YALIYONIKUTA TANGA (22)
ILIPOISHIA
Yule jini alipoondoka, yule
mwanamke alituuliza tulichozungumza, tukamueleza.
“Sasa kesho mtakuja?” akatuuliza.
“Tutakuja kesho asubuhi”
nikamjibu.
“Ngoja nikupe dawa yangu”
akatuambia na kuinuka.
Aikwenda pembeni mwa chumba
hicho. Alikuwa ameweka makorokoro yake ya kiganga. Akachukua pembe moja ya
mnyama aliyokuwa ameifunga kitambaa cheusi. Ule upande uliokuwa na shina la ile
pembe aliukung’uta kwenye kiganja chake, ukatoka unga mweusi.
Alinifungia unga huo kwenye
kikaratasi.
“Usiku utatia dawa hii kwenye
maji yako ya kuoga halafu utaoga” akaniambia.
Nikakichuku kile kikaratasi
na kukitia mfukoni.
“Niitie yote au niibakishe?”
nikamuuliza.
“Tia yote”
“Sawa”
SASA ENDELEA
Mganga huyo nilimpa shilingi
elfu kumi tukaondoka. Tuliporudi nyumbani nilifanya kama
nilivyoagizwa na mganga huyo. Usiku kabla ya kulala nilitia ile dawa kwenye
ndoo ya maji ya kuoga kisha nikaenda kuoga.
Nilipotoka kuoga nilikaa
barazani mwa nyumba yetu nikazungumza na ndugu na jamaa waliokuwa pale nyumbani
hadi muda wa kulala ulipowadia.
Asubuhi kulipokucha baada ya
kunywa chai nilichukua kile kisanduku nikakitia ndani ya saflet na
kukibeba kama mzigo. Tukatoka na mama kuelekea kwa yule mganga.
Tulipofika, nilikitoa kile
kisanduku na kumuonesha.
“Kisanduku chenyewe ndio
hiki?” Mgnga akaniuliza.
“Ndio hicho” nikamjibu.
“Hebu kifungue” akaniambia.
Nikakifungua. Mganga alishangaa
alipoona mapambo ya dhahabu yaliyokuwemo ndani.
“Hivi vyote vinaweza kufika
shilingi ngapi?” akaniuliza.
Mara moja nikagundua kuwa
mganga huyo alikuwa ameshapata tamaa ya zile dhahabu.
“Bei ya dhahabu kwa sasa
imeshuka. Hizo zote zinaweza kufika shilingi laki mbili” nikamdanganya.
“Laki mbili tu zikutoe roho
yako!”
“Kwanini?”
“Naona ni pesa ndogo sana”
“Hata mimi nimeona ni ujinga
kutolewa roho yangu kwa pesa hizo ndio maana tumekuja kwako uwazuie hao majini
wasinifuate”
Mganga huyo akanifanyia
uganga wake kisha akatuma mtu aende akachukue mchanga wa kaburini. Alitaka
aletewe kiasi kidogo cha mchanga huo. Mtu aliyemtuma alimletea mchanga huo
alioufunga kwenye kitambaa. Akamuagiza tena akamletee kinyesi cha nguruwe.
Kinyesi hicho kilipatikana
katika nyumba ya jirani ambako walikuwa wanafuga nguruwe.
“Sasa nenda kaninunulie bangi
moja” Mganga akamuagiza tena yule mtu.
Kutokana na kazi yangu ya
upolisi, “neno” bangi ninapolisikia huwa nasisimkwa na mwili na akili yangu
inakwenda kwenye sheria. Lakini muda ule nilitulia kimya kama maji ya mtungi kama vile bangi ilikuwa kitu cha kawaida kwangu.
Hata hivyo nilikuwa
nikijiuliza bangi ilikuwa inatumikaje katika uganga wakati kilikuwa kilevi
kisichokubalika? Sikupata jibu la swali hilo.
Yule mtu aliyetumwa bangi
hakuchelewa sana
akarudi akiwa na bangi yake mkononi. Nikahisi kwamba bangi ilikuwa ikiuzwa sana pale kijijini.
Nikakumbuka zamani
nilishuhudia kesi ya mvuta bangi mmoja aliyedai kuwa akivuta bangi huwa anapata
nguvu ya kulima. Nikajiambia huenda
zilitumika pale kijijini kwa sababu hiyo.
Ile bangi ilipoletwa
ilichanganywa na vile vitu vingine vilivyoletwa kwanza, yaani ule mchanga wa
kaburini na kile kinyesi cha nguruwe.
Baada ya vitu hivyo
kuchanganywa vilitiwa kwenye chungu na kuwekwa kwenye jiko. Baada ya sekunde
chache vilianza kuungua na kutoa moshi. Yule mganga alikuwa ameshika mwiko
akivigeuza huku na huku.
Vilikuwa vikitoa harufu mbaya
iliyokuwa inaumiza kichwa. Mama yangu alipiga chafya mara mbili.
“Kama
unasikia vibaya toka nje” Mganga huyo akamwambia mama.
Mama akatoka nje. Mganga
aliendelea kuvichoma vile vitu mpaka vikaungua na kuwa vyeusi. Aliepua kile
chungu na kukiweka kando ya jiko.
ITAENDELEAKESHO, Usikose kufuatilia mfululizo wa uhondo huu nini kitatokea hapo kesho kupitia blog yako hii makini www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment