Kama tumeshaoa tunachukua mke wetu tunaondoka” Msimamizi wangu akachachamaa.

“Msiondoke jamani, sherehe bado zinaendelea. Mkiondoka nyinyi mtatukatisha”

Msimamizi wangu akanishika mkono na kuniinua.

“Sisi tunaondoka. Nyinyi endeleeni na sherehe zenu. Na sisi huko tuna sherehe zetu”

Tukatoka.

“Jamani mnaondoka!” Wenyeji wetu wakalalamika.

“Waswahili bwana, wanataka tuendelee kukaa hapa, tufanye nini? Kwani sisi hatuna kwetu?” Msimamizi wangu alisikika akisema peke yake.

Tulitoka nje, gari zilikuwa zikitusubiri. Tukajipakia. Mimi nilipanda gari moja na mke wangu pamoja na wapambe wetu.

Gari nyingine mbili zikapanda watu wengine.

Tukaelekea Msambweni ilikokuwa nyumba yangu.

Nyumbani kwangu pia kulikuwa na sherehe. Tulipokewa kwa vifijo na hoihoi. Tulipoingia chumbani. Wapambe wetu wakatuacha.

Sherehe ziliendelea hadi saa sita usiku. Sisi tulikuwa chumbani tumelala.

Nilikuwa nimeomba ruhusa ya siku tatu kazini kwangu. Kwa hiyo nilikaa siku tatu bila kwenda kazini. Katika siku hizo tatu sikuchezea mbali. Muda wote nilikuwa chumbani na mke wangu Salma. Mara chache nilitoka peke yangu na kukaa sebuleni.

Baada ya siku hizo tatu kwisha nilikwenda kazini. Huko nilipata pongezi nyingi sana kwa kupata jiko (kuoa).

Sasa nikawa nimefungua ukurasa mpya wa maisha yangu. Siku za mwanzo mwanzo nilipotoka kazini tu nilirudi nyumbani haraka. Siku za jumapili sikuondoka nyumbani.

Ile tabia ya kula kwenye mikahawa ikaisha, nikawa nakula nyumbani tena chakula kizuri kilichopikwa na laazizi wangu. Naam. Maisha yalikuwa matamu sana!

Ilikuwa imepita miezi mitatu. Usiku mmoja wakati tumelala na Salma, Salama alianza kuweweseka akiwa  usingizini. Nilimuamsha na kumuuliza alikuwa na nini, akaniambia alikuwa anaota kuna msichana mmoja anamuamrisha aondoke pale nyumbani.

“Ananiambia hapa si kwangu, ni kwake yeye” Salma aliniambia.

Nikashituka na kumuuliza.

“Huyo msichana yukoje?”

“Umbo lake ni kama mimi ila yeye ni mweupe sana na ana sura kama muarabu”

Mara moja nikamkumbuka Zena ambaye nilikuwa nimeshamsahau.

“Anakwambia uondoke hapa nyumbani?”

“Ndio. Tena amenishikia bakora, anataka kunichapa”

Ili kumtoa hofu Salama nikajaribu kuzuga.

“Unajua ulikuwa umelala kichali chali halafu ulishiba sana. Lazima uote  ndoto zisizoeleweka”

“Nilaleje sasa?” Salma akaniuliza kwa hofu.

“Lala kiubavu ubavu, elekea huku kwangu” nikamwambia”

Salma alipoelekea upande wangu akaniambia.

“Nikumbatie naogopa”

Nikamkumbatia. Salma hakuchelewa kupata usingizi. Akalala fofo. Mawazo yakabaki kwangu.

Asubuhi tulipoamka nilimuuliza.

“Uliota tena”

“Hapana, sikuota” akaniambia.

Nikashukuru aliponiambia hivyo. Nikajitayarisha kwenda kazini. Muda wangu wa kutoka ulipowadia nikatoka.

Nilichapa kazi hadi saa kumi jioni nikarudi nyumbani. Nilikuta nyumba ilikuwa imefungwa. Funguo nilipewa na mpangaji mwenzangu wa upande wa pili.

“Mke wako aliondoka, akaniachia hizi funguo. Amesema ukija nikupe”

“Amekwambia amekwenda wapi?”

“Hakuniambia”

Nikazichukua zile funguo na kufungua mlango huku nikiwa na mawazo. Nilipoingia chumbani nilikuta karatasi ya barua iliyokuwa imeachwa kitandani. Nikaichukua na kuisoma.

Mwandiko ulikuwa wa mke wangu Salma. Iliandikwa.

“Nimelazimika kuondoka hapa nyumbani ili kuokoa maisha yangu. Ile ndoto ilinijia tena mchana. Nilimuota tena yule msichana. Aliniuliza kwanini sijaondoka. Akaanza kunitandika bakora. Ngozi yangu ya mgongo imeharibika kwa jinsi alivyonichapa. Hali yangu ni mbaya. Ninakwenda hospitali na nikitoka hospitali narudi kwetu. Naomba uniletee talaka yangu. Huyo msichana ninayemuota ameniambia kama nitaendelea kukaa ataniua”

Salama alimaliza barua yake kwa kuweka jina lake.

Kusema kweli maneno ya Salma aliyokuwa ameniandikia yalinishitua sana. Nilipomaliza kusoma barua ile niliona miguu ikininyong’onyea na kuishiwa na nguvu.


UNAJUA BALAA? HILI NI BALAA LINALOMKUTA KIJANA HUYU! HAYA TWENDE NAYE POLE POLE HADI HAPO KESHO TUONE NINI KITATOKEA

No comments:

Post a Comment