SIMULIZI ZA FAKI 0655 340572
MWANAMKE 43
ILIPOISHIA
Nilishindwa kuamini
macho
yangu! Lilikuwa dude kubwa kama joka
lililokuwa na mikono yenye vidole vyenye kucha ndefu. Urefu wake ulikuwa
kama guzo la umeme. Lilipokuwa ndani ya ile boti lilikuwa
limejikunja. Mwili wake ulikuwa na magamba makubwa kama
ya samaki.
Kwa kutumia kucha zake
lilimvamia mtu mmoja na kuruka naye juu kisha likajitosa baharini likiwa na mtu
huyo.
Sote tulikuwa tumetaharuki na
hatukujua ni jambo gani lilitaka kutokea. Wakati wale watu wanajiinua pale
chini, joka hilo
likaibuka tena likiwa halina mtu. Likavamia mtu mwingine na kuruka naye kisha
likajitosa baharini.
Watu hao wakawa wanapigana
vikumbo ndani ya boti kutafuta pa kujificha. Kutahamaki joka hilo likatokea tena, likamnyakua mtu mwingine
na kuzama naye chini ya bahari. Watu wote wakamalizwa nikabaki mimi na Mapama
Mapama alikuwa akihangaika
akijua kwamba joka hilo
litaibuka tena na kumchukua yeye.lakini dakika zikapita hatukuliona. Kwa sababu
ya hofu na kujiona amebaki peke yake mtu huyo alikuja kunifungua zile kamba.
“Njoo huku” akiniambia
akitangulia kuingia katika kile kijichumba kilichokuwa ndani ya ile boti.
Nikainuka na kumfuata. Mikono
yangu ilikuwa imekufa ganzi kutoka na kufungwa kamba kwa muda mrefu. Nikawa
ninainyooshanyoosha.
Ndani ya chumba hicho
kulikuwa na kioo cha kutazamia mbele. Pia kulikuwa na sukani na mitambo ya
boti.
“Samahani bwana, naona
tumebaki sisi wawili tu. Sijui lile lilikuwa joka gani na limetokea wapi?”
Mapama akaniambia kwa hofu.
SASA ENDELEA
“Nadhani limekuja kuwaua
kutokana na ule unyama wenu wa kututosa baharini bila hatia”
“Sio mimi, ni wale jamaa.
Mimi sikuweza kuwazuia”
Nikaona yule mtu alikuwa
akijitetea kwa kusema uongo wakati yeye ndiye aliyeamrisha tutoswe.
Sikutaka kumsuta kwa sababu
hata mimi nilikuwa nimepata hofu na sikuwa nikijua hatima yangu.
“Lakini sidhani kama litakuja tena” nikamwambia kumpa moyo. Hata hivyo
nilijisemea tu bila kuwa na uhakika.
Mapama alikuwa akiendesha
lile boti huku akiwa matu matu. Kila mara alikuwa akitupa macho pande zote za
boti. Nilijua alikuwa akihofia lile joka ambalo hata mimi liliniweka katika
hali ya wasiwasi.
“Tuombe Mungu. Tukinusurika
tutatajirika” Mapama akaniambia.
“Kwani tunaelekea wapi?”
nikamuuliza.
“Tunakwenda Somalia”
“Kumbe mlikuwa mnakwenda Somalia?”
“Mnunuzi wa hizi pembe yuko Somalia,
ndio tulikuwa tunampelekea”
“Ni mali ya nani?”
“Mwenyewe yuko Dar. Mimi
ndiye msimamizi wake na mmiliki wa hii boti. Mara kwa mara ananituma kupeleka
pembe zake Somalia”
“Huwa mnazihifadhi kwenye
kile kisiwa?”
“Pale ndio tunazificha tunapozikusanya
kutoka kwa majangili”
“Mnapokwenda pale mnachinja
mbuzi kwa ajili ya nini?’
“Kile kisiwa kinakaa majini.
Hivyo tunapofika tunawapa kafara ili wasitudhuru. Na wewe ulifuata nini pale?”
“Pale nilifika jana kwa
kogelea. Mimi nilikuwa ninatoka Pemba kwenda
Dar. Boti yetu ilizama.”
“Ndiyo nilisikia. Kwa hiyo
ulilala pale pale?’
“Ndiyo nililala juu ya mti.
Sasa nilipowaona leo asubuhi nikawafuata kuwaomba msaada lakini inaelekea
hamkunielewa”
“Unajua hii kazi ni ya siri
na ya hatari, wale wenzangu walipokuona walidhani wewe ni mpelelezi ulikwenda
pale kufanya uchunguzi”
Jamaa yule alikuwa
akiwasingizia wenzake kila kitu wakati yeye ndiye aliyekuwa akinituhumu.
“Sasa ukifika Somalia unarudi lini huku Tanzania”
“Tukifika tu tunapakua huu
mzigo na kuupakia kwenye boti nyingine halafu tunarudi”
“Hiyo boti tutaikuta wapi?”
“Tukiingia Somalia tu tunaikuta inatusubiri”
“Halafu hizi pembe
zinapelekwa wapi?’
“Zinasafirishwa kwa meli na
kupelekwa nchi za kiarabu. Waarabu wanatengezea mipini ya majambia”
Sikuwa nikijua kuwa pembe za
ndovu hutengezwa mipini ya majambia. Hata hivyo niliyaacha yale mazungumzo ya
pembe. Dukuduku langu lilikuwa ni kurudi nyumbani.
“Tutafika leo huko Somalia?”
nikamuuliza.
“Hapa tuko katika bahari ya Mombasa nchini Kenya. Mpaka ikifika saa kumi na
moja alfajiri tutaingia Somalia”
“Eh! Kumbe safari bado ni
ndefu?”
“lakini tumeshafika nusu ya
safari yetu”
“Kama
ni kurudi itakuwa kesho”
“Kesho si mbali. Sasa hivi
jua litakuchwa, usiku utaingia”
Mapama aliposema hivyo alitoa
kicheko cha kujilazimisha akaondoka kwenye sukani baada ya kuitegesha muelekeo
aliokuwa anautaka. Akafungua kabati lililokuwa humo ndani na kutoa sufuri
iliyokuwa imefunikwa.
Aliiweka kwenye kimeza kisha
akafunua ule mfiniko. Ndani ya sufuria hiyo mlikuwa na pilau na vipande vya
nyama. Sijui ilikuwa nyama ya nini.
Akapakua ile pilau kwenye
sahani na kuniambia.
“Tule”
Kusema kweli nilikuwa na njaa
lakini zile nyama ziliniogopesha kwa sababu zilikuwa nyingi na sikujua zilikuwa
nyama za mnyama gani kwani zilikuwa na mafuta mengi.
“Hizi ni nyama za nini?”
nikamuuliza.
“Nyama ya nyati, ni tamu sana. Hebu onja”
Aliokota kipande cha nyama
bila kuosha mkono akanipa.
Alinishangza sana. Mikono yake ilikuwa
imeshika kila kitu. Imeshika magwanda ya polisi waliowatosa baharini. Imeshika
mapembe ya ndovu. Imeshika sukani ya boti. Imeshika bangi…loh! Hawa watu
wachafu kweli!
Alipoona nimesita nikimtazama
akagutuka na kuinuka.
“Ngoja nioshe mkono”
akaniambia.
Aliosha mkono kwa kutumia
maji yaliyokuwa yamewekwa kwenye dumu.
“Na wewe njoo uoshe mikono
yako” akaniambia.
Wakati wote nilikuwa nikisema
na moyo wangu kuhusu kile chakula. Nilikuwa nikijiuliza nile kile chakula au
nisile. Ukweli ni kwamba nilikuwa na njaa na njaa haina ustaarabu. Ikikushika
unaweza kula hata kisocholika. Japokuwa kwanza nilisita sita lakini hatimaye
niliinuka kwenda kuosha mikono.
Baada ya kuosha mikono
tukarudi pale tulipokuwa.
“Kula” Mapama akaniambia.
Tukaanza kula. Pilau ilikuwa
ikinuka moshi wa kuni. Nikahisi kwamba waliipika wao wenyewe kwa kutumia kuni
walizoziokota fukweni mwa bahari..
Kwa sababu ya njaa niliyokuwa
nayo nilikula sana
mpaka nikahisi kwammba ningevimbiwa. Pilau ilikuwa nyingi hatukuimaliza.
Nilimuacha Mapama akiendelea
kula.
“Ukiwa katika hali ya baridi
unatakiwa ule sana”
Mapama aliniambia.
Tonge zake zilikuwa kubwa na
nilihisi alikuwa akimeza bila kutafuna.
Alipotosheka na yeye
aliiacha. Akairudisha sinia kwenye kabati.
Baada ya kuosha mikono Mapama
alinipa maji ya kunywa nikayanywa. Na yeye akanywa.
“Sasa baridi hatutaisikia.
Tunaweza kuendelea na safari” Mapama akaniambia.
Tukakaa na kuendelea
kuzungumza. Mara moja moja alikuwa akitazama mitambo. Nilikuwa nimejifunza
kwamba boti haikuwa ikiendeshwa kama gari.
Haihitaji kushikiliwa sukani
wakati wa kuendesha. Unaweza kuweka muelekeo wako na ukaiacha iende yenyewe.
Ndivyo Mapama alivyokuwa
akifanya. Hatimaye Mapama alianza kusinzia. Alikuwa akisinzia huku akishituka.
“Nikuache uangalie, mimi
najinyoosha kidogo” akaniambia.
Nikajua kuwa pilau aliyokuwa
ameila kwa wingi ilikuwa imemlewesha.
“Wewe lala, baadaye
nitakuamsha” nikamwambia.
Mapama akajitupa chini. Baada
ya muda kidogo nilimsikia akikoroma.
Huku boti ilikuwa ikiendelea
na safari. Masaa yalipita. Saa yangu ilikuwa imesimama kutokana na kuingia maji
ya chumvi, sikuweza kujua ilikuwa saa ngapi.
Je nini kitatokea? TUKUTANE
KESHO
Ni Tangakumekucha pekee inayokupa Uhondo
No comments:
Post a Comment