HADITHI
MWANAMKE 36
ILIPOISHIA
Nikaagana na kaka na kwenda
nyumbani kwa mama. Nilimueleza ile habari. Akaniambia ameshaelezwa na mwanawe,
yaani kaka yangu.
“Ni jambo zuri” akasema.
“Kesho kutwa tutakuja kufanya
kikao cha harusi hapa kwako”
“Kwani mambo tayari?’
“kaka atapeleka mahari kesho
kutwa”
“Hizo shilingi laki tano?”
“Ndio”
“Umeshampa?”
“Nimemwambia nitampa kesho”
“Yeye atakusaidia shilingi
ngapi?’
“Ameniambia atanitolea
shilingi laki moja, mimi mwenyewe nitatoa laki nne”
“Kwa hiyo mnasubiri mmpeleke
mahari ndio tufanye kikao”
“Ndiyo”
“Mimi nawaunga mkono.
Nilitaka sana
wewe uwe na mke. Hilo
wazo nililitoa mimi”
“Lilikuwa wazo zuri na
natumaini nikiwa na mke matatizo yangu yatapungua’
“Utakuwa vizuri mwanangu”
“Sawa mama, basi mimi narudi
nyumbani”
Nikaagana na mama na
kuondoka.
SASA ENDELEA
Siku iliyofuata nilikwenda
benki, nikatoa shilingi laki tano kutoka katika akaunti yangu. Jioni nilipotoka
kazini nikampelekea kaka shilingi laki nne kama
tulivyokubaliana.
Nilipotoka kwa kaka nikaenda
kwa mama. Nikamueleza kuwa nimeshampa kaka shilingi laki nne.
Mama akafurahi.
“Nawatakia heri na mafanikio”
akaniambia na kuniuliza.
“Zitapelekwa kesho?”
“Kaka ameniambia atazipeleka
kesho na kesho hiyo hiyo tutakuwa na kikao hapa kwako”
“Saa ngapi?’
“Nadhani itakuwa usiku”
“Sawa wanangu, nawasubiri”
Siku iliyofuata ilikuwa
jumapili, sikwenda kazini. Nilibaki nyumbani kufanya usafi na kufua nguo zangu
zilizochafuka.
Saa saba ndipo nilipotoka. Nilikwenda
kwenye mkahawa mmoja kula chakula. Nilipotoka hapo nikaenda kwa kaka.
Aliniambia ndio kwanza amerudi kutoka chumbageni.
“Mzee ameniambia baada ya
kupata mahari anachosubiri ni kutajiwa siku ya harusi” kaka akaniambia.
“Sasa tujiandae, tupeleke siku”
“Kwani tutakutana saa ngapi
kwa mama?’
“Nimemwambia tutakutana
usiku”
“Usiku saa ngapi?’
“Tukutane kuanzia saa moja”
“Sawa”
“Naona mambo yanakwenda
vizuri”
“Yanakwenda vizuri sana”
Saa mbili usiku tulikutna
nyumbani kwa mama. Mimi nilifika mapema zaidi kabla ya kaka. Ilibidi niwahi kwa
sababu mimi ndiye niliyekuwa na shughuli, ilikuwa vyema mwenzangu anikute pale
nyumbani na sio nimkute yeye.
Kaka alipofika tukaanza
mazungumzo. Mazungumzo yetu yalikuwa marefu na yaliishia saa nne usiku. Tulipanga
kila kitu. Kwa vile mimi nilikuwa na
akiba yangu ambayo nilipanga niitumie kwa ajili ya harusi yangu, tulikubaliana
kwamba harusi ifanyike haraka, baada ya wiki mbili.
“Hizi wiki mbili ndio za
kufanya maandalizi, mnaonaje zinatosha au tuongeze siku?” kaka alituuliza
wakati tunaendelea na kikao chetu.
Nikamtazama mama, nikaona
mama naye ananitazama mimi.
“Mimi naona zinatosha, hakuna
haja ya kuongeza siku zaidi” nikasema.
“Mama unasemaje?” Kaka
akamuuliza mama aliyekuwa kimya.
“Mimi sina usemi, nawasikiliza
nyinyi”
“Na wewe unaafiki kwamba wiki
mbili zinatosha kwa maandalizi?” Kaka akamuuliza.
“Kama Amour mwenyewe amesema
zinatosha na mimi nasema hivyo hivyo zinatosha”
“Sawa. Naona tumeafikiana kwa
hilo. Sasa
tupange siku yenyewe ya kufunga ndoa” kaka akatuambia.
“Tuweke siku ya ijumaa baada
ya mshuko. Muda huo ni mzursana kufunga ndoa” nikasema.
“Mimi pia naafikiana na muda
huo. Kwa hiyo hatuhitaji kwenda kutazamia siku wala saa?’
“Enzi zetu tulikuwa
tunatazamia siku lakini siku hizi mambo yamebadilika” mama akasema.
“Mama unajua kutazamia siku
ni kuleta ushirikina. Siku zote zinafaa kuoa na saa zote mtu unaweza kuoa.
Mtume ametuambia saa nzuri ni baada ya mshuko wa ijumaa” nikamwambia mama.
“Swadakta Amour, umesema
sawa. Umekuwa answar sunna” Kaka akanikubalia.
“Si lazima niwe answaar
sunna. Hivi ndivyo tulivyofundishwa na mtume wetu. Kufanya vinginevyo ni
ushirikina”
“Wanasema kwamba usipotazamia
siku unaweza kuoa siku mbaya na maisha yako ya ndoa yakawa ya mikosi na vifo”
kaka akayuambia.
“Uongo mtupu. Ni imani tu za
watu” nikasema.
“Sawa. Tumeshakubaliana
kwamba ndoa itafanyika baada ya mshuko wa ijumaa. Kutahitajika tende kidogo na
kahawa au siyo”
“Ndiyo”
“Ndoa itafanyika wapi?”
“Msikiti wa ijumaa”
“Msikiti ule ni mkubwa, siku
za ijumaa unakuwa na watu wengi, haluwa haitatosha. Tuchague msikiti mwingine”
kaka akashauri.
“Basi tutatafuta msikiti
mwingine kule kule Chumbageni”
“Hilo tumelimaza. Sasa tayarisha kadi mapema
uzitoe kwa wafanyakazi na rafiki zako. Na mimi nitachukua kiasi. Baada ya wiki
moja tukutane tena tuone tumepata kiasi gain”
“Sawa kaka”
Tulimaliza mazungumzo yetu.
Nikampakia kaka kwenye pikipiki yake kumrudisha nyumbani kwake. Na mimi
nikarudi nyumbani kwangu.
Usiku wa siku ile ndoto zangu
zote zilikuwa za harusi. Niliota ninamuoa Salma aliyekuwa akingara kama mwezi. Ingawa mwenyewe nilipanga kumuoa mchana,
niliota ninamuoa usiku wa manane.
Ndoa yenyewe ilifanyika
kwenye kisiwa kisicho na watu. Tulikuwa mimi na yeye na muozeshaji wetu..
Baada ya kuota ninaona na
salama nikaota Salama amepata mtoto wa kiume, mzuri ajabu.
Nilipoamka asubuhi na
kiondoka nyumbani nilikwenda kazini kwangu. Siku ile ile nikashughulikia mpango
wa kuchapisha kadi za harusi ambazo nilizipata siku ile ile.
Wakati tunatoka kazini jioni
nilimkabidhi kiasi kikubwa cha kadi msichana mmoja ambaye ni mfanya kazi
mwenzangu ili anichangie kwa marafiki zake na kwa wafanyakazi wenzetu.
Nikawataarifu baadhi ya wafanyakazi wenzangu kuhusu ndoa yangu.
Nilipotoka kazini nilikwenda
nyumbani kwa kaka. Naye nikampa kiasi cha kadi ili azigawe kwa marafiki zake.
Mimi mwenyewe nilibaki na
kiasi kidogo cha kadi hizo kwa ajili ya kuwagaia marafiki zangu.
Nilishukuru kwa jinsi
nilivyoungwa mkono. Kadi zote ziligaiwa kwa watu na kila aliyepewa kadi
aliahidi kunichangia baada ya wiki moja.
Kweli, baada ya wiki moja nilipata mchango wa kutosha sana ambao ulinipa
matumaini kuwa ndoa yangu itafanikiwa. Ile wiki tuliyopanga nifunge ndoa, kaka
alipeleka taarifa ukweni kuwa ndoa itafanyika siku ya ijumaa. Tulikuwa tumewapa
siku saba tu za maandalizi lakini walikubaliana na sisi.
Naam siku ikawadia. Niliwekwa
ndani kama mwari, nikasingwa kwa msio na
mafuta ya nazi. Walionisinga walikuwa ni
binamu zangu. Ilikuwa raha asana.
Ndoa ilifungwa katika msikiti
mmoja uliokuwa maeneo ya Chumbageni.
Nakumbuka hadi leo jinsi
sheikh mmoja alivyonifungisha ile ndoa.
Aliniita jina langu kisha
akaniambia nimuitikie “Labaika”
“Labaika” nikamuitikia.
Akaniita tena.
“Amour Amrani”
“Labaika” nikamuitikia.
“Ninakuozesha Salama binti
Riyami kwa mahari mliyokubaliana, umekubali?”
“Ndiyo” nikamuitikia huku
midomo yangu ikitetemeka. Sikujua ilitetemeka kwa sababu gani.
“Hapana. Hilo silo jibu linalotakiwa ujibu. Unatakiwa
useme nimekubali kumuoa Salama binti Riyami kwa mahari tuliyokubaliana”
“Sawa”
“Amour binti Amraani” Sheikh
akaniita tena.
“Labaika”
“Ninakuozesha Salama binti
Riyami kwa mahari mliyokubaliana, umekubali?”
Nikayakumbuka yale maneno
aliyonifundisha.
“Nimekubali kumuoa Salama
binti Riyami kwa mahari tuliyokubaliana” nikajibu.
Sheikh alirudia tena
kuniambia hivyo mara tatu na mimi
nilijibu mara tatu. Baada ya hapo ikasomwa hutuba ya ndoa iliyochukua karibu
nusu saa.
JE NINI KITATOKEA? TUKUTANE
TENA KESHO. EID MUBARAK!
No comments:
Post a Comment