SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 39
ILIPOISHIA
Nilirudi nyumbani, nikapanga
baadhi ya nguo zangu kwenye begi. Nilikuwa na akiba ya pesa nilizokuwa
nimeziweka kwenye kabati. Nikazichukua.
Kwa vile kichwa kilikuwa
kimenichafuka, nilimuachia funguo mwenzangu wa upande wa pili nikaenda kulala
gesti.
Kitu ambacho kilinikera sana, niliota Zena
amesimama kwenye jangwa akinicheka. Alikuwa akinicheka hadi anayumba kama mlevi.
Asubuhi kulipokucha nilitoka
nikaenda kituo cha mabasi. Nilipanda basi la kuelekea Dar. Nilifika Dar saa
sita mchana nikaenda kutafuta gesti. Nilipopata gesti niliacha begi langu na
kwenda kwenye mkahawa uliokuwa karibu kupata chakula kwani sikuwa nimekula
chochote tangu subuhi.
Baada ya kula chakula
nilirudi pale gesti. Kulikuwa na mgeni mmoja wa kipemba aliyekuwa amepangisha
chumba. Tulikutana ukumbini. Nikamsalimia na kumuuliza kama alikuwa anatoka Zanzibar.
“Natoka Mwanza, ndio niko
safarini kuelekea Zanzibar”
akaniambia.
“Unakwenda Unguja au Pemba?”
“Mimi naenda Pemba”
“Unatarajia kwenda lini?”
“Kesho asubuhi Mungu
akipenda”
“Basi tutaondoka sote,
nilikuwa na tatizo linalohusu huko Pemba na
nitakueleza”
“Ni tatizo gani?”
“Hebu njoo huku chumbani
kwangu nikueleze”
Yule mtu alikubali kuingia
chumbani kwangu. Nikamueleza yale matatizo yangu.
SASA ENDELEA
“Sasa shida yangu ni kupata
mganga ambaye ataliondoa hili tatizo” nikamwambia.
Mpemba alinyamaza kimya
akafikiri kisha akaniambia.
“Yuko mama mmoja pale Pemba
ni mganga anayetegemewa sana
kwa matatizo ya majini. Kama yeye atashindwa
ujue hutapata tena mganga ambaye atamuweza huyo jini wako”
“Ningekuomba unipeleke kwa
huyo mwanamke”
“Nitakuelekeza na hutapotea”
“Lakini wewe pia si unakwenda
huko huko”
“Ndio, mimi nakwenda Pemba lakini ninakokwenda ni kwingine na huyo mganga yuko
kwingine. Yaani hata tukienda sote tutaachana bandarini”
“Si kitu, wewe nielekeze tu,
nitafika”
Kwa vile mji wenyewe nilikuwa
siujui, yule mtu alinichorea ramani ikianzia bandari ya Pemba
hadi ulikokuwa mtaa huo. Akaniambia nyumba ya mganga huyo iko kwenye kona. Ni
nyumba kubwa lakini ni ya kizamani sana
na imepakwa chokaa nyeupe.
“Alama yake ni kuwa mlango wa
mbele wa nyumba hiyo umechorwa picha ya nyota na mwezi” akaniambia.
“Nitapaelewa tu” nikamwambia.
Asubuhi ya siku iliyofuata
tukasafiri sote kwenye boti. Tulipofika Pemba akanielekeza tena. Nikaenda
mwenyewe katika huo mtaa.
Kwa vile nilikwenda kwa miguu
ili nisipotee nilitembea sana
Mara kwa mara nilikuw a
nawauliza watu niliokutana nao njiani kama
wanamfahamu mganga huyo. Baadhi ya watu hao walikuwa wanamfahamu na
wakanielekeza zaidi mtaa aliokuwa anaishi.
Baada ya mwendo mrefu
nikafika katika mtaa huo, nikawa naitafuta ile nyumba. Baada ya kuhangaika sana nikaiona. Ilikuwa
kwenye kona na ilipakwa chokaa nyeupe.
Alama kubwa iliyonipa moyo ni
picha ya nyota na mwezi niliyoikuta kwenye mlango.
Kama alivyonieleza yule mtu
niliyesafiri naye, nyumba hiyo ilikuwa ya kizamani sana na ilikuwa kwenye hatari ya kuanguka
kwani ilikuwa ni nyumba iliyojengwa kwa mawe na udongo ingawa ilipauliwa kwa
bati. Bati hilo
lilikuwa limeota kutu na kuchakaa.
Nikaenda kwenye mlango na
kubisha. Nilibisha mara mbili bila kupata jibu. Nilipobisha mara ya tatu nikajibiwa.
“Karibu” Ilikuwa sauti ya
mwanamke. Nilishaambiwa kuwa mgaga mwenyewe ni mwanamke.
Baada ya sekunde chache
mlango ukafunguliwa. Ndani kulikuwa
kiza. Hata mtu aliyenifungulia mlango sikuweza kumuona vizuri.
“Karibu ndani” Sauti ya
mwanamke ikaniambia.
Nikaingia. Kulikuwa na ukumbi
mpana uliokuwa umetandikwa jamvi.
“Karibu ukae kwenye jamvi”
Nikakaa. Yule mwanamke naye
akakaa kando yangu.
“Pole kwa safari, naona
umetoka mbali” akaniambia huku akinitazama. Sasa pale ndipo nilipomuona vizuri.
Kumbe alikuwa Zena!
Nilishituka sana nilipogundua kuwa mwanamke mwenyewe
alikuwa Zena.
Nilishindwa kuelewa kwanini
amekuwa Zena wakati niliambiwa kulikuwa na mwanamke ambaye ni mganga.
“Habari za huko?” Zena
aliniuliza alipoona nimepigwa na butwaa.
Niligeza haraka uso wangu
nisitazamane naye. Nikawa natazama chini.
“Nzuri” nikamjibu. Sauti
yangu ilikuwa nzito ya mtu aliyetahayari.
“Mbona umekuja huku, una
shida gani?” akaniuliza huku akinitazama kwa makini. Nilikuwa nimeinamisha uso
wangu lakini nilikuwa namuona kwa pembeni mwa macho yangu.
Nilishindwa kujibu Swali lake kwa
sababu sikujua ningemjibu nini. Nimjibu kuwa nimekwenda Pemba
kufuata mganga na badala yake nakutana na yeye? Hapana.
“Nimekuja kutembea tu”
nikamwambia baada ya kushindwa kumueleza
ukweli.
“Umekuja kutembea tu huku Pemba?” Zena akaniuliza kwa sauti iliyoonesha kuwa
hakuyaamini maneno yangu.
“Ndio” nikamjibu.
“Sasa umeshatembea na kuuona
mji?”
“Ndio”
“Umeuonaje?”
“Ni mji mzuri”
“Kumbe unatembea hadi huku Pemba?’
“Ni leo tu”
“Umepanga kurudi lini?”
“Nitarudi leo”
“Si ulale uondoke kesho?”
Nikatikisa kichwa.
“Nitaondoka leo leo”
“Nisubiri basi tuondoke sote”
Zena akainuka. Aliingia
kwenye chumba kimojawapo ambacho mlango wake ulikuwa wazi. Nikamuona anavaa
baibui. Akachukua mkoba wake na kutoka.
“Twendezetu” akaniambia kama vile tulikuja safari moja.
Nikainuka na kumfuata.
Tulitoka kwenye ile nyumba tukashika njia
ya kuelekea bandarini.
Wakati wote nilikuwa
nikijiuliza kwanini nilimkuta Zena pale nyumbani. Huyo mganga mwenyewe alikuwa
wapi?
Ile ilikuwa ni miujiza ya
ajabu ambayo sikuwahi kuiona katika maisha yangu.
Matarajio yangu ya kumpata
mganga wa kuliondoa tatizo langu yalififia kabisa moyoni mwangu. Huyu jini
alikuwa amenizingira kila pembe.
Tulipofika bandarini Zena
alikata tikiti mbili za boti inayokwenda kasi. Boti hiyo ilikuwa inakwenda Dar.
Siku ile hakukuwa na chombo chohote kinachokwenda Tanga.
Tulipojipakia kwenye boti
nilikaa na Zena siti zilizokuwa zimepakana. Tulisubiri kwa muda wa saa nzima kabla
ya safari kuanza.
Kweli kupambana na jini aina
ya Zena ni kazi! Sasa alikuwa akinirudisha Dar. Niliamini kuwa alikuwa akijua
kilichonipeleka Pemba ingawa hakuniambia. Kitu
ambacho nilishindwa kuelewa ni jinsi nilivyomkuta yeye pale nyumbani kama vile ni kwake.
Wakati boti iko katikati ya
safari nilimuona Zena amelala usingizi kabisa. Nikawa namtazama. Alikuwa na
weupe uliochanganyika na wekundu. Uso wake ulikuwa na pozi la kiarabu ingawa
alionekana kuchanganya damu ya Kiafrika. Sikujua kama majini nao wanakuwa
machotara kama binaadamu.
Kwa uzuri alikuwa mzuri sana, sikuwahi kuona msichana mwenye mvuto wa sura na
umbile kama yeye. Tatizo lake ni
kwamba alikuwa jini tena jini mbaya mwenye vituko vilivyoshindikana.
Hadi pale nilikuwa nimesalimu
amri. Nilishasema kuwa Zena sitamuweza tena na hakukuwa na mganga yeyote
atakayemuweza.
Ghafla tuliona boti ikikata
moto. Ikawa inasuasua juu ya bahari. Muda si muda ikapigwa na wimbi kubwa. Sote
tulitikiswa. Hapo ndipo watu walipoanza kwenda mbio na kuifanya boti ilale
upande mmoja.
Baadhi ya abiria wakaanza
kujitosa baharini. Nikaona sasa hali ilikuwa mbaya. Nilijikuta nikimuamsha Zena
bila kupenda. Zena akaamka.
“Nini. Mbona kuna hekaheka?”
akaniuliza.
“Boti inazama” nikamwambia.
“Boti inazama?” akaniuliza
kwa fadhaa.
Kabla sijamjibu, ule upande
wa boti uliokuwa unazama ukazidi kulala.
“Duh ni kweli, twende
tukaruke, tutakufa humu!” akaniambia huku akiinuka kwenye siti.
Tulikwenda kwenye mlango wa
boti tukatoka. Watu walikuwa wakiendelea kuchupa baharini.
“Chupa!” Zena akaniambia.
Laiti angejua jinsi ambavyo
sikuwa nikijua kuogelea asingeniambia chupa.
Upande wa pili wa boti nao
ikaanza kuzama.
“Chupa, boti inazama!”
akaniambia tena.
Sikuthubutu. Nilibaki
kuitazama bahari.
“Amour unasubiri kufa humu
ndani ya boti?” Zena akaniuliza kwa hasira.
Nikatikisa kichwa.
“Siwezi kuogelea, nikiruka
ndio nimekwisha!”
“Mwanaume mzima unasema
huwezi kuogelea, mimi mwanamke nisemeje?” akaniuliza.
Sikuwa na jibu. Nikaendelea
kutikisa kichwa changu.
Sikujua ilikuwaje. Zena
alinishika mkanda wa suruali yangu kwa nyuma kisha akanirusha baharini. Hadi
leo nashindwa kujua alinirushaje.
Kabla ya kutumbukia baharini,
nilijiambia ule ulikuwa ndio mwisho wangu.
Nilitanguliza mikono na
kichwa, Nikazama chini kabisa.
No comments:
Post a Comment