Friday, April 8, 2016

HADITHI MWANAMKE ALIENICHUNUKU SEHEMU YA (8)

HADITHI na Faki . A . Faki 0713 340572 , 0655 340572
 
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 8
 
Kutoka siku ile yule jini hakunifuata tena, nikawa nimefurahi. Lakini baada ya kupita juma moja nilianza kuota ndoto za ajabu ajabu, nyingine zikiwa za kutisha.
 
Kusema kweli hazikuwa ndoto za kawaida kwani zilifululiza kama mkanda wa sinema, ikimalizika hii inakuja hii. Wakati mwingine ninaota nipo kwenye majabali marefu nikiwa na  msichana  ambaye ghafla huanza kunilaumu kuwa nimemgeuka. Lakini mara sura yake hubadilika na kuwa ya yule msichana wa kijini. Hapo huanza kumkimbia na kila ninavyokimbia yule msichana hutokea mbele yangu.
 
Wakati mwingine huzinduka usingizini lakini usingizi unaponijia tena, ile ndoto huendelea. Inapoendelea hujikuta nimefika kingoni mwa jabali ambapo yule msichana hunisukuma, nikajiona naanguka kutoka juu ya jabali refu huku ninapiga kelele.
 
Inapomalizika ndoto hii inakuja nyingine. Huota nipo kwenye maeneo ya makaburi. Ghafla miili ya watu waliokufa hutoka katika makaburi na kunifuata ikiwa mifupa mitupu. Ninatoka mbio lakini najiona ninavutwa kwa nyuma kama ninayevutwa kwa sumaku hadi ile mifupa inanikaribia na kunigombania na ndipo ninapozinduka.
 
Ndoto za namna hiyo ziliniandama karibu kila siku. Mwisho nilirudi tena kwa yule Mchungaji kumueleza, akanifanyia maombi tena lakini ndoto hazikukoma. Nilipoona hali inazidi kuwa mbaya nikahamia kwa rafiki yangu Juma.
 
Kwa Juma pia sikupata nafuu yoyote. Ndoto ziliendelea kuniandama huko huko. Siku moja niliota nachinjwa nikapiga ukulele uliomuamsha Juma. Alipoamka aliniuliza.
 
“Una nini Alfred?”
 
Jasho lilikuwa linanitoka na moyo ulikuwa unanienda mbio kama ulitaka kutoka. Nikaketi kitandani na kumueleza nilivyoota Hata yeye aliogopa. Siku ile hatukulala tena hadi asubuhi.
 
“Uende kwa mganga” Juma akaniambia asubuhi. Alinielekeza kwa mganga mmoja aliyekuwa akikaa kitongoji cha Amboni. Kitongoji hicho kipo umbali wa kilometa 10 hivi kutoka jiji la Tanga.
 
Akaniambia kaka yake alikuwa na tatizo kama langu la kuota ndoto za kutisha lakini alipokwenda kwa mganga huyo tatizo hilo likamalizika.
 
“Huyo mganga anaitwa nani?”
 
“Anaitwa Mtemi Wembe”
 
“Nitakwenda Amboni kumuulizia”
 
“Ningekupeleka lakini ndiyo hivyo ninakwenda kazini na kurudi ni jioni”
 
“Hakuna tatizo, kwa vile umeshanielekeza nitakwenda mwenyewe”
 
Juma alipoondoka kwenda kazini kwake na mimi niliondoka kwenda huko Amboni. Nilikwenda stendi nikapanda daladala za kwenda Amboni. Nilipofika Amboni nilimkuta mtu mmoja akichoma mahindi ya kuuza palepale kwenye kituo cha daladala. Nikamuuliza kama anamfahamu mganga Mtemi Wembe.”
 
“Ni maarufu” akanijibu na kuongeza..
 
“Kamata barabara hii, nenda moja kwa moja. Mbele kule utakuta njia mbili, moja inaelekea kulia na nyingine kushoto. Fuata ile ya kushoto, ukienda mbele utakuta mbuyu. Ukiupita mbuyu utakata tena kushoto. Nyumba utakayoikuta mbele yako ndiyo hiyo ya Mtemi Wembe”
 
Ilikuwa kama alivyonielekeza Juma. Nikamshukuru yule mtu kisha nikafuata ile barabara aliyonielekeza hadi nikauona ule mbuyu. Nilipokata kona kushoto nikaiona ile nyumba. Nikaenda
 
Nilikuta watu kadhaa wakiwa nje wameketi kwenye gogo la mnazi wakisubiri zamu ya kuingia. Na mimi nikaenda kujiunga nao. Kulikuwa na watu wengine waliokuja nyuma yangu. Sote tukawa tunasonga taratibu kuelekea kwenye mlango wa nyumba ya mganga.
 
Ghafla nilisikia harufu ya manukato makali puani mwangu, nikageuza uso wangu na kumtazama msichana aliyekuwa ameketi kushotoni kwangu. Nikashituka nilipoona ni yule msichana wa kijini. Alikuwa ameketi sambamba na mimi. Wakati namtazama na  yeye alikuwa akinitazama.
 
“Amekuja muda gani?” nikajiuliza kimoyomoyo huku nikiwa nimepatwa na mshangao.
 
Ukweli ni kuwa nilipofika hapo, msichana huyo hakuwepo. Bila shaka alikuwa miongoni mwa watu wanne waliokuja baada ya mimi. Lakini kwa vyovyote vile kuja kwake kulikuwa kwa kimiujiza kwani sikumuona alivyofika, nilishitukia tu yupo hapo baada ya kusikia harufu ya manukato yake.
 
Kwa jinsi nilivyoshituka, moyo wangu ulianza kunienda mbio. Sikuwa na raha tena. Nikanyanyuka ghafla na kuondoka kama mtu ambaye nilikuwa nimeghairi kuingia kwa mganga kwani nilihisi angenifuata humo ndani.
 
Nilitenbea haraka haraka nikakata kona kwenye ule mbuyu kisha nikaanza kukimbia. Nilipokata kona nyingine kuelekea upande wa kulia. Ghafla nikamuona yule msichana mbele yangu.
 
Nikasisimama ghafla. Kwa kweli niligwaya. Nikawa namtazama na yeye akanitazama. Macho yake yalikuwa makali kama kaa la moto na uso alikuwa ameukunja.
 
“Unajisumbua bure!” akaniambia.
 
Ingawa alionekana kukasirika lakini sauti yake ilikuwa tulivu.
 
“Mimi sikimbiliki. Nimeshakuzunguka pande zote. Kama unaweza kuingia chini ya ardhi ingia, ndio sitaweza kukufuata. Lakini huku juu ya ardhi hata kama utakimbilia Ulaya nitakufuata tu!” akaniambia.
 
Nilikuwa nimenyamaza kimya nikimtazama na kumsikiliza huku nikirudi nyuma taratibu. Pakapita ukimya mfupi.
 
“Ulienda kwa mganga kufuata nini?” akaniuliza ghafla na kuongeza.
 
“Unadhani mganga ataweza kunifukuza mimi? Mimi sifukuziki!”
 
Akaendelea kuniambia “Mimi ni Banuna mwana wa Ziraili. Ukoo wetu ni wa wachawi. Babu yangu ni mkuu wa wachawi! Hakuna mganga atakayeniweza mimi”
 
Akanyamza na kunitazama jinsi nilivyokuwa ninahema kisha akaendelea.
 
“Ni kwa sababu tu nimekupenda ninakuruhusu urudi nyumbani. Lakini ninakupa muda mwingine mfupi ufanye maamuzi sahihi. Ukiendelea kuniletea kisoi utajuta!”
 
Baada ya kuniambia hivyo alichora msitari chini kwa mguu wake, akaniambia.
 
“Vuka huu msitari urudi nyumbani”
 
Nilikuwa nimepatwa na hofu isiyo na kifani. Sikuelewa alikuwa ananiambia nini,mpaka aliporudia kwa mara ya pili.
 
“Nimekuambia vuka huu msitari urudi nyumbani. Nisikuone tena kwenye nyumba za waganga!’
 
Nikapiga hatua haraka haraka kuvuka ule msitari aliouchora chini kwani alikuwa amesogea kando. Nilipouvuka tu ule msitari nikajikuta nipo mbele ya nyumba ninayoishi.  Sikuwapo tena mahali pale nilipokuwa na yule msichana wa kijini!.
 
Huku nikiwa nimeshikwa na mshangao uliochanganyika na hofu, niliangalia upande wa kulia na wa kushoto. Sikumuona tena yule msichana
 
Nikawa najiuliza nimefikaje pale nyumbani? Hatua moja tu niliyopiga kuvuka ule msitari imenifikisha katika nyumba ninayoishi? Ilikuwa miujiza mikubwa!.
 
Badala ya kuingia ndani niligeuka nikaelekea nyumbani kwa Juma,  Juma alikuwa yupo kazini kwake lakini kwa vile alikuwa ameniachia ufunguo mmoja, nilifungua mlango nikaingia ndani. Nikafikia kujilaza kitandani.
 
Ingawa sikuwa na yule msichana, hofu ilikuwa imenitawala na kusababisha nijisikie kupata homa.
 
Siku ile sikutoka tena mle chumbani mpaka Juma aliporudi jioni. Alikuta nilikuwa nikitetemeka kwa homa.
 
“Alfred unaumwa?” akaniuliza.
 
“Nasikia homa”
 
“Tangu saa ngapi?”
 
“Tangu asubuhi”
 
“Dah! Umeshakula dawa?”
 
“Bado. Kwanza hebu kaa nikueleze yaliyotokea kule kwa mganga”
 
Huku akionekana kupata wasiwasi, Juma alikaa kwenye kiti. Nikamueleza yale yaliyonitokea kule Amboni na nilivyorudishwa nyumbani kimiujiza.
 
Juma akashangaa.
 
Je nini kitatokea. Endelea kufuatilia kesho hapa hapa Tangakumekuchablog


No comments:

Post a Comment