Wednesday, July 13, 2016

HADITHI , MWANAMKE SEHEMU YA 41

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572

MWANAMKE  41

ILIPOISHIA

“Usiniambie habari ya ndugu zako, nyote nyinyi ni kitu kimoja”

“Mbona hutaki kunisikiliza Zena!”

“Sitakusikiliza. Wewe ni muongo ingawa sipendi kukuita hivyo. Wewe hunitaki mimi wakati mimi nimekusaidia sana. Kwanza niambie ulifuata nini Pemba?”

“Si nimekwambia kwamba nilikwenda kutembea”

“Usinidanganye. Usinifanye mimi sina akili. Wewe ulikwenda Pemba baada ya kuambiwa kuna mganga ambaye ataweza kupambana na mimi”

Nikajikuta natikisa kichwa changu kwa fadhaa.

“Si kweli” nikamwambia lakini uso wangu ulikuwa umetahayari.

“Unaona aibu mwenyewe kutokana na hila zako, Unadhani kuna mganga ataniweza mimi?”

Nikabaki kimya. La kusema nilikuwa sina.

“Sasa usinipotezee muda wangu, nataka jibu lako. Tutakwenda ujinini kuoana au hatutakwenda?” Zena akaniuliza.

Nilikuwa nimeinamisha kichwa changu nikiwaza. Sikuwa na jibu la kumpa, nikabaki kutikisa kichwa kuashiria kutokukubaliana naye.

“Amour nakuuliza tena, tutakwenda ujinini tukaoane au hatutakwenda?”

Niliendelea kutikisa kichwa.

“Una maana huko tayari siyo?”

Sikumjibu.

“Sasa mimi nakwenda zangu, nakuacha hapa hapa. Hutaniona tena”

Nikainua uso wangu haraka ili nimwambie asiniache pale lakini Zena alitoweka ghafla kama upepo. Kama alivyoniambia sitamuona tena na kweli sikumuona tena!

Nikatazama huku na huku, Zena hakuweko. Nikabaki peke yangu kwenye kisiwa kile cha majoka!

SASA ENDELEA

Kile kiatu chake alichokivua na kulipiga lile joka nikabaki nacho. Mwenyewe amekwenda na kiatu kimoja.

Nilipata hofu kweli kweli.

Jua lilikuwa limeshakuchwa na kiza kilikuwa kinaingia. Nikajiuliza “nitafanyaje Amour?”

Zena alikuwa ameshaniacha peke yangu. Nikawa nahisabu dakika zangu za kufa au kuliwa na majoka.

Nikaondoka mahali pale nilipokuwa nakwenda kupanda juu ya mti nikiwa na kile kiatu. Nilikaa kwenye tawi moja nikawa naitazama bahari. Hakukuwa na mtumbwi wala ngarawa iliyokuwa ikipita. Bahari ilikuwa nyeupe.

Kusema kweli nilijuta kufunga safari ile ya kwenda Pemba kufuata mganga. Na kama niliamua kwenda ningekwenda na ndugu yangu na si peke yangu kama nilivyofanya.

Nilianza kusikia baridi mwilini, sikujua itakapofika usiku ingekuwaje.

Nilitamani Zena anionee huruma aje anichukue. Lakini mawazo yangu yalikuwa sawa na dua  la kuku. Hakuna aliyelisikia.

Wakati nimekaa kwenye tawi nikiendelea kuwaza nikasikia majani yakichakachika juu ya ule mti kama vile kulikuwa na kitu kinatambaa.

Nikainua uso wangu juu kutazama kulikuwa na nini.

Nikashituka. Niliona kichwa cha joka kikiwa karibu yangu kabisa. Kumbe katika ule mti niliokuwa nimeupanda kulikuwa na joka ambalo sikuliona.

Kile kiatu cha Zena nilikuwa nacho mkononi, nikakipiga kile kichwa. Nikadhani lile joka lingeniangukia lakini pale pale lilitoweka. Sikuliona tena.

Nikagundua kuwa licha ya Zena kunikimbia alikuwa ameniachia silaha ya maana sana.

Nikaangaza angaza juu ya ule mti kuona kama kulikuwa na joka  jingine. Sikuona joka.

Hata hivyo sikuamini. Kila wakati nilikuwa natazama tena.

Kiza kiliendelea kushamiri na baridi ilizidi kuwa kali lakini sikuwa na la kufanya. Nilibaki kutetemeka tu.

Nilijiambia kama nitakufa pale kisiwani maiti yangu haitapatikana. Mama yangu na kaka yangu hawatajua nimepotelea wapi na hawatajua kuwa mwenzao ni marehemu.

Eti wakati nawaza vile nikapitiwa na usingizi ghafla. Nikalala pale pale juu ya mti bila kujitambua.

Nikaota nimelala chumbani kwangu, mara nikaona mwanamke ametokea kwenye dirisha langu lakini alikuwa kama kivuli. Sikuweza kumuona sura yake. Akaniambia.

“Ni mpaka uirithi pete ya Sulaiman Dauud na hutairithi mpaka uishuhudie damu ya kaka yako ikimwagika”

Hapo hapo nikazinduka. Ile ndoto haikuwa ngeni kwangu nakumbuka katika kipindi cha mwaka mmoja nilishaiota zaidi ya mara tatu. Lakini sikujua maana yake.

Wakati nazinduka niliona mawingu yakianza kun’gaa. Kumbe kulikuwa kunanaanza kupambazuka. Nikatambua kuwa nililala usiku kucha pale juu ya mti ingawa niliona nililala kwa muda mfupi.

Wakati naangaza macho baharini nikaona boti moja kubwa inakuja kwa kasi. Nikashukuru ingawa sikujua ilikuwa boti ya kina nani.

Boti ile ilikuja hadi maji madogo ikatia nanga. Nikaona watu watano wanashuka na kutembea kuelekea ufukweni. Walikuwa wamesega suruali zao ili zisitote.

Mmoja wa watu hao alikuwa amebeba tenga kubwa kichwani. Nikasikia sauti kama ya mlio wa mbuzi.

Watu hao walipofika ufukweni walitembea hadi kwenye ule msitu. Yule aliyebeba tenga akalitua chini. Ule mlio wa mbuzi uliendelea kusikika.

Nikaona mbuzi mweusi anatolewa kwenye tenga hilo. Sikuweza kuona vizuri kilichokuwa kinaendelea isipokuwa niliona kama walikuwa wanamchinja yule mbuzi na kumuacha pale chini.

Nikapata hisia kwamba watu hao walikuwa wanafanya kafara lakini ghafla nikaona wanaingia katika ule msitu.

Baada ya muda wa kama nusu saa hivi wakaanza kutoka mmoja mmoja lakini kila aliyetoka alikuwa amebeba pembe nne za ndovu.

Walikwenda nazo kwenye ile boti wakazipakia kisha wakarudia zingine.

Walirudia mara kumi, zilikuwa pembe nyingi sana. Ile mara ya kumi waliobeba pembe walikuwa watu wawili. Nikahisi walikuwa wamemaliza pembe zao na kwamba walikuwa wanakwenda zao.

Nikadhania tu kuwa wale watu walikuwa wafanya magendo na walikuwa wakificha pembe zao katika kisiwa kile.

Nikaona nisiipoteze ile nafasi ingawa sikujua watu wale walikuwa wanaelekea wapi.

Nikashuka haraka kwenye ule mti na kuwakimbilia.

“Jamani naomba mnichukue!” nikawa nawapigia kelele.

Watu hao walipoona ninawafuata huku nikiwaomba msaada wakasimama na kunisubiri.

Nilipowafikia, mtu mmoja mfupi aliyekuwa amevaa pama jeusi akaniuliza.

“Wewe nani na umetokea wapi?”

“Mimi ni mwananchi niliyekuwa natokea Pemba nikielekea Dar kwa boti inayokwenda kasi ambayo ilizama jana” nikamwambia.

“Boti ilizama jana mbona wewe upo hadi leo”

“Nilinusurika baada ya kuogelea….”

Kabla sijamaliza kile nilichotaka kumueleza akanikatiza.
“Ulifuata nini kwenye kisiwa hiki?”

“Niliogelea hadi nikafika hapa”

“Tangu jana ulikuwa unafanya nini hapa?”

“Nilikuwa nimekaa tu nikisubiri msaada”

“Wewe ni muongo sana!”

“Hapana. Ninachokieleza ni ukweli mtupu”

“Wewe ni mpelelezi siyo, umekuja kutupeleleza sisi?”

“Hapana, hapana. Mimi siwajui, nimewaona tu hapa. Ninachoomba ni msaada wenu tu”

“Haya twende tukaingie kwenye boti”

“Asante bwana, nakushukuru sana kwa maana nilikuwa sijui ningefikaje Tanga”

Nilifuatana na wale watu hadi kwenye boti yao nikajipakia. Yule mtu aliyekuwa akinihoji ambaye alionekana kama mwenye mali alikuwa akiamrisha kila kitu ndani ya ile boti.

Safari ikaanza. Nikadhani kwamba nilikuwa nimenusurika. Sikujua tulikuwa tunaelekea wapi na jinsi nilivyowaona watu wenyewe ni wakali nilishindwa kuwauliza.

Nilikuwa nimeshaamua popote watakaponifikisha patatosha. Kama watanirudisha Pemba au kama watakwenda Unguja au Dar itakuwa sawa.

Boti iliendelea na safari kwa kasi. Kitu kilichonishitua ni kwamba baada ya kukiacha kile kisiwa, yule mtu aliyekuwa amevaa pama jeusi alikwenda kukaa peke yake akatoa bangi na kuanza kuvuta.

Moshi wa bangi ulienea kwenye boti ukawa unaniumiza kichwa lakini yule mtu hakujali kabisa. Alikuwa akiendelea kuvuta tu.

Baada ya kwenda mwendo wa karibu kilometa thelathini tukaona boti nyingine inatufuata. Wale watu walipoiona ile boti walishituka.

Yule mtu aliyevaa pama akakitupa kipisi cha bangi baharini kisha akanitazama na kuniambia.

“Polisi wenzako wanatufuata, mimi nilishajua kuwa wewe ni mpelelezi!”

“Polisi gani?” nikamuuliza.

MAMBO YANAZIDI KUPAMBA MOTO! SI MCHEZO! TUKUTANE KESHO.


No comments:

Post a Comment