Mara baada ya kuwasili na kuweka kambi kwenye hotel ya Sea Breeze, kocha mkuu wa timu hiyo, Kinnah Phiri, amezungumza na mtandao huu na kusema kuwa anamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kufika salama jijini Tanga hasa baada ya safari ndefu yenye zaidi ya kilomita 900.
"Ilikuwa ni safari ndefu, ni kilomita zaidi ya 900 kutoka Mbeya mpaka hapa, wote tuko salama tunamshukuru Mungu kwa kutufikisha katika hali hii, jioni ya leo tutafanya mazoezi kwenye uwanja wa Mkwakwani kwa jili ya kuweka sawa miili yetu pia kujaribu kuizoea kwa haraka hali ya hewa ya Tanga, hapa kuna joto hii ni tofauti kubwa na kule tulipotoka alisema."
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha utabibu Dk Joshua Kaseko, amethibitisha kuwa hali za wachezaji hao ziko sawa na ataitumia nafasi ya mazoezi ya jioni ya leo kurejesha uimara wa misuli ya baadhi ya nyota ambao kwa namna moja ama nyingine watakuwa wamepatwa na uchovu mkubwa.
"Hakuna shaka wote wako sawa, ila nitatumia mazoezi ya jioni ya leo kama ambavyo programu ya mwalimu inasema ili kuwaimarisha wale ambao miili yao itakuwa imepata uchovu mkubwa kutokana na safari, kuwasili mapema imetusaidia kwa sababu katika hali ya kawaida mchezaji anapwasa apate japo saa 24 za kupumzika kabla ya kuingia kwenye mchezo alisema."
Baadhi ya nyota waliosafiri kwa ajili ya mchezo huo ni pamoja na Juma Kaseja,Hanningtony Kalyesubula,John Kabanda,Tumba Lui,Raphael Daud,Kenny Ally,Ditram Nchimbi,Yohana Moriss,Meshack Samwel,John Jerome,Hamidu Mohamed na wengine.

No comments:
Post a Comment