SIMULIZI YA FAKI A FAKI
MWANAMKE 34
ILIPOISHIA
Wakati natoka mle chumbani
yale maneno yake kwamba hilo jini limenitawala sana na kwamba itakuwa
vigumu kuliepuka, yalikuwa yakinirudia akilini mwangu.
Kusema kweli niliondoka pale
gesti nikiwa na fadhaa sana.
Nilipanda pikipiki yangu. Sikutaka kwenda kwa kaka ingawa hapakuwa mbali na
pale gesti, nikaenda kazini kwangu.
Nilifanya kazi huku nikiwaza
jinsi zile kucha zilivyopotea kwenye kibiriti. Kwa kuzingatia maneno ya yule
mganga iliwezekana kwamba zile kucha zilipotezwa na Zainush.
Lakini kubwa ambalo lilinitia
fadhaa ni yale maneno ya yule mganga kwamba hilo
jini limenitawala sana
na itakuwa vigumu kuliepuka.
Kama mganga wa majini amesema hivyo, je juhudi zangu za
kumuondoa zainush zitafanikiwa kweli, nikajiuliza kwa fadhaa.
Mganga mwenyewe amenifukuza,
nikaendelea kuwaza, bila shaka na yeye alikuwa amepata hofu baada ya kuona
jinsi zile kucha zilivyotoweka kwenye kibiriti.
“Una nini leo Amour?” Wafanya
kai wenzangu walikuwa wakiniuliza.
“Nikoje?’
SASA ENDELE
“Leo unaonekana una mawazo sana” Mfanyakazi mmoja
akaniambia.
“Kawaida tu”
“Tuambie kama kuna kitu
kimekukwaza”
“Kwa hapa kazini?”
“Popote tu”
“Hakuna kitu. Binaadamu
kuwaza ni kawaida”
“Mwenzetu leo umezidi sana”
“Basi nitapunguza” nikasema
kwa utani kisha nikacheka ili kukatisha yale mazungumzo yake.
Nilipomwambia hivyo naye
akacheka, akaniambia.
“Sawa bwana”
Maneno yakaishia hapo hapo.
Sikujua kama wafanyakazi wenzangu walikuwa wananiona nilikuwa na mawazo. Baada
ya hapo nikajitia kufanya kazi ili nionekane wa kawaida. Sikutaka mtu yeyote
ajue lililokuwa moyoni mwangu.
Jioni nilipotoka kazini
nikaenda Chuda kwa kaka. Nilimueleza juhudi nilizozifanya jana yake hadi
nikafanikiwa kupata zile kucha na hatimaye zikatoweka zikiwa ndani ya kibiriti
wakati nikiwa kwa yule mganga.
“Mganga alipata hasira
akanifukuza. Aliniambia niondoke na kwamba yule jini ameshanitawala, itakuwa
vigumu kumuondoa” nikamwambia.
“Sasa kwanini alikufukuza?’
“Sijui”
“Na hizo kucha zilitoweka
vipi?’
“Sijui. Mgosingwa aliniletea
asubuhi zikiwa ndani ya kibiriti. Sasa nafika kwa mganga nafungua kibiriti,
kucha hazimo!”
“Na wewe ulihakikisha
ulipopewa hicho kibiriti kucha zilikuwemo?”
“Ndio. Mgosingwa aliponipa
hicho kibiriti alinifungulia akanionesha. Kucha zilikuwemo”
“Mganga alikwambia hizo kucha
zimnmekwenda wapi?’
“Aliniambia huyo jini ndiye
anayeniharibia mambo yangu”
“Kwa hiyo huyo jini ndiye
aliyezipoteza?’
“Itakuwa ni yeye”
Kaka alifikiri kisha
akaniuliza.
“Hizo kucha zilikuwa ndogo sana?”
“Ndio zilikuwa ndogo”
“Inawezekana zilichomoka moja
moja kwenye kibiriti bila wewe kujua. Siamini kwamba huyo jini amezichukua
yeye”
“Unafikiria hivyo?’
“Acha wasiwasi. Kwanza huyo jini kuna muda mrefu hajakutokea. Mimi
nafikiri ameshakata tamaa”
“Sawa kaka, nimekuelewa”
Sikuwa na uhakika kwamba kaka
alikuwa akiniambia ukweli kutoka ndani ya moyo wake au alikuwa akinituliza tu.
Baada ya mazungumzo yetu
mafupi nikamuaga na kuondoka.
Baada ya wiki moja kaka yangu
aliniita na kunishauri nioe.
“Umeshakuwa mkubwa sasa,
unatakiwa uwe na mke wako” aliniambia.
“Ni kweli kaka. Haya mambo ya
huyu jini aliyekuwa akiniandama ndio yaliyonizubaisha”
“Mimi naamini akikuona una
mke hatakufuata tena. Atakwenda kutafuta mtu mwingine. Kama
atakubali, awe mke mwenza” Kaka akanichekesha.
Tukacheka sote.
“Nadhani hawezi kukubali kuwa
mke mwenza” nikamwambia.
“Ndio atakuacha sasa”
“Ni kweli kaka, ni bora niwe
na mke”
“Sasa unaye msichana
unayemfikiria kwamba anafaa kuwa mke wako ili tukakuposee”
“Nitakujibu”
“Lini?”
“Nipe siku mbili tu”
“Sawa”
Lile wazo la kuoa alilonipa
kaka nilikwenda kulitafakari nyumbani na kuona lilikuwa wazo la busara sana. Mbali ya kwamba
nilishafikia umriwa kuwa na mke pia niliona nitakuwa na mwenzangu wa kunifariji
kutokana na matatizo yaliyokuwa yananikabili.
Pia nilizingatia kauli ya
kaka kwamba nikioa, huenda yule jini akaacha kuniandama.
Kulikuwa na msichana mmoja
aliyekuwa akiishi mtaa wa pili na ule niliokuwa nikiishi mimi. Alikuwa akiitwa
Salma.
Salama nilikuwa nikimfahamu
tangu alipokuwa anasoma shule ya sekondari ya Usagara. Alipomaliza kidato cha
nne niliwahi kumtamkia kuwa ninampenda.
Akaniuliza. “Unanipenda kweli
au unanidanganya?’
“Ninakupenda kweli”
nikamjibu.
“Sasa kama unanipenda kweli,
waone wazazi wangu. Mimi nimeshakukubalia”
Kwa vile muda ule sikuwa na
mawazo ya kuoa, sikumpatiliza tena ila kila tulipoonana nilimtania kwa
kumwambia, “Nitakuja kwa wazazi wako”
Na yeye hucheka na kunijibu.
“Njoo tu, njia nyeupe”
Alikuwa mzuri mwenye heshima
na alikuwa na sifa zote zinazostahili kuwa mke wangu.
Yeye ndiye niliyemfikiria.
Hata hivyo wakati ule wazazi
wake walikuwa wameshahama katika mtaa waliokuwa wakiishi. Mwenyewe aliniambia
walihamia Chumbageni.
Kwa wakati ule Salama alikuwa
akifanya kazi Shirika la Posta. Nikapanga nimfuate nizungumze naye ili
nimueleze nia yangu ya kupeleka posa yangu kwa wazazi wake.
Siku iliyofuata nikaenda
kazini. Saa nne wakati wa kwenda kunywa chai nikaenda posta. Nikamkuta.
Nilisubiri watu wawili
aliokuwa akiwahudumia walipoondoka nikamsalimia.
“Hujambo mrembo?”
“Sijambo, sijui wewe”
“Mimi ni mzima tu kama unavyoniona, hivi kule Chumbageni unaishi mtaa
gani?” nikamuuliza.
Salama akanielekeza mtaa
anaoishi. Kwa vile na mimi nilikuwa mwenyeji wa mitaa ya Chumbageni niliifahamu
mpaka nyumba waliyokuwa wanaishi.
“Si ile inayotazamana na
Cumbageni Guest House?” nikamuuliza.
“Ndiyo hiyo hiyo”
“Natarajia kutuma mshenga
kwenu” nikamdokeza.
Salama hakunijibu kitu.
Nikaridhika. Kuwa kimya inachukuliwa na masheikh wa kiislamu kuwa ni ishara ya
kukubali, kwa vile suala hilo
tulishalizungumza.
Nilipotoka kazini jioni
nilikwenda kwa kaka nikamueleza kuhusu msichana huyo.
“Umeshazungumza naye”
akaniuliza.
“Niliwahi kuzungumza naye
siku nyingi lakini ilikuwa kama mzaha, leo
ndio nilimfuta kazini kwake nikamwambia kuwa nitatuma mshenga kwao akanyamaza.
Nimechukulia ishara kwamba amekubali”
“Sasa tujaribu kupeleka
ujumbe kwao?”
“Ndio hivyo”
JAMANI NIMECHOKA KUSIMULIA.
KWA LEO NAISHIA HAPA. TUKUTANE TENA KESHO.
No comments:
Post a Comment