Tuesday, March 3, 2015

MGOGORO WA MASHAMBA NA VIWANJA MASIWANI SHAMBA TANGA

Tangakumekuchablog

Tanga,MGOGORO wa mashamba kijiji cha Masiwanishamba Tanga, umeingia sura mpya baada ya kuundwa kamati ya mgogoro ambayo inatarajia kufanya safari kuonana na  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Samweli Sitta.

Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya  miaka saba unadaiwa kulelewa na Idara ya Mipangomiji kwa kulifumbia macho jambo hilo  ambalo sasa limekuwa kubwa na wavamizi kukomba mashamba hadi makazi ya watu. 

Wakizungumza katika mkutano wa wananchi mapema leo asubuhi, wakazi hao walisema  eneo lao limevamiwa na kuwekwa alama kwa nguvu ilhali taarifa zimeshafikishwa Idara ya Mipango miji na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hadi sasa.

Walisema kutokana na hali hiyo wananchi wanashindwa kuendeleza maeneo yao kwa kujenga na baadhi yao kupata kitisho cha kuvunjiwa  nyumba zao ambazo wamejenga na kuishi na familia zao.

“Mgogoro huu  kila siku umekuwa ukifukuta na kuwekana roho juu na kushindwa kuendelea shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi----tumeamua kwa sauti moja kuunda kamati ya mgogoro” alisema Hamis Ramadhani

“Kamati hii itafanya safari hadi ofisi ya waziri wa ardhi nyumba na makazi kumpelekea kilio chetu ambacho kwa muda mrefu kimekuwa hakina msikilizaji ” alisema

Kwa upande wake mkazi wa kijiji hicho, Sada Amour, alisema wavamizi wamekuwa wakijichukulia mashamba ya watu kwa nguvu bila kuwasiliana na uongozi wa serikali ya kijiji.

Alisema kama Idara ya Mipango miji kwa kushirikiana na halmashauri ya jiji haitachukua hatua za kisheria kunaweza kutokea hali ya kutofautiana baina ya pande mbili hizo na hivyo ni nyema kupatikana muafaka mapema.

Alisema wakazi wengi wamekuchukuliwa maeneo yao kwa nguvu na hata pale ambapo wamekuwa wakipeleka malalamiko yao katika iadara husika wamekuwa wakishindwa kupata msaada.

“Kila siku tumekuwa tukipanga foleni mipango miji kulalamika mashamba yetu yanavyochukuliwa kwa nguvu lakini hakuna msaada wowote ---kwa vile umasikini ndio sababu ya kudhulumiwa” alisema Sada

Aliwataka wananchi kuwa na uvumilivu na kuacha kutumia kauli zenye kuhatarisha uvunjifu wa amani wakati suala lao likishughulikiwa ngazi ya juu ambako wako na imani kuwa kero yao itasikilizwa.

                                         Mwisho

 Mkazi wa kijiji cha Masiwanishamba halmashauri ya jiji la Tanga, Lucyiana Antony, akilalamika mashamba na viwanja vyao kuvamia na watu ambapo wameingiwa na hofu ya kuingiliwa hadi viwanja katika nyumba zao.
 Mwenyekiti wa mgogoro kijiji cha Masiwanishamba halmashauri ya jiji la Tanga, Ramadhani Chombo, akizungumza na wanachi wa kijiji cha Masiwanishamba wakati wa mkutano baada ya mgogoro wa uvamizi wa mashamba na viwanja kuibuka kwa kasi na kuadhimia kuonana na Waziri wa Ardhi, Nyuma na Makaazi, Samwel Sitta.


 Wakazi wa kijiji cha Masiwanishamba halmashauri ya jiji la Tanga, wakionyeshana alama iliyowekwa na watu wasiojulikana na kutakiwa kuachia mashamba hayo kwa hiyari vyenginevyo uvamizi utaendelea hadi katika viwanja vyao vilivyoko katika makazi.

No comments:

Post a Comment