SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572
MWANAMKE 42
ILIPOISHIA
Kabla sijamaliza kile
nilichotaka kumueleza akanikatiza.
“Ulifuata nini kwenye kisiwa
hiki?”
“Niliogelea hadi nikafika
hapa”
“Tangu jana ulikuwa unafanya
nini hapa?”
“Nilikuwa nimekaa tu
nikisubiri msaada”
“Wewe ni muongo sana!”
“Hapana. Ninachokieleza ni
ukweli mtupu”
“Wewe ni mpelelezi siyo,
umekuja kutupeleleza sisi?”
“Hapana, hapana. Mimi
siwajui, nimewaona tu hapa. Ninachoomba ni msaada wenu tu”
“Haya twende tukaingie kwenye
boti”
“Asante
bwana, nakushukuru sana
kwa maana nilikuwa sijui ningefikaje Tanga”
Nilifuatana na wale watu hadi
kwenye boti yao
nikajipakia. Yule mtu aliyekuwa akinihoji ambaye alionekana kama mwenye mali
alikuwa akiamrisha kila kitu ndani ya ile boti.
Safari ikaanza. Nikadhani
kwamba nilikuwa nimenusurika. Sikujua tulikuwa tunaelekea wapi na jinsi
nilivyowaona watu wenyewe ni wakali nilishindwa kuwauliza.
Nilikuwa nimeshaamua popote
watakaponifikisha patatosha. Kama watanirudisha Pemba au kama
watakwenda Unguja au Dar itakuwa sawa.
Boti iliendelea na safari kwa
kasi. Kitu kilichonishitua ni kwamba baada ya kukiacha kile kisiwa, yule mtu
aliyekuwa amevaa pama jeusi alikwenda kukaa peke yake akatoa bangi na kuanza
kuvuta.
Moshi wa bangi ulienea kwenye
boti ukawa unaniumiza kichwa lakini yule mtu hakujali kabisa. Alikuwa
akiendelea kuvuta tu.
Baada ya kwenda mwendo wa
karibu kilometa thelathini tukaona boti nyingine inatufuata. Wale watu
walipoiona ile boti walishituka.
Yule mtu aliyevaa pama
akakitupa kipisi cha bangi baharini kisha akanitazama na kuniambia.
“Polisi wenzako wanatufuata,
mimi nilishajua kuwa wewe ni mpelelezi!”
“Polisi gani?” nikamuuliza.
SASA ENDELEA
“Utawaona sasa hivi”
Mazungumzo ya polisi yakaanza
ndani ya boti huku wale watu
wakinishutumu mimi kuwa ni mpelelezi niliyekuwa nimetumwa katika kile
kisiwa kuwachunguza.
Kumbe ile boti iliyokuwa
inatufuata ilikuwa boti ya polisi wanamaji iliyokuwa kwenye doria.
Upande mmoja wa moyo wangu
nilipata hofu lakini kwa upande mwingine nilipata matumaini. Nilipata hofu kutokana
na zile shutuma nilizokuwa ninazipata kutoka kwa wale watu kuwa mimi ni
mpelelezi. Na nilipata matumaini kujua kuwa kulikuwa na polisi wanatufuata.
Sikuwa na hofu na polisi hao
kwa sababu sikuhusika na wafanya magendo hao ambao hata sikujua walikuwa
wanaelekea wapi.
Kadiri ile boti ilivyokuwa
inatukaribia wale watu walikuwa wakihaha huku wakitukana.
Boti ya polisi ilipotufikia
polisi wanne waliingia kwenye ile boti. Polisi mmoja alikuwa ameshika bunduki.
“Mnakwenda wapi?” Polisi
aliyeshika bunduki akatuuliza.
Polisi hao hawakupata jibu.
Jamaa wote walikuwa kimya.
Katika kukagua kagua ndani ya
ile boti, polisi hao wakaziona zile pembe za tembo.
“Kuna meno ya tembo mengi sana wanayasafirisha!”
Polisi mmoja akawapigia kelele polisi wengine waliokuwa kwenye boti ya pili.
Yule mtu aliyevaa pama
aliingia kwenye kijichumba kilichokuwa ndani ya boti hiyo. Muda ule ule alitoka akiwa ameshika kitu kama chupa kubwa iliyokuwa na utambi uliokuwa ikiwaka
moto, akairusha ile chupa kuelekea kwenye boti ya polisi. Ile chupa ilipotua
chini ililipuaka kama bomu.
Kitendo kile kilinishitua.
Mara moja ile boti ya polisi ililipuka moto. Wale polisi walioingia kwenye boti
niliyokuwemo walikuwa wameduwaa. Hapo hapo wakavamiwa na wale watu, wakapigwa
na kufungwa kamba. Yule polisi aliyekuwa na bunduki alinyanganywa bunduki yake.
Jambo lililonishitua zaidi ni
kuwa hata mimi nilikamatwa nikafungwa pamoja na
polisi hao.
“Tutakwenda kuwatosa huko
mbele ya safari” aliyekuwa amevaa pama akatuambia.
“Lakini mimi ninahusikaje,
mimi niliwaomba msaada tu kwanini mnataka kwenda kunitosa?” nikawalalamikia.
“Wewe ndio mpelelezi
uliyekuwa ukitoa taarifa kwa wenzako. Pale nilipokuwa nakupakia nilishakupangia
kwenda kukutosa” Mwenye pama akaniambia.
“Balaa gani hili jamani
linalonikuta. Jana nilikaribia kufa, leo tena balaa jingine linaningoja.
Nimekosa nini jamani!” nikalalamika peke yangu.
Wakati huo ile boti ya polisi
tulishaiacha mbali ikiendelea kuwaka.
Mpaka jua linafika utosini
ikiashiria ilikuwa saa sita mchana, boti ya watu hao ambao sasa niliwahisi
walikuwa majambazi ilikuwa ikiendelea kukata maji.
Nilikuwa nimeshafuta mawazo
kwamba tulikuwa tunaelekea katika miji iliyokuwa karibu kama Pemba
au Unguja. Nilihisi kwamba tulikuwa tunaelekea mahali kwingine kusikojulikana.
Hofu ya kuuawa ilikuwa
imenitawala. Wakati wote moyo wangu ulikuwa ukienda mbio. Sikujua kwamba
tungeuawa au tungetoswa baharini saa ngapi.
Mara nikamuona yule mtu
aliyekuwa amevaa pama akitoka kwenye kile chumba kilichokuwamo ndani ya boti,
akawambia wenzake.
“Eneo hili lina papa wengi,
tuwatose hapa hapa”
Kauli yake ile ilinishitua.
Ilikuwa kama nyundo ya moto iliyopigwa kwenye moyo wangu.
Mapama aliposema hivyo
aliwaagiza watu watatu wamuinue polisi mmoja na kumtosa. Polisi huyo
alilalamika kuomba asitoswe lakini hakukuwa na aliyekuwa akimsikiza. Jamaa hao
walimbeba na kumtosa baharini akiwa amefungwa kamba miguu na mikono.
Mara moja tukaona damu kwenye
eneo lile la bahari. Kipande kimoja cha mwili wa polisi huyo kiliibuka juu na
kwenda na maji. Bila shaka kipande kingine kilikuwa kimeshamezwa na papa.
Hapo hapo tukamuona papa
upanga akibuka kutoka chini ya bahari na kuking’ata kipande kingine cha ule
mwili na kuzama nacho baharini.
Tayari jamaa hao walikuwa
wameshambeba polisi wa pili ambaye kama mwenzake
alikuwa akilalamika bila kusikilizwa, naye akatoswa.
Polisi wa tatu naye akatoswa.
Nikabaki mimi na polisi mmoja. Nilikuwa nikiomba toba kimoyomoyo ili nipate
msamaha huko ahera ninakokwenda.
Machozi yalikuwa yametosa
kifua changu na yalikuwa yakiendelea kunitoka hasa nilivyoona vipande vya miili
ya wale polisi ilivyokuwa ikidakwa na papa.
Wale jamaa wakatufuata tena.
Sikujua ilikuwa zamu ya nani, mimi au yule polisi?
Jibu nililipata baada ya nusu
dakika. Watu hao wakamshika mwenzangu. Bila shaka mimi waliniweka mwisho.
Polisi huyo alibebwa juu juu. Ingawa alikuwa akipiga kelele, hakukuwa na
aliyemjali. Kiasi cha kufumba na kufumbua tu akawa ametoswa baharini. Kwa vile
alikuwa mnene na mzito kuliko wenzake waliokuwa
wametoswa, alisababisha kishindo kukubwa, maji ya bahari yakaruka na kuingia kwenye boti!
Wakati wote nilikuwa na
matumaini kuwa wangewatosa wale polisi kwa kuamini kuwa mimi sikuwa mwenzao na
ndio maana waliniacha.
Lakini matumaini yangu
yaliyayuka mara tu nilipowaona wale watu wakinifuata mimi baada ya kumtosa yule
polisi wa mwisho,
Nilipoona wananishika
nikawambia.
“Jamani, jamani mimi nina
kosa gani. Kuwaomba msaada ndio kosa, mnataka mniue”
Hawakunijibu na hawakuonesha kama walihitaji kunijibu, Walinibeba kama walivyowabeba
wenzangu. Vile ambavyo mwili wangu haukuwa mzito walinichota kama
takataka. Wakanipeleka kwenye ukingo wa boti.
Kufika hapo waliniinua juu
wakahesabu moja...mbili…
Kabla hawajafika tatu,
kuliibuka kitu kilichotokea baharini. Kiliibuka kwa nguvu na kwa kishindo huku
kikitoa mlio uliofanana na mlio wa fataki iliyorushwa.
Yale maji yaliyorushwa juu na
kitu hicho yalitutosa wote. Ghafla kitu hicho kikatuvamia. Mimi niliachiwa
nikaangukia ndani ya boti. Wale watu pia walianguka na kulaliwa na kitu hicho kizito
kilichotua ndani ya boti.
Nilikuwa nimefungwa kamba
mikono na miguu. Nilipoanguka sikuweza kusimama ila niliweza kujigeuza ili
nikione kitu hicho kilichoibuka kutoka baharini na kuvamia ndani ya boti ile.
Nilishindwa kuamini
macho
yangu! Lilikuwa dude kubwa kama joka
lililokuwa na mikono yenye vidole vyenye kucha ndefu. Urefu wake ulikuwa
kama guzo la umeme. Lilipokuwa ndani ya ile boti lilikuwa
limejikunja. Mwili wake ulikuwa na magamba makubwa kama
ya samaki.
Kwa kutumia kucha zake
lilimvamia mtu mmoja na kuruka naye juu kisha likajitosa baharini likiwa na mtu
huyo.
Sote tulikuwa tumetaharuki na
hatukujua ni jambo gani lilitaka kutokea. Wakati wale watu wanajiinua pale
chini, joka hilo
likaibuka tena likiwa halina mtu. Likavamia mtu mwingine na kuruka naye kisha
likajitosa baharini.
Watu hao wakawa wanapigana
vikumbo ndani ya boti kutafuta pa kujificha. Kutahamaki joka hilo likatokea tena, likamnyakua mtu mwingine
na kuzama naye chini ya bahari. Watu wote wakamalizwa nikabaki mimi na Mapama
Mapama alikuwa akihangaika
akijua kwamba joka hilo
litaibuka tena na kumchukua yeye.lakini dakika zikapita hatukuliona. Kwa sababu
ya hofu na kujiona amebaki peke yake mtu huyo alikuja kunifungua zile kamba.
“Njoo huku” akiniambia
akitangulia kuingia katika kile kijichumba kilichokuwa ndani ya ile boti.
Nikainuka na kumfuata. Mikono
yangu ilikuwa imekufa ganzi kutoka na kufungwa kamba kwa muda mrefu. Nikawa
ninainyooshanyoosha.
Ndani ya chumba hicho
kulikuwa na kioo cha kutazamia mbele. Pia kulikuwa na sukani na mitambo ya
boti.
“Samahani bwana, naona
tumebaki sisi wawili tu. Sijui lile lilikuwa joka gani na limetokea wapi?”
Mapama akaniambia kwa hofu.
MAMBO MAKUBWA NI KESHO.
Usikose Mshikaji wangu. Utakosa uhondo bure!!!
No comments:
Post a Comment