HADITHI
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 6
ILIPOISHIA
Mchungaji alikwenda kutoa
gari lake akanipakia na tukaelekea Gofu. Tulifika
katika lile ghala nililokuwa ninalinda nikamuonesha. Kisha tukaenda katika lile
jumba la zamani lililokaa kama gofu.
“Ndipo hapa?” akaniuliza huku
akishangaa.
“Ndipo hapa” nikamjibu.
Tulishuka kwenye gari tukawa
tunalitazama gofu hilo.
“Wewe ulikuja saa nane usiku
mahali hapa?”
“Ndiyo, nilikuja kumfuata
yule msichana”
“Inaelekea una roho jasiri sana. Mahali hapa wakati
wa usiku panatisha sana.
Hebu tuingie ndani”
Sikutaka kutangulia kuingia.
Nilimuacha Mchungaji atangulie yeye. Kabla ya kuingia alisali kwanza na mimi
nikasali kisha tukaingia.
Tulikwenda hadi katika kile
chumba nilichomkuta yule msichana akiwa na mwenzake wakiwa katika maumbo yasiyo
ya kibinaadamu.
Tulipoingia ndani ya chumba
hicho tulikuta mafiga matatu ya jiko na rundo la majivu. Licha ya kulikagua
jumba lote hatukukuta mtu zaidi ya makorokoro ambayo tulihisi yalirundikwa na
wendawazimu.
“Basi twende zetu” Mchungaji
akaniambia.
Tulitoka, tukapanda gari na
kuondoka.
“Una hakika hukuwa umeota?” Mchungaji akaniuliza.
“Sikuota, nilifika kweli na
kuwaona hao wasichana”
Mchungaji akanyamaza kimya.
Tulikwenda hadi katika lango
la kanisa. Mchungaji akaniambia.
“Kesho ni jumapili, uje
katika ibada ya asubuhi. Tutakufanyia maombi”
“Nitakuja kesho asubuhi
lakini nataka kuuliza, kwa leo hatanifuata tena?”
“Hatakufuata kwa maana ameona
umejisalimisha mahali ambapo hapawezekani”
“Namshukuru sana Yesu”
“Ondoa wasiwasi, tatizo lako
litakwisha. Sasa unaweza kushuka uende zako”
“Asante baba Mchungaji”
Nikashuka kwenye gari na
kufunga mlango na kwenda zangu. Nilizungukazunguka mjini kasha nikarudi
nyumbani.
Ilipofika usiku, nilikwenda
kula chakula kisha nikarudi. Sikuwa na
matembezi ya usiku. Baada ya kukaa kidogo nilichukua Biblia yangu nikasali kisha
nikalala.
Ilipofika saa nane usiku
nilishituka usingizini, nikaona taa ilikuwa inawaka. Kumbe nilisahau kuizima
kabla ya kulala. Mara nilisikia mlango wa chumba changu unabishwa. Moyo wangu
ukashituka na kuanza kunienda mbio.
Nikasikia sauti ya msichana
ikiita “Alfred! Alfred! Nifungulie…”
Mara moja niliitambua sauti
ya yule msichana, nikanyamaza kimya. Lakini ghafla niliona mlango wa chumba
unafunguka.
“Mama yangu wee…nimekwisha!”
nikajisemea kimoyomoyo.
Mlango ulifunguka na kuwa
wazi kabisa. Mbele ya mlango nilimuona msichana amesimama akiangalia ndani.
Sikujua ule mlango aliufungua yeye au ulifunguka wenyewe kwani mikono yake
haikuwa imeshika mlango.
Alikuwa amevaa dera jeupe
lililoziba viatu vyake. Na sikujua kama
alikuwa na viatu au kwato. Alijitanda upande wa kitambaa cheupe kichwani, akauziba
uso wake kwa mtindo wa kiarabu. Masikio yake hayakuwa yakionekana.
Ilikuwa ajabu, jinsi macho ya
msichana yule yalivyokuwa yanabadilika. Nilivyoyaona usiku ule hayakuwa kama nilivyoyaona wakati wa mchana pale kwenye lango la
kanisa. Muda ule wa mchana yalikuwa macho ya kawaida lakini sasa yalikuwa
yamebadilika na kuwa na mboni za kijivu.
Alikuwa ameyapaka wanja mkali
na kwenye nyusi pia alipaka wanja mweusi uliokaa kama
upindi wa mvua.
Alikuwa akitabasamu peke yake
na kuifanya sura yake ionekane ya kupendeza na ya kirafiki.
Mlango ulipokuwa wazi aliinua
hatua na kuingia ndani. Moyo ulinilipuka ukawa unanienda mbio na kijasho
chembamba kikaanza kunivuja.
Kitu ambacho kilinishangaza
muda wote ni kuwa nilikuwa nimejifinika shuka gubigubi na kuziba uso wangu
lakini bado nilikuwa namuona yule msichana.
Alipoingia ndani alisimama
katikati ya chumba na kukitupia macho chumba changu kisha nikamuona anatikisa
kichwa kama vile chumba changu
hakikumridhisha.
Wakati amesimama hapo, kupuo
la harufu ya manukato yake ilienea chumba kizima. Sijawahi kusikia manukato
mazuri kama yale niliyoyasikia usiku ule.
Baadaye nilimsikia akishusha
pumzi kisha akaenda kuketi kwenye kiti kilichokuwa kando ya meza, akauweka mguu
wake mmoja juu ya mwingine kisha akanitazama.
“Alfred!” akaniita. “Inuka
tuzungumze, nimekufuata wewe mpenzi wangu”
Nikanyamaza kimya.
“Usiniendee kwa Mchungaji.
Mimi si adui yako. Mimi ni rafiki yako mwenye lengo la kukusaidia” akaniambia.
Ingawa nilijifanya nimelala,
aliendelea kunisemesha kama vile alijua kuwa
nilikuwa macho.
“Alfred nataka tuwe marafiki.
Tangu siku nilipokuona nilikuchunuka. Sitaficha kukwambia kuwa nimekupenda na
utakuwa mume wangu”
Ndani ya moyo wangu nilikuwa
najiuliza, huyu msichana alikuwa kiumbe wa aina gani?
Hapo hapo nikamsikia
akinijibu. “Mimi ninaitwa Banuna. Ninatoka katika kizazi cha familia ya kijini.
Kwetu ni chini ya bahari, karibu na kisiwa cha Unguja.”
Alivyoniambia kwamba yeye ni
jini anayeishi chini ya bahari alinishitua sana, nikakurupuka pale kitandani na kutoka
mbio huku nikiburuza shuka. Nilifungua mlango nikatoka ukumbini nikiwa na chupi
tu, shuka nilikuwa nimeishikilia. Nilikimbilia mlango wa mbele nikaufungua na
kutoka nje kisha nikaufunga tena.
Nilijifunga ile shuka kwenye
shingo nikatembea kwa mwendo wa haraka haraka kuelekea mtaa wa pili alikokuwa
akiishi rafiki yangu fulani aliyeitwa Juma.
Nilikuwa natembea huku
nikiangalia nyuma. Nilikuwa na wasiwasi kwamba yule msichana anaweza kunifuata.
Lakini hadi ninafika katika
mtaa huo sikumuona yule msichana. Nikaenda katika ile nyumba anayoishi Juma.
Nilibisha kwenye dirisha la chumba chake
lililokuwa upande wa mbele.
“Juma! Juma!” nilimuita.
“Amka unifungulie mlango”
Baada ya muda kidogo, sauti
ya Juma ikasikika ikiuliza.
“Nani wewe?”
“Ni mimi rafiki yako Alfred,
nimepata matatizo, nifungulie mlango”
“Wewe ni Alfred?”
“Ndiyo”
“Subiri”
ITAENDELEA KESHO
| ||||||||||||||||||||||||||
Wednesday, April 6, 2016
HADITHI SEHEMU YA ( 6 )
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment