MWANAMKE 16 na Faki A Faki 0655 340572
ILIPOISHIA
Nikanyanyuka kwenye kiti na
kumfuata haraka. Wale vijana walikuwa wameshafika barabarani wakaelekea upande
wa Chumbageni kwa mwendo wa kasi.
“Wamepora mkoba wako?”
nikamuuliza.
“Basi waache tu, huwezi
kuwafanya kitu” Zena alisema. Sauti yake ilikuwa tulivu lakini ilionesha
ghadhabu.
“Wale vijana walikuwa wamekaa
muda mrefu nyuma yetu, kumbe walikuwa na lao wanalongojea”
“Hakuna tatizo”
Nilikuwa nafuatana naye
kuelekea kwenye lango la kutokea kwenye bustani hiyo.
“Dah!....”
“Usijali, waache tu. Mimi
nakwenda zangu”
Ile teksi iliyomleta Zena
ikatokea tena na kusimama mahali pale pale pa mwanzo.
Zena akaifuata na kujipakia.
Teksi ikaondoka. Niliisindikiza kwa macho hadi ilipokata kona.
“Majini pia wanapanda teksi!”
nikajisemea moyoni mwangu kisha nikaanza kutembea kwa miguu kurudi nyumbani.
SASA ENDELEA
Kile kitendo cha wale vijana
kilikuwa kimefadhaisha akili yangu.
Sikurudi nyumbani moja kwa
moja, nilikwenda nyumbani kwa kaka. Aliponiona tu akaniuliza.
“Ulifika huko Uhuru Park?”
“Nimefika na nimekutana naye”
“Enhe amekueleza nini?”
“Kwanza
amenirudishia hiki kitabu changu nilichokuwa nimemuazima siku ile kisha akaniomba msamaha kwa usumbufu wowote ambao
niliupata kutokana na yeye”
“Enhe…?”
“Baada ya hapo
akanithibitishia mwenyewe kwamba yeye ni
jinni. Akaniambia kwamba nisimuogope
kwani hatakuwa na madhara na mimi. Lakini la msingi aliloniambia ni kuwa
anataka niwe mume wake…”
“Mume wake kivipi?”
“Nafikiri anataka tuoane”
“Eh…utamuweza kweli mke wa
kijini? Kumbe ana makubwa!”
“Nimemuuliza kwani majini
wanaoana na binaadamu? Akaniambia niende nikamuulize bibi mzaa baba, eti baba
yangu baada ya kumuacha yeye alioa mke gani?”
“Alikuwa na maana gani?”
“Ameniambia nikamuulize tu
halafu nije nimpe jibu”
“Kumbe anamjua pia bibi
yetu?”
“Ameniambia amekuwa na mimi
tangu nikiwa mdogo lakini hakuwa amejitokeza, kwa hiyo familia yetu atakuwa
anaijua”
“Itakubidi hayo maneno ukamueleze
mama”
“Nitakwenda kumueleza”
“Twende kwake sasa hivi”
Tukatoka na kaka kwenda
nyumbani kwa mama. Tulienda kwa miguu. Njiani tulikuwa tukiendelea kuzungumza.
“Ameniambia kama
nitaoana naye atanipa utajiri”
“Hilo si tatizo, tatizo ni kuwa na mke jini”
Kaka akaniambia.
Nikajua suala hilo lilikuwa limemshitua
na yeye.
Tulipofika nyumbani kwa mama,
nikamueleza mazungumzo yote tuliyozungumza na Zena. Mama naye akashituka.
“Hebu nenda ukamuulize bibi yako kuhusu huyo babu yako
usikie atakueleza nini lakini nakushauri usikubali kuoana na huyo mwanamke hata
kama atakupa utajiri” Mama akaniambia.
“Mimi sijakubali, bado niko
kwenye utafiti”
“Wewe ni binaadamu huwezi
kuishi na mwanamke ambaye ni jini” Mama aliendelea kunisisitizia.
“Nitazingatia ushauri wako na
nitakwenda kwa bibi hapo kesho” nikamwambia.
Bibi mwenyewe alikuwa akiishi
Mwambani, mwendo wa kama kilometa kumi kutoka
Tanga mjini. Kitongoji hicho kipo upande wa Kaskazini mwa jiji la Tanga katika
barabara inayoelekea wilaya ya Pangani.
Siku ya pili yake nikaenda
huko Mwambani kwa kutumia pikipiki yangu. Nilipofika nilimkuta bibi yuko
barazani mwa nyumba yake akisuka ukili wake. Ingawa alikuwa kikongwe
sana lakini
bado alikuwa akijiweza kiasi kwamba alikuwa anaweza kusuka ukili wake.
Nilikuwa nimemnunulia kilo
tano za sukari, nikampa.
Baada ya kuulizana hali
nilimwambia licha ya kwenda kumsalimia pia nilikuwa na shida yangu.
“Shida gani?” akaniuliza.
“Nilikuwa nataka kujua eti
baada ya wewe kuachana na marehemu mume wako yaani babu yangu, babu alioa mke
mwingine?”
“Ndio alioa”
“Enhe niambie alimuoa nani?”
“Inasemekana alioa mke wa
kijini, alikuwa akiitwa Zena na huyo Zena ndiye aliyefanya babu yako aniache
mimi. Lakini mimi sikuwahi kumuona”
Nikashituka niliposikia
maneno yale.
“Alimpata wapi huyo mke wa
kijini?” nikamuuliza.
“Alimchunuka tu akamwambia
aniache mimi amuoe yeye. Babu yako akakubali kuniacha kwa ajili ya kupata
utajiri”
“Na ni kweli alipata
utajiri?”
“Alipata utajiri mkubwa sana lakini siku chache
kabla ya kufa kwake utajiri wote ulipotoea na huyo mke wake alitoweka pia”
“Wakati huo alikuwa
umeshamzaa baba?”
“Baba yako alikuwa ameshazaliwa pamoja na
kaka yake Abdul yaani baba yako mkubwa ambaye alifariki nchi za nje”
“Sasa baada ya babu kuoa mke
wa kijini, nani aliwalea kina baba?”
“Aliniachia nao mimi,
nikawalea hadi wakawa wakubwa”
Nikanyamaza kimya nikijiuliza
kama Zena anayemsema bibi ndiye yule anayetaka
nioane naye.
“Kwanini umeniuliza hivyo?”
Bibi aliniuliza na kunizindua.
“Nimekuuliza tu bibi, kuna
mzee mmoja alikuwa akifahamiana na marehemu babu, alinieleza kuhusu kisa hicho
ndio nikaona nije nikuulize” nikamdanganya bibi. Sikutaka kumueleza ukweli kwamba
kuna mwanamke wa kijini alinituma nimuulize.
“Ulikuwa huamini?”
“Nilikuwa siamini lakini
baada ya wewe kunithibitishia sasa ninaamini”
“Wakati babu yako anakufa,
watu walishangaa kuona mali
yote aliyokuwa nayo imepotea. Na yule mke wake naye hakuonekana tena. Alitoweka
wiki moja kabla ya kifo cha babu yako”
“Na huyo babu na mke wake
walikuwa wakiishi maisha ya aina gani?”
“Waliishi maisha ya kawaida
tu lakini mke wake alikuwa hajitokezi katika shughuli za watu”
“Babu alipokuacha uliona
uchungu sana
bibi?”
“Kwa kweli niliumia sana kwa sababu sikuwa
nimemtenda kosa lolote na bado nilikuwa nampenda babu yako”
“Pole sana bibi”
“Oh! Wanipa pole leo wakati
mambo yameshapita zamani!”
“Lakini bibi uliona babu
alifanya jambo la busara kuoa mwanamke wa kijini?”
“Alilazimishwa na yule jini
na aliahidiwa kupata utajiri. Kuna mganga mmoja aliniambia kama
babu yako asingeniacha yule jini angeniua”
“Eh kumbe ni viumbe hatari
kiasi hicho!”
“Ndivyo nilivyoambiwa, sijui kama ningeuliwa kweli”
Pakapita ukimya wa
sekunde kadhaa. Bibi alikuwa akiendelea kusuka ukili wake na mimi nilikuwa
nikiumiza kichwa kwa kuwaza. Hatimaye nikauondoa ule ukimya.
“Kwa mfano mimi nikipata mke
wa kijini, unanishaurije nioane naye?” nikamuuliza.
Bibi akacheka.
“Bibi mbona unanicheka?”
“Unanichekesha. Huyo mke wa
kijini utampata wapi?”
“Kwani babu alimpata wapi?”
“Yule ni mpaka akuchunuke
mwenyewe”
“Sawa. Je akinichunuka na
kuniambia anataka tuoane, nikubaliane naye?”
“Hayo ni mawazo yako sasa,
mimi nikushauri nini?”
“Unaweza kunishauri kwamba
nioane naye au la”
“Hilo
sio jambo la kushauriwa, ni uamuzi wako na huyo jini kama
utampata. Kwani na wewe unataka kupata utajiri?”
“Hakuna asiyetaka utajiri
bibi”
“Angalia sana, utajiri mwingine una matatizo. Ni bora
uishi masikini hivyo hivyo”
Baada ya kimya kingine kifupi
nikamuaga bibi. Wakati nataka kuondoka nikampa shilingi elfu ishirini. Bibi
akanishukuru.
“Haya bibi nakwenda”
nikamuaga bibi na kupanda pikipiki yangu.
“Uende salama, nisalimie wenzako”
“Nitakusalimia”
JE JAMAA ATACHUKUA UAMUZI
GANI? HEBU ENDELEA KUFUATILIA HADITHI HII HAPO KESHO
No comments:
Post a Comment