Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu cha Candle Education Centre. Kituo kiko na walimu waliobobea. Wapo Tanga mkabala na banki ya CRDB simu 0715 772746
JAMBO LEO
Mwalimu wa shule ya Sekondari Kibasila,
Gaudensia Albert aliyekuwa akihifadhi kinyesi ndani kwak kwa miaka
miwili amepelekwa Hospitali ya Muhimbili baada ya daktari wa Hospitali
ya Temeke kubaini ana matatizo ya akili.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo,
Kyando amesema baada ya kugundulika kwa tukio hilo walimpeleka Hospitali
ya Temeke kwa kuangalia afya yake ambapo daktari akasema ana tatizo la
akili, wakamuhamishia Muhimbili.
Baada ya kufikishwa Muhimbili madaktari walimpatia dawa ambazo anatumia mpaka sasa pamoja na ushauri.
“Sisi bado tunamhitaji kutokana na tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi ulioko nchini”—alisema Mwalimu Kyando na kuongeza kuwa mbali na tatizo la kukutwa na kinyesi bado mwalimu huyo alikuwa anafundisha vizuri.
MWANANCHI
Licha ya kampeni kubwa ya kupambana na
kuzuia usafirishaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya Tanzania bado
Watanzania wameendelea kufanya biashara hiyo, katika kipindi cha siku
30 mabinti 12 wamekamatwa wakisafirisha dawa hizo ndani na nje ya nchi.
Taarifa zilizolifikia gazeti la MWANANCHI na kuthibitishwa na Kamishna wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa
zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya Watanzania waliokamatwa katika kipindi
hicho ni mabinti wenye umri mdogo ambapo mabinti wanane wamekamatwa
Uwanja wa Ndege wa Hong Kong na wanne katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Dar es Salaam.
Kamishna Nzowa alisema ingawa vyombo vya
habari na wafungwa walioko Hong Kong wamejaribu kuwashauri Watanzania
wasifanye biashara hiyo, bado wamekuwa na ‘shingo ngumu.’
Wakati huo huo Padri John Wotherspon
aliyekuwa nchini kwa ajili ya kampeni ya kuwazuia vijana wa Kitanzania
kusafirisha dawa za kulevya amesema wanawake wanane wa Kitanzania pia
wamekamatwa katika uwanja wa ndege wa Hong Kong katika kipindi hicho
hicho.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amedokeza kuwa
matukio ya watu wasiojulikana kuvamia vituo vya polisi, kupora silaha na
kuwashambulia askari ‘yana sifa za ujambazi na mwelekeo wa kigaidi’
huku akisema hali ya usalama nchini ni nzuri kutokana na matukio hayo
pamoja na mengine ya mauaji ya albino.
“Matukio haya yana sura mbili. Yana sura
ya ujambazi, lakini pia baadhi yake yana dalili za ugaidi. Vyombo vyetu
vya usalama vinaendelea kufanya kazi yake ya uchambuzi wa kila tukio na
kulipa nafasi yake stahiki,”– Rais Kikwete.
Rais Kikwete alitoa orodha ya matukio ya
kuvamiwa vituo vya polisi ambavyo ni pamoja na vya Newala mkoa wa
Mtwara, Ikwiriri Wilaya ya Rufiji, Kimanzichana vilivyovamiwa ndani ya
kipindi cha miezi 12 na jumla ya bunduki 38 ziliporwa na askari polisi
saba kuuawa.
Rais Kikwete ametoa pongezi kwa polisi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) kwa kazi nzuri ya kupambana na uhalifu nchini.
MWANANCHI
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
limesema linaendelea na kazi ya kurekebisha hitilafu kwenye mfumo wa
LUKU kwa njia ya mitandao ya simu ili kuwalipa ‘units’ wateja wake
waliokatwa pesa zao kabla ya kupata huduma hiyo ambapo kwa zaidi ya siku
mbili huduma hiyo imekuwa haipatikani kwa njia ya simu.
Akizungumzia suala hilo, Meneja Uhusiano
wa Tanesco, Adrian Severin alisema jambo la kwanza ni kuwapa ‘units’
wateja ambao tayari wameshalipia, baadaye wateja wengine watanunua umeme
kupitia simu zao.
“Kuna hitilafu ya kiufundi imetokea
kwenye mfumo wa Luku, tunatarajia usiku wa leo (jana) kazi itakamilika.
Baada ya hapo tutatoa huduma kwa wote waliokatwa pesa zao bila kupata
huduma,” — Adrian Severin.
Msemaji huyo wa Tanesco alisema huduma ya Luku bado inapatikana kupitia Maxi Malipo na Benki za CRDB, NMB.
Alisisitiza watu kutumia miamala ya kibenki kulipia umeme ili kupunguza foleni kwenye mashine za Maxi Malipo.
Mkazi wa Tabata Segerea, George Ismail
alisema; “Jana nimekaa kibandani saa matatu nikisubiri kununua umeme.
Sijazoea hali hii, ninajua kuna shida fulani, lakini sijui tatizo ni
nini, sijapata taarifa zozote kutoka Tanesco,” alisema Ismail na
kuongeza kuwa alijaribu kwa njia ya simu pia huduma hiyo ilishindikana.
Hata hivyo, jana Tanesco lilitoa taarifa
kupitia gazeti hili juu ya tatizo la kiufundi lililotokea kuanzia
Februari 28 na kubainisha kuwa mafundi walikuwa wakiendelea kulifanyia
kazi tatizo hilo.
Hii siyo mara ya kwanza huduma ya Luku
kuleta adha kwa wananchi, Januari mwaka huu kulikuwa na tatizo la
upatikanaji wa Luku katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam.
MWANANCHI
Waziri wa Ujenzi, John Magufuli
ameupongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuwachukulia
hatua watendaji wa Kampuni ya Dott Services kwa kosa la kuchelewesha
ujenzi wa barabara ya Mkumbara hadi Same yenye urefu wa kilomita 96.
Kampuni hiyo yenye makao yake makuu
Uganda, imeshindwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo unaogharimu
Sh103.8 bilioni huku kampuni ya Strabag iliyochukua ukandarasi wa
kujenga barabara kama hiyo ya Korogwe hadi Mkumbara, ikimaliza kazi yake
Desemba 3 mwaka jana kama ilivyosaini mkataba.
Dk Magufuli alitoa pongezi hizo wakati akikagua barabara hizo baada ya Mtendaji Mkuu wa Tanroad, Patrick Mfugale
kuelezea kwamba alilazimika kuwafukuza baadhi ya mameneja wa Kampuni ya
Dott Services wanaodaiwa kusababisha isikamilike kwa wakati.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa
hiyo, Dk Magufuli alielezea kutoridhishwa kwake na hatua ya Kampuni ya
Dott Services ya kuchelewesha ujenzi huo na kuitaka iharakishe ili Rais Kikwete aweze kuifungua kabla hajaondoka madarakani.
Aliipongeza Strabag kwa kukamilisha
ujenzi kwa wakati na kuitaka kufanyia marekebisho madogo katika maeneo
yaliyoonyesha dalili ya lami kuvimba.
NIPASHE
Rais Kikwete jana ameongoza umati wa watu kuaga mwili wa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba ambapo
mwili huo pia ulipokelewa na kuagwa na umati kikubwa wa wakazi wa
Manispaa ya Songea katika uwanja wa ndege na wa mpira wa Maji Maji.
Shughuli za kuuaga mwili huo zilifanyika
katika viwanja vya Karimjee na kuhudhuriwa na umati wa wananchi
wakiwamo viongozi wa serikali, mawaziri, wabunge, vyama vya siasa na
asasi mbalimbali za kiraia.
Spika wa Bunge, Anne Makinda
ni miongoni mwa viongozi waliobubujikwa machozi hasa wakati ukiimbwa
wimbo maalum wa maombolezo ambao uliwahi kuimbwa na Komba mwenyewe enzi
za uhai wake wakati wa msiba wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1999, lakini ukiwa umeingizwa vibwagizo vingine vilivyokuwa vikimtaja mbunge huyo.
Wengine walioshindwa kuzuia hisia zao ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho, Yusuph Makamba.
Spika Makinda alisema Komba
amezimika kama kibatari huku akitunga nyimbo na akijiandaa kwenda
Ethiopia na wabunge wenzake wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii.
“Alifariki dunia akiandika nyimbo…sisi
sote ni wa Mungu, tutaondoka..huko kuna raha, inategemeana na mtu
alivyoishi. Alikuwa ni mtu wa kucheka na yeyote na yeye amekwenda
kupeleka hesabu za kazi alizozifanya,” alisema Makinda na kuongeza.
“Alikuwa kipenzi cha wengi na sisi CCM
tunaamini Mungu atatupatia Komba mwingine. Naomba tuache kusema vibaya
juu yake….nafikiri Komba angeambiwa kwamba baada ya robo saa utakufa,
jambo la kwanza ambalo angeeleza angeomba msamaha.”—Spika Makinda.
NIPASHE
Mbunge William Ngeleja leo
amepandishwa katika Baraza la Maadili ya viongozi wa umma kuhojiwa juu
ya tuhuma zinazomkabili za kunufaika na mgawo Sh. milioni 40 kutoka
katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Baraza hilo jana liliahirisha shughuli zake za kumhoji Mkurugenzi wa Sheria, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma kutokana na shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni Komba katika viwanja vya Karimjee, eneo ambalo Baraza hilo linafanyia mahojiano hayo.
Wakati Baraza likimhoji Ngeleja leo, tayari limekwisha wahoji Wabunge Andrew Chenge na Prof. Anna Tibaijuka ambapo Baraza hilo litaendelea na shauri la Prof. Tibaijuka Machi 13, mwaka huu baada ya Wakili wake Dk. Rugemaleza Nshala, kuomba udhuru wa kwenda Marekani kwa siku 10.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu Hamisi Msumi, alisema shauri hilo litaamuliwa kama liwe la uamuzi wa ndani au hadharani.
Kwa upande wa Chenge, tayari alikwishakata rufaa katika Mahakama Kuu kuzuia shauri lake lisijadiliwe.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment