NILIJUA NIMEUA (1)
Kijuana kwangu na Halima
kulikuwa kwa bahati sana. Awali sikuwa na mawazo kabisa ya kwamba nitakuja
kukutana na kusuhubiana na msichana mrembo kama yeye.
Siku moja ambayo
ninaikumbuka hadi leo nikiwa kwenye teksi yangu maarufu kama Majombi Teksi,
nilikuwa ninatoka hospitali ya Bombo ambayo ni hospitali ya mkoa iliyoko Tanga.
Nilikuwa nimempeleka
mama mmoja mjamzito kutoka hospitali ya Ngamiani. Mama huyo alipelekwa hospitalini
hapo kujifungua lakini kutokana na umri wake kuwa mkubwa madaktari wakaamua
wamhamishie Bombo.
Ndugu zake waliiona
teksi yangu ambayo huiegesha karibu na hospitali hiyo kusubiri abiria,
wakanikodi niwapeleke Bombo.
Wakati narudi kutoka
Bombo mvua ilikuwa imeanza kunyesha. Nikaona msichana aliyekuwa amesimama
pembeni mwa barabara akinipungia mkono kwa bidii huku akitota na mvua. Ilikuwa
wazi kuwa mvua ilimkuta ghafla njiani na mahali alipokuwa hapakuwa na sehemu ya
kujisitiri. Mimi kama dereva wa teksi nilishukuru kwa hilo.
Nilipunguza mwendo na
kuisimamisha gari pembeni mwa barabara. Nilikuwa nimempita kidogo. Alipoona
teksi imesimama aliifuata haraka akafungua mlango wa nyuma na kujipakia.
“Unakwenda wapi?”
nikamuuliza.
“Nipeleke barabara 20
nyuma ya CCM” akaniambia. Sauti yake ilikuwa nyembamba na nyororo.
Alijisogeza katikati ya
siti ili kukwepa upepea wa mvua uliokuwa ukipenya kwenye dirisha. Nikawa
namuona vizuri kwenye kioo cha gari cha kutazamia nyuma.
Wakati naiondoa teksi
nilikuwa namkodolea macho kupitia kwenye kioo hicho bila mwenyewe kujua.
Uso wake ulikuwa
umenywea kutokana na fadhaa ya kutoswa na mvua lakini alikuwa na sura jamali ya
macho makubwa aliyoyapaka wanja mzito. Juu ya macho yake pembeni mwa kopi
alikuwa amepaka rangi iliyoendana na nguo aliyokuwa amevaa.
Pua yake ilikuwa ndefu
na midomo ya wastani aliyokuwa ameipaka rangi hafifu ya waridi.
Nilimuona tangu
alipokuwa amesimama alikuwa mrefu , mweupe na mwenye mwili wa wastani. Vazi alilokuwa
amevaa, dera la maua ya rangi ya bluu ya kung’aza na ushungi wake aliokuwa
ameutanda kichwani vilimfanya aonekane alikuwa msichana aliyejistahi sana.
“Mvua za ghafla namna
hii zinatuharibia bajeti” akasema kwa sauti ya kuchukia.
“Kwanini?” nikamuuliza
huku nikitia gea ya pili.
“”Mahesabu yangu
yalikuwa kupanda bodaboda, sasa nalazimika nipande teksi ili nisitote, huoni
kuwa nimeshaharibu bajeti yangu?’
Nikatoa tabasamu jepesi.
“Na sisi ndio tunapata
riziki zetu, usiilani”
“Kwa hiyo unaiombea ili
upate abiria kwa wingi eti?”
“Ndiyo maisha yalivyo.
Huwezi kumwambia daktari unaombea watu waumwe ili waje kwako upate pesa, au
huwezi kumwambia muosha maiti kuwa anafurahia watu wafe apate kazi. Yeye pia
anasikitika mtu akifa lakini ndiyo maisha. Kwa mmoja kukienda kilio kwa
mwingine kunakwenda furaha”
“Sawa bwana, umeshinda
wewe”
Nikacheka. “Sasa unataka
nikalie wapi dadangu kama sio kwenu?”
“Basi nipunguzie kidogo”
“Ni shilingi elfu tano
tu”
“Ndiyo nakwambia
nipunguzie, nitakupa elfu tatu”
Nikatikisa kichwa.
Tabasamu lililokuwa usoni kwangu likatoweka. Sikutaka masihara yaingie kwenye
kazi yangu. Teksi ile haikuwa mali yangu. Nilikuwa nimeajiriwa na mwenyewe
alitaka nimpelekee shilingi elfu ishirini kila baada ya masaa ishirini na nne,
bila kujali nimeingiza kiasi gani.
“Elfu tano ndio kima
chetu, haipungui. Petroli imepanda sana” nikamwambia.
Wakati nampa jibu hilo
simu yake iliyokuwa kwenye mkoba wake ilianza kuita. Akaitoa na kuipokea.
ITAENDELEA KESHO, usipitwe na uhondo huu wa kusisimua kupitia blog hii www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment