HADITHI na Faki . Faki 0655 340572 / 0713 340572
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 10 inaletwa kwenu na Mkombozi Sanitarium Clinic Tanga, mabingwa wa Tiba na hutoa ushauri wa kitaalmamu na wako na vifaa vya kisasa, Wapo Tanga barabara ya 12 Ngamiani, simu 0654 361333
ILIPOISHIA
“Sasa
mzee nimekuja na zile pesa. Umesema vile vifaa vinagharimu kiasi gani?” Juma
akamuuliza mganga huyo.
“Ni
elfu arubaini”
Juma
akamuhisabia shilingi elfu arubaini na kumpa.
“Vifaa
vyote vinavyohitajika ninavyo hapa. Kazi yenu itafanyika ufukweni mwa bahari.
Itabidi twende huko pamoja na vifaa vyote”
Baada
ya kutuambia hivyo mganga aliwaita wasaidizi wake wawili. Mmoja akamwambia
atangulie na sisi huko ufukweni mwa bahari na mwingine akampa kazi ya
kwenda kuchukua vifaa vilivyohitajika.
Sisi
tukatoka na yule mtu, tukaenda kwa miguu huko ufukweni. Ulikuwa mwendo mrefu
kidogo. Tulipofika hapo mahali, bahari tulikuwa tunaiona mbele yetu. Tukakaa
kwenye mchanga mkavu wa ufukweni kumsubiri mganga.
Mganga
alifika baada ya saa moja hivi akiwa na msiidizi wake wa pili. Mganga mwenyewe
alikuwa ameshika mkuki na kapu lililokuwa na vifaa. Na msaidizi wake alikuwa
ameshika kapu jingine na mkono mwingine alikokota mbuzi mweusi.
SASA
ENDELEA
Nilipowaona mwili
ulinisisimka. Sikujua ni kwanini. Pia nilijiona nikipata hofu. Nilihisi labda
ni kwa sababu shughuli hizo zilikuwa za kishirikina wakati mimi nilikuwa ni
muumini wa kanisa. Pamoja na ukweli huo niliona sikuwa na budi nikabiliane na
ushirikina huo kwani matatizo yaliyonikuta hayakuwa madogo.
Mganga na msaidizi wake
wakapanga vifaa vyao pale chini. Palikuwa na vifaa vingi vya kiganga zikiwemo
nazi saba, kijungu, mchanga mweusi ambao niliambiwa ni mchanga wa kaburi na
vitu vingine.
Vitu hivyo vilipangwa
kuzunguka duara na mimi nikaambiwa nikae katikati ya duara hilo. Mganga akaniambia nisiwe na hofu.
“Tatizo lako litakwisha leo.
Nitamuita yule jini hapahapa na nitawafarakanisha. Hatakufuata tena”
akaniambia.
Maneno yake kwa upande mmoja
yalinipa matumaini lakini kwa upande mwingine yaliniongezea hofu.
Yaliniongezea hofu kwa sababu
yule msichana wa kijini alikwishanionya kuwa nisiende tena kwa mganga na kwamba
yeye amezaliwa katika ukoo wa wachawi na hakuna mganga atakayemuweza.
Lakini mganga huyo
nilipomueleza maneno hayo alionekana kuyapuuza na kutoyatilia maanani.
Akaniambia kuwa yeye ni kiboko wa majini.
Hakuna jini anayemshinda yeye.
“Maneno yake ni vitisho tu.
Alitaka kukutisha ili usije kwangu, anajua mimi ni mkali” Mganga huyo
akaniambia kwa kujitumainisha
Mara tu baada ya mimi kuketi
katikati ya lile duara, mganga alielekea upande wa baharini akapaza sauti yake
na kutamka maneno ya kiarabu ambayo sikuweza kujua maana yake. Baadaye akasema
kwa Kiswahili.
“Ewe Banuna mwana wa Ziraili
wa ukoo wa Ummi Subiani, ninakuita hapa kwa Alfred, uje hapa haraka sana, nina shughuli na
wewe”
Aliyarudia maneno hayo mara
tatu. Baada ya hapo alianza kusoma kwa kiarabu huku uso wake ukutazama
baharini.
Alisoma kwa kiaribu kwa
karibu saa nzima. Kwanza kulikuwa kimya.
Kilichokuwa kikisikika ni mvumo wa mawimbi ya bahari. Lakini ghafla nazi tatu
zikapasuka zenyewe vipandevipande!.
Hapo hapo tukaona wimbi kubwa
la maji ya bahari linakuja huku likitoa ngurumo kali.
Nilitaka kukimbia lakini
mganga alinizuia.
“Usiondoke, jini wako
anakuja!” akaniambia.
Niliendelea kukaa huku
nikitetemeka.
Lile wimbi lilikuja kwa kasi,
likawa limesimama kama ukuta, halafu
lilitoweka ghafla. Lilipotoweka liliacha msichana aliyekuwa akitembea juu ya
bahari bila kuzama kama aliyekuwa anatembea
kwenye ardhi.
Nikashangaa na kumuangalia
kwa makini. Alipozidi kutukaribia nilimuona vizuri na kuweza kumtambua. Alikuwa
ni Banuna yule msichana wa kijini. Alikuwa amevaa gauni refu jeupe
alilolishikilia ili lisiloe maji.
Alikuwa akitembea kwa
taratibu huku mganga huyo akiendelea kumuita.
“Njoo haraka njoo haraka!”
Alipofika mwisho wa bahari alianza
kutembea kwenye tope lakini miguu yake ambayo haikuwa na viatu wala kwato
haikuwa ikititia kwenye tope hizo
Alikuja taratibu hadi pale
tulipokuwa. Mara moja tukasikia kupuo la manukato yake.
“Ni nani aliyeniita mimi
binti wa ukoo wa kifalme?” Msichana huyo akauliza kwa sauti kali ya kiburi huku
akimuangalia yule mganga kwa macho makali.
Mganga akajitutumua na
kumjibu.
“Nimekuita mimi mganga
nina…..”
“Unataka nini?” Msichana huyo
akamkatiza. Uso wake ulikuwa umeiva na kuwa mwekundu.
“Zungumza na mimi kwa adabu. Kama…..”
“Wewe nani?” Msichana
alimkatiza tena sasa akionesha kiburi cha wazi.
“Mimi Mtemi Wembe…..’
Msichana huyo akamkatiza
tena.
”Kama
wewe ni Mtemi Wembe, mimi ni Banuna mwana wa Ziraili…mimi wa ukoo wa kifalme.
Wewe huwezi kuniita mimi….”
“Nakwambia…..!” Mtemi wembe
alitaka kusema lakini Banuna hakumpa nafasi.
“Una shida gani na mimi?”
akaendelea kumuuliza kwa sauti yake kali na ya kiburi.
“Nataka kukutenganisha na
Alfred, leo iwe mwisho wako kumfuata!” Mganga akamwambia kwa sauti kali.
Bananuna kwa jeuri alikishika
kiuno chake akamwambia mganga.
“Nakwambia huniwezi! Alfred
nitakuwa naye hadi kifo chake. Simuachi! Unasemaje?”
Hapo hapo mganga naye
akapandisha jini lake.
“Shiit! Wewe nani Tanzania?
Utakwenda tu!. Leo nitakuondoa kwa sababu umekosa adabu!” Jini wa mganga huyo
akasema kwa ghadhabu.
TUKUTANE TENA KESHO UONE NINI
KITATOKEA KATI YA MGANGA NA BANUNA?
| |||||||||||||||||
Sunday, April 10, 2016
HADITHI MWANAMKE ALIENICHUNUKU SEHEMU YA (10)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment