SIMULIZI YA FAKI A FAKI
MWANAMKE 40
ILIPOISHIA
Kabla sijamjibu, ule upande
wa boti uliokuwa unazama ukazidi kulala.
“Duh ni kweli, twende
tukaruke, tutakufa humu!” akaniambia huku akiinuka kwenye siti.
Tulikwenda kwenye mlango wa
boti tukatoka. Watu walikuwa wakiendelea kuchupa baharini.
“Chupa!” Zena akaniambia.
Laiti angejua jinsi ambavyo
sikuwa nikijua kuogelea asingeniambia chupa.
Upande wa pili wa boti nao
ikaanza kuzama.
“Chupa, boti inazama!”
akaniambia tena.
Sikuthubutu. Nilibaki
kuitazama bahari.
“Amour unasubiri kufa humu ndani
ya boti?” Zena akaniuliza kwa hasira.
Nikatikisa kichwa.
“Siwezi kuogelea, nikiruka
ndio nimekwisha!”
“Mwanaume mzima unasema
huwezi kuogelea, mimi mwanamke nisemeje?” akaniuliza.
Sikuwa na jibu. Nikaendelea
kutikisa kichwa changu.
Sikujua ilikuwaje. Zena
alinishika mkanda wa suruali yangu kwa nyuma kisha akanirusha baharini. Hadi
leo nashindwa kujua alinirushaje.
Kabla ya kutumbukia baharini,
nilijiambia ule ulikuwa ndio mwisho wangu.
Nilitanguliza mikono na
kichwa, Nikazama chini kabisa.
SASA ENDELEA
kisha nikarudishwa tena juu. Wakati natokeza
juu nilimuona Zena akijirusha baharini. Alichupa kama samaki. Akawahi kunishika
kabla sijazama kwa mara ya pili.
Nilivamia mwili wake ili
nijiokoe kwani pumzi zilikuwa zimeniishia.
“Usinivamie, tutazama sote.
Tuliza akili yako” akaniambia huku akielea juu ya maji.
Niliendelea kumg’ang’ania.
“Usining’ang’anie, tutazama
sote. Shika miguu yangu. Usishike mwili wangu!” Zena alinipigia kelele. Sasa
nilikuwa kama hayawani nisiyejielewa.
Zena alipoona bado simsikilizi
alinipiga ngumi ya shavu, nikamuachia na kuzama chini. Wakati niko ndani ya
maji nikipelekwa chini, Zena alipiga mbizi akaniwekea mgongo wake kwenye kifua
changu kisha akaibuka na mimi juu ya maji.
”Tulia kwenye mgongo wangu,
ukifurukuta nakuacha. Nishike mabega yangu” akaniambia.
Nikafanya vile alivyotaka.
Zena akaanza kuogelea huku
nikiwa kwenye mgongo wake. Yule msichana alikuwa hodari sana.
Aliweza kuogelea kwa mwendo
mrefu akiwa na mimi bila kunidondosha na bila kuonesha kuchoka.
Ile boti iliyokuwa inazama
tuliiacha mbali kabisa.
Zena aliendelea kuogelea tu kama vile alikuwa na mashine iliyokuwa inampa nguvu.
Nikakumbuka maneno ya watu wanaosema
kwamba majini huzaliwa baharini. Nikahisi kuwa
hiyo ndio sababu akawa na uzoevu mkubwa wa kuogelea.
Hatimaye ile boti sikuiona
tena. Sasa nikawa najiuliza tunaelekea
wapi. Sikupata jibu. Jua lilikuwa linakuchwa kwa haraka upande wa magharibi na
tayari lilionekana likitoa mionzi ya kimanjano iliyoashiria kuwa wakati wa
magharibi ulikuwa unakaribia.
Mbele yangu nikaona kitu
kimejitokeza. Baadaye niligundua kuwa tulikuwa tunatokea kwenye kisiwa.
Kilikuwa bado kiko mbali na sisi. Kwanza
nilianza kuona majani ya miti yaliounda
shada kubwa la rangi ya kijani. Halafu nilianza kuona msitu mkubwa.
Kadiri tulivyokuwa
tunakikaribia kisiwa hicho ndivyo nilivyoweza kukiona vizuri. Naam kilikuwa ni
kisiwa. Sasa ardhi yake ilionekana waziwazi. Kilikuwa kisiwa kidogo kilichokuwa
na msitu mkubwa wa miti.
Tulipofika maji madogo Zena
aliniambia niondoke mgongoni kwake.
Sikumsikia vizuri, nilikuwa
nimeendelea kumshikilia. Ile harufu ya udi wa mawaridi niliyokuwa nikisikia
mgongoni mwake ilikuwa imenilewesha.
“Ondoka bwana, mwenzako
nimechoka!” akaniambia kwa sauti ya ukali.
Nikajaribu kuishusha miguu
yangu taratibu, taratibu, nikaona ninakanyaga mchanga lakini maji yalikuwa
yakinifika kwenye kifua. Nikaanza kutembea kwa miguu nikiwa bado nimemshikilia
Zena. Ilibidi nipate kitu cha kushika, vinginevyo maji yangeweza kunikupua.
Niliendelea kutembea hadi
maji yaliponifikia kiunoni ndipo nilipomuacha Zena. Sasa tulikuwa tukitembea
pamoja. Nguo zetu zilitota chapa. Maji ya chumvi yalikuwa yakitutiririka
mwilini.
Tulifika ufukweni mwa kisiwa
hicho. Fukwe yake ilikuwa nzuri yenye mchanga mweupe.
“Hapa ni wapi?” nikamuuliza
Zena.
Zena aliyeonesha wazi kuwa
alikuwa amechoka hakunijibu chochote, aliendelea kwenda hadi tukaingia kwenye
ule msitu.
Zena alitafuta sehemu
iliyokuwa juu akapanda na kujilaza chini.
“Oh leo nimechoka sana. Sijaogelea mwendo
mrefu kama leo” Zena akajisemea peke yake
akiwa amejilaza kichali chali.
Baibui alilokuwa amevaa
lililoa maji na kuonya kama kioo. Nguo
aliokuwa amevaa ndani nayo ilikuwa ikionya kwa sababu ya kutota maji. Ngozi
nyeupe ya mwili wa Zena iliyokuwa na malaika marefu ilikuwa ikionekana wazi
wazi.
Mimi nilikuwa nimeketi
nikihema huku nikiyatembeza macho yangu kila upande wa kile kisiwa. Sikujua
tulikuwa katika kisiwa gani na kilikuwa wapi.
Pia sikujua tungeondokaje
katika kisiwa hicho ambacho hakikuonesha dalili yoyote ya kuishi watu. Nilikuwa
nikijiambia kama kutakuwa na wanayama wakali
wanaweza kutudhuru.
“Unangoja hizo nguo zako
zikaukie mwilini mwako?” Zena akaniuliza.
“Sasa nizifanye nini?”
“Si uzivue?”
“Nizivue nikae uchi?”
“Kwani huna chupi?”
“Acha tu, zitakauka humu
humu”
“Mimi nguo zangu ni nyepezi,
zitakauka mara moja”
Niliyapuuza yale maneno ya
Zena. Akili yangu ilikuwa kwingine. Nilikuwa nikijiuliza jinsi tutakavyoondoka
kwenye kisiwa kile.
“Tutaondokaje hapa?”
nikamuuliza Zena.
Kabla ya Zena kunijibu
nikaona kitu kikitokeza kwenye miti mbele yetu. Nilishituka nilipogundua kuwa
lilikuwa joka kubwa na refu. Lingeweza hata kutumeza mimi na Zena kwa wakati
mmoja.
“Zena! Zena!” nikamuita Zena.
Zena akainua kichwa na
kunitazama.
“Nini?’ akaniuliza.
“Angalia kule!” nikamwambia
huku nikimuonesha lile joka kwa kidole.
Zena akapeleka macho yake na
kuliona.
“Sijakwambia lakini sasa
nakwambia, hiki kisiwa ni cha majini. Lile si joka kama
unavyoliona ni jini limejigeuza joka. Wako wengi tu hapa”
Maneno yake yalizidi
kunitisha.
“Sasa kwanini tumekuja hapa?”
nikamuuliza kwa taharuki.
“Unawaogopa? Si majini
wakubwa kama sisi, ni visubiani vya ovyo ovyo
tu. Ngoja nitamfukuza”
Lile joka lilikuwa
limetusogelea, likitaka kupandisha kichwa chake juu ya ile sehemu tuliyokuwa.
Zena akaanza kulifokea kwa
lugha ya kikwao. Mimi nilisogea nyuma ya Zena kwa hofu. Zena akanyanyuka na
kulifuata kabisa huku akiendelea kulifokea.
Lile joka lilibaki pale pale
likinitazama mimi.
Zena akavua kiatu chake
akakishika na kulipiga kichwani. Joka hilo
likatoweka hapo hapo.
“Shika” alinipa kile kiatu.
Akaniambia.
“Ukiona joka linakufuata lipige na hiki kiatu changu,
litatokomea”
“Halitanimeza?” nikamuuliza
huku nikipokea kile kiatu.
“Hapana”
“Kumbe hapa mahali ni pa hatari
namna hii?”
“Wewe ndio umetaka tufike
hapa”
“Nimetaka mimi?”
“Ndio”
“Nilikwambia kuwa tuje hapa?”
“Kwani wewe siku zote unajua
mimi nataka nini kwako?”
Hapo nikagwaya.
Zena akaendelea kuniuliza.
“Ulifuata nini Pemba?”
Sikuwa na la kumjibu.
“Sasa niambie utanioa niwe
mke wako au bado hutaki?”
“Nikishakuoa tutakwenda
kuishi wapi?’ nikamuuliza.
“Kule kule unakoishi wewe”
“Turudi kule kwanza ndio
tupange mipango ya ndoa, si hapa”
“Nataka tukirudi niwe tayari
ni mke wako”
“Kwani tutakwenda kuoana
wapi?” nikamuuliza Zena.
“Mtu huolewa kwao na mimi
utakwenda kunioa kwetu”
“Kwenu wapi?”
“Kwetu hukujui?”
“Sikujui”
“Kwetu ni ujinini”
“Yaani tutakwenda kuoana
kwenu ujinini?”
“Ndio”
“Sasa ungeacha kwanza nirudi
nyumbani nikajiandae. Hatuwezi kuoana ghafla”
“Wewe umekuwa mkaidi mara
nyingi. Siwezi kukupa nafasi hiyo. Madhumuni yangu ya kukuleta hapa ni kuwa
twende tukaoane. Muda umeshafika”
Nikanyamaza kimya.
Zena alikuwa akiendelea
kuniambia.
“Ile boti niliizamisha mimi
kusudi ili nikulete hapa. Ninajua tukiwa hapa hutakuwa na ujanja wowote”
Ndipo nilipogundua kuwa Zena
alikuwa amenizunguka! Kumbe ile boti aliizamisha yeye ili anipate mimi…
Kufika Kwetu pale kisiwani
nilidhani nilikuwa nimesalimika na kifo, kumbe nilikuwa ninasubiriwa na
matatizo mengine.
Kama alivyoniambia Zena, ni kweli pale kisiwani
nisingekuwa na ujanja wowote zaidi ya kusalimu amri.
Lakini akili yangu bado
ilikuwa haikubaliani na mawazo ya Zena. Kumuoa jini lilikuwa jambo ambalo
sikuwa tayari nalo.
“Sikiliza Zena, naona sasa
unatumia jazba ambayo si nzuri” nikamwambia Zena. Lakini hataka kabla
sijamaliza sentensi yangu au alinikatiza.
“Kumbe ulitaka nifanye nini?”
Sasa sauti yake ilikuwa ya
hamaki.
“Nilitaka unisikilize
ninachokwambia”
“Kipi?”
“Turudi Tanga ili nijiandae
kwa jambo hilo,
kwanini wewe unachukulia nguvu?”
“Nachukulia nguvu kwa sababu
nimeshaakuona kuwa huko tayari kunioa”
“Niko tayari, nani kakwambia kama siko tayari. Ninachotaka mimi unipe muda tu wa
kujiandaa”
“Amour usinidanganye, huko
tayari. Kama ungekuwa tayari usingekwenda
kumuoa yule mwanamke wako niliyemfukuza pale nyumbani”
“Yule nilimuoa kwa sababu
ndugu zangu walimtaka yeye lakini sasa nitawaambia kuwa nataka kuoana na wewe”
“Usiniambie habari ya ndugu
zako, nyote nyinyi ni kitu kimoja”
“Mbona hutaki kunisikiliza
Zena!”
“Sitakusikiliza. Wewe ni
muongo ingawa sipendi kukuita hivyo. Wewe hunitaki mimi wakati mimi
nimekusaidia sana.
Kwanza niambie ulifuata nini Pemba?”
“Si nimekwambia kwamba
nilikwenda kutembea”
“Usinidanganye. Usinifanye
mimi sina akili. Wewe ulikwenda Pe,mba baada ya kuambiwa kuna mganga ambaye
ataweza kupambana na mimi”
Nikajikuta natikisa kichwa
changu kwa fadhaa.
“Si kweli” nikamwambia lakini
uso wangu ulikuwa umetahayari.
“Unaona aibu mwenyewe
kutokana na hila zako, Unadhani kuna mganga ataniweza mimi?”
Nikabaki kimya. La kusema
nilikuwa sina.
“Sasa usinipotezee muda
wangu, nataka jibu lako. Tutakwenda ujinini kuoana au hatutakwenda?” Zena
akaniuliza.
Nilikuwa nimeinamisha kichwa
changu nikiwaza. Sikuwa na jibu la kumpa, nikabaki kutikisa kichwa kuashiria
kutokukubaliana naye.
“Amour nakuuliza tena,
tutakwenda ujinini tukaoane au hatutakwenda?”
Niliendelea kutikisa kichwa.
“Una maana huko tayari siyo?”
Sikumjibu.
“Sasa mimi nakwenda zangu,
nakuacha hapa hapa. Hutaniona tena”
Nikainua uso wangu haraka ili
nimwambie asiniache pale lakini Zena alitoweka ghafla kama
upepo. Kama alivyoniambia sitamuona tena na
kweli sikumuona tena!
Nikatazama huku na huku, Zena
hakuweko. Nikabaki peke yangu kwenye kisiwa kile cha majoka!
DUH!
HAYA ATAFANYA NINO HUYU
LKIJANA WA WATU MASIKINI!
NAONA KESHO NI MBALI LAKINI
NITAFANYAJE!
No comments:
Post a Comment